Habari za Punde

Serikali yaahidi kukamilisha kiwanda cha kusarifu mazao Kizimbani

Na Hafsa Golo
 WIZARA ya Biashara, Viwanda na Masoko imesema itaingilia kati kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuendeleza ujenzi wa kituo cha Mafunzo cha kusarifu mazao kilichopo Kizimbani.
 Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazurui, baada ya kutembelea kituo hicho na kubaini kusita kwa ujenzi huo,ambapo Mkandarasi wake ameshindwa kukamilisha kazi na kuamua kuondoka huku Mfadhili wa mradi huo kukatisha mkataba wa mradi huo.
Kutokana na hali iliyojitokeza, kuna uwezekano mkubwa zana na vifaa vilivyowekwa kwa mradi huo kuharibika kutokana na muda pamoja na kukosa utunzaji wa kitaalamu.

Waziri huyo alisema wizara yake haina sababu ya kutoingilia suala hilo kwani kumalizika kwa kituo hicho kutawapa fursa wakulima na wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye kiwango na kuweza kusarifu matunda kwa njia tofauti kutokana na wingi wa mazao yaliyopo eneo hilo na Zanzibar kwa jumla ili kuepuka wakulima kupoteza nguvu, bila mafanikio.
Waziri Mazrui alisema kuwepo kwa Kituo cha Usarifu wa Mazao Zanzibar ni muhimi kwani kitawezesha kusaidia vijana kupata ajira huku wakulima na wajasiriamali wakijiandaa kupata mafunzo na wakulima kupata soko kwa mazao yao.
Aidha alisema lengo la kiwanda hicho pamoja na kusarifu matunza lakini pia kingetumika kutoa mafunzo kwa wajasiriamali, mbali mbali na pia kingetumika kulisarifu zao la muhogo na matunda mengine ili kuvutia watalii wanaolitembele eneo hilo kila siku.

Hata hivyo, alisema pamoja na changamoto iliyojitokeza lakini jambo la msingi ni kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa tena kwa wakati unaofaa.
 
"Hili ni jambo zuri kwani wajasiriamali na wakulima watapata ujuzi na wataweza kupewa mafunzo watu wengi kwani taasisi hii ingetoa msukumo wa ajira pia itashajiisha wakulima kuwa na ari ya kuzalisha mazao bora," alisema.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya Mratibu wa usarifu wa mazao Kizimbani, Saleh Muhammed  Juma, alisema sababu kuu ya kusita mradi huo, ni Mkandarasi wa mradi huo kubeba majukumu mengine ya ujenzi, huko Morogoro, hali inayodaiwa kusababisha ujenzi huo kusuasua kwa muda mrefu hadi kufikia kukatishwa mkataba.
 
Alisema Mradi huo kwa jumla uliofadhiliwa na KOICA uligharimu dola milioni 2.3 za Marekani, ambapo ujenzi wa kituo ulitengewa dola 450,000.
 
Aidha alisema kuwa mradi huo pia umewasilisha vifaa mbali mbali vikiwemo mashine za kusagia matunda, vifaa vya maabara na mashine za kusagia uwanga.
 
Pia alimuomba Waziri huyo kuhakikisha jitihada zinachukuliwa kukamilisha mradi huo ili kuihamasisha jamii kukitumia kituo hicho kujifunza utengenezaji bidhaa mbali mbali za matunda na viungo.
 
Naye Mkururugezi uendeshaji na utumishi, Wizara ya Kilimo, Asha Ali Juma, alisema kuwa ni vyema serikali kwa kushirikiana na wizara hizo mbili kutafuta mbinu mbadala ili kituo hicho kimalizike kwa wakati ili vifaa vilivyopo viweze kutumika kabla havijamaliza muda.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.