Habari za Punde

Madiwani Chadema Arusha waonywa

Joseph Ngilisho, Arusha
CHAMA cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) kimetoa onyo kali kwa baadhi ya madiwani wake jijini Arusha walioshiriki katika mchakato wa maandalizi ya uzinduzi wa jiji la Arusha kinyume na msimamo wa chama hicho.
Pia,chama hicho juzi kiliwaweka kiti moto madiwani hao na kuwahoji kuhusu tuhuma za kushiriki vikao vya Baraza la madiwani la jiji hilo sanjari na kuchukua posho mbalimbali za vikao hivo ambapo walijieleza na maelezo yao kufikishwa katika ngazi za juu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, katibu mkuu wa Chadema ,Dk Willbrod Slaa alisema kuwa iwapo itabainika baadhi ya madiwani hao walijipenyeza na kushiriki mchakato wa uzinduzi wa jiji hilo pamoja na kuchukua posho za vikao mbalimbali wataadhibiwa kwa mujibu wa taratibu za chama hicho.
Dk, Slaa alisema kuwa msimamo wa chama hicho ni kutomtambua meya wa Arusha ,Gaudence Lyimo(ccm)kwa kile alichodai taratibu za kupatikana kwake hazikufuatwa,na kusisitiza kuwa iwapo madiwani wake wanajipenyeza na kushiriki vikao vya halmashauri vinavyoongozwa na meya huyo ni utovu wa nidhamu.
‘’kitendo cha kushiriki vikao vya halimashauri ni kuhalalisha kumtambua meya wa Arusha sasa sisi msimamo wetu ni kutoshiriki vikao na hata madiwani wanalijua hilo ila kama wanashiriki kinyemela na kuchukua posho tutapambana nao’’alisema Dk Slaa.
Aidha dkt Slaa alionya kuwa kitendo cha madiwani wake kushiriki vikao vya manispaa ni mwanzo mbaya wa kuambikizwa madhambi ya ufisadi yaliyopo ndani ya manispaa hiyo ukiwemo matumizi mabaya ya fedha za wananchi.
Hata hivyo mwandishi alipotaka kujua msimamo wa Chadema utaisha lini wakati wananchi wanaendelea kusota kwa kukosa wawakilishi kwenye kata zao,alisema kuwa diwani anapaswa kushiriki maendeleo kwenye kata yake na wananchi wake na si kushiriki vikao vya halmashauri.

Aliongeza kuwa diwani anapaswa kumfuata ofisini mkurugenzi wa jiji na kumweleza matatizo yaliyopo kwenye kata yake bila kushiriki vikao vya baraza la madiwani.

Alipotafutwa mwenyekiti wa madiwani wa Chadema jijini hapa,Isaya Doita ambaye ni diwani wa kata ya Ngarenaro alikiri hatua ya wao kuhojiwa na Dk Slaa huku akisema kwamba kwa sasa hawana la kusema kwa kuwa wanasubiri maelekezo kutoka ngazi za juu za chama.
Hatahivyo,alikiri wao kushiriki mchakato wa uzinduzi wa jiji la Arusha hivi karibuni huku akidai ya kwamba suala la kushiriki na kupokea posho za vikao mbalimbali ni halali yao.
Itakumbukwa ya kwamba onyo lililotolewa na Dk Slaa limekuja siku chache baada ya madiwani wa CCM,Tlp na Chadema jijini Arusha kushiriki mchakato wa uzinduzi wa jiji hilo kitendo ambacho kimeibua gumzo jijini hapa huku ikikumbukwa ya kwamba madiwani wa Chadema waliweka msimamo wa kutomtatabua meya wa jiji la Arusha.
Baadhi ya madiwani wa Chadema walioshiriki mchakato wa uzinduzi wa jiji hilo hivi karibuni waliongozwa na diwani wa kata ya Levolosi,Efatha Nanyaro ambapo alichaguliwa kuwa katibu wa maandalizi ya chakula cha Rais huku mwenyekiti wake akiwa ni diwani wa kata ya Moshono,Paul Matyhsen(CCM).
Vilevile itakumbukwa ya kwamba Chadema kiliwahi kuwatimua madiwani wake watano mwaka jana ambao ni John Bayo,Ruben Ngowi,Estomi Malah na Rehema Mohamed kwa kosa kuingia mwafaka wa kumtabua meya wa jiji la Arusha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.