Habari za Punde

Ripoti ya Kamati ya Kuchunguza Kudhibiti Hesabu za Serekali na Mashirika ya Umma

MUHTASARI WA RIPOTI YA KAZI MAALUM YA  KAMATI YA KUCHUNGUZA NA KUDHIBITI HESABU ZA SERIKALI NA MASHIKIKA (P.A.C) JUU YA UTENDAJI WA SHIRIKA LA UMEME LA ZANZIBAR, 2012/2013:
Mheshimiwa Spika:
Naomba nianze kwa kumshukuru sana M/Mungu mtukufu kwa kutujaalia uhai na afya iliyotuwezesha kuhudhuria kikao hichi kwa lengo la kulitumikia Taifa na wananchi wetu. Aidha naomba niitumie fursa hii kwa kukushukuru Mh. Spika kwa kunipa nafasi ya kusimama mbele ya Baraza lako tukufu kwa nia ya kuwasilisha ripoti ya kamati yangu ya PAC kufuatia kazi iliyopewa na Baraza lako katika kikao cha tarehe 12/04/2012 cha Baraza lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika:
Kuwasilishwa kwa ripoti hii kunaifanya kuwa ni ripoti ya tatu kwa Baraza la saba na ni ripoti ya kwanza kwa mwaka huu wa 2013. Hali hii inadhihirisha umakini mkubwa ulionao Mh, Spika, katika kutekeleza na kusimamia majukumu ya chombo hichi ambacho ndio ngome ya wananchi wa Zanzibar. Aidha inadhihirisha utekelezaji wa dhana ya utawala bora kwa misingi ya mgawanyo wa madaraka kati ya Baraza la Wawakilishi kama chombo kinachowawakilisha wananchi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama chombo kilichopewa dhamana ya shughuli za utendaji.

Mheshimiwa Spika:
Kazi hii haikuwa rahisi kiutekelezaji na ilihitaji muda mwingi uliotufanya sisi Wajumbe wa Kamati, tuwe nje ya majimbo yetu kwa muda mrefu. Kwa niaba ya wajumbe wenzangu nawashkuru sana wapiga kura majimboni mwetu kwa uvumilivu wao wa kutokuwa pamoja nasi wawakilishi wao katika kipindi ambacho tupo katika utekelezaji wa majukumu yetu KITAIFA. Tunazidi kumuomba M/Mungu azidi kuwapa subira wananchi wetu, nasi wawakilishi wenu tunaahidi kuwa pamoja nanyi na kuwatumikia kwa moyo na nguvu zetu zote kwa maslahi yenu na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika:
Kwa niaba ya kamati yangu naomba niitumie fursa hii kuishukuru sana afisi yako Mh, Spika kwa namna ulivyoiwezesha, kuishauri na kuipa maelekezo mbali mbali kamati hii hali iliyopelekea kamati kuweza kutekeleza na kukamilisha majukumu yake kwa wakati. Aidha pia naomba niishukuru afisi ya Katibu wa Baraza la Wawakilishi kwa namna nae alivyweza kuisaidia kamati hadi katika hatua hii. Ni matumaini ya kamati kuwa mchango na msaada wenu utaendelea hata baada ya kamati kuwasilisha ripoti ya kazi yake leo hii.
Mheshimiwa Spika:
Naomba nimalizie shukurani zangu kwa kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa kamati yangu pamoja na secretary ya kamati kwa mashirikiano na mashauriano makubwa yaliyopelekea hatimae kukamilisha kazi hii na hatimae leo tunaiwasilisha mbele yenu Wawakilishi na wananchi.
Mheshimiwa Spika :
Kazi ya kupiga vita dhulma, rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na UFISADI wa aina yoyote, inahitaji ujasiri mkubwa na pasipokuwepo watu wa kuondosha kasoro hizo, jamii haitaweza kukalika na itakuwa kila mtu mwenye nguvu, atatumia nguvu zake dhidi ya mnyonge. Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nimnukuu baba wa Taifa la Tanzania, Mwalim Julius Kambarage Nyerere, kwa kauli yake inayopiga vita rushwa na inayoonesha athari zake kama ifuatavyo :

“SERIKALI YA WALA RUSHWA HAIKUSANYI KODI. ITABAKI KUFUKUZANA FUKUZANA NA VIJITU VIDOGO VIDOGO MABARABARANI HIVI TU BASI”
Mheshimiwa Spika:
Ninachotaka Wajumbe wako wafahamu ni kwamba, Shirika la Umeme la Zanzibar lina dhima kubwa ya kutoa huduma bora kwa wananchi wetu, lakini pia kukusanya mapato kwa utaratibu walioekewa kisheria, lakini inapotokezea kuwepo kwa Uongozi ambao umeona rushwa kuwa ndio kipaumbele kwao, kamwe mapato ya Shirika hayataonekana na wao watabaki kuwa matajiri na kushindana kwa Ujenzi wa majengo ya Kifahari na mambo mengine ya anasa, huku wananchi wakiendelea kupata tabu na kukosa huduma wanazozitarajia.
Mheshimiwa Spika:
Nukuu wa Baba wa Taifa niliyoinukuu hapo kabla inaashiria kwamba, iwapo Uongozi wa Shirika utaendeleza vitendo vya Rushwa, Upendeleo, Ubinafsi na aina yoyote ya dhulma, watakao pata tabu sio matajiri wala Viongozi wa nchi hii, badala yake, ni wananchi wetu walio wengi, ndio wanaokamuliwa kwa gharama kubwa wasizoziweza za uugwaji wa Umeme, malipo ya kila mwezi na gharama nyenginezo, huku Matajiri wenye Makampuni yao, Viongozi wenye pesa zao, wataendelea kukinigiwa kifua na matokeo yake hawataona ubaya wowote wa wanayoyafanya, alimuradi maisha yao na matilaba yao yanaendelea kuimarika.
Mheshimiwa Spika:
Suala la huduma ya umeme lina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Sote tunafahamu ni kwa kiasi gani Nchi yetu ilivyolipa umuhimu jambo hili, ambapo pamoja na umasikini wetu tulionao lakini Serikali imejitahidi kutandika miundombinu pamoja na mazingira mazuri ambayo yataiwezesha huduma hii kupatikanwa na kila mmoja wetu tena kwa urahisi.

