Habari za Punde

Ligi kuu Bara kurudi Jan. 26

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
 
WAKATI mzunguko wa pili wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara unatarajiwa kuanza kutimua vumbi Jumamosi Januari 26, mwaka huu, ngwe ya pili ya ligi daraja la kwanza imesogezwa mbele kwa wiki moja.
 
Ligi hiyo ya daraja la kwanza Bara, sasa itarudi viwanjani Februari 2, mwaka huu. Uamuzi wa VPL kuendelea Januari 26 mwaka huu ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na klabu za ligi hiyo kilichofanyika juzi Januari 21 jijini Dar es Salaam.

 
Hata hivyo, uamuzi huo umefikiwa huku yakiwepo masharti kadhaa kutokana na uamuzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukamata shilingi milioni 157 kwenye akaunti za TFF, fedha ambazo zilitoka kwa mdhamini wa ligi kuu kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom kwa ajili ya timu zinazoshiriki ligi hiyo.
Masharti hayo yatawasilishwa na Kamati ya Ligi kwa maandishi kwa Katibu Mkuu TFF, nakala kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
 
Awali klabu kupitia Kamati ya Ligi zilisisitiza zisingecheza ligi hadi fedha hizo zitakaporejeshwa. Kwa upande wa ligi daraja la kwanza, itaanza bila timu ya Small Kids ya Rukwa ambayo imeshushwa daraja kwa mujibu wa kanuni baada ya kushindwa kucheza mechi mbili katika mzunguko wa kwanza.
 
Kwa mujibu wa kanuni za ligi hiyo, matokeo yote ya mechi ambazo Small Kids ilicheza katika mzunguko huo wa kwanza yamefutwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.