Habari za Punde

Manispaa yakamata wafanyabiashara 319


Na Salama Thalaba, ZJMMC
BARAZA la Manispaa limewatia nguvuni wafanya biashara ndogo ndogo 319, likiwatuhumu kufanya biashara katika maeneo yasiyoruhusuwa.

Ofisa Uhusiano wa Baraza hilo, Khamis Mbaraka Abdalla, alieleza hayo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Alisema wafanyabiashara hao wamekamatwa katika kipindi hiki cha Ramadhani wakifanya biashara katika maeneo ya Manispaa ya mji wa Zanzibar ambayo yalipigwa marufuku kufanywa biashara.


Alifahamisha kuwa baada ya kukamatwa baadhi ya wafanyabiashara hao wamepelekwa mahakamani na wamehukumiwa kwa mujibu wa sheria.


 “Wanachukuliwa hatua mbali mbali kama kutoleshwa faini kwa kufanya biashara kinyume na sheria’’, alisema Khamis.


Kuhusu eneo la Vikokotoni, Khamis alisisitiza kuwa eneo hilo sio la biashara bali ni eneo la skuli ya Vikokotoni na kwamba wafanyabishara hawatakiwi kufanya biashara katika eneo hilo.

Aidha aliwataka wafanyabiashara hao kuhamia eneo la Saateni  walilopangiwa kisheria kwa kufanya biashara zao.

“Waende Saateni wakafanye biashara zao na wateja watawafuata huko huko”, alisema Khamis.

Khamis aliendelea kusema kuwa wafanya biashara wengi hawafuati utaratibu wala kanuni zilizowekwa na Baraza la Manispaa jambo ambalo limekuwa likipelekea kutokufahamiana baina ya wafanyabiashara hao na Baraza.

Alisisitiza kuwa mwanachi yeyote anaetaka kuanzisha biashara lazima afike Baraza la Manispaa ili kupata maelezo juu ya biashara yake.

Wafanyabiashara ni lazima wabadilike wafuate taratibu zilizowekwa na Baraza La Manispaa ili wapate kufanya biashara huru na halali.
 
Katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifanya biashara maeneo ya mjini ambayo baadhi yao yamekuwa hayaruhusiwi kisheria.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.