Azma ya Serikali ni nzuri kwa kuamini kwamba, huduma ya umeme kwa wananchi wake si kitu cha anasa kama ambavyo wengine wanavyodhani, bali ni kitu cha lazima kwa kila mmoja wetu kukitumia. Hii ina maana kwamba hatuwezi kuifikisha Nchi yetu kwenye maendeleo bila ya kuifanya nishati hii kuwa ndio kichocheo kikuu na nyenzo ya kuyafikia maendeleo hayo katika ustawi wa jamii yenyewe, lakini pia katika nyanja ya ukuzaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika :
Sehemu kubwa ya lengo hili imefikiwa, kwani kwa hivi sasa huduma hii ya umeme imesambaa maeneo mengi ya mijini na vijijini kwa Unguja na Pemba. Leo si ajabu tena vijijini kuwa na umeme na la kufurahisha zaidi ni kwamba, huduma hii ikiwa pia inatumiwa na wale wananchi wenye kipato cha chini.
Katika kufanikisha azma hiyo njema ya Serikali, ndipo Serikali ilipoanzisha Shirika la Umeme limeanzishwa kwa mujibu wa Sheria Nam. 3  ya Mwaka 2006, ili kuweza kusimamia upatikanaji wa huduma hiyo. Pamoja na utoaji huo wa huduma, lakini kama Shirika, lina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa nalo ni moja kati ya eneo la kuingiza mapato kwa ajili ya kujihudumia wenyewe na kutoa mchango wake kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika :
Kwa maana hiyo iliyoelezwa hapo juu, mapato ya Shirika yanategemea sana malipo ya huduma ambazo Shirika inazitoa kwa wananchi, wakati huo huo na wananchi nao hutegemea mno huduma wanazozipata ziendane na malipo wanayotoa. Vyenginevyo mambo haya mawili yasipoenda sambamba huzusha manung’uniko kwa wananchi wetu ambao ndio walengwa wa huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika :
Katika hili kuna kutokuridhika kwa wananchi ambapo baadhi yao wanadhani taratibu za kisheria za upatikanaji wa huduma hii hazifatwi. Hali ambayo wengine ama kucheleweshwa kuipata huduma hiyo, jambo ambalo linaleta usumbufu mkubwa au wakati mwengine kulipa malipo makubwa yakitafautiana na wengine, ijapokuwa aina ya huduma hiyo inafanana. 

Aidha kwa upande mwengine wananchi kwa kuamini kwamba ZECO ndio Taasisi iliyopewa mamlaka ya kuunga na kuuza umeme hapa Zanzibar kwa mujibu wa Sheria, wanashangaa mno wanapoona kazi hii huwa wakati mwengine inapofanywa na Kampuni nyengine binafsi, hasa kwenye miradi mikubwa kama vile kwenye minara ya simu na baadhi ya hoteli.
Mheshimiwa Spika :
Tunapozungumza kuanzishwa kwa Taasisi kwa mfano huo wa Shirika la Umeme hapa Zanzibar, huwa tunategemea pia suala la kupatikana kwa ajira zitawanufaisha wananchi wetu, ambao bila ya shaka ndio wahusika wakuu wa kuipata neema hiyo. Na kwa sababu ajira ni haki ya kila mwananchi mwenye sifa zinazostahili kuipata, basi ni imani yetu kwamba haki hiyo itakuwa ni mali ya kila mwenye kustahili. Haitakuwa haki ya watu fulani ama kwa uzawa wao, eneo au rangi zao.

Halikadhalika ndani ya ajira yenyewe taratibu za kazi zitakuwa zinafuatwa katika kutimiza majukumu ya kazi, lakini vilevile katika kutoa haki na fursa zilizo sawa kwa wote, hii ni kwa mfano kwenye upatikanaji wa mafunzo ya kazi na upandishaji wa vyeo au madaraja. Lakini jengine kubwa zaidi ni kuthamini kazi yenyewe na utunzaji bora wa mali za Shirika. Taratibu za ununuzi na uondoaji wa mali ziwe ndio muongozo wa uwajibikaji.
Mheshimiwa Spika :
Aidha katika kuhakikisha Shirika linawahudumia vyema wananchi, ni lazima lijenge mazingira ya kuwa na huduma endelevu ambayo huwa haikosekani hata kwa wakati wa dharura. Kama tunavyofahamu kwamba huduma hii inapatikana kwa kununuliwa kutoka kwa Shirika la Ugavi wa Umeme, Tanzania (TANESCO), bila ya shaka kuna gharama zake na wakati mwengine ama kwa dharura ya matengenezo au vyenginevyo huduma hii hukosekana kwa muda.
Mheshimiwa Spika :
Hali hiyo ama hutokea kwenye mitambo yao au mara nyengine kwenye mitambo yetu, kama ambavyo imetokezea mwaka  2010 kwa kipindi cha karibu miezi mitatu, kisiwa cha Unguja kilipokosa umeme. Hapa ndipo ambapo Shirika linahitaji kutumia umeme wake wa akiba. Kwa vyovyote vile hatuna njia nyengine mbadala isipokuwa kutumia majenereta yetu ya akiba. Ni kwa kiasi gani hayo yanatekelezwa na Shirika ni maswali yanayoulizwa na wananchi na yanataka majibu. Lakini je gharama za kila siku za Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuilipa TANESCO haiwi kwamba ni mzigo mkubwa wenye kutuelemea! Na kama kuna deni la nyuma ni deni gani hilo lisilokwisha na ivi ni halali kuendelea nalo?.
Mheshimiwa Spika :
Chimbuko la Kazi kwa Kamati:             
Hayo yaliyoelezwa juu ni miongoni mwa baadhi ya maswali mengi ya wananchi kwa Shirika lao, ambayo kwa kweli yanakuja kutokana na matokeo yaliyo kinyume na matarajio yao.  Kwa vile Shirika hili ni la Serikali kwa asilimia mia moja (100%) maana yake ni kwamba, hii ni mali ya walipa kodi wa nchi hii ambao ni wananchi, na wananchi wasemaji wao ni Wawakilishi waliowachagua, hayo  ndiyo  yaliyomfanya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Kuchaguliwa na Wananchi kupitia Jimbo la Kiwani  Mhe. Hija Hassan Hija kwa kutumia haki yake chini ya kanuni za Baraza ya 27(l)(m), 27(3), 48(1) na 49(1) Toleo la 2011, kwenye Mkutano wa Saba wa Baraza la Nane, kuwasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa Kanuni ya 117 ya kanuni za Baraza,  kwa kulitaka Baraza liridhie  kuunda Kamati Teule kwa ajili ya kulichunguza Shirika la Umeme kwa kuangalia maeneo yafuatayo:-
  1. Upotevu wa fedha za Shirika unaotokana na uungwaji wa umeme unaofanywa na watendaji wasio waaminifu.

  1. Sababu za usumbufu wanaoupata wananchi wakati wa kuomba na baada ya kulipia huduma ya kuungiwa umeme pamoja na suala la bei kubwa wanazopewa ukilinganisha na baadhi ya watu, makampuni, mahoteli, mabenki na makapuni ya minara ya simu za mikononi.

  1. Taratibu  za ajira katika Shirika zinazodaiwa kuwa za upendeleo Unguja na Pemba.

  1. Iwapo mali za Shirika zinauzwa kwa kufuata taratibu za Sheria ya Uuzwaji na Ugavi wa Mali za Serikali na Sheria nyengine.

  1. Iwapo upatikanaji wa majenereta 32 yaliyopo Mtoni ulifuata sheria zinazohusika na kwa nini hayatumiwi kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar, na

  1. Kiwango cha deni linalodaiwa Zanzibar na TANESCO na iwapo kuna sababu za msingi za kuendelea kuwepo kwa deni hilo na athari zake kwa  Maslahi ya Zanzibar.
Maelezo ya Mhe. Hija yalimalizika kwa kutoa Hoja iliyosisitiza haja ya kuundwa kwa Kamati Teule kwa lengo la kufanya kazi hadidu zote alizozieleza na ikabaki kazi ya Baraza la Wawakilishi kuamua juu ya hoja hiyo.

