Habari za Punde

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Zanzibar yaeleza nafasi kwenye uchaguzi mkuu

KAMISHANA  wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Zanzibar, Mhe. Khatib Mwinyichande, amesema Tume hiyo, ina nafasi ya kikatiba katika kuhakikisha uchaguzi mkuu nchini unakuwa huru haki na kuzingatia misingi ya utawala bora.

Mwinyichande ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), kwenye banda la Tume hiyo.

Alibainisha kuwa jukumu kubwa la Tume hiyo ni kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na misingi ya utawala bora, suala alilolieleza kuwa na nafasi ya moja kwa moja kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu.

"Uchaguzi si tukio la kisiasa pekee, bali ni jambo linalogusa haki na msingi ya wananchi, kwa kuwa nchi yetu ya kidemokrasia hupatikana kupitia uchaguzi huru na wa haki". Alieleza Kamishna Mwinyichande.
 
Alisema jukumu kuu la kuu la THBUB ni kuhakikisha misingi ya kisheria na haki za binadamu zinalindwa katika kila hatua ya uchaguzi,"

Mhe. Mwinyichande alieleza THBUB inakuwa miongoni mwa waangalizi wa uchaguzi kuanzia kampeni, hadi siku ya kupiga kura, huku akisisitiza kuwa Tume itakuwa ikifuatilia mwenendo wa uchaguzi na kuandika ripoti itakayowasilishwa kwa mamlaka husika.

"Katika kila hatua ya uchaguzi, Tume itachunguza, ikibaini changamoto au mapungufu, na kuyawasilisha kwa mamlaka ya uchaguzi kwa ajili ya marekebisho kwenye uchaguzi unaofuata. Hii ni njia mojawapo ya kulinda haki za wananchi," aliongeza.

Kuhusu Maonyesho ya Sabasaba, Kamishna Mwinyichande ameeleza ushiriki wa THBUB kwenye Maonyesho ya Sabasaba, ni sehemu ya kutekeleza jukumu lake la kuelimisha umma kuhusu haki, wajibu na namna ya kuishi kwa kuheshimu sheria na misingi ya demokrasia.

"Maonyesho haya yanatukutanisha moja kwa moja na wananchi, kupokea malalamiko yao, kutoa elimu ya haki za binadamu, na kuwaeleza kuwa sisi ni watetezi wao pale wanapokwazwa na kukosa haki zao," ameeleza Mhe. Mwinyichande.

Amesisitiza elimu hiyo inawasaidia wananchi kufahamu kuwa, haki zao zinalindwa kisheria na kwamba Tume ipo kwa ajili ya kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaguliwa au kunyimwa haki zake kwa misingi yoyote.

Maonyesho ya Sabasaba yanatumiwa na taasisi mbalimbali kama jukwaa la kuwasiliana moja kwa moja na wananchi. 

THBUB pia inatumia fursa hiyo kuimarisha uelewa wa umma kuhusu haki za misingi ya utawala bora na njia sahihi za kudai haki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.