Na
Mwantanga Ame
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,
amesema serikali inataimarisha bajeti ya matumizi ya dawa, ili kutoa matibabu
bora katika hospitali za umma.
Pia
alisema huduma nyengine ambazo serikali itaziimarisha ni ya chakula kwa
wagonjwa na vifaa vya matibabu kutokana
na hivi sasa kutumia fedha nyingi kutafuta matibabu nje.
Dk
.Shein aliyasema hayo jana wakati akifungua mradi wa bohari kuu ya dawa Zanzibar, Maruhubi mkoa wa
mjini Unguja.
Alisema hivi sasa kumekuwa na tatizo kubwa la
kuwepo bajeti ndogo katika sekta ya afya hasa inayohusu chakula kwa wagonjwa,
dawa na vifaa vya matibabu, lakini tayari inajiandaa kukabiliana na hali hiyo ili hospitali za serikali zitoe matibabu bora.
“Tutagharamia
chakula cha wagonjwa, hivi sasa hali hairidhishi wagonjwa wanapewa wali, nyama
moja iko huko, maji ya mchuzi unakolezwa bizari nyingi hatuwezi kwenda hivi
kwani kuna wagonjwa wanahitaji mlo maalum kulingana na ugonjwa wake sio tumpe
muhogo na makopa,” alisema Dk.Shein.
Alisema
serikali inalazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na umuhimu wa kutoa matibabu
bora, ikiwa ni kuendelza dhana ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambapo Rais wa
kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume, aliwaahidi Wazanzibari kuwapa
matibabu bure.
Alisema
malengo ya Mapinduzi bado yataendelezwa,
licha ya kukumbwa na changamoto za kiuchumi, jambo ambalo limeifanya serikali
kuwataka wananchi kuchangia kiasi kidogo cha fedha.
Hali
hiyo, alisema imechangiwa zaidi na ongezeko la idadi ya watu baada ya Mapinduzi
ya Zanzibar
huku zao la karafuu likiwa limeanguka bei jambo ambalo limesababisha mapato ya
nchi kushuka.
Alisema
serikali imejikuta ikilazimika ndani ya bajeti yake kutegemea zaidi wafadhili
ikiwemo serikali ya China, Marekani na Denmark, ikiwa ni hatua ya kuweza
kuimarisha sekta hiyo ya kutoa huduma kwa jamii.
Alisema
hivi sasa bajeti inayotengwa kwa ajili ya manunuzi imeanza kuongezwa kutoka
shilingi milioni 17.5 ya mwaka 2009 hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni 1.
Hata
hivyo, alisema serikali inakabiliwa na tatizo kubwa la kutofahamika mahitaji
kamili ya dawa katika hospitali za Zanzibar
kunakosababisha kuifanya serikali kutoelewa hali halisi ya mahitaji kwa watu wake.
Alisema
katika kukabiliana na hali hiyo serikali tayari imeanza kujipanga kwa kuandaa mazingira
bora ya watumishi katika sekta ya afya.
Kutokana
na hali hiyo Dk. Shein, aliwataka watendaji katika sekta ya afya kubadilika kwa
kutekeleza majukumu yao
vizuri badala ya kuendelea kufanya kazi kwa mazoea.
Dk.
Shein, alizishukuru serikali za Marekani, Jamhuri ya Watu wa China na Denmark kwa michango inayoitoa
kuimarisha sekta ya afya nchini.
Mapema
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Dk. Sira Ubwa Mamboya, alisema kujengwa kwa bohari
hiyo itaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa dawa nyingi.
Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Mohammed Saleh Jidawi, alisema jengo hilo
limegharimu dola za Marekani milioni
1.2 ambazo zilitolewa na serikali
ya Marekani kwa kushirikiana na DANIDA huku serikali ya Zanzibar ikitoa zaidi ya shilingi milioni
278.
Balozi
wa Marekani nchini Tanzania , Alfonso Lenhardt, akitoa maelezo yake alisema
serikali yao itaendelea kuisaidia Zanzibar katika kuinua
sekta ya afya hasa eneo linalohusu huduma za kijamii kwa wanawake na watoto.
Nae
Mwakilishi wa Serikali ya Denmark , Stean Underson, akitoa maelezo yake alisema
nchi yao itaendelea kushirikiana na Zanzibar , kwa vile imekuwa ikiipa nafasi
kubwa katika bajeti yao.
Nae
Mkurugenzi wa bohari hiyo, Mayasa Salum, alisema mfumo wa usalama katika bohari
hiyo utaweza kuimarisha utoaji huduma bora za matumizi ya dawa katika hospitali
kuu ya Mnazimmoja na vituo vyengine vya afya kwa Unguja na Pemba.
No comments:
Post a Comment