Na Mwandishi wetu
WIZARA ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Wanawake na Watoto
imeshtushwa na vitendo vya udhalilishaji watoto kingono vinavyofanywa na watu
wasiojulikana ambao wamekuwa wakirusha kwa njia ya simu, kuweka katika mitandao
na kutengeza video zinazowaonesha watoto wa kike wakifanyiwa unyama huo.
Taarifa iliyotolewa na Iddi Ramadhan Mapuri kwa niaba ya
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alisema picha hizo zimesambazwa kwa kasi kupitia
njia hizo.
Alisema kitendo cha kuandaa, kurusha na kusambaza picha
hizo ni kosa chini ya sheria ya mtoto
nambari 6 ya mwaka 2011.
“Kifungu nambari 33(i) cha sheria hiyo kinasema kuwa hakuna
mtu yeyote anaeruhusiwa kuchapisha habari au picha zinazoweza kupelekea kutambuliwa
kwa mtoto aliyedhalilishwa isipokuwa kwa ruhusa ya mahakama,” alinukuu sehemu
ya sheria hiyo.
Alisema adhabu ya kosa hilo ni faini isiyopungua shilingi 500,000 na
isiyozidi shilingi 3,000,000 au kifungo kisichopungua miezi 6 na kisichozidi
miaka miwili au adhabu zote mbili.
Alisema vitendo hivyo vinawakosesha amani watoto na wazee
wao, lakini pia vinakiuka sheria, heshima na maadili ya Wazanzibari.
Aidha wizara hiyo imeviomba vyombo vya dola, ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), mahakama na wanasheria kuchukua hatua za
kuwakamata na kuwachukulia hatua za kuwafikisha mahakamani wote wanaohusika na
uandaaji,usambazaji, kuzionesha na kuziangalia picha hizo.
Aidha imewaomba wananchi kutovishabikia vitendo hivyo vya aibu vinavyokwenda kinyume na silka, utamaduni
na maadili ya Wazanzibari.
No comments:
Post a Comment