Na Hafsa Golo
MAKAMU wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema serikali inahitaji wataalamu
wengi katika sekta ya kilimo ili kufikia malengo ya uzalishaji mzuri wa chakula
nchini.
Aliyasema hayo baada
ya kuzindua dakhalia ya chuo cha kilimo Kizimbani katika shamra shamra za miaka
49 ya Mapinduzi Zanzibar.
Alisema mahitaji
ya wataalamu ni makubwa hivyo aliwataka
wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili taifa liwe na idadi kubwa ya wataalamu
watakaokidhi haja ya mahitaji sambamba na kupunguza kwa asilimia 50 za uagizaji
wa chakula kutoka nje.
Balozi Seif
alisema ndani ya nchi kuna shehia 287 ambazo zinahitaji huduma za ugani ambapo
maafisa wa ugani waliopo ni 141 ambapo kuna upungufu wa maafisa 146.
Hata hivyo,
alisema hao waliopo hawana elimu ya kutosha ambapo wengi wameishia elimu ya
stashahada, hivyo alisema dakhalia hiyo itakuwa chachu ya kuzalisha wataalamu
wengi zaidi.
Aidha alisema dakhalia
zina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya elimu ya kilimo nchini kwani itasaidia
kukijengea uwezo chuo hicho kufikia malengo.
Alisema
mashirikiano ya utendaji ndio nyenzo kubwa ya mafanikio ya maendeleo sambamba
na kutekeleza majukumu ipasavyo bila ya kukiuka utaratibu wa utoaji elimu.
Pia aliwataka
walimu waandae mikakati bora ambayo itawezesha kuwabana wanafunzi hao kushiriki
masomo yao kikamilifu
ili waweze kufaulu vizuri katika kiwango cha stashahada.
Alisema vijana na
wanafunzi wana fursa kubwa ya kupata elimu ya juu nchini kutokana
na kuongezeka kwa vyuo vikuu ili kupunguza gharama zisizo za lazima.
Alisema utafiti
umebainisha kwamba mwanafunzi anayepata shahada ya kwanza kwanza nchini Uingereza analazimika kulipiwa
zaidi ya shilingi milioni 57,000,000 fedha ambazo zinaweza kugharamia wanafunzi
kadhaa nchini wakati kiwango na ubora wa elimu kinafanana.
“Tumefikia wakati Zanzibar hakuna sababu
kwa elimu ya ngazi ya shahada na stashahada kufuatwa tena nchi za nje
hasa tabia iliyojengeka kwa vijana kwenda Ulaya kwani tayari tumeshakuwa na
vyuo vikuu vinavyotosheleza mahitaji,” alisema.
Aliutaka uongozi
wa chuo cha kilimo Kizimbani kuongeza juhudi za kutoa taaluma ili taifa likidhi
mahitaji ya wataalamu wa kilimo ambao hivi sasa wapo 141 wakati mahitaji ni
wataalamu 287 kukiwa na upungufu wa wataalamu 146.
Balozi Seif
alifahamisha kwamba ujenzi wa dakhalia uliofanywa na chuo ni mabadiliko makubwa
yatakayoiwezesha Zanzibar
kuwa na wataalamu wake na kuacha mfumo wa kutegemea watalaamu wa kigeni ambao
wanaibebesha mzigo serikali.
Naye Katibu Mkuu
Wizara ya Kilimo na Maliasili, Afan Othman Maalim alisema katika kukijengea
uwezo zaidi wa kitaaluma chuo, Wizara tayari inawaandaa walimu 10 kupata
mafunzo ya juu kwa ajili ya kukiwezesha chuo hicho kutoa elimu ya shahada ya
kwanza.
Alisema hatua
hiyo imelenga kuondosha tatizo la uhaba wa mabwana na mabibi shamba uliopo
ambao unachangia kudumaza juhudi za wakulima katika uzalishaji wa kilimo.
Akitoa taarifa ya
ujenzi wa dakhalia hiyo pamoja na mikakati ya baadaye ya chuo, Mkurugenzi wa
chuo,Mohammed Khamis Rashid alisema ujenzi wa dakhalia hiyo yenye vyumba saba
na kuhudumia wanafunzi 42 umekuja kutokana na changamoto iliyojitokeza ya
ongezeko kubwa la vijana wanaotaka kujiunga na chuo hicho.
Alisema mbali ya
wanafunzi wa chuo hicho lakini pia dakhalia hiyo itatumiwa na wakulima wa
mafunzo na muda mfupi kipindi ambacho wanafunzi wa chuo hicho watakuwa likizo.
Dakhalia hiyo
imegharimu jumla ya shilingi 399,000,000 na kugharamiwa na Mfuko wa Kimataifa
wa Kuendeleza Kilimo (IFAD).
Aliwataka kulienzi
jengo jipya la Dakhalia hiyo ili liweze kuendelea kutumika muda mrefu likiwa
katika mazingira mazuri na wanafunzi wengine waje kutumia bila ya kikwazo
chochote.
Naye Mkurugenzi wa
Chuo cha Kilimo Kizimbani Mohammed Khamis Rashid alisema chuo hicho kimepata
usajili katika baraza linalisimamia Mafunzo ya Ufundi Tanzania (NACTE) usajili
huo ambao utakiwezesha chuo hicho kuwa miongoni mwa vyuo vinavyotambulika rasmi
katika utoaji wa mafunzo ya Kilimo, Mifugo na Maliasili ambapo sasa kimeanza
kutoa ngazi ya Diploma.
Alisema jumla ya
shilingi milioni 399,000,000 zimetumika katika ujenzi wa Dakhalia hiyo ambayo
ina uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 42,na wanafunzi wa kike ngazi ya Diploma ndio watakaoishi katika
dakhalia hiyo, ambaoyo pia itatumika kwa ajili ya wakulima ambao watapatiwa
mafunzo ya muda mfupi katika chuo hicho.
Mwalimu Mkuu wa
Chuo hicho Nassor Salim Mohammed alisema miongoni mwa mafunzo ya wanayotoa
chuoni hapo ntiba ya wanyama,uchunguzi wa maradhi,Udhalishaji bora wa
mazao,matunzo na kinga,utumiaji wa dawa kwa kiwango kinachokubalika na sahihi.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo alikiri kuwepo kwa upungufu wa Mabibi shamba na mabwana katika
sekta ya kilimo hivyo Wizara imeanza kutafuta mbinu mbadala mbali mbali ikiwemo
kusomesha wanafunzi hao hivyo mara tu ya kuhitimu watawaajiri ili waweze
kutekeleza jukumu hilo.
No comments:
Post a Comment