Joseph Ngilisho,Manyara
WANAWAKE wafanyabiashara wa pombe za kienyeji Wilayani
Hanang Mkoani Manyara,wameandamana hadi
kwa Mkuu wa Wilaya hiyo wakimuomba aondoe amri ya kupiga marufuku kutengeneza
pombe kwa kutumia nafaka.
Wanawake hao zaidi ya 300 waliandamana jana hadi kwa mkuu
wa wilaya hiyo, Christina Mndeme,wakidai kuwa amri hiyo imewaathiri kwani
wanaitegemea biashara hiyo kwa ajili ya kuendesha maisha yao ikiwemo kuwasomesha watoto wao.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya, wanawake hao walidai
kuwa hivi sasa maisha yao yamekuwa magumu kwani
wanategemea biashara hiyo kwa ajili ya kuendeshea maisha yao hivyo wanaomba waendelee nayo.
“Mkuu hivi sasa maisha yetu yamekuwa magumu, tunaomba
tuendelee na biashara hii kwani wengine tunaitegemea kwa ajili ya kusomesha
watoto wetu wanaoingia kidato cha kwanza,” walisema wanawake hao.
Walimuomba Mkuu huyo wa wilaya waendeleze biashara hiyo kwa
muda wakati huu ambao wanawapeleka watoto wao shule,halafu wataachana na
biashara hiyo pindi hali ya chakula itakapokuwa nzuri kwenye wilaya hiyo.
Hata hivyo,Mkuu huyo wa wilaya aliwapokea wanawake hao na
kuwataka wabuni vyanzo vingine vya biashara ili waweze kujiingizia kipato
kuliko kutegemea biashara hiyo ya kutengeneza pombe kwa kutumia nafaka.
“Hivi sasa sehemu kubwa ya wilaya yetu ina upungufu mkubwa
wa chakula hivyo siyo vizuri tukatumia mtama au mahindi kidogo tuliyonayo kwa
ajili ya kutengeneza pombe za kienyeji, kisha tuwe na njaa,” alisema.
Alisema agizo lake la kupiga marufuku utengenezaji wa pombe
za kienyeji kwa kutumia nafaka litaendelea wilayani humo,kwani ameshawaagiza
viongozi wote wahakikishe nafaka haitumiki kutengenezea pombe za kienyeji.
No comments:
Post a Comment