Mheshimiwa Spika :
Muundo wa Kamati          
Kutokana na umuhimu wa jambo hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, akichangia hoja hiyo ya Mhe. Hija, alikubaliana na kuendelea kwa mapambano dhidi ya ubadhirifu ndani ya vyombo vya umma, huku akiunga mkono jitihada zinazofanywa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika mapambano yao dhidi ya ubadhirifu wa mali za Umma na hivyo alipendekeza kuwa, badala ya kuunda Kamati Teule, kazi hiyo ya kufuatilia Hoja Sita alizozieleza Mhe. Hija, zikabidhiwe Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika (P.A.C), huku Mhe, Hija akipendekezwa kuwemo katika Kamati hiyo. Hebu na tumnukuu Mhe. Mohammed Aboud Mohammed kama ifuatavyo:
“Mhe. Spika, kwa kuwa hoja ya Mhe. Hija imeeleza kwa kina kuhusu upotevu wa pesa za Serikali. Mhe. Spika, naomba nipendekeleze kwa Baraza lako Tukufu kumuomba Mhe. Hija Hassan Hija kwamba badala ya kuunda Kamati Teule, basi kwa kuwa Kamati yetu ya P.A.C ina utaalamu mkubwa sana wa kufanya kazi hizi za kutizama upotevu wa fedha za Serikali, pamoja na mali za Serikali. Hivyo, naliomba Baraza lako likubali kwamba Kamati ya P.A.C ndio ifanye kazi hii, ikimjumuisha na Mhe. Hija Hassan ambaye ana habari nyingi. Naomba kutoa hoja1

Jambo la kusisitiza katika nukuu hiyo ni kwamba, Baraza lilikubaliana na hoja ya Mhe. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, baada ya Mtoa Hoja (Mhe. Hija Hassan Hija), kukubalina na pendekezo la Mhe. Waziri, na hivyo ni sawa na kusema kwamba, kazi hii ni maalum kwa Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali, ikitofautiana na zile kazi zake za kawaida, lakini ina uzito ule ule wa kazi za Kamati Teule na ripoti yake inatarajiwa pia kubeba maudhui ya Kamati Teule zinazoendelea kuudwa na Baraza la Wawakilishi. Hivyo kwa ujumla Kamati ilikuwa na Wajumbe wafuatao :-
  1. Mhe. Omar Ali Shehe                           Mwenyekiti
  2. Mhe. Fatma Mbarouk Said                             Makamo Mwenyekiti
  3. Mhe. Abdallah Juma Abdallah                      Mjumbe
  4. Mhe. Mbarouk Wadi Mussa (Mtando)        Mjumbe
  5. Mhe. Shadya Mohammed Suleiman                Mjumbe
  6. Mhe. Farida Amour Mohammed                     Mjumbe
  7. Mhe. Mohamed Mbwana Hamad                   Mjumbe
  8. Mhe. Hija Hassan Hija                                  Mjumbe
  9. Mhe. Shamsi Vuai Nahodha                   Mjumbe.
Halikadhalika Kamati ilikuwa na Makatibu wawili ambao ni :-
  1. Ndg Amour Mohammed Amour na
  2. Ndg Othman Ali Haji.
Mheshimiwa Spika :
Hadidu Rejea
Katika kufanya kazi hiyo Kamati ilikuwa inaongozwa na Hadidu Rejea zifuatazo :-
  1. Upotevu wa fedha za Shirika unaotokana na uungwaji wa umeme unaofanywa na watendaji wasio waaminifu.
  2. Sababu za usumbufu wanaoupata wananchi wakati wa kuomba na na baada ya kulipia huduma ya kuungiwa umeme pamoja na suala la bei kubwa wanazopewa ukilinganisha na baadhi ya watu, makampuni ya mahoteli, mabenki na makapuni ya minara ya simu za mikononi.
  3. Taratibu  za ajira katika Shirika zinazodaiwa kuwa za upendeleo Unguja na Pemba.
  4. Iwapo mali za Shirika zinauzwa kwa kufuata taratibu za Sheria ya Uuzwaji na Ugavi wa Mali za Serikali na Sheria nyengine.
  5. Iwapo upatikanaji wa majenereta 32 yaliyopo Mtoni ulifuata sheria zinazohusika na kwa nini hayatumiwi kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar, na
  6. Kiwango cha deni linalodaiwa Zanzibar na TANESCO na iwapo kuna sababu za msingi za kuendelea kuwepo kwa deni hilo na athari zake kwa  Maslahi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika :
Utaratibu wa Kazi
Utaratibu uliyotumika katika kuzifanya kazi Hadidu Rejea zilizohusika, Kamati ilifanya majadiliano na Uongozi wa Shirika kuhusiana na hoja mbali mbali; iliamua ni maeneo gani ya kutembelea pale ilipohitajika kufanya hivyo, ambapo kwa kuanzia Kamati ilianza kufanya kazi Kisiwani Pemba. Kuanzia Tarehe 30/04/2012 hadi tarehe 05/05/2012, na kuendelea Unguja kuanzia tarehe 7/05/2012 hadi 11/05/2012 ambapo ni awamu ya mwanzo na baadae kazi ziliendelea kwa awamu tofauti kwa mnasaba wa ruhusa ya Spika, na hatimae zilimalizika tarehe 01/10/2012, wakati Kamati ilipokutana na TANESCO.
Mheshimiwa Spika :
Katika kutekeleza majukumu yake, wakati Kamati inapokutana na Uongozi wa Shirika, ilianza kazi zake kwa kuzungumza na wafanyakazi wote wa Shirika kwa kuwa na mikutano nao kwa ujumla wao kwa pande zote mbili, Unguja na Pemba. Mbali na Wafanyakazi, pia Kamati ilipokutana na Managementi ya Shirika, iliendelea na tabia hii ya kujitambulisha kwao pamoja na madhumuni ya kazi zake na hatimae kuendelea na kazi.
Mheshimiwa Spika :
Katika mikutano hiyo ya wafanyakazi kwa ujumla wao, kuna baadhi ya mambo yaliyojitokeza ambayo yalinasibika na kazi ambayo Kamati iliiendea. Kwa mfano katika mkutano wa wafanyakazi wa Pemba baadhi ya mambo yafuatayo yalijitokeza :-
    1. Manunguniko ya nafasi za masomo Pemba zinatolewa kwa upendeleo.
    2. Ubadhirifu katika suala zima katika Uungwaji wa Umeme.
    3. Pesa za likizo kwa wafanyakazi wa Shirika, hutolewa kwa upendelo.
    4. Kuna upendeleo katika nafasi ya ajira kwa wafanyakazi wanaoajiriwa kwa muda, kutoajiriwa katika Mikataba ya kudumu ukizingatia kwamba, nafasi za ajira zinapotokezea, Shirika linachagua na kuajiri watu wengine huku likiwaacha wale wenye uzoefu wa kutosha.
    5. Kamati imepokea malalamiko ya Vijana waliopeleka malalamiko yao kwenye Tume ya Utumishi Serikalini, kufuatia kutoajiriwa katika Nafasi ya Cashier wakati walioajiriwa katika nafasi hiyo hawana sifa na Uajiri wao umefanyika kwa misingi ya upendeleo.
    6. Suala la Kampuni ya GECCO kuwatumia baadhi ya wafanyakazi wa Shirika, wakati wa saa za kazi.
    7. Hofu ya wafanyakazi na hatma yao kufuatia kusuasua kwa Shirika.
    8. Uwepo wa makundi ya wafanyakazi kama vile Kundi la State Fuel na kundi la ZECO.



