Habari za Punde

Maalim Seif azindua tume ya kitaifa ya kuratibu na kudhibiti madawa ya kulevya

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika uzinduzi wa  Tume ya Kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya katika hafla iliyofanyika jumba la wananchi forodhani

Baadhi ya wajumbe wa tume ya Kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya wakimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad wakati akizindua tume hiyo katika hafla iliyofanyika jumba la wananchi forodhani. (Picha na Salmin Said, OMKR)

Na Hassan Hamad OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema juhudi za serikali za kuleta maendeleo hazitakuwa na tija iwapo  vijana  wataendelea kuwa wahanga wa matumizi ya dawa za kulevya.
 
Amesema hatma ya Taifa  itategemea zaidi vijana wenye mwelekeo makini na waliojiepusha na matumizi ya mihadharati kwa vile wao ndio nguvu kazi kubwa ya taifa.
 
Maalim Seif ametoa changamoto hiyo leo wakati akizindua Tume ya Kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya katika hafla iliyofanyika jumba la wananchi forodhani.


Amesema programu mbali mbali zimeandaliwa kwa ajili ya kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya chini ya ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa huduma za nyumba za kurekebisha tabia “sober houses” kwa ajili ya vijana walioamua kuachana na matumizi ya dawa hizo.
 
Amefahamisha kuwa tangu kuanzishwa kwa mpango huo miaka mitatu iliyopita, zaidi ya vijana 2000 wamepayiwa huduma hiyo ambapo zaidi ya vijana 400 wameweza kuacha kabisa matumizi na kuendelea na harakati zao za kimaendeleo.
 
Hata hivyo amesema mafanikio hayo hayatokuwa endelevu iwapo harakati za usafirishaji, uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya hazitoendelea kupigwa vita.
 
Tume hiyo imeanzishwa kufuatia mabadiliko ya sheria namba 12 ya mwaka 2011, juu ya udhibiti wa dawa za kulevya, ambayo kwa sasa inatoa mamlaka kamili ya kisheria katika mambano dhidi ya dawa za kulevya  nchini.
 
Makamu wa Kwanza wa Rais ametanabahisha kuwa kazi ya kukabiliana na dawa za ngumu na yenye changamoto nyingi, na kwamba inahitaji ustahamilivu na mikakati imara katika utekelezaji wake.
Amewata wajumbe wa tume hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliyomo kwenye kauli mbiu ya “Zanzibar bila ya dawa za kulevya inawezekana”.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.