Habari za Punde

Huduma za wajawazito kusimamiwa – Dk. Sira


Hafsa Golo na Gilbert Massawe
WIZARA ya Afya imesema serikali itahakikisha wanatoa huduma za kina mama wajawazito na kujifunguwa zinatolewa bila ya malipo ili kuondosha vikwazo ambavyo vinaweza kujitokeza na kuwahatayarishia maisha kinamama kwa kutomudu fedha za kununulia vifaa.

Naibu wa wizara ya Afya Dk. Sira Ubwa Mwamboya alisema hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati alipokuwa akijibu suala lililoulizwa na Mwakilishi wa jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na wizara katika  kuhakikisha akinamama wanajifungua  katika hospitali za serikali  wanapata huduma hizo bure kama alivyoagizwa Rais.

Alisema kuwa serikali kupitia bajeti ya wizara ya afya ya mwaka 2012/2013 itaiongezea fedha ili kuweza kukidhi mahitaji ya huduma hizo za akina mama.


Sambamba na hayo, alisema hatua ambazo serikali imezichukuwa  ni kuwaruhusu kutiliana mkataba wa muda mrefu na wanunuzi na wasambazaji wa dawa waliopata tenda.

Alisema kuwa pamoja na mpango wa huduma za kinamama na watoto utachangia vifaa muhimu kwa ajili ya kuisaidia kutekeleza agizo hilo.

Akijibu la nyongeza lililoulizwa na Mwakilishi wa jimbo la Muyuni na Jaku Hashim ambaye alitaka kujua wizara inampango gani wakuongeza madaktari ili kuondoa kilio mama wajawazito.

Alisema kuwa suali hilo halina njia ya kuweza kufanyika kwani wanawake wenyewe hawana hamu ya kusomea fani hiyo, ndio maana madaktari wengi wa maradhi ya wanawake ni wanaume.

“Suala la maradhi ya kike la kuongeza madaktari wanawake kuchukuwa fani ya utaalamu wa maradhi ya kike (gynecologist) halina uhusiano wa moja kwa moja kwa sababu hii ni hiyari na maamuzi ya daktari mwenyewe”,alisema.

Hivyo alisema katika kutatua tatizo hilo ni vyema kujipanga upya na kuwahimiza watoto kosoma masomo ya sayansi na kuwashawishi wasomee udaktari wa wanawake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.