Habari za Punde

Misri yaja kushiriki ‘Mapinduzi Cup’

Na Salum Vuai, Maelezo
 
TIMU ya Taifa ya Misri ‘Pharaohs’, ni miongoni mwa timu nane zilizoalikwa kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2013.
 
Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kupitia mjumbe wake wa Kamati Tendaji Masoud Attai, kimesema tayari timu hiyo imethibitisha kushiriki mashindano hayo yanayofanyika kuadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 
Kikosi cha timu hiyo kutoka nchi yenye mafanikio makubwa kisoka katika bara la Afrika, kinaundwa na wachezaji mahiri kutoka klabu maarufu za nchi hiyo, ikiwemo Zamalek na Al Ahly. Mbali na Pharaohs, timu nyengine iliyoalikwa kutoka nje ya Tanzania na kuthibitisha, ni Tusker ya Kenya.


Attai alizitaja timu nyengine zilizoalikwa kuwa ni Simba na Yanga pamoja na mabingwa watetezi wa ubingwa huo Azam FC zote za Dar es Salaam.
 
Nyengine ni Mtibwa Sugar kutoka Morogoro, na Jamhuri na Mafunzo za Zanzibar.
Hata hivyo, Attai amesema kutokana na kuwepo taarifa za klabu za Yanga na Simba kuwa zinakusudia kupiga kambi nje ya nchi kwa ajili ya kujiandaa na michuano mbalimbali ikiwemo mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara, huenda kukawa na mabadiliko hapo baadae.
 
Kutokana na hali hiyo, Attai amesema kamati ya michuano hiyo imeialika Coastal Union kama mbadala iwapo klabu yoyote kati ya hizo, itajiondoa kwenye mashindano hayo.
 
Timu ya Taifa Misri, Tusker, Mtibwa na Coastal Union ya Tanga, tayari zimethibitisha kushiriki mashindano hayo, yaliyopangwa kuanza kutimua vumbi Januari 1, mwakani katika viwanja vya Amaan Unguja na Gombani kisiwani Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.