Mheshimiwa Spika :
Halikadhalika na kwa upande wa wafanyakazi wa Unguja ambao walikutana na Kamati Tarehe 7 Mei, 2012 nao walitoa madukuduku yao ambayo yalilenga kwenye maeneo yafuatayo :-
  1. Wafanyakazi hao walikuwa na wasiwasi na baadhi ya watendaji wenzao kwamba wanashiriki katika suala zima la uungwaji wa umeme usiofata sheria hasa kwa baadhi ya  miradi ya mahoteli ya kitalii.
  2. Walitilia mashaka juu ya matumizi makubwa ya Shirika kwa kuingia gharama zisizo za lazima, kwa mfano suala la kukodi gari ya kubebea nguzo za kuwekea umeme hasa baada ya ile iliyokuwa ikitumika kupinduka. Gari hilo lenye   Nam. za usajili Z 158 BE, limekodiwa kwa gharama kubwa ambazo zingewezesha kununua nyengine mpya.
  3. Waliielezea Kamati  kwamba, kuna upendeleo mkubwa katika utoaji wa nafasi za masomo, ambapo kuna baadhi ya wafanyakazi hupewa fursa hiyo kwa gharama kubwa bila ya kujali nafasi waliyonayo na mafunzo wanayoyasomea, wakati wafanyakazi wengine hawapewi fursa hiyo hata kama mafunzo wanayoomba ndio yanayooendana na aina ya kazi zao na yakiwa kwa gharama nafuu.
  4. Kuna uhamisho usiofata taratibu na unaoashiria chuki na aina ya sindikizo kwa baadhi ya wafanyakazi.
  5. Utata wa ajira hasa kwa baadhi ya watumishi, kwa mfano ajira ya Mhasibu wa Tawi la ZECO Pemba, lakini pia wafanyakazi walionesha wasiwasi wao pia juu ya ajira za watumishi  katika ngazi za Umeneja. Walikuwa wanajiuliza ni kwanini katika ngazi hizo watafutwe watu nje ya Shirika, wakiamini kwamba wenye sifa kama hizo na uwezo wapo.
  6. Kuna watumishi ambao wana elimu ya kutosha kwa baadhi ya fani lakini Shirika haliwatumii ipasavyo.
  7. Hakuna ushirikishwaji kwa wafanyakazi kupitia umoja wao, kiasi  cha kupendekezwa kwa Muundo wa Utumishi wa Shirika ambapo chombo cha wafanyakazi cha TWICO hakikushirikishwa.
  8. Wafanyakazi walionesha kutoridhika na Management ya Shirika.
  9. Kuwepo kwa makundi ya wafanyakazi baina kundi la State Fuel na kundi la ZECO.
10) Shirika hutumia fedha nyingi kwa safari za wakubwa, Vikao vya Bodi  ambavyo hazileti tija kwa Shirika.
11) Wasiwasi juu ya kiwango cha mshahara anaolipwa Mshauri wa Teknolojia
(IT Consultant) pamoja na Mkataba wake.
12). Kuna utaratibu usio wa kawaida wa mambo ya manunuzi kama vile vifaa vya matumizi ya Ofisi. Baadhi ya maduka yaliyopewa Tenda ya kuuza vifaa vya umeme hayana sifa.  Kuwepo kwa utata na sababu ya kukataliwa kwa nguzo za Kampuni ya SANA.
Mheshimiwa Spika :
Aidha, Kamati ilipata fursa ya kukutana na Meneja Mkuu pamoja na Wakuu wa Idara mbali mbali wa Shirika kwa nyakati tofauti. Katika vikao hivyo, wakuu hao wa Idara aghalabu walionesha kushutumiana kwa Idara moja kuzorotesha maendeleo ya Idara nyengine na Idara moja kuhujumu Idara nyengine.
Mheshimiwa Spika :
Kamati vilevile katika kuifanya kazi hii ilitumia Picha (kamera) pamoja na kurekodi maneno (Hansard) wakati wa mahojiano na wafanyakazi, halikadhalika kufanya marejeo kwa baadhi ya nyaraka za Shirika, Sheria mbali mbali pamoja na taarifa nyengine zilizopatikana kupitia Taasisi zilizohusika, ikiwa ni pamoja na Tume ya Utumishi Serikalini, na kupita kwa watu mbali mbali walioitwa na kuwasilisha ushahidi wao kwa Kamati.
Mheshimiwa Spika :
Kwa kuwa Kanuni zetu zinatutaka tutoe ufafanuzi wa Maudhui ya Ripoti zetu katika Sehemu ya Pili ya Ripoti, nawaomba Wajumbe wako wafungue ukurasa wa 9 wa ripoti, ili waweze kufahamu Maudhui kamili ya Ripoti yetu. Aidha, sehemu hii inasomeka kama ifuatavyo :
        
SEHEMU YA PILI :
UCHANGANUZI WA HADIDU REJEA ZILIZOKABIDHIWA KWA KAMATI:

HADIDU REJEA NAM. 1 NA NAM.2 :

  1.                      UPOTEVU WA FEDHA UNAOTOKANA NA UUNGWAJI WA UMEME UNAOFANYWA  NA WATENDAJI WASIO WAAMINIFU.

  1. SABABU ZA USUMBUFU WANAOUPATA WANANCHI WAKATI WA KUOMBA NA BAADA YA KULIPIA HUDUMA YA KUUNGIWA UMEME PAMOJA NA SUALA LA BEI KUBWA  WANAZOPEWA UKILINGANISHA NA BAADHI YA WATU, MAKAMPUNI YA MAHOTELI, MABENKI NA MAKAMPUNI YA MINARA YA SIMU ZA MIKONONI.

