Na Haji Nassor, Pemba
SIKU chache baada ya Amani
Ibrahim Makungu kutangaza kujiuzulu nafasi ya urais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), uamuzi huo umeonekana kuwagawa wadau wa
soka kisiwani Pemba, huku wengine wakiiomba
kamati tendaji ya ZFA kutomkubalia.
Wakizungumza na gazeti hili
kwa nyakati tafauti, baadhi ya wadau hao wamesema Makungu ameshaonesha mwelekeo
katika kuendeleza mpira wa miguu hapa Zanzibar,
hivyo haitakuwa busara kumfungulia njia ya kuondoka madarakani.
Wamesema kiongozi huyo ndie
pekee aliyeonesha nia ya kweli ya kukuza soka la visiwa hivi kutokana na mipango
na mikakati yake ambayo muda mfupi tu baada ya kukaa madarakani imeanza
kuonesha mwanga wa matumaini.
Meneja wa klabu ya Jamhuri Abdallah
Abeid Mohammed ‘Elisha’, alisema hivi karibuni ZFA ilikuwa na mgogoro mkubwa ambao
tayari umeshasuluhishwa kutokana na busara za Rais huyo, hivyo akasema si vyema
kuendeleza mivutano isiyokuwa na tija kwa taifa.
Elisha amesema, hata kama Rais
huyo alifuata taratibu za kuwasilisha barua ya kuomba kujiuzulu katika kamati tendaji,
ni vyema kamati hiyo ilikatae ombi lake
hilo, ili kumpa nafasi
zaidi ya kutekeleza mipango yake ya kuendeleza soka hapa nchini.
Kwa upande mwengine, Meneja
huyo alionesha wasiwasi juu ya kufeli kwa mpango wa timu yake kuwaleta
washindani wenzao katika ligi ya mabingwa barani Afrika timu ya St. George ya Ethiopia,
iwApo Makungu ataachiwe akiachIe kitI cha urais wa ZFA.
“Kutokana na hali ngumu ya
kifedha inayotukabili, Makungu ametuhakikishia kutusaidia kwa asilimia kubwa,
sasa sijui itakuwaje kama akiondoa mkono wake
ndani ya ZFA. Mimi nasema kama kuna mgogoro
viongozi wawekwe kitako ili waumalize’’, alifafanua Elisha.
Kwa upande wake, Msemaji wa
timu ya Super Falcon Harith Bakari, alisema haoni sababu kwa Makungu kuachia
ngazi, kwa kile alichodai kwamba viongozi wa ZFA Pemba wako makini katika kazi
zao na haamini kuachia kwake ngazi kumetokana na kunyimwa ushirikiano.
Juzi, Amani Ibrahim Makungu
aliandika barua kwa kamati tendaji ya ZFA kuomba kujiuzulu urais kwa madai ya
kugomewa na wasaidizi wake wakuu kisiwani Pemba
ambao haukuungana na ujumbe wa ZFA kutoka Unguja uliokwenda huko kuangalia
maendeleo ya soka.
No comments:
Post a Comment