Habari za Punde

13 wanusurika kufa Pemba


Na Masanja Mabula,Pemba
WATU 13 wamenusurika kufa kufuatia ajali ya gari ya kampuni ya HYOUNG inayojenga barabara tano katika mkoa wa kaskazini Pemba kuacha njia na kupinduka katika eneo la Tumgamaa wilaya ya Wete.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba , Kamishna Msaidizi Mwandamizi Yahya Rashid Bugi alisema tukio hilo limetokea jana majira ta saa 12:45 asubuhi wakati gari hilo lilipokuwa limechukua wafanyakazi wa ujenzi wa barabara kuwapeleka Mtambwe kuendelea na kazi za ujenzi.

Alisema ajali hiyo imelihuisha gari lenye namba za usajili Z518 BK ambalo lilikuwa linaendeshwa na Hassan Mohammed mkaazi wa Pandani ambaye ni miongoni wa majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Wete.

Kamanda Bugi amesema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya gari hilo kugoma breki  wakati dereva akiwa anataka kubadilisha gia alipokuwa akipandisha mlima na hivyo gari kuacha njia na kuangukia bondeni.


"Licha ya kwamba uchunguzi wa ajali hiyo bado unaendelea, lakini taarifa ambazo tunazo ni kuwa gari hilo liliacha njia na kuanguka baada ya gia kugoma, na dereva kushindwa kulidhibiti na kusababisha kuangukia bondeni," alifahamisha Bugi.

Naye Mkuu wa wauguzi  katika hospitali ya Wete, Dk. Seif Said amesema wamepokea majeruhi 11 wa ajali hiyo na kwamba baadhi yao hali zao ni mbaya.

Aliwataja majeruhi waliofikishwa katika hospitali hiyo kuwa ni Salma Abdullah Ali aliyepata maumivu katika sehemu za kiuno , mgongo na sehemu za shingoni na  Fatma Juma Said , ambaye ameumia kwa kuvunjika mkono na mguu pamoja na sehemu za usoni.

Wengine ni Fadhila Rashid Mbarouk , Abdillah Hamad Baucha , Said Ubwa Daudi , Joseph Owino, Madila  S Soud , Abdalla Mohemmed Said , Andros Wakenya pamoja na mtoto mwenye umri wa miaka 6 Abdi Juma Machano aliyeumia kwa kuvunjika mkono.

Kufuatia ajali hiyo,Kamanda Bugi amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuweza kuzuia kutokea ajali zisizokuwa za lazima.

Hii ni ajali ya pili kutokea katika Mkoa wa Kaskazini Pemba katika kipindi hichi cha mwezi Januari ambapo wiki iliyopita ajali iliyotokea katika wilaya ya Micheweni ilisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kujeruhiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.