Mheshimiwa Spika 
Katika kuifanyia kazi hadidu rejea nambari moja ambayo ilihusu Upotevu wa fedha za Shirika unaosababishwa na uungwaji wa umeme unaofanywa na watendaji wasio waaminifu, Kamati iliona ni vyema kazi hii ikaifanya kwa pamoja na hadidu rejea nambari mbili, ambayo ilihusiana na Sababu za usumbufu wanaoupata wananchi wakati wa kuomba na baada ya kulipia huduma ya kuungiwa umeme pamoja na suala la bei kubwa wanazopewa ukilinganisha na makampuni ya minara ya simu za mkononi, mabenki na mahoteli.
Mheshimiwa Spika :
Hii ni kwa sababu dhana ya upotevu wa fedha kwa uungwaji wa huduma ya umeme  usiofuata taratibu, unaofanywa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu matokeo yake ni kuleta usumbufu kwa wananchi wakati wa kabla na baada ya kuungiwa umeme huo. Aidha, hali hii huwa nafuu sana kwa baadhi ya watu, Makampuni ya Mahoteli, Simu na baadhi ya Makampuni mengine. Ili kupata ufafanuzi wa kina kuhusiana na hadidu hizi zote, ripoti ya Kamati itajikita katika maeneo yafuatayo :
Mheshimiwa Spika :
Mapato ya Shirika la Umeme yanayotokana na uungwaji wa umeme:     
Kwa mnasaba wa maelezo ya hapo juu, inafahamika wazi kwamba, unapozungumzia mapato ya Shirika, hutaacha kuzungumzia suala zima la utoaji wake wa huduma bora kwa wananchi, huku suala hili huwa chanzo cha mapato mazuri ya Shirika, na kwa vyovyote vile huduma zake za msingi haziishii kwenye uungwaji na uuzaji wa umeme tu, lakini ili mauzo hayo yakamilike ni lazima huduma za malipo ziwe ni endelevu. Bila ya shaka kuzifanya huduma hizo kuwa endelevu maana yake ni kuwa na wateja waliopata huduma hiyo kisheria. Wawe wameomba kwa mujibu wa taratibu na wanalipa kwa utaratibu ule ule uliowekwa kutokana na matumizi yao halisi.
Mheshimiwa Spika :
Uungwaji wa umeme huo utakuwa ama kwa kuingiziwa ndani ya majumba yao au sehemu zao za biashara au kwenye maeneo ya uwekezaji au sehemu nyengine yoyote ambayo kisheria inakubalika kuwekwa huduma hiyo. Bila ya shaka katika kutekeleza kazi hii Shirika limejipangia utaratibu wa kufuatwa pamoja na  bei kwa ajili ya malipo ya kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika :
Madhumuni makubwa ya kuweka utaratibu huo, kwanza ni kujua idadi ya wanaotumia huduma hiyo, mahitaji  yaliyopo, huduma halisi zilizopo lakini jambo jengine kubwa zaidi ni suala la udhibiti wa mapato yanayotokana na malipo ya matumizi ya huduma hiyo. Shirika pia linaweza kuweka miundombinu yake vizuri katika kuhakikisha kwamba huduma hii inawafika wateja wengi na kwa urahisi, jambo ambalo litaliwezesha Shirika vilevile kukagua na kufanya matengenezo ya miundombinu hiyo kwa pale inapotokezea haja  ya kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika :
Katika utaratibu mzima unaohusu upangaji wa bei kwa ajili ya kuungiwa umeme, kumekuwa na tafauti ya viwango ambavyo ndivyo vinavyotofautisha malipo hayo. Bei hizo hutafautiana kwa njia mbalimbali;  hii hutegemea sana aina ya maombi ya  matumizi ya mteja ambae yeye mwenyewe anakusudia kuutumia. Madhumuni yake hayo ndio yatakayoonesha ni kiwango kipi kitakidhi mahitaji yake.  Kwa  mfano  wale  wenye kuhitaji umeme mkubwa (High Tension) malipo yao huwa tafauti na wale wenye kuhitaji umeme wa kiasi (Low Tension). Tafauti hii  pia  hutegemea na masafa ya eneo ambalo umeme huo unatarajiwa kuchukuliwa na pale ambapo unahitaji kufikishwa,  hii ina maana kwamba kwa ujumla wake huo, hesabu yake inajumuisha pamoja na  idadi ya vifaa vitakavyotumika katika kazi hiyo; kama vile nguzo, waya, vikombe, stay n.k (Kiambatisho Nam 1). Kwa tafsiri hiyo maana yake ni kwamba wateja wa Shirika wamegawika makundi makuu mawili; kuna Wateja wadogo na Wateja wakubwa.
Mheshimiwa Spika:
Kwa msingi huu, endapo utaratibu  uliopo utafuatwa na Shirika kwa maana ya Watendaji wake,  kama  ulivyowekwa,  basi Shirika litaingiza mapato kwa kiwango kikubwa, kwani wahitaji wa huduma hii ni wengi na kadiri msukumo wa maendeleo unavyowakumba wananchi wetu, na kwa vile kwa mujibu wa sheria Nam.3 ya 2006 imelipa mamlaka Shirika kuwa  ndio muuzaji pekee wa umeme hapa  Zanzibar, basi hapana shaka mapato hayo ni ya kudumu kwani hayana eneo jengine yanakokwenda. Kwa lugha nyepesi tunaweza kusema kwamba hii ni biashara isiyo na mpinzani.
Mheshimiwa Spika :
Utaratibu wa Kufatwa katika Uungwaji wa umeme:        
Ili Wajumbe wafahamu kuhusiana na Taratibu zinazotakiwa kufuatwa kwa kila mteja katika kuugiwa Umeme, ni vyema wakaisoma Ripoti yetu kutoka Ukurasa wa 11 hadi Ukurasa wa 12, ingawaje napenda kusisitiza kwamba, Kuna wateja wa aina mbili na taratibu zao zinalingana sana mpaka wakapata huduma ya umeme. Aidha, Shirika pia limetoa kibali maalum cha Kuruhusu Makampuni maalum kuuza vifaa vya umeme, kama inavyoelezewa katika Ripoti yetu katika ukurasa wa 12-13.
Mheshimiwa Spika :
Wateja waliotembelewa na Kamati:
Baada ya kufahamu aina za wateja wa Shirika na utaratibu wao wa kupatiwa huduma ya Umeme, Kamati imechagua baadhi ya Wateja wa Shirika na kuwatembelea. Imefanya hivi kwa lengo la kujiridhisha na kuona ukweli juu ya jambo hili linalohusu upotevu wa mapato ya Shirika katika eneo hili la utoaji wa huduma kwa njia ya uungwaji wa umeme na usumbufu wanaoupata  wananchi wakati wa kuomba huduma hiyo, iliamua kufika katika maeneo ambayo huduma hii inapelekwa, yaani walimo Wateja haswa, na ilifanya hivyo ili kuhakikisha kwamba Shirika linazifata kikamilifu taratibu walizojipangia wenyewe,  ambazo ndizo zitakazotoa hali halisi ya upatikanaji na udhibiti wa mapato yake. Kamati katika kulifanya kazi hili, iliwakagua baadhi ya Wateja wa Shirika katika Kisiwa cha Pemba na Unguja, na imeona ni vyema kutoa ufafanuzi ufuatao:


