Habari za Punde

Oman wachagua Mabaraza ya Manispaa. Ni uchaguzi wa kwanza katika historia .Kuna wagombea wanawake 49

Na Juma Khamis, Bakar Mussa, Oman
WANANCHI wa Oman leo (Disemba 22) wanashiriki katika uchaguzi wa mabaraza ya manispaa ambao ni wa kwanza kufanyika katika historia ya taifa hili la kiarabu.

Uchaguzi huo utafanyika katika manispaa zote 11 na utaendeshwa kwa kutumia mfumo wa kisasa wa elektroniki.

Tayari maandalizi yote ya uchaguzi yameshakamilika, ikiwemo kituo cha kukusanyia matokeo kwa ajili ya waandishi wa habari, ambacho kina huduma zote zitakazowasaidia kufanya kazi zao kwa urahisi na ufanisi.

Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzisha saa moja za asubuhi (saa 12: 00 asubuhi za nyumbani) na kufungwa saa moja usiku (saa 12 jioni) kwa saa za nyumbani.

Karibu raia 546,000 wanaostahiki kupiga kura watashiriki katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, vyama vingi vimepigwa marufuku nchini humo.

Oman ilikuwa na baraza moja tu la Manispaa katika mji mkuu wa nchi hii Muscat na wajumbe wake walikuwa wanateuliwa.

Aidha baraza jipya la manispaa pia litakuwa na baadhi ya wajumbe wa kuteuliwa.

Hata hivyo, baraza hilo jipya halitakuwa na mamlaka ya kiutendaji kwa mujibu wa kanuni iliyotolewa na Sultan Qaboos mwaka uliopita, ambapo alisema baraza jipya “litawasilisha mapendekezo kuhusiana na kuimarisha huduma katika manispaa za taifa hili,” lakini halitakuwa na mamlaka ya kuyatekeleza mapendekezo hayo.

Kwa mujibu wa mtandao wa Middle East Online, raia yeyote aliefikisha umri wa miaka 30 ana haki ya kugombea katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, wajumbe wa Majlis Ash’shura (Bunge), wafanyakazi wa serikali na maafisa wa usalama hawaruhusiwi kugombea.

Kuna wagombea wapatao 1,636 wanaoshindana katika uchaguzi huo wakiwemo wanawake 49 tu.

Wagombea wanaruhusiwa kupiga kampeni kuanzia siku ambayo wameteuliwa hadi siku moja kabla ya uchaguzi, lakini kampeni za aina yoyote haziruhusiwi katika siku ya uchaguzi.

Mwandishi wa habari wa Oman, Aziza Al Habsi alisema serikali inajaribu kutumia uchaguzi huo kuongeza ushiriki wa raia wake katika masuala ya uendeshaji wa serikali yao.

“Uchaguzi wa Manispaa ni hatua nyengine ya kuanzisha demokrasia nchini,” alisema.

Waandishi wa habari kutoka kila pembe ya nchi rafiki wamealikwa kushuhudia jinsi uchaguzi huo unavyoendeshwa.




No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.