Na Mwashamba Juma
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema
itazifutia usajili Jumuiya zote za kiraia zinazokwenda kinyume na sheria na
katiba ya nchi.
Mrajis Mkuu wa serikali Abdulla Waziri,
alisema hayo huko ofisini kwake Forodhani katika hafla fupi ya kuwakabidhi hati
ya usajili Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria Zanzibar “Paralegal.”
Mrajis huyo alisema lazima sheria ifanye
kazi, ili kuziwajibisha Jumuiya zote ambazo zinavunya shria za nchi na kwenda
kinyume na katiba zao katika ufanisi wa malengo yake.
“Hatuwezi kuwa na Jumuiya nyingi za kiraia
ambazo zinakwenda kinyume na sheria, licha yakuwa zimesajiliwa kisheria”, alisema
Mrajis huyo wa serikali.
Alisema watafanya uchambuzi dhidi ya Jumuiya
zote za kiraia ambazo haziwajibiki katika kuwasilisha ripoti zao za kila mwaka
kwenye ofisi yake na kuziwajibisha.
Alizitaka jumuiya hizo kuwajibika katika
kutekeleza majukumu yao kwa wanachama wao na walengwa wao, sambamba na kuachana
na tabia yakujiona kuwa wako juu ya sheria kwa kutowajibika kisheria.
Alisema uwajibikaji na utekelezaji wa
majukumu kwa Jumuiya hizo ni hatua moja wa kufikia malengo waliyoyakusudia,
hivyo alizitaka jumuiya hizo kuondokana na dhana ya kutegemea wafadili na
badala yake wawajibike kwa wanachama wao
ili maendeleo yao yatokane na bidii zao.
Mrajis huyo alisema kukabidhiwa kwa hati ya
usajili kwa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria imekuja kufuatia kukamilisha mashari
ya usajili, na kuwa jumuiya halali yenye katiba.
Aidha alizitaka Jumuiya za kiraia
kuwasilisha ripoti zao za kila mwaka ili kuisaidia serikali kuweza kutathmini
kwa kiasi gani jumuiya hizo zinatoa mchango kwa jamii, pamoja na kuitaka
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria kuwa mfano mzuri katika uwajibikaji wa majukumu
yake hasa katika ufanisi wa kazi zake.
Nae Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Ramadhan
Khalfan Khamis alisema lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo ni kutokana na
uhaba wa wanasheria nchini ambao hawamudu kuwafikia wananchi wote kwa kutoa
msaada wa sheria.
Aidha Ramadhan alisema kuwepo kwa wasaidizi
wa sheria kutawasaidia wananchi kuwashauri kisheria, pamoja na kuwa nao karibu
kwa kuwapa msaada wa sheria.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo aliiomba ofisi ya
mrajisi mkuu wa serikali kuwa karibu zaidi za Jumuiya za kiraia kwa lengo la kufuatilia kwa karibu zaidi
utendaji wao.
Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria Paralegal
imesajiliwa chini ya sheria ya Jumuiya za kiraia, sheria namba 6 ya mwaka 1995
sheria za Zanzibar.
Kwa sasa Jumuiya hiyo ina wanachama 65 kwa
Unguja na Pemba na wanachama wengine zaidi ya wanachama 30 wako masomoni
kukamilisha mafunzo ya wasaidizi sheria Paralegal.
No comments:
Post a Comment