Na Rajab Mkasaba, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amezindua uvunaji mpunga wa NERICA kwa
kutumia ‘Combine Harvester’ mpya huko katika shamba la kilimo Bambi na kueleza
kuwa hatua hiyo ina lengo la kuwakomboa na kuwarahisishia wakulima namna
ya kulima na kuvuna.
Dk. Shein alieleza kuwa serikali imechukua
hatua hiyo ikiwa ni hatua ya kuleta mapinduzi ya kilimo hali ambayo itawasaidia
wakulima katika kupunguza muda wao wa kazi na kuweza kulima na kuvuna kwa
ufanisi zaidi.
Alisema kuwa mashine hizo za kuvuna zina
uwezo wa kuvuna eka moja kwa dakika 45 zitasaidia kufanikiwa kwa mapinduzi ya
kilimo huku akitoa agizo kwa wizara ya Kilimo na Maliasili kuongeza matrekta 20
mwakani hadi kufikia 54.
Alisema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi
kikubwa kwani pia mipango ya kuziongeza ‘Combine Haverstoe’ upo hadi kufikia 45
awamu kwa awamu.
Dk. Shein alisema serikali ina mipango ya
kujikita zaidi kwenye kilimo cha mpunga cha umwagiliaji, huku zaidi ya heka
2000 zikitengwa kwa kilimo hicho Unguja na Pemba.
Alibainisha mambo makubwa matano ambayo serikali
imefanya juhudi za makusudi katika kuwasaidia wakulima ikiwa ni pamoja na
punguzo la asilimia 75 la bei ya mbegu, mbolea, dawa pamoja na kuongeza Mabibi
Shamba na Mabwana Shamba na wataalamu.
Alieleza juhudi za kuiimarisha taasisi ya utafiti
Kizimbani ambayo tayari wameshajitokeza wahisani kuiunga mkono ikiwemo serikali
ya Norway na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Tanzania.
Dk. Shein alisema kuwa bonde la Cheju
litalimwa kwa kilimo cha umwagiliaji maji na kuepuka mitihani iliyotokea
katika msimu uliopita ambapo serikali itatoa taarifa maalum kwa lengo la
kuwatazama wakulima ambao mpunga wao umeharibika.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini
Unguja ambaye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi Khamis alisema
kuwa hatua hiyo ya uzinduzi wa ‘Combine Havester’ mpya ni miongoni mwa ahadi
alizozitoa Dk. Shein kwa wakulima.
Alisema kuwa Dk. Shein amekuwa bingwa wa
kutimiza ahadi zake ikiwemo hiyo ya mashine hizo pamoja na nyengine kadhaa
ambazo hivi sasa zinaendelea na nyengine tayari zimeshatekelezwa ikiwemo miradi
mbali mbali ya maendeleo.
Naye Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Affan Othman Maalim alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa
kuwatimizia ahadi aliyoahidi Mei 23 mwaka jana kuwa atahakikisha wanavuna kwa
kutumia vifaa hivyo.
Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa katika mapinduzi
ya kilimo, serikali imedhamiria katika kuwasaidia wakulima wake kilimo cha
uhakikika ikiwa ni pamoja na pembejeo, mbolea, mbegu, dawa za kuulia magugu na
utaalamu.
Pamoja
na hayo, Katibu Mkuu huyo alitoa maelezo juu ya jitihada kubwa zilizofanywa na
mafundi wa matrekta katika kuziunga ‘Combine harvester’ hizo mpya kwa kushirikiana
na wataalamu kutoka China ambako ndiko zilikonunuliwa kazi ambayo waliifanya kwa muda wa siku mbili
tu.
Alisema kuwa wataalamu hao kutoka China
walitoa pongezi za pekee kwa mafundi hao kutokana na uweledi wao mkubwa na
kusema kuwa hawajawahi kwenda nchi hata moja na kukuta utaalamu kama waliokuta
kutoka kwa mafundi hao wazoefu na wenye ujuzi mkubwa.
Aidha Katibu Mkuu huyo aliwasilisha ombi la
mafundi hao kwa Dk. Shein.
No comments:
Post a Comment