Habari za Punde

Dk Shein Atuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Ghana

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambi rambi Rais wa Ghana Mhe. Dramani Mahama, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Mhe. John Atta Milla. 

Katika salamu hizo Dk. Shein alisema kuwa yeye mwenyewe binafsi pamoja na wananchi wa Zanzibar wamepata mshtuko na huzuni kubwa baada ya kupata taarifa ya kifo cha kiongozi huyo kilichotokea hapo juzi. 


Salamu hizo za rambi rambi zilieleza kuwa Dk. Shein amepokea kwa mshtuko mkubwa, masikitiko na huzuni nyingi taarifa ya kifo cha Rais John Atta Milla. Aidha, salamu hizo za trambirambi zilieleza kuwa Dk. Shein kwa upande wake pamoja na wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao wa Ghana katika msiba huo mkubwa lililoikumba taifa hilo. 

Salamu hizo zilieleza kuwa Rais John Atta Mills atakubukwa kwa ushujaa wake na umahiri katika kujenga demokrasia na uchumi wa nchi hiyo pamoja na Afrika kwa ujumla. 

Katika salamu hizo Dk. Shein amesema “Kiongozi huyu ni mpiganaji mkubwa wa haki na usawa wa watu wote na atakumbukwa kwa hayo”, alisema Dk. Shein. 

Salamu hizo, zilimuomba MwenyeziMungu awape moyo wa subira na uvumilivu wanafamilia pamoja na wananchi wote wa Ghana ili waweze kuhimili kipindi hiki cha msiba mkubwa na majonzi. 

Rais Dramani Mahama mwenye umri wa miaka 53, aliapishwa saa kadhaa baada ya kifo hicho cha kiongozi huyo Rais John Atta Milla aliyekuwa na umri wa miaka 68 kufariki dunia hospitalini mjini Accra baada ya kuiongoza nchi hiyo tokea mwaka 2009. 

Akiapishwa mbele ya kikao maalum cha Bunge kilichoitishwa kwa dharua, Rais Mahama ambaye kabla ya wadhifa huo alikuwa Makamu wa Rais aliahidi kuwahudumia raia wote wa Ghana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.