Joseph Ngilisho, ARUSHA
MKAZI kijiji cha Olkeijulongishu aliyefahamika kwa jina la Neisisiri Mokoroo (25), amekufa baada ya kupigwa fimbo za tumbo na mumewe kwa madai kuwa ujauzito alioubeba sio wa kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha ACP Liberatus Sabas, alisema tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji cha Olkeijulongishu wilayani Longido majira ya saa 11: 00 jioni.
Alisema marehemu alikutwa na mauti baada ya mumewe aitwaye Kapaito Naanjarati, kumshambulia mkewe kwa kumpiga na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyomsababishia kufikwa na mauti.
Aidha alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba, tukio hilo lilitokea baada ya wawili hao kwenda shambani kukata nyasi na walipofika huko, ndipo mtuhumiwa ambaye ni mume wa marehemu alipomtuhumu mkewe kwamba ujauzito alionao si wa kwake.
Alisema kuwa bwana huyo aliendelea kumkamia mkewe kwa kumueza kuwa ujauzito huo amepewa na mwanamume mwingine na kiuanza kumchapa fimbo.
Kamanda Sabas alisema kulizuka malumbano kwa wawili hao hali ilisababisha mumewe kuanza kumshambulia kwa fimbo tumboni, hadi marehemu kuishiwa nguvu na baadae alifariki dunia.
Baada ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa alikimbia na kuelekea kusiko julikana, ambapo jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi wilayani humo wameanza msako wa kumtafuta mtuhumiwa huyo.
Alisema mara tu atakaposhikwa na uchunguzi kukamilika atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yake yanayomkabili, ambapo alisema mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Longido kwa uchunguzi zaidi.
Wakati huo huo, mwili wa mtu asiyefahamika mwenye ulemavu wa ngozi, (Albino) umetelekezwa kwenye chumba cha maiti katika hospitali ya Mkoa Mout Meru, akiwa amekatwa mikono na kunyofolewa sehemu za siri na watu wasiofahamika.
Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda Sabas na kuwataka wananchi kujitokeza kuutambua mwili huo.
No comments:
Post a Comment