Na Madina Issa
WATENDAJI wa tasisi mbali mbali zilizo chini ya Tawala za Mikoa wametakiwa kubadilika kwa kufanya kazi kwa mashirikiano ili kuweza kufikia malengo.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib, Abdalla Mwinyi Khamis aliyasema hayo alipokutana na viongozi wa Mkoa huo, viongozi wa Baraza la Manispaa, Halmashauri ya Wilaya ya Magharib, Madiwani pamoja na Masheha.
Alisema ili kuyafikia malengo ya taasisi zao ni wajibu wa viongozi kufanya kazi kwa mashirikiano na taasisi nyengine za nje.
Alisema taasisi hizo ndizo kioo cha mji wa Zanzibar na vitongoji vyake hivyo kufanya vibaya ni sawa na kuharibu jina zima la Zanzibar ambayo imekua ikisifika kuwa na mazingira mazuri.
Aliwataka watendaji kufanya kazi zao kwa uangalifu wa hali ya juu ili kuhakikisha mji wa Zanzibar unakuwa safi.
Alifahamisha kuwa hivi sasa watu wengi wamekuwa mashuhuda wa kuona mji wa Zanzibar unavyoendelea kuchafuka huku kukiwa na ongezeko kubwa la uzururaji wa wanyama.
"Hebu tujitizameni wenyewe sisi tuliokuwepo hapa kweli tunashindwa kuweka mji katika hali ya usafi na kuwadhibiti ng’ombe wasizurure," alihoji Mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa upande wa washiriki wa semina hiyo walisema wapo tayari kuufanyia usafi mji wa Zanzibar ili uendelee kuwa kivutio.
No comments:
Post a Comment