Na Mwantanga Ame
WIZARA ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, imesema inaandaa mpango wa kuufanyia matengenezo uwanja wa Mao Tse Tung kwa kushirikiana na serikali ya China.
Naibu wa wizara hiyo Bihindi Hamad Khamis, ameliambia Baraza la Wawakilishi jana, kuwa matengenezo hayo yatafanyika baada ya Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar kukubali kufanya hivyo.
Alikuwa akijibu suali la Mwakilishi wa Rahaleo Nassor Salim Ali aliyehoji sababu za wizara hiyo kushindwa kutoa mchango wake wa kuufanyia marekebisho uwanja huo, na badala yake kukiachia Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) pekee.
Naibu Waziri huyo alisema, wizara yake inaamini kuwa gharama zilizotumika kuufanyia matengenezo uwanja huo, zilikuwa ndani ya uwezo wa uongozi wa ZFA uliopo sasa, na haikutarajia kama ingelihitaji mchango wa wizara katika ujenzi huo.
Mchango wa wizara katika kazi hiyo alisema, kwa kutumia Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), Kamisheni ya Michezo na Utamaduni, ilikuwa ni kutoa ushauri na miongozo kwa ZFA juu ya namna ya kuufanya uwanja huo uwe bora.
Akijibu suali jengine la Mwakilishi huyo, Bihindi alisema tayari wizara yake imeanza maandalizi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha timu ya taifa ya soka Zanzibar Heroes, inafanya vizuri katika mashindano ya Chalenji yatayofanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini Kenya.
Alisema serikali inatambua umuhimu wa mashindano hayo kwa timu ya Taifa, na ndio maana serikali imejidhatiti kuifanyia matayarisho mazuri.
No comments:
Post a Comment