Habari za Punde

Yeye asema aliyoyaona yametosha



Na Abdi Suleiman, Pemba                                      
LICHA ya viongozi wa klabu mbalimbali kisiwani Pemba na wengine wa Chama cha Soka Zanzibar wilaya tafauti kushikilia msimamo wa kumtaka Amani Ibrahim Makungu asiachie ngazi, Rais huyo wa ZFA amesema wakati umefika aondoke kuliko kuendeleza malumbano na viongozi wanaojali maslahi binafsi.
 
Akizungumza na viongozi wa klabu za madaraja mbalimbali na viongozi wa ZFA Wilaya ya Mkoani wakati akihitimisha ziara yake kisiwani Pemba, Makungu alisema tangu aingie madarakani kukiongoza chama hicho takriban miezi saba sasa, malumbano kutoka kwa baadhi ya viongozi wanaojali matumbo yao yameendelea kukitafuna chama hicho.
 
“Sasa naona bora nishughulikie biashara zangu  kuliko kuendeleza malumbano na watu wasiokuwa na imani na chama. Natamka wazi kuwa nimefikia kikomo kukiongoza chama”, alisema kwa masikitiko.

Akifafanua namna alivyokosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho, Makungu alisema baadhi ya wajumbe walifikia kumwambia kuwa uongozi wake mwisho Nungwi, hali aliyodai kuikubali kufuatia wasaidizi wake muhimu kutokujumuika pamoja naye kwenye ziara yake aliyoifanya Pemba hivi karibuni.
 

“Nashangaa sana, baadhi ya watendaji wakuu wa chama kuniambia kuwa mabadiliko ninayoyataka nitayasikia tu, na pia kusema wazi kwamba mwisho wangu Nungwi. Sasa nimekubali kauli hizo na wakati umefika kuwaachia chama chao”, alieleza Makungu.

Hata hivyo, alisema anaona fahari kukiacha chama hicho akiwa amejenga msingi mzuri wa kukiletea mabadiliko ambapo kwa miezi saba aliyokalia kiti cha urais, angalau dalili za maendeleo zimeanza kuonekana kutokana na juhudi zake binafsi.
 
Hata hivyo, pamoja na kunuia kung’atuka, Rais huyo aliwataka viongozi wa ZFA wilaya zote, kuendeleza soka hasa la vijana, huku akiahidi kuzitekeleza ahadi alizowapa ikiwemo kutoa zawadi za fedha kwa washindi wa ligi za daraya la pili  wilaya, la tatu, central na ligi ya watoto (juvenile).
 
Aidha alisema kuna haja kubwa ya kuifanyia mabadiliko katiba ya chama hicho, ingawa  alisema wapo baadhi ya viongozi wanaokwamisha dhamira hiyo kwa kulinda maslahi binafsi.
 
Viongozi wa klabu mbalimbali waliohudhuria mkutano huo, walishauri kuifanyia marekebisho katiba, ili kuondosha matatizo na mivutano isiyokuwa ya lazima inayodumaza soka la Zanzibar.
 
Mwenyekiti wa ZFA Wilaya ya Mkoani Seif Mohammed Seif, na Katibu wa Central Nassor Hakim, wamesema ujio huo wa Rais wa ZFA umewapa faraja kwani ni muda mrefu hakuna hata kiongozi mmoja wa juu aliyepata kuwatembelea na kuzungumza nao.
 
 “Ziara hii imetufariji na kutujengea imani kwa  uongozi wa sasa wa ZFA, kwani ni jambo ambalo halijawahi kutokea kabla. Ipo haja kwa viongozi wote kukaa pamoja na kumaliza tafauti zao kwa maslahi ya timu zetu na taifa kwa jumla ”, alisema Hakim.

Pamoja na kusisitiza azma yake ya kujiuzulu, Makungu alihitimisha mkutano na ziara hiyo kwa kuchangia shilingi milioni moja kwa ajili ya kutafuta ofisi ya kudumu kwa ZFA wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.