Habari za Punde

Dk. Kawambwa Amkingia Kifua Ndalichako

Na Kunze Mswanyama, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa amesema utaratibu unaotumika kusahihisha mitihani ya taifa ukiwemo wa kidato cha IV na cha VI hautoai mwanya na nafasi ya upendeleo.

Waziri huyo alieleza hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa ufafanuzi dhidi ya madai ya kuwepo kwa upendeleo wa usahihishaji wa mitihani unaofanywa na Baraza la Mitihani Tanzan (NECTA).

Katika malalamiko ya hivi karibuni Baraza la Wakuu wa skuli za Kiislamu, hivi karibuni walidai kutokuridhishwa na ufaulu wa watahiniwa katika somo la elimu ya kiislam katika mitihani ya kidato cha VI.

Dk. Kawambwa alisema mfumo wa NECTA katika usahihishaji wa mitihani hauwezi kubaini wala kuonesha dini, kabila na hata itikadi ya kisiasa ya mtahiniwa.

Alisema katika mfumo wa usahihishaji mitihani hiyo hakuna uwezekano upendeleo kwani kila msahihishaji husahihisha suali moja kwa kila mtihani na kumpa msahihishaji mwingine kuendelea kusahihisha suali jingine.

Dk. Kawambwa alisema kuwa utaratibu unaotumika kuwapata wasahihishaji mitihani hauruhusu mkuu yoyote wa skuli kuandika kabila la mwalimu yoyote anayependelezwa kuteuliwa kuwa msahihishaji wa mitihani.

Alisema dosari zilizotokea ni za kibinadamu na kamwe zisihusishwe na hujuma yoyote huku akifafanua zaidi kuwa hata kwenye mitihani ya watahiniwa hakuandikwi jina bali ni namba ambayo msahihishaji hawezi kumfahamu kirahisi.

Alisema baada ya kuwepo kwa lalamiko hilo serikali ilihakiki tena matokeo ya mitihani ya masomo hayo ya kiislamu na kwamba matokeo waliyoyapata yanalingana na kumbukumbu za matokeo yaliyotolewa na NECTA.

"Baada ya kugundua dosari hiyo kwa somo la elimu ya kiislamu,uhakiki ulifanywa upya kwa masomo yote ya kidato cha sita ili kujiridhisha kama kuna dosari yoyote. Matokeo ya uhakiki huo yalionesha kuwa alama sanifu zilizokokotolewa na mfumo wa kompyuta ni sawa na alama zilizokokotolewa na kikokotozi. Hivyo hakuna dosari yoyote iliyobainika katika masomo mengine",alihitimisha waziri huyo.

Waziri huyo alisema kuwa pamoja na marekebisho, wizara hiyo itaunda kamati ya wataalamu kuiwezesha serikali kujiridhisha zaidi na hatua zilizochukuliwa na Baraza la Mitihani ili kuepuka dosari ya aina hiyo isijitokeze tena kwa siku zijazo.

Waziri huyo aliwatoa hofu wazazi, walezi na waumini wa dini mbali mbali kuwa suala hilo tayari limeshapatiwa ufumbuzi na kwamba waliorekebishiwa matokeo yao watajiunga na Vyuo Vikuu endapo watakuwa na sifa za kujiunga.

Ufafanuzi huo umekuja siku kadhaa baada ya kuwepo migongano baina ya NECTA, Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) na Baraza la Wakuu wa Skuli za kiislamu waliotaka Mkurugenzi Mtendaji wa NECTA DK. Joyce Ndalichako avuliwe madaraka kutokana na kushindwa kuwajibika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.