Ameir Khalid na Fatma Omar, DJS
WAZIRI wa Nchi Ofisa ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi Haji Makame, amewataka wahitamu wa mafunzo ya
kikosi kazi cha doria ya utalii kujiepusha na vitendo viovu dhidi ya watalii.
Waziri huyo alieleza hayo jana alipokua akifunga mafunzo ya kikosi kazi cha ulinzi wa utalii huko katika viwanja vya polisi Ziwani sherehe ambazo zilihudhuriwa na viongozi mbali mbali na maofsa wa vikosi vya SMZ na viongozi wa sekta ya utalii.
Alisema watalii wanahitaji ulinzi na usalama wa mali zao hivyo kuwepo kwa kikosi hicho kutawawezesha watalii hao, kuishi kwa amani pamoja na mali zao kwa lengo la kuzidi kuimarisha soko la utalii Zanzibar
Alisema nchi nyingi zinawekeza katika sekta ya utalii hivyo serikali haina budi kuimarisha zaidi katika sekta ya ulinzi kwa watalii ili kuingia katika soko la ushindani kwa kuingiza watalii wengi zaidi .
"Serikali ya mapinduzi Zanzibar ina tegemea utalii kwa 80% katika pato lake la taifa hivyo si vyema kuona watalii wanafika nchini wanabughudhiwa kwa kunyang’anywa mali zao, na kuhatarishiwa maisha yao,kwa hiyo mna wajibu wa kuwalinda watalii hao’’alisema.
Aliongeza kuwa wahitimu hao wanapashwa kuwa wajasiri kwa kupambana na wahalifu na kuhakikisha kuwa wanawapa ulinzi wa kutosha wageni ambao wameamua kuja kwa ajili ya utalii.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema kuwa mafunazo hayo yaliotolewa yataweza kuleta maendeleo ya utalii, kwa vile viterndo vingi vya uhalifu dhidi wa wageni vitapungua kwa kiasi kikubwa.
Kamishna huyo aliiomba kukitumia Chuo cha Polisi katika mafunzo na masuala yote ambayo yanahusiana na sekta ya ulinzi, kwani chuo hicho kina walimu wazuri wa fani hiyo.
Mafaunzo ambayo ni miongoni mwa mikakati ya serikali ya kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa kwa kiasi kikubwa, hasa ukichukulia dhana ambayo hivi sasa ipo ya utalii kwa wote, ambapo jumla ya askari 123 wamemaliza mafunzo yao ya miezi miwili.
No comments:
Post a Comment