Habari za Punde

Wanaochangia Damu Wasikimbie Majibu

Na Salum Vuai, MAELEZO
KITENGO cha damu salama Zanzibar, jana kimezindua wiki ya uchangiaji damu huku, jamii ikishauriwa kuongeza kasi katika kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wakati wa dharura.

Uzinduzi huo ulifanyika katika viwanja vya Wizara ya Afya Mnazimmoja, ambapo Naibu Waziri wa Afya Dk. Sira Ubwa Mamboya aliwaongoza wafanyakazi wa wizara hiyo katika uchangiaji damu kwa hiyari.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyoandaliwa na kitengo cha Benki ya Damu, Dk. Sira aliishajiisha jamii kutokuogopa kujitokeza kwa ajili ya kuchangia damu, akisema itasaidia kuokoa maisha kutokana na ajali mbalimbali pamoja na kinamama wanaohitaji wakati wa kujifungua.

Alisema kuchangia damu ni jukumu la kila mwananchi anayeipenda nchi na binadamu wenzake, na hivyo ni vyema watu wahamasike kuchangia ili kukidhi mahitaji ya benki.

"Kama mtu anajihisi anayo damu ya kutosha, kwa nini asichangie wakati kufanya hivyo kunasaidia upatikanaji wake badala ya kusubiri ndugu watafutane pale kunapotokea dharura kama vile ajali", alisisitiza.

Naye Katibu wa Jumuiya ya Wachangiaji Damu kwa Hiyari Zanzibar (JUWADAHIZA) Bakari Magarawa, alieleza changamoto mbalimbali zinazoikabili jumuiya hiyo, ikiwemo wananchi wengi wanaojitokeza kuchangia kwa mara ya kwanza, kutokurudi kuchukua majibu yao wakihofia kuambukizwa maradhi mbalimbali hasa virusi vya UKIMWI.

Alisema hilo si lengo la kuwahamasisha wananchi kuchangia, na kuwataka waache woga kwani hata kama watabainika kuwa na maradhi tafauti, hupatiwa ushauri nasaha na taarifa zao kufanywa siri, na zaidi kuweza kutambua matatizo yanayowakabili ili waweze kujitibu.

Alifahamisha kuwa mahitaji ya benki kwa sasa ni kupata chupa 60 za damu iliyo salama kila siku, ili kuweza kuwa na akiba ya kutosha na hivyo kuwaondoshea usumbufu watu wanaoihitaji kwa matumizi katika hospitali za Unguja na Pemba.

Mchangiaji Arabia Mohammed, alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wengine wajenge utamaduni wa kuchangia damu, kwa kusema kuwa si vyema kuogopa kwani hata wakiwa na maradhi itakuwa vyema kwa kuwa watapata kujitibu.

Alieleza kuwa benki ya damu ni kitengo muhimu kwa kujenga taifa lenye wananchi wenye afya bora, na pia inajenga imani ya kusaidiana wakati wa shida.

Uzinduzi huo umefanyika katika maandalizi ya kuadhimisha Siku ya Uchangiaji Damu Duniani inayofikia kilele Juni 14, ambapo mwaka huu Zanzibar itafanya maadhimisho yake kwenye uwanja wa Gombani Wilaya ya Chake Chake Pemba.

Ujumbe wa mwaka huu ni "Tuchangie damu kwa wingi tuokoe maisha ya wengi".

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.