ZACADIA
-Wazanzibari waishio Canada wataendelea Kuisaidia Benki ya Watu wa
Zanzibar (PBZ Ltd)
Mradi Mpya wa Kuwasaidia Watoto Masikini Zanzibar Wazinduliwa
Nchini Canada

Wazanzibari waishio Canada chini ya
Kikundi cha ZACADIA (Zanzibar-Canadian Diaspora Association)
Wamekusudia kuendelea kufanya kazi na
Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ Ltd) katika juhudi zake za utumaji pesa kwa
gharama ndogo na wa kuaminika kwa njia ya haraka hadi Zanzibar wakiwa katika
nyumba zao nchini Canada, kwa kutumia njia tafauti ikiwa ni pamoja na kutumia
kadi zao za debit/credit na njia ya moja kwa moja kwa kutumia kompyuta. (Online
bank transfers).
ZACADIA,
ambayo lengo lake kuu ni kusaidia kuitangaza Zanzibar nchini Canada na nchi za
nje kwa jumla, pia inafanya kazi ikiwa kama ni kiungo kati ya Wazanzibari
waishio Canada na nchi yao asili ya Zanzibar.
ZACADIA ina mawasiliano ya moja kwa moja
na Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na
Kitengo cha “Zanzibar Diaspora” katika Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais wa
Zanzibar.
Mwenyekiti wa Mteule wa Kamati Maalum ya
ZACADIA aliwasilisha taarifa yake siku ya Jumamosi tarehe 14 Julai, 2012,
katika ukumbi wa Driftwood Community
Centre, Toronto, ambapo ndipo palipofanyika mkutano wa Kamati hiyo, baada
ya kurejea Canada kutoka Zanzibar ambako alikuweko kwa ziara ya kikazi kwa muda
usipungua miezi sita, akijaribu kukutana na Jumuia mbali mbali za wananchi wa
Zanzibar ambazo zina lengo sawa na Jumuia ya ZACADIA.
Wakiipokea taarifa ya Mwenyekiti Mteule,
wajumbe wa Kamati Maalum walifurahishwa na hatua hiyo na wakaonesha moyo wao wa
kutaka kuendelea kufanaya kazi na Benki ya Watu wa Zanzibar kwa ajili ya kupata
njia yenye gharama ndogo ya huduma ya kutuma pesa kutoka Canada kupitia Benki
hiyo. Kwa mujibu wa data za Benki Kuu ya
Dunia (http://remittanceprices.worldbank.org),
kuna makampuni mengi ya aina hiyo, lakini jitahada kubwa inahitajika ili
kampuni iweze kukubaliwa.
“Wakati watu wengine katika nchi kadhaa
duniani wakiwa wanazisaidia nchi zao kwa juhudi ya hali ya juu kabisa kwa
mpango wa kutuma pesa kwa kutumia njia ya Benki kwa Benki, na sisi Wazanzibari tunahitaji
kufanya kama hivyo kwa msaada wa taasisi zetu za fedha huko Zanzibar.”
Aliwahamasisha wajumbe wa Kamati Maalum walioaminiwa na kupewa jukumu la
kutafuta njia za namna ya kuisaidia Zanzibar kuendelea mbele.
“Sisi
Wazanzibari tuishio nje tuna hamu na nia
ya kuzipeleka rasilimali zetu chache tulizonazo katika visiwa vyetu kwa ajili
ya kuwaboresha wananchi wa nchi yetu, lakini hatutoweza kufanya hivyo kwa
kutumia njia zilizopo sasa hivi ambazo zinatoza gharama kubwa kupita kiasi,” mjumbe mwengine alikemea miongoni mwa wajumbe
wa Kamati Maalum.
Mwenyekiti
Mteule aliwaelezawajumbe wa Kamati Maalum kwamba wakati akiwa Zanzibar,
alionana na maofisa wa PBZ, na kwa hiyo, ZACADIA sasa inaweza kuwasaidia
Wazanzibari wanaoishi Canada kufugua hesabu zao za fedha za kigeni katika Benki
ya PBZ bila ya wao kwenda Zanzibar. Ametoa wito kwa Wazanzibari waishio Canada
kujitokeza mbele ya Kamati ya Uongozi ya ZACADIA ili waweze kusaidiwa mara moja
namna ya kuweza kufungua hesabu hizo ili waweze kuisaidia Zanzibar kiuchumi.
Pia aliahidi kuwa ZACADIA itapanua msaada wake kwa taasisi zote za kitaifa za
Zanzibar kwa ajili ya kuiokoa Zanzibar kiuchumi-jamii ambao kwa sasa umeenea
duniani.
Wakati
huo huo, mradi mpya unaotarajiwa kuzinduliwa na ZACADIA ulifikishwa katika
kikao hicho. Mradi huo ambao utajulikana kwa jina la “Zanzibar Children’s Fund Program-ZCFP” utawasaidia kuwapatia
huduma za kuondoa umasikini kwa kuwapatia elimu miongoni mwa watoto masikini na
mayatima katika vijiji vya Zanzibar, Unguja na Pemba ambao wazee wao wamo
katika hali duni ya kimaisha na wanashindwa kuwapatia mahitaji ya skuli watoto
wao.
Mradi
huo utatoa misaada ya kifedha usio wa moja kwa moja kwa watoto hao ikiwa
ni huduma za msingi kama vile viatu,
vitabu, madaftari, nguo, n.k. Mradi huu utafanikiwa kwa kuwahamasisha
Wazanzibari na wafadhili wengine duniani kwa kila mmoja kumdhamini mtoto mmoja,
ambapo kwa kila mdhamini huyo atakuwa akichangia dola 1 ya Kimarekani kwa siku.
Hata hivyo, ikiwa hiyo itakuwa ni mzigo kwa mtu mmoja kumchangia mtoto mmoja
kwa mwezi dola moja, basi wajumbe wamekubaliana kuwa hata kama watu 4
watashirikiana kumdhamini mtoto mmoja mpaka mtoto huyo atakapomaliza skuli ya
sekondari, kwa kuchangia senti 25 za Kimarekani kila mmoja kwa siku. Mradi huo
pia umekusudia kuwasaidia wazee wa watoto husika wawe wenye kujitosheleza na
kujitegemea wenyewe kwa kuwapatia mafunzo, vifaa na pesa ili waweze kuzitumia
katika uzalishaji mdogo mdogo kwa kujiondoshea umasikini na kuweza kuyamudu
maisha yao.
Katibu
ZACADIA
No comments:
Post a Comment