Na Mwandishi Wetu
MSANII mkongwe nchini ambaye kwa sasa anaugua Fatma bint Baraka ‘Bi Kidude’, amesafirishwa kwenda Dar es Salaam jana kwa matibabu zaidi.
Taarifa zilizopatikana na gazeti hili, zimefahamisha kuwa, msanii huyo alichukuliwa kutoka hospitali ya Zanzibar Medical Group alikuwa akipatiwa matibabu ma mmoja wa viongozi wa redio Clouds FM ya Dar es Salaam, Ruge Mutabaha kumpeleka hospitali ya Hindu Mandal.
Hata hivyo, wakati anasafirishwa, Bi Kidude hakuwa amezidiwa, bali afya yake ilikuwa ikizidi kuimarika.
Mmoja wa waratibu wa matibabu ya msanii huyo kutoka taasisi ya Busara Promotions Journey Ramadhan, amethibitisha kuwa Bi Kidude amesafirishwa,
Lakini, alisema wao wakiwa ndio wanaosimamia malipo katika hospitali aliyokuwepo, hawakushauriwa juu ya uamuzi wa kumuondoa na kumpeleka Dar es Salaam.
“Sisi Busara hatukuwa na taarifa yoyote, tulipokwenda asubuhi kumuona hosptali na kufanya taratibu za kawaida, hatukumkuta na tukaambiwa amesafirishwa na Ruge”, alifafanua Ramadhan.
Jitihada za kumpata Ruge Mutabaha kwa siku ya jana, hazikuweza kufanikiwa kwa vile hatukuwa na njia ya kupata mawasiliano naye.
Kwa muda sasa, Bi Kidude amekuwa akiugua ugonjwa wa kisukari, kuvimba miguu na mara kadhaa tumbo, na tayari Baraza la Sanaa Zanzibar (BASAZA), limemzuia asiendelee na kazi za usanii.
No comments:
Post a Comment