Na Khamis Amani
VYOMBO vya dola
nchini, vimetakiwa kutekeleza ipasavyo wajibu na majukumu yao kwa kusimamia haki kwa mujibu wa
sheria.
Vyombo hivyo
vimefahamishwa kuwa, kila mtu ana wajibu wa kupata haki zake za msingi
anazostahiki kwa mujibu wa sheria, bila ya ubaguzi wala upendeleo wa aina
yoyote.
Agizo hilo
limetolewa na hakimu Ame Msaraka Pinja wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe,
kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na washitakiwa saba wa kesi ya uchochezi
na kufanya fujo na vitendo vya ukiukwaji wa sheria wanavyofanyiwa wakiwa
kizuizini mahabusu ya Chuo cha Mafunzo Kilimani mjini Unguja.
Kauli hiyo ya
hakimu Pinja, ni msisitizo wa agizo lake alilolitoa mahakamani hapo katika
kikao kilichopita cha Novemba 7 mwaka huu, la kutaka washitakiwa hao kutendewa
haki kisheria kama wanavyotendewa mahabusu wengine.
Mambo mengine wanayodaiwa
kufanyiwa ni kuwekwa kila mshitakiwa ndani ya chumba chake bila ya kutoka nje
isipokua nyakati za asubuhi kwenda haja na mchana wakati wa kula, pamoja na
kutopewa haki ya kuabudu kwa kuchanganyika kusali sala ya jamaa na Ijumaa
pamoja na mahabusu wengine.
Madai ya
washitakiwa hao wakiwemo viongozi wakuu watatu wa Jumuiya ya Uamsho na
Mihadhara ya Kiisilamu (JUMIKI) pamoja na wafuasi wao wanne,yaliwasilishwa
mahakamani Na Mawakili Salum Taufik na Abdallah Juma.
Katika kikao cha
jana, Wakili Abdallah Juma aliiomba mahakama Isisitize agizo lake la wiki iliyopita kuhusu ukiukwaji wa sheria.
"Mheshiwa kwanza nawapongeza maafisa wa
Vyuo vya Mafunzo kwa kutekeleza agizo lako kwa baadhi ya mambo kama kubadilisha
nguo, na kunyolewa ndevu, kwa masuala hayo hivi sasa wateja wetu hawafanyiwi
kama unavyoona, wamebadilisha nguo na hawakunyolewa tena ndevu", alisedai
Wakili huyo wa utetezi.
Sambamba na hoja
hizo, Wakili huyo wa utetezi aliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia masharti ya
dhamana wateja wao hao, kwani masharti yaliopo hivi sasa ni mazito na hayawezi
kutekelezeka.
Alidai kuwa,
suala la kumpata mfanyakazi wa serikali kwa wateja wao ni ngumu kutokana na
mazingira ya kesi hiyo, na suala la fedha taslimu shilingi 1,000,000 ni kikwazo
kutokana na wengi wa Wazanzibari wanaishi katika kiwango cha umasikini
halikadhalika na wateja wao.
Ukijibu hoja hizo upande wa mashitaka
ulioongozwa na Mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP) Ramadhan Abdallah, pamoja na kudai kutoamini kwake kama washitakiwa hao
wamekosa wadhamini wenye sifa kwa mujibu wa kauli ya Wakili wao, lakini kwa
upande wake hakukuwa na hoja juu ya ya suala hilo.
Kuhusu
kutotendewa haki kwa washitakiwa hao, pande huo wa mashitaka ulidai kuwa suala
hilo lipo juu ya mahakama kwani tayari imeshatoa maelekezo kwa mamlaka
zinazohusika zitekeleze matakwa yao kwa mujibu wa sheria.
Hivyo alishauri
kama wanaona matakwa hayo hayatekelezwi, wanapaswa watumie uzoefu na usomi wao
kwa kufuata taratibu nyengine za kisheria kwa kwenda Mahakama Kuu kwa lengo la
kutafuta haki za wateja wao.
Akitetea hoja
hizo, Wakili Abdallah Juma alisema kuwa, sehemu pekee ya kutoa malalamiko hayo
ni mahakamani, kwani mahakama inapaswa itambue kuwa wateja wao wamepelekwa
rumande kwa amri yake, na mahakama haikusema wafanyiwe vitendo hivyo vya
ukiukwaji wa sheria wanavyofanyiwa.
"Mheshimiwa
suala la chakula na matibabu ni haki yao ya msingi, hivi leo wakiumwa kama
hawapatiwi matibabu tupeleke malalamiko Mahakama Kuu", alihoji Wakili huyo
wa utetezi.
Baada ya hoja
hizo na kuzitolea maamuzi hayo, hakimu Pinja pia aliridhika na hoja za pande
mbili hizo juu ya suala la dhamana kwa washitakiwa hao, na kuwataka kuwasilisha
fedha taslimu shilingi 500,000 kila mshitakiwa badala ya 1,000,000 za awali,
pamoja na kiwango kama hicho cha fedha taslimu kwa wadhamini wawili badala ya
wote watatu.
Sambamba na
sharti hilo, wadhamini wawili wawe ni wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ), badala ya watatu waliowekwa awali na masharti mengine yataakia kama
yalivyo.
Washitakiwa
katika kesi hiyo ni Mselem Ali Mselem (52) mkaazi wa Kwamtipura, Farid Had
Ahmed (41) wa Mbuyuni ambaye ni msemaji mkuu wa Jumuiya hiyo, pamoja na Azan
Khalid Hamdani (43) anayeishi Mfenesini.
Wengine ni Mussa
Juma Issa (37) mkaazi wa Makadara, Suleiman Juma Suleiman wa Makadara, Khamis
Ali Suleiman (59) anayeishi Mwanakwerekwe na Hassan Bakari Suleiman (39) mkaazi
wa Tomondo.
Wote hao
wanakabiliwa na mashitaka ya uchochezi wa kufanya fujo, tukio ambalo lilidaiwa
kutokea saa 11:00 za jioni ya Agosti 17 mwaka huu.
Kinyume na
kifungu cha 45 (1) (a) (b) cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za
Zanzibar, walidaiwa kutoa matamko ya uchochezi yanayoashiria uvunjifu wa amani
na kusababisha fujo, maafa mbali mbali na mtafaruku kwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar.
Tukio hilo
lilidaiwa kutokea maeneo ya Magogoni Msumbiji wilaya ya Magharibi Unguja,
wakati washitakiwa hao wakiwa ni wahadhiri toka Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara
ya Kiisilamu.
Upelelezi wa
kesi hiyo ya jinai namba 380/2012 bado haujakamilika, na imeahirishwa hadi
Disemba 4 mwaka huu kwa kujwa na washitakiwa wote hao wamerejeshwa rumande
wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Polisi wa Kikosi maalumu cha kutuliza
ghasia (FFU).
Hali ya amani
ilitawala kwa muda wote wakati washitakiwa hao wakiwa mahakamani hapo, kutokana
na eneo zima linalolizunguka mahakama hiyo kudhibitiwa na askari Polisi wenye
silaha mikononi wakisaidiwa na askari wa Vikosi.
Waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali hasa
wapiga picha, jana walijikuta katika wakati mgumu katika utendaji wa kazi zao
baada ya kutakiwa kukaa mbali na eneo la mahakama kufanya shughuli zao.
Ndugu na jamaa
wa washitakiwa hao, nao pia kwa upande wao walitakiwa kukaa mbali na mahakama hiyo
wakiwa wamezuiwa barabara kuu itokayo Amani kuelekea Kiembesamaki.
No comments:
Post a Comment