Mheshimiwa Spika :
Wateja husika:
Kwa mujibu wa Ripoti hii, tunapozungumzia Wateja Wadogo maana yake ni wale watumiaji wa huduma ya umeme wa kawaida (Low Tension), ambao mara nyingi huwa unatumiwa kwenye majumba na sehemu za biashara ndogo ndogo na za kati. Hivyo,  tunaanzia na maelezo yanayowahusu wateja hao wadogo walioko Kisiwani Pemba, lakini hata hivyo katika kuiweka sawa taarifa hii kwa upande huo tutakuwa na baadhi ya mifano ya wateja wakubwa.
Mheshimiwa Spika :
Yaliyojitokeza
Kwa kutambua tafsiri ya uhalali wa mteja kwamba ni yule aliefuata utaratibu ulioelekezwa ambao unajenga mazingira ya kumtambua kila mmoja, alipo na aina ya huduma anayoipata lakini pia malipo aliyolipa kwa ajili ya huduma hiyo na anayoendelea kulipa  wakati akiendelea kuitumia huduma hiyo, basi ni dhahir kwamba, anayekwenda kinyume na hivyo, maana yake ni kupoteza uaminifu wake kwa kutenda kosa hilo lakini pia anasababisha upotevu wa fedha nyingi kwa Shirika,  kwani kwa kutokufuata taratibu hizo  ndiko kunakosababisha kutokuwa  na usahihi wa kujua idadi halisi ya wateja wa Shirika na hivyo kulifanya kutoa huduma kubwa kwa malipo yasiyolingana na huduma yenyewe.
Kwa vile utendaji wa makosa hayo kamwe hautokamilika bila ya uwepo wa ushiriki wa  baadhi ya watendaji wa Shirika, kwa maana hiyo ni dhahir kusema kwa lugha nyepesi kwamba, Shirika lina baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu ambao wanalisababishia kupoteza mapato yake kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Spika :
Kutokana na ukweli huo, Kamati imebaini kwamba kuna baadhi ya Wateja kwa kushirikiana na baadhi ya Watumishi wa Shirika hawafuati taratibu katika upatikanaji na utumiaji wa huduma hiyo ya umeme, jambo ambalo ndilo linalosababisha upotevu mkubwa unaotokana na eneo hilo la mapato ambapo kuna  mambo yafuatayo yamebainika kujitokeza:-
  1. Kuna tofauti ya malipo kwa kazi zinazofanana, au wakati mwengine kazi kubwa kuwa na malipo madogo.
  2. Malipo halisi wanayolipa wateja kwa kazi hiyo ya kuungiwa umeme, hutofautiana na thamani  iliyopo kwenye risiti wanazoandikiwa.
  3. Kuwepo kwa upendeleo unaosababishwa na baadhi ya Watendaji wa Shirika katika kuunga au kutoa huduma za umeme kunakosababisha Wateja kuchelewa kuipata huduma hiyo ama huwapelekea Wateja hao kukata tamaa na kuwajengea mazingira ya kutoa rushwa.
  4. Kuna Malipo yanayolipwa na baadhi ya Wateja bila ya kupewa risiti kabisa.
  5. Kazi kubwa ya kuunga umeme kwenye minara ya simu za mkononi kupewa Kampuni binafsi badala Shirika kuifanya kazi hiyo mwenyewe.
  6. Baadhi ya Wateja kutumia huduma hii bila ya kusajiliwa na hivyo kutumia umeme bure. (Hawamo katika orodha ya Wateja wa Shirika).
Mheshimiwa Spika :
Baada ya kutaja maeneo yaliyobainika na Kamati kwa udhaifu wake mbali mbali, sasa ni vyema tukapata ufafanuzi wa maeneo hayo kama ifuatavyo :
Tofauti ya malipo kwa kazi inayofanana, au wakati mwengine kazi kubwa kuwa na malipo madogo.
Katika suala hili Kamati kwanza imefanya ziara ya kuwakagua baadhi ya wateja wadogo wa Shirika waliyoko Pemba, kwa mujibu wa sampuli iliyojipangia kama tulivyoeleza mwanzo, na katika kufanya kazi hiyo mifano ifuatayo imepatikana:-
Mheshimiwa Spika :
  • Kuna Nyumba ya Bw. Juma Mohd Dadi wa Chokocho ameunganishiwa umeme kwa masafa ya nguzo moja na Roof poll moja ambapo vifaa vyote ni vya Shirika, ameunganishiwa  Tarehe 22/2/2012 akiwa amelipia huduma hiyo kwa Sh. 442,593/-, wakati Bibi Zuhura Nassir Nassor wa Ngezi na yeye ameungiwa kwa hiyo hiyo nguzo moja na Roof Poll moja kama alivyofanyiwa mwenzake,  ametozwa jumla ya Sh.1,236,747.02 siku ya Tarehe 7/2/2012. Kazi hiyo imefanyika kwa mwezi huo huo mmoja. Halikadhalika nae Bibi Asha Ali Omar wa Madungu mwenye nguzo moja na Roof poll moja malipo yake ni Sh.442,593.22 ya Tarehe 2/3/2011. Kazi iliyofanyika mwezi mmoja tu baadae.
Mheshimiwa Spika :
Bw. Ussi Moh’d wa Michenzani yeye ameunganishiwa umeme kwa nguzo mbili na ‘Roof poll’ moja kwa Sh.194,000/- Tarehe 6/10/2008 wakati Ndg. Hamad Abdallah wa Matangatuani (Kifundi), ameungiwa kwa nguzo mbili na ‘Roof poll’ moja na malipo yake ni Sh.537,750/- kupitia risiti ya Tarehe 1/11/2011. Wakati Ndg.Khamis Ali Makame wa Tundauwa mwenye Akaunti namba DO 04015, ameungiwa umeme kwa kutumia nguzo mbili za Shirika kwa gharama ya Tsh. 506,824.16 zilizolipwa kwa risiti nambari 00000866800 ya Tarehe 31/01/2011.
Mheshimiwa Spika :
Malipo wanayolipa Wateja kwa kazi ambapo hutofautiana na thamani ya malipo yaliyomo kwenye risiti zinazotolewa.

Kamati ilifanya mahojiano na baadhi ya Wateja wa Shirika ambao walilalamika juu ya kupewa risiti hizo zenye tofauti na bei, ijapokuwa wengine hawakujali kufanyiwa hivyo kwani kwao wao walichokitaka ni kuipata hiyo huduma ya umeme tu, bila ya kujali kupata huko ni kwa njia au ni kwa gharama gani.
Mheshimiwa Spika :
Mifano ya Wateja waliopata kadhia hiyo ni:
    • Bw. Mohd Habibu Suleiman wa Kigongo (Wambaa) ameungiwa umeme kwa masafa ya nguzo kumi na mbili na amethibitisha mbele ya Kamati kwamba amelipa Shilingi Milioni nane (8,000,000/-), wakati risiti aliyopewa na Shirika ni yenye thamani ya Sh.167,320/- tu.
    • Mteja mwengine Ndg. Khamis Makame wa Tundauwa, Pemba, mwenye Akaunti Namba DO04015, ameungiwa umeme kwa kutumia nguzo mbili za Shirika, kwa gharama za Tsh. 506,824.16/- zilizolipwa kwa risiti namba 00000866800 ya tarehe 31/01/2011 na kiwango alicholipa kina utata, kwani kinaonekana ni kidogo kuliko uhalisia wa kazi yenyewe ilivyo (Angalia Ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa Shirika ya  Januari-Machi, 2012, ambayo ni Kiambatanisho Nam 2)
Mheshimiwa Spika :
    • Mteja mwengine ni Ndg. Amani Ibrahim Makungu, mwenye Hoteli ya Pemba Misali na mwenye Akaunti Namba, Ac. D O 03220 ameungiwa umeme mkubwa (Three Phase) kwa masafa ya nguzo kumi na nne. Risiti ya malipo yake zinaonesha amelipia Tsh. 2,052,696/- lakini yeye mwenyewe alikiri kwamba amelipa Tsh.37,720,000/- (na sio 2,052,696/-, lakini fedha hizo amezilipa katika Akaunti binafsi ya Ndg. Zakia Juma Azani, Mfanyakazi wa Shiriki kupita Akaunti yake yenye Namba 2022500868, iliyopo kwenye National Microfinance Bank (NMB) Tawi la Pemba. (Waheshimiwa Nawaomba Msome Ripoti yetu kuhusiana na kadhia hii, katika ukurasa wa 16 huku pia mkifanya marejeo ya Kiambatanisho Nam 3.

