Habari za Punde

Dk Shein afanya mazungumzo na wafanyabiashara na wenyeviwanda wa Vietnam

 Awataka kushirikiana na Zanzibar
 
 Na Rajab Mkasaba, Vietnam
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenyeviwanda nchini Vietnam kushirikiana na Zanzibar katika sekta husika ikiwa ni njia moja wapo ya kuinua uchumi na kuimarisha mahusiano kati ya pande mbili hizo.
Akizungumza katika mkutano maalum na wajumbe wa Jumuiya hiyo mjini Hanoi, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeimarisha Sera za uwekezaji Zanzibar ili kuwavutia zaidi wawekezaji, wafanyabiashara na wenyeviwanda kutoka maeneo mbali mbali duniani.
Dk. Shein ambaye yuko nchini humo kwa ziara maalum kufuatia mualiko wa kiongozi wa nchi hiyo alisema kuwa kuwa hatua hiyo inathibitisha utayari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukuza ushirikiao na uhusiano kati yake na Vietnam.
Aidha, alisema kuwa Zanzibar inayo fursa ya kushirikiana na Vietnam katika nyanja za kiuchumi na kibiashara pamoja na uimarishaji wa sekta ya viwanda na kutoa pongezi kwa mafanikio makubwa ya kiuchumi yaliopatikana nchini humo.
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha taratibu za kuekeza zinafanywa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi serikali imeunda Mamlaka ya Vitega Uchumi (ZIPA) ambayo inashughulikia masuala ya uwekezaji Zanzibar.
Akitoa maelezo juu ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa wafanyabiashara na wawekezaji hao Mkurugeni Mwendeshaji wa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Bwana Salum Khamis Nassor alisema kuwa Sera ya Uwekezaji ya Zanzibar imeanzishwa ili kuweka mwongozo kwa taasisi za umma na za binafsi katika la kukaribisha mitaji ya uwekezaji kwa lengo la kuongeza ukuaji wa uchumi wa nchi na kwa maslahi ya pande zote mbili.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa Mamlaka hiyo ya Vitega Uchumi imeshatoa idhini kwa miradi ipatayo 501 yenye mtaji wa Dola za Kimarekani zipatazo milioi 3.2 katika sekta mbali mbali.
Alisema kuwa miongoni mwa sekta hizo sekta ya utalii inaongoza ambayo ina miradi yenye zaidi ya asilimia 60 na kusisitiza kuwa miundombinu na huduma za kibenki zimeimarishwa. Aidha, Mkurugrnzi huyo alisema kuwa Zanzibar inayo maeneo mengi ya kuekeza hasa kwenye sekta ya utalii na sekta nyenginezo.
Akizungumzia kuhusu uwekezaji, Mkurugenzi huyo alisema kuwa zaidi ya utalii, wawekezaji wanayo nafasi ya kuekeza katika maeneo ya uvuvi na usindikaji wa samaki pamoja na mazao mengine ya baharini.
Aliendelea kueleza kuwa wawekezaji wanaendelea kukaribishwa Zanzibar katika sekta za uvuvi, miundombinu, maeneo huru ya kiuchumi yakiwemo Amani, Micheweni, Fumba, Bandari huru ya Mpigaduri, kiwancha cha ndege na sehemu nyenginezo.
Pia, alizitaja fursa katika sekta ya kilimo pamoja na vivutio kadhaa vya utalii vilivyopo Zanzibar ambavyo vinatoa fursa kwa wafanyabiashara na hata wenyevinda kuekeza Zanzibar kutokana na utajiri wa rasilimali za kitalii zikiwemo sehemu za kihistoria, utamaduni wa Kizanzibari, fukwe, misitu ya asili ya Ngezi na Jozani na ima punju.
Nao wajumbe wa Jumuiya hiyo walieleza hatua wanazozichukua katika kuendeleza mbele shughuli za jumuiya yao. Aidha, walieleza umuhimu na haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja ya kijumuiya kati ya Vietnam na Zanzibar.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na baadhi ya Mabalozi wa nchi za SADCwanaoziwakilisha nchi zao nchini Vietnam huko mjini Hanoi ambao walimueleza Dk. Shein jinsi walivyopata mafanikio katika ushirikiano na nchi hiyo ambayo imekuwa ikipiga hatua siku hadi siku.
Mabalozi hao waliipongeza ziara hiyo ya Dk. Shein nchini humo na kueleza kuwa itakuwa chachu katika kuinua hatua za maendeleo ya kiuchumi kwa Zanzibar.
Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa viongozi hao wanaoziwakilisha nchi zao nchini Vietnam na kueleza kuwa umefika wakati kwa nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara kuzidi kupanua wigo wa kimaendeleo sambamba na kuendelea kukuza uhusiano na ushirikiano miongoni mwao pamoja na nchi zote rafiki duniani.
Dk. Shein anatarajia kurejea nchini kesho baada ya kumaliza ziara yake nchini Vietnam iliyotokana na mwaliko rasmi wa kiongozi wa nchi hiyo.
Ambapo katika ziara yake hiyo Dk. Shein alifuatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein pamoja na viongozi wengine akiwemo Waziri wa Kilimo na Maliasili Mhe. Suleiman Othman Nyanga, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdillah Jihad Hassan.
Viongozi wengine ni Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Mhe. Haroun Ali Suleiman, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Mahadhi Juma Maalim, Mshauri wa Rais, Ushirikiano wa Kimataifa na Uwekezaji Balozi Ramia Abdiwawa pamoja na Maafisa wengine wa Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.