Habari za Punde

Wazimbabwe kuzihukumu Stars, Gambia

DAR ES SALAAM
WAKATI timu ya Taifa ya Gambia 'The Scorpions' ilikuwa ikitarajiwa kuwasili nchini saa 9:20 alfajiri ya kuamkia leo, kwa ndege ya Kenya Airways kuikabili Taifa Stars, Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa) limetaja waamuzi kutoka Zimbabwe kuwa ndio watakaochezesha mechi hiyo.

Mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa keshokutwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ni wa mchujo wa kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, ambazo zitafanyika nchini Brazil.

Mwamuzi wa kati aliyeteuliwa kuhukumu mpambano huo ni Ruzive Ruzive akisaidiwa na Salani Ncube na Edgar Rumeck wakati mwamuzi wa akiba ni Norman Matemera.

Kamishna wa mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 jioni ni Fanie Wallace Mabuza kutoka Swaziland wakati mtathmini wa waamuzi (referee assessor) ni Ali Baligeya Waiswa.

Waamuzi hao wanatarajiwa kuwasili leo saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways, huku Kamishna akitua saa 12.50 jioni kwa ndege ya South African Airways na Mtathmini wa waamuzi atafika nchini leo saa 7.55 mchana kwa ndege ya Kenya Airways.

Nayo timu ya Taifa ya Gambia 'The Scorpions', inakuja na wachezaji 22 wakiwemo tisa wanaocheza mpira wa kulipwa nje ya nchi hiyo.

Wachezaji waliomo katika kikosi hicho ni Musa Camara, Abdou Jammeh, Momodou Futty Danso, Lamin Basmen Samateh, Ousman Koli, Pa Saikou Kujabi, Mustapha Kebba Jarju, Yankuba Mal Ceesay na Demba Savage.

Wengine ni Saihou Gassama, Alieu Darboe, Momodou Ceesay, Pa Modou Jagne, Tijan Jaiteh, Bubacarr Sanyang, Christopher Allen, Musa Yaffa, Sulayman Marr, Mamut Saine, Hamsa Barry, Ali Sowe, Omar Colley na Saloum Faal.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.