Habari za Punde

Simba hadi ubalozini Angola Yasaka mikanda ya Recretivo de Libolo

 Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
 
UONGOZI wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba SC umepiga hodi ubalozi wa Tanzania nchini Angola kwa ajili ya kusaka video za wapinzani wao kwenye ligi ya mabingwa Afrika.
 
Simba ilikuwa Oman kwa kambi maalumu ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi kuu Bara utakoanza Januari 26, pamoja na ligi ya mabingwa Afrika ambapo itaanza kwa kuivaa Recretivo de Libolo ya Angola kati ya Februari 17 na 19 jijini Dar es Salaam.


Makamu Mwenyekiti wa Simba Geofrey Nyange ‘Kaburu’, amesema kwamba kocha mkuu wa timu hiyo Patrick Liewig ametaka mikanda ya video za mechi za wapinzani wao hao ili kuweza kuifanyia kazi kabla ya kukwaana nao.
 
“Unajua wapinzani wetu hatuwafahamu vizuri hivyo tumeona ni vizuri kusaka mikanda yao ili kuweza kuifanyia kazi kabla ya kukutana nao na tayari tumeshauomba ubalozi wetu nchini Angola utusaidie kwa hili”, alisema.
 
Kuhusiana na kambi ya timu hiyo nchini Oman, alisema imekuwa na mafanikio makubwa na kocha ameridhishwa na kiwango walichofikia wachezaji wake baada ya kukaa pamoja kwa wiki mbili sambamba na michezo mitatu ya kujipima nguvu na timu za huko.
 
“Kocha ameridhika na wachezaji kuanza kuelewana, hivyo anaamini kwa kiasi kikubwa ametimiza malengo yake aliyojiwekea katika kuhakikisha anaijenga timu tayari kwa mashindano yoyote”, alisema Kaburu.
 
Kaburu aliongeza kuwa, timu hiyo ilitarajia kufanya mazoezi ya mwisho jana kabla ya leo asubuhi kuondoka huko na itakapowasili nchini itaingia kambini moja kwa moja kuendelea na maandalizi yake, kabla ya kuivaa Black Leopards ya Afrika Kusini kesho kwenye uwanja wa Taifa.
 
Ikiwa Oman Simba ilicheza mechi tatu za kujipima uwezo ambapo ilianza kwa kukwaana na timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 23 na kufungwa bao 1-0, kabla ya kufungwa 3-2 na Qaboos na juzi ikaitandika Ahili Sidabi mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.