Mheshimiwa Spika :
  • Mfano wa Mteja mwengine ambao Kamati iliupata ni wa NMB Bank Chake Chake (Munawar House) ambae nae aliungiwa umeme huo uliotoka Posta  Madungu kwa masafa ya nguzo  kumi na moja (11) Ukiwa na waya  wa 50mm bunch cable na malipo yake yalikuwa ni Sh. 3,718,903.58 tu, wakati katika makisio ya gharama za kupatiwa huduma hiyo yalionesha wingi wa vifaa vilivyotumika pamoja na bei zake, lakini la kushangaza vifaa hivyo vimetoka kwenye Shirika.
Mheshimiwa Spika :
Hata hivyo, Kamati ilipata nakala nyengine ya makisio ya kuungiwa umeme kwa Mteja huyu ya tarehe 1/9/2010 ambayo ina thamani ya Sh. 14,889,047. Hapa kwa mara nyengine tena Kamati ilipata utata na kujiuliza ni kwanini Shirika  lifanye makisio hayo mara mbili kwa Mteja mmoja. (Inashangaza kuona kwamba  fomu yenye makisio makubwa huwa haiwekwi saini na aliyeitayarisha.) Hata hivyo, kilichoonekana na Kamati ni kwamba, tafauti inayowekwa baina ya makisio hayo mawili huwa ni kubwa  mno, kwa mfano wa fomu hii kuna tafauti ya Sh. 11,170,146.42/-, ukilinganisha na yale makisio ya mwanzo ya Sh. 3,718,903.58.
Mheshimiwa Spika :
  • Mteja mwengine ni Bw. Nassor Omar Abdalla wa Mgogoni Mpakani ambae nae amelipa gharama za nguzo moja kwa thamani ya Shs. 150,000/-, waya kwa thamani ya shs. 280,000/- gharama za kuungiwa umeme shs. 442,595/- na shs. 8,000/- ikiwa ni gharama za fomu ya maombi jumla ya malipo hayo aliyofanya ni Shs. 880,593/- wakati risiti alizopewa ni mbili, No. 28388 ya tarehe 19/4/2012 yenye kuonesha malipo ya shs. 442,593/- kama gharama za kuungiwa umeme na risiti No. 27043 yenye kuonesha malipo ya shs. 8,000/- ikiwa ni gharama za fomu za maombi. Kwa mahesabu hiyo maana yake ni kwamba, jumla ya Shs. 430,000/- zilizobakia zikiwa ni gharama za nguzo na waya hazikutolewa risiti zake. Nguzo hiyo na waya huo ni mali ya Shirika !
Mheshimiwa Spika :
  • Aidha Bw. Hemed Suleiman wa Konde nae amewekewa huduma hiyo ya umeme kwenye msikiti wa Msuka Mchikichini kwa kuunganishwa kwa nguzo saba. Kwa kazi hiyo alikiri kutoa shs. 3,000,000/- lakini risiti aliyopewa na Shirika ni shs. 213,000/-.
Mheshimiwa Spika :
  • Wakati mteja mwengine  Bw. Nassor Hamad Fadhil wa Msuka Mchikichini, alilipia nguzo tatu kwa jumla ya shs. 390,000/-. Akalipa tena Sh. 1,780,000/-  (Laki tano mara mbili hatimae Sh. 780,000/-) risiti aliyopewa na Shirika inaonesha thamani  ya  malipo ya Sh. 221,553/-. Hata hivyo baada ya kadhia yote hiyo umeme alicheleweshwa mno kuungiwa na laiti asingechukua hatua ya kutumia nguvu ya kudai chake, akitumia maneno yaliyoashiria kwamba asipoungiwa umeme huo  aibu kubwa ingetoka nje, basi ni dhahir hata kwa kulanguliwa huko alikofanyiwa,  asingeliupata umeme huo hadi leo.
Mheshimiwa Spika :
  • Nae  Bw. Rashid  Mbarouk  wa  Pandani  ambae  pamoja  na  kulipa  Sh.442,593/- ambazo zilikuwa ni gharama za kuungiwa umeme tu, lakini alitoa fedha nyengine zaidi ambazo ni shs 500,000/- ikiwa ni madai ya nauli za mafundi waliyomuungia. Fedha hizo zilizodaiwa kuwa ni nauli za watumishi wa Shirika hazikuwa na risiti, dai ambalo lilidaiwa  kwa nguvu kubwa na hatimae Mteja ambae ni mhitaji alizitoa. Madai haya ya Mteja yalitolewa mbele ya Kamati na Uongozi wa Shirika ukishuhudia, bila ya kupinga chochote.
Mheshimiwa Spika :
  • Katika mazingira hayahaya, Baobab Beach Bungalows/ Mr. Misali Kamati haikuweza kupata kitu chengine chochote zaidi ya risiti ya malipo yenye kuonesha malipo ya Sh. 2,164,050/- ikiwa ni kwa kazi ya kuunga umeme tu kwa madai ya kuwa vifaa ni vyake mwenyewe, lakini Kamati haikuweza kupata ushahidi wowote juu ya hilo zaidi ya barua ya mhusika yenye kutaja tu baadhi yake kama vile Transformers, H.T Poles, Cross Arms n.k. Kamati haikuweza kupata risiti za manunuzi yake wala vielelezo vyovyote vilivyonesha kuingia na kutoka kwa mali kwenye ghala, kama maelezo haya yanavyothibitika katika Kiambatanisho Nam 8 cha Ripoti yetu.
Mheshimiwa Spika :
    • Kamati ilipata utata kwa mteja mwengine anayejulikana kama Mnarani Kigomasha wa Makangale, mwenye nambari ya akaunti DO 02748. Tarehe 30/10/2009 aliarifiwa kwa barua yenye nam. ZECOP/P/T/VOL/06 kwamba, makisio yake yaliyohusiana na maombi ya kuungiwa kwa umeme kwenye eneo lake kwamba yamekubaliwa na alitakiwa kwenda kulipa jumla ya Sh.1,387,836/- na alifanya hivyo kupitia risiti nam. 005091102000313 ya Tarehe 2/11/2009.  Lakini baadae alifanyiwa makisio mawili tofauti kama ifuatavyo:
          Previous Estimate                                 Current Estimate
Tansformer
Installation         415,800.00                                         415,800.00

Construction
Of  l. V. Line    485,088.00                                         485,800.00

Construction
Of  H.T. Line    486,948.00                                         1,303,333.60 
           TOTAL  1,387,836.00                                    2,205,221.60   

Mheshimiwa Spika :
Kamati iliingiwa na wasi wasi juu ya mteja mmoja kufanyiwa makisio mara mbili tena kwa wakati tafauti uliopishana kwa mwaka mzima. Huku yakitofautia kiasi kikubwa cha bei baina ya makisio ya zamani na mapya. Huu si ndio usumbufu wanaoupata wananchi wetu?
Mheshimiwa Spika :
Kuhusu suala la kuwepo kwa upendeleo unaosababishwa na watendaji wa Shirika katika kuunga au kutoa huduma za umeme kunakosababisha wateja ama kukata tamaa au kuwajengea mazingira ya kutoa rushwa. Kamati imegundua kwamba, hali hii husababisha Shirika kupoteza au kukosa mapato kwani idadi ya wateja haiongezeki kwa kasi halisi kwani baadhi yao wanakaa muda mrefu bila ya kupata huduma, lakini wengine wanakuwa wazito kuomba huduma hiyo kutokana na kuona usumbufu wanaoupata wenzao. Wanapoamua basi hujilazimisha kutoa chochote ili waepukane na usumbufu huo. Kwa mnasaba huo na wale ambao huomba na kukamilisha taratibu za kisheria na kukaa tu huku wakisubiri majaaliwa ya Shirika maana yake ni kwamba, kwa muda wote huo wa kusubiri  ambao walikuwa tayari wawe wateja wa Shirika, hufanya Shirika hili kuwa limejipotezea mapato yake kwa makusudi kama wao wanavyowakosesha huduma wananchi hao.
Mheshimiwa Spika :
Kamati ingeridhika kama ingekuwa uchelewashaji huu una sababu maalum kama vile upungufu wa vifaa, hali ya hewa au miundombinu, lakini imebaini kwamba wala hakukuwa na sababu za msingi zinazopelekea matokeo hayo. Maana yake ni kwamba hayo hutokea kwa utashi tu.  Kwa lugha nyepesi ni kusema kwamba hili hufanywa kwa makusudi.
Mheshimiwa Spika :
Mfano wa ucheleweshwaji huo ni:-
  • Bw. Salum Makame Juma wa Mgagadu amejaza fomu na kulipa gharama zote zilizohitajika ambazo ni Sh. 554,729/- kwa risiti ya Tarehe 30/12/2011. Hadi Kamati inamtembelea Tarehe 3/5/2012 alikuwa hajapatiwa huduma hiyo, wakati Bw. Rashid  Mbarouk  Rashid wa Pandani mwenye mita No. 07101423916, ameomba Tarehe 18/1/2012  na kupatiwa huduma hiyo tarehe 23/1/2012  (Ndani ya siku tano) akiwa amelipia Sh. 442,593/- tena malipo aliyafanya Tarehe 24/1/2012. Yaani hata hayo malipo ya kuungiwa umeme huo, ameyafanya siku moja baada ya kupewa huduma hiyo. Mazingira hayo yamedhihirisha wazi kwamba Ndg. Salum Makame amecheleweshwa kwa makusudi.
Mheshimiwa Spika :
Kamati ilishangaa sana kuona kwamba Ndg. Salum ameomba kupatiwa huduma hiyo mwanzo (Mwishoni mwa mwezi Disemba, 2011) wakati Ndg. Rashid ameomba mwisho (Mwishoni mwa Mwezi Januari, 2012) kukiwa na tafauti ya mwezi mmoja tu, lakini alieomba mwisho amepata kabla ya wiki kwisha na yule wa mwanzo miezi mitano imepita hajapatiwa huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika :
Hivi kwanini tusiseme kwamba huduma hiyo inatolewa kwa upendeleo? Na kwa mazingira haya ni kiasi gani cha mapato ambayo Shirika linapoteza kwa kukosa kuongeza idadi ya wateja.   Sasa hebu kwa mfano, chukua malipo ya Tsh. 554,729/ anayotakiwa alipe mteja wa kawaida kwa lengo la kupatiwa umeme, kama alivyotakiwa Ndg. Salum Makame Juma, ambae hakupatiwa huduma hiyo, ukifanya kwa wateja 100 wanaohitaji kupatiwa huduma kama mwananchi huyu, ni wazi kwamba Shirika linapoteza Tsh.55,472,900/- kwa mwezi ama zaidi, huku Shirika hili likiendelea kupiga kelele za kukosa uwezo wa kulipa umeme kwa TANESCO ama kuendesha majenereta ya 32 ya dharura, kwa dai la kukosa fedha!
Mheshimiwa Spika :
Malipo yanayolipwa bila ya wateja kupewa risiti kabisa:
Pamoja na kuunga umeme, bado Shirika linaendelea kuwa na dhima nyengine ya kutoa huduma kwa wateja hasa pale ambapo huduma zile zinakosekana kwa uharibifu au maharibiko ya aina yoyote yasiyosababishwa na mteja. Mfano kuanguka kwa nguzo au kukatika kwa waya kwenye njia kuu za umeme na mambo mengine yanayolingana na hayo.
Mheshimiwa Spika :
Mfano wa matukio haya ni: -
  • Kuna nguzo 2 zilianguka kwa sababu ya ubovu, kwenye njia ya kwenda nyumbani kwa Bw. Mohd Habibu Suleiman wa Kigongo, lakini Shirika halikuchukua hatua  za mara moja pamoja na kujuulishwa mapema. Na matokeo yake alilanguliwa Tsh.340,000/- za nguzo na 170,000/- za Ufundi na watu waliojitambulisha wafanyakazi wa Shirika. Waheshimiwa ufafanuzi wa haya unapatikana katika ukurasa wa 27   hadi 28 wa Ripoti yetu.
Mheshimiwa Spika :
Kazi kubwa ya kuunga umeme kwenye minara ya simu za mkononi kupewa Kampuni binafsi:
Kamati ilitarajia sana kwamba Shirika lingeingia mkataba wa uunganishaji wa umeme kwenye minara ya simu za mkononi, ambapo Shirika lingefanya biashara kubwa na kuingiza fedha nyingi, lakini matokeo yake biashara hizo hupewa kampuni nyengine huku kampuni hizo hutumia rasilimali za Shirika kama vile wafanyakazi na magari. Kamati imepewa taarifa na Shirika kwamba Pemba, kuna jumla ya minara ya simu 49 kati ya jumla hiyo, minara 40 ni ya kampuni ya simu  ya Zantel, minara minne ni ya Kampuni ya simu ya TIGO, minara mitatu ni ya AIRTEL na minara miwili ni ya VODACOM.


Mheshimiwa Spika :
Kati ya minara hiyo ya kampuni ya simu ya Zantel ambayo ni jumla ya 40 kwa wakati huo ambao Kamati inafanya kazi, ni minara mitatu tu iliyoungwa umeme na Shirika la Umeme (ZECO), huku minara iliyobakia (yote 37) kazi hiyo ilifanywa  na kampuni ya GECCO. Na  kwa upande mwengine wa minara ya kampuni zilizobakia, (Minara 9 iliyosailia) minara ya mitatu (3) ilifanyiwa kazi hiyo na kampuni binafsi ya POMY na iliyobaki  ilikuwa ni kazi ya GECCO.
Mheshimiwa Spika :
Sasa tuendelee kutoa ufafanuzi wa hii minara mitatu ya Kampuni ya Zantel, iliyopatiwa huduma ya umeme na Shirika, kwamba kati ya hiyo mitatu, Mnara mmoja uliopo Kifumbikai, Wete umelipiwa Tsh.792,379.80  zikiwa ni gharama za nguvu kazi tu (Labour Cost) kwa ajili ya kuweka umeme kwenye mnara huo, ambapo gharama nyengine za vifaa husika zinazofikia  jumla ya Shs.3,247,400, hazikulipwa kwa Shirika na Kamati imepata maelezo ya kuridhisha kwamba, vifaa hivyo huuzwa na Kampuni binafsi ya GECCO wakati hata Shirika lingeliweza kuuza pamoja na kuvifunga vifaa hivyo