Uharamia
na biashara ya usafirishaji wa binadamu ni changamoto inayotafutiwa ufumbuzi na
vyombo vya Usalama vya Umoja wa Maendeleo wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Arusha leo Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na Usalama
cha SADC, Kanali Gerson Sangiza alisema dunia kwa ujumla bado
inaangalia namna ya kutatua tatizo hilo.
Alisema
ufumbuzi wa suala hilo ni mgumu kutokana na ukweli kwamba maharamia
na wale wanaojihusisha na biashara ya uuzaji wa binadamu hushirikiana kwa
karibu na kwa siri na wananchi wa nchi husika. "Tatizo ni kwamba
wananchi ndiyo wanaoendesha vitendo hivyo kwa hiyo namna ya kuwakamata inakuwa
ni shida" Alisema Kanali Sangiza.
Mkuu
huyo aliongeza kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo ushirikiano wa karibu kati
ya wananchi na taasisi zinazoshughulikia masuala hayo unahitajika. Mpaka sasa
nia na madhumuni ya biashara hiyo ya uuzaji wa binadamu bado
haijajulikana na
wale waliokamatwa wakijihusisha na bado wanashikiliwa.
"Inasikitisha
kuona binadamu wengi wanasafirishwa kutoka Somalia kupitia Kenya, Tanzania,
Malawi na kupelekwa Afrika ya Kusini ambapo mpaka sasa Afrika kusini ina
wahamiaji haramu milioni tano", alisema kanali Sangiza.
Mkuu
huyo wa kitengo cha Ulinzi na Usalama cha SADC alisema pamoja na tatizo la
uharamia na usafirishaji wa binadamu, nchi wanachama wa Jumuiya hiyo pia
zinakabiliwa na changamoto ya matishio ya kufanyika kwa vitendo vya kigaidi
ambavyo vinahatarisha uhusiano kati ya nchi zilizoendelea na zile
zinazoendelea.
SADC
kupitia chombo chake cha Ulinzi na Usalama imeandaa mikakati maalumu
kuhakikisha kwamba nchi wanachama wa jumuiya hiyo hazisumbuliwi na matatizo ya
uharamia na usafirishaji wa binadamu. Katika hatua ya kukabiliana na changamoto
hizo, wakuu wa Polisi wa nchi zote 15 za SADC walikutana mwezi Septemba
Zanzibar ili kujadili mambo mbalimbali ya ulinzi na usalama likiwemo tatizo la
uharamia na biashara ya usafirishaji wa binadamu.
No comments:
Post a Comment