Habari za Punde

Gesi ya Mtwara, Lindi lazima ipelekwe Dar


Na Mwandishi wetu
SERIKALI imesema uamuzi wa kiuchumi ndio uliolazimisha kusafirisha gesi asilia kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara na kuipeleka Dar es Salaam ambako itatumika kufua umeme na kutumika moja kwa moja viwandani, majumbani na kwenye magari.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo alisema Dar es Salaam ndiko kuna miundombinu mikubwa ya usafirishaji na usambazaji umeme kuliko mikoa mingine.

Alisema kuweka mitandao ya usambazaji wa gesi kutoka kwenye bomba la gesi asilia linalojengwa kutarahisisha matumizi ya gesi asilia viwandani na majumbani katika Mikoa ya Mtwara na Lindi, na mikoa mingine kwa siku za baadae.

Aidha alisema serikali imetenga maeneo katika pwani ya Mikoa ya Kusini ikiwemo Lindi na Mtwara kwa ajili ya uanzishwaji wa maeneo ya viwanda vikiwemo vya mbolea na petrochemicals.

Prof. Muhongo alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu miradi ya utafutaji na uvunaji wa gesi asilia nchini.

Aidha alisema ujenzi wa kiwanja cha simenti uko katika hatua za mwisho za maandalizi.

Alisema ili kutengeneza mazingira mazuri ya biashara ya gesi asilia na mafuta kwa kampuni za huduma, malighafi na vitendea kazi, serikali imetenga eneo maalumu Mtwara, ambalo litawekewa miundombinu ya msingi ili kutoa vivutio mbalimbali kwa makampuni hayo.

Alifafanua kuwa eneo hilo litapewa hadhi ya ukanda huru wa bandari.

“Ni lazima shughuli za kusafisha na kusafirisha gesi asilia zitatoa ajira katika maeneo husika,” alisema.

Kwa mfano alisema mitambo ya kusafishia gesi inayojengwa Madimba (Mtwara vijijini) na SongoSongo (Kilwa, Lindi), kila mtambo utahitaji wafanyakazi na wengine watatoka Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Aliwakumbusha Watanzania kuwa raslimali zilizopo nchini ikiwemo gesi asilia, madini, makaa ya mawe, wanyama pori, misitu, milima ya utalii, mito, maziwa, bahari ni za Watanzania wote kwa mujibu wa katiba.

Alisema raslimali hizo zinapatikana, zinatunzwa na kuzalishwa maeneo mbalimbali nchini na mapato yake yanatumika kwa maendeleo ya Watanzania wote bila kujali maeneo raslimali hizo zilipo.

“Tusikubali kuvunja nchi yetu vipande vipade kwa kisingizio cha raslimali zilizopo mikoani mwetu. Tusikubali kuvunjavunja mikoa yetu kwa kisingizio cha raslimali zilipo kwenye wilaya zetu,” alitanabahisha.

Prof. Muhongo aliwakumbusha wananchi wa mikoa hiyo na wanasiasa walioandaa maandamano kupinga gesi kusafirishwa Dar es Salaam, kuwa serikali kwa kushirikiana na Shirika la Mafuta la Tanzania (TPDC), inatumia fedha za walipa kodi wa nchi nzima kwa shughuli za kuvutia, kuratibu na kusimamia utafutaji na uendelezaji wa gesi asilia ikiwemo Mikoa ya Mtwara na Lindi.

Lakini alisema cha kustaajabisha walipa kodi bado hawajalalamika wala hawajafanya maandamano ya kudai fedha zao za kodi zisitumike Mtwara.

“Ni muhimu pia tukaelewa kwamba gesi asilia iliyopo Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) inazalisha umeme peke yake kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi,” alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.