Habari za Punde

Magunia 16 ya karafuu kavu yanaswa

Na Masanja Mabula, Pemba
ASKARI wa kikosi cha KMKM Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamelazimika kutumia risasi za moto kuzuia gari lililokuwa na karafuu kavu, ambazo zilikuwa zisafirishwe kwa magendo nje ya nchi.

Gari hilo lilikuwa limebeba magunia 16 ya karafuu kavu na magunia matatu ya makonyo.
Karafuu hizo zilikamatwa katika kijiji cha Msuka, wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi alisema karafuu itakayokamatwa ikiwa katika harakati za kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa magendo itauzwa na fedha kubakia kwenye shirika la ZSTC.

Alisema serikali ya mkoa itaendelea kusimamia suala la karafuu ili kuhakikisha hakuna mwanya unaotumika kuhujumu uchumi wa nchi.

Ameliagiza shirika la Biashara la Taifa kuhakikisha karafuu hizo zinauzwa na fedha zitakazopatikana zinabakia katika shirika.

"Serikali haiwezi kuchezewa kiasi chote hicho, karafuu ndio uchumi wa nchi na bado wapo baadhi ya wananchi wanaendelea kuhujumu uchumi wa nchi, suala hili hatuwezi kulifumbia macho," alitanabahisha.

Aidha alisema serikali katika mkoa huo itaweka sheria zake ndogo ndogo , ambazo zitakuwa zikitumika kuwabana wanaotaka kufanya udanganyifu kwa kufanya magendo ya karafuu.

Amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuzidisha ushirikianao katika suala la ulinzi hasa mazao ya biashara ikiwemo karafuu kwa kuweka vituo ambavyo vitatumika kuyafanyia upekuzi magari yote yanayopita hasa nyakati za usiku.

"Baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mwanya wa kuwa wao ni CCM kufanya udanganyifu wa kuhujumu uchumi wa nchi, serikali haitajali kuwa huyu alikuwa ni mgombea, hili hatuwezi kulivumilia kwa kisingizio cha siasa , mtu yeyoye tutamkamata," alifahamisha.

Mapema akizungumza mbele ya kamati hiyo mtuhumiwa wa magendo ya karafuu hizo, Salum Nafoo alisema karafuu hizo zilikuwa ni mali ya mdogo wake na zilikuwa kwenye harakati za kuingizwa ndani na sio kusafirishwa nje.

"Karafuu hizo si mali yangu lakini ni mali ya mdogo wangu na zilikuwa zinataka kuingizwa ndani sio kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa magendo kama ilivyodhaniwa, kwani hatuwezi kuendesha biashara ya magendo," alisema.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Juma Abdalla Ali alisema kwa mujibu wa sheria ya karafuu ni marufuku kusafirishwa muda wa kuanzia saa kumi na mbili za jioni, lakini karafuu hizo zilikamatwa majira ya saa sita za usiku.

"Kama zilikuwa zinaingizwa ndani ilikuwaje zisafirishwe muda wa usiku , tunajua kuwa mwisho wa kusafirisha karafuu ni saa kumi na mbili za jioni,, iweje sasa asafirishe muda wa usiku," alihoji Mkuu huyo wa wilaya.

Kukamatwa kwa karafuu hizo kunafuatia msaada kutoa kwa raia wema ambao walitoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi baada ya kubaini kuwa karafuu zinataka kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.