Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Ndugu Khatib Mwinchandeakimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ripoti ya Utumishi wa miaka Mitano wa tume hiyo inayomaliza muda wake tarehe 1/1/2013.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wajumbe na Makamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar wanao maliza muda wake tarehe 1/1/2013 wakiongozwa na mwenyekiti wao Nd. Khatib Mwinchande
Na Othman Khamis Ame OMPR
Joto la Uchaguzi miongoni mwa Viongozi wa vyama vya siasa sambamba na wanachama pamoja na wapenzi wa vyama vya siasa litapungua au kuondoka kabisa endapo Tume ya Uchaguzi itaendelea kuwa karibu na washirika wake.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar { ZEC } Ndugu Khatibu Mwinchande alisema hayo wakati yeye na wajumbe wa Tume hiyo walipokuwa wakimuaga rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakikaribia kumaliza muda wao wa utumishi wa miaka mitano unaomalizika Januari Mosi 2013.
Ndugu Khatib Mwinchande ambae katika mazungumzo hayo akimkabidhi Balozi Seif Ripoti kamili ya Utumishi wao wa Miaka Mitano alisema ukaribu wa Tume ya Uchaguzi kwa washirika wake ndio njia pekee ya kuondosha malalamiko au dhana potovu ya wadau hao dhidi ya Tume hiyo.
“ Ni mara ya kwanza katika Historia ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutoa fursa kwa Vyama vya Siasa kupatiwa fursa ya kulikaguwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hii ni ishara kwa Tume hii kuwa karibu na wadau wake ili kupunguza joto la Uchaguzi”. Alifafanua Ndugu Khatib Mwinchande.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Nd. Mwinchande alifahamisha kwamba daftari la wapiga kura litaendelea kuwa la kudumu katika dhana ya kuimarisha Demokrasia licha ya changamoto zilizopo za ukosefu wa fedha kwa ajili ya kuendeleza zoezi hilo.
Alisema harakati za kimaisha zinazoendelea kukuwa kila siku zinachangia kulifanya daftari hilo kuwa la kudumu kutokana na ongezeko la idadi ya watu sambamba na baadhi ya wananchi kuhama sehemu moja kwenda nyengine.
Akizungumzia uhusiano wa Kitaifa na Kimataifa Ndugu Mwinchande alisema Tume ya Uchaguzi Zanzibar imefanikiwa kuoneza ushirikiano wa karibu kati yake na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania { NEC } sambamba na Tume za Kimataifa za Nchi za Sadc na zile za Umoja wa Afrika { AU }.
Alisema hatua hiyo imeijengea uwezo zaidi Tume ya Uchaguzi Zanzibar na kufikia kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Nchi za Kusini na Mashariki mwa Bara la Afrika { Sadc }.
“ Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } imefikia daraja ya kuwa sehemu ya Tume ya Uchaguzi ya Umoja wa Afrika { AU }”. Alifafanua Mwenyekiti huto wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Nd. Mwinchande.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuijengea uwezo Tume hiyo uliosaidia kufanikisha majukumu waliyopangiwa baada ya kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa watendaji wa wizara tofauti za Serikalini.
Akitoa pongezi zake kwa kazi kubwa iliyotekelezwa na Wajumbe wa Tume hiyo ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar imefanya kura ya maoni iliyopelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kuingia katika historia mpya ya amani na utulivu.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Uongozi makini wa Tume hiyo kwa kiasi kikubwa umesaidia kusimamia kupunguza joto la kisiasa ndani ya visiwa vya Zanzibar lililodumu kwa kipindi kirefu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wajumbe wa Tume hiyo inayomaliza muda wake kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuona Tume mpya itakayochaguliwa itapatiwa vitendea kazi pamoja na fedha kwa lengo la kufanikisha kazi za zake.
“ Tutahakikisha changamoto zilizojichomoza ndani ya kipindi cha utumishi wenu wa miaka mitano, Serikali inazipatia ufumbuzi wa kudumu”. Alisisitiza Balozi Seif.
Mwinchande na wenzake ALLAH atawalipa wanayostahili kama waliitendea haki jamii ya wazanzibari au waliidhulumu watapata malipo yao.
ReplyDelete