Habari za Punde

Asilimia 50 ya wajawazito wajifungulia nyumbani


Joseph Ngilisho,Arusha
TANZANIA bado inakabiliwa na idadi kubwa ya akina mama wajawazito, wanaojifungulia majumbani, ambapo hadi kufikia mwaka 2012 asilimia hamsini ya wajawazito nchini hujifungulia majumbani, licha ya jitihada za serikali zinazofanywa.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii, Dk. Hussein Mwinyi, wakati akimkaribisha Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal,
kwenye mkutano wa unaozungumzia uboreshaji na maendeleo ya mama na mtoto, unaofanyika jijini Arusha na kuwashirikisha wajumbe zaidi ya 800
kutoka nchi 68 duniani.

Alisema serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na vifo vya akinamama na watoto, ikiwa pamoja na utoaji wa huduma ya kujifungua na vifaa vyake bure, lakini bado akina mama wanakwepa
kwenda hospitali na vituo vya afya kujifungua.

Dk. Mwinyi alisema zipo sababu nyingi zinazosababisha vifo hivyo, lakini pia kubwa linachangiwa na mimba za utotoni chini ya miaka 18 ambapo sasa serikali inajikita kuelimisha wanafunzi na wazazi madhara ya kubeba mimba katika umri mdogo.


“Lakini pia tunataka ifikapo mwaka 2015 angalau kila kijiji kiwe na kituo cha afya na kila Kata iwe na zahanati, ili kusogeza huduma ya kujifungulia karibu na jamii,” alisema.

Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa mpango wa kila familia, katika kuhakikisha afya ya mama na mtoto inalindwa.

Alisema ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za sekta ya afya,serikali imetoa fedha nyingi katika kuhakikisha vijana 7,000,wanasoma katika vyuo vya afya, kila mwaka na wanapohitimu serikali
inahakikisha inawaajiri katika hospitali na zahanati za serikali ili kupunguza tatizo hilo.

Naye Makamu wa Rais Tanzania, Dk.  Mohammed Gharib Bilal, akifungua mkutano huo alisema licha ya Tanzania kukimbizana katika kutimiza malengo ya
milenia, lakini bado tatizo la vifo vya watoto ni kubwa, ambapo kila penye watoto 20, mtoto mmoja hufa hali ambayo inapaswa kutiliwa mkazo kuondoa hilo.

“Hii takwimu siyo nzuri na inatisha kuona watoto hawa wanapoteza maisha, wakati upo uwezekano wa kulimaliza hili na kuokoa maisha ya watoto wetu,” alisema.

Alisema kwa Tanzania tatizo la vifo vya akinamama ni kubwa, lakini limepunguzwa kutoka 770 mwaka 1990 hadi 454 mwaka 2010 kati ya akinamama 100,000 wanaofika hospitalini kujifungua.

Alisema vifo vya kinamama na watoto, vinazidi kuongezeka haswa katika nchi zilizoendelea, lakini kwa upande wa Tanzania inahakikisha hakuna
mtoto wala mama atakayekufa, kutokana na matatizo ya uzazi ifikapo 2015.

Pia alitoa rai kwa watalaamu wa afya duniani, kuendelea kufanya tafiti za vyanzo vya vifo hivyo na kuzitoa, huku wakihakikisha zinafanyiwa kazi.

Kwa upande wake Waziri wa afya, kutoka nchini Rwanda, Dk. Agnes Binangwaho alisema Rwanda, inafanikiwa kupunguza vifo vya mama na mtoto, kutokana na kutoa elimu kwa wananchi juu ya uzazi wa mpango, pamoja na kusambaza simu kwa kila muuguzi wa kituo cha afya na kutoa namba kwa wananchi ili wakiwa na matatizo gari la wagonjwa huwafuata mahali walipo na kuwakimbiza hospitali, kupata huduma mbalimbali ikiwemo kujifungua.

1 comment:

  1. unyanyasaji na mateso yamekithiri kutoka kwa manesi na madaktari , nani atakwenda kujifungua hospitali? matusi ya nguoni , kufinywa na kupigwa wakati mwengine au kubwanwa na mikasi huku unapewa matusi mazito mazito , unajuta kubeba mimba.....aaah jamani.... sijui niseme nini .. tena hao wazalishaji wengi ni wanawake ambao nao uchungu wanaojua lakini madhila wanayotufanyia sina maneno....

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.