Habari za Punde

Azam njia panda KINSHASA, DRC

Azam njia panda KINSHASA, DRC
 
KLABU ya Azam FC ya Dar es Salaam, jana iliangukia pua kwa kufungwa mabao 2-0 na Shark FC ya hapa, katika mchezo wake wa mwisho wa kundi B, kwenye michuano Kombe la Hisani.
 
Mabao ya washindi, timu inayomilikiwa na mdogo wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila yalifungwa na Ndibu Kalala dakika ya 23 na Kalala Kabongo mnamo dakika ya 34.
 
Hata hivyo, kipigo hicho kilichangiwa kwa kiasi kikubwa na uchezeshaji mbovu wa marefa, ambao tangu mwanzo walionekana kuwapendelea wenyeji.


Azam ilifungwa magoli yote mawili wakitoka kushambulia, makosa ambayo walirekebisha na hawakuyarudia kipindi cha pili. Kipindi cha kwanza, timu zilishambuliana kwa zamu, lakini kipindi cha pili Azam walitawala zaidi mchezo ingawa hawakuweza kuziona nyavu za wapinzani wao.
 
Kwa matokeo hayo, Shark inaongoza Kundi B kwa pointi tatu, ikifuatiwa na Dragons iliyotoka 1-1 na Azam katika mchezo wa kwanza, na sasa Azam itaomba Shark iifunge zaidi ya mabao 2-0 Dragons katika mechi ya mwisho ya kundi hilo Disemba 23, ili ifuzu nusu fainali.
 
Azam imecheza mechi zote mbili bila makocha wake Waingereza Stewart Hall na msaidizi wake, Kali Ongala ambao walibaki Nairobi, Kenya pamoja na daktari Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche raia wa Ivory Coast, kutokana na kukosa viza za kuingia DRC.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.