Na Rose Chapewa, MOROGORO
KAMANDA wa polisi mkoani hapa Faustine Shirogile amepiga marufuku
maandamao na mikutano iliyokuwa imepangwa kufanywa na
vyama vya siasa vya Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na chama
cha Mapinduzi (CCM).
Shirogile alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari mjini hapa kufutia maombi ya vyama hivyo kuomba mikutano
hiyo kwa muda na tarehe zinazofanana.
Alisema jeshi hilo limeamua kupiga marufuku maandamano na mikutano
kutokana na sherehe za Nanenane na mgomo wa walimu hadi hapo jeshi hilo
litakapotoa taarifa nyengine.
Alisema kuwa CCM waliomba kufanya mkutano wa hadhara
kuanzia Agosti 4 hadi Agosti 8 mwaka huu katika maeneo ya Manispaa
ya Morogoro katika uwanja wa skuli ya Kiwanja cha Ndege huku
CHADEMA nao wakiwa wameomba kwa tarehe hizo hizo na maeneo sawa.
Kamanda huyo alisema kuwa kutokana na kuwepo na shughuli hizo za
kitaifa waliona jeshi hilo litazidiwa na hivyo kuamua kuzuia mikutano
na maandamao hayo ili kutoa fursa kwa polisi kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
“Askari tulionao ni wachache hatuwezi kuwagawanya katika shughuli
zote hizo kwa wakati mmoja, maandamao na mikutano lazima yalindwe, na polisi
kwa sasa wako mitaani kuangalia suala la walimu sambamba na shughuli za kitaifa
za Nane nane hivyo mikutano hiyo tunasitisha hadi hapo tutakapoona shughuli
hizo zimekwisha’’, alisema.
Hata hivyo aliwatahadharisha wananchi mkoani hapa kutojihusisha na
mikutano na maandamano na kwamba atakayejihusisha atachukuliwa hatua za
kisheria.
“Wananchi wasijihusishe na suala la mikusanyiko yeyote tumepiga
marufuku, waendelee na shughuli zao kinyume na hapo hatua za kisheria
zitachukuliwa kwa yeyote atakayejihusisha na mikusanyiko”, alisema Kamanda huyo.
Kwa upande wao CCM wamekiri kupokea barua ya katazo hilo na
kudai kuwa wamesitisha mikutano yao kufutia amri hiyo ya polisi na hadi
hapo watakapotaarifiwa kufanya hivyo.
Katibu wa CCM wilaya ya Morogoro mjini Ali Issa alisema kuwa
walipanga kufanya mikutano hiyo na kwamba baada ya katazo hilo
wamesitisha kutokana na majukumu hayo ya kitaifa.
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Morogoro ambaye ndiye anaratibu
shughuli hizo Suzan Kiwanga, alisema kuwa wao kama CHADEMA hawako tayari kutii
agizo hilo na kwamba maandamano yako pale pale.
No comments:
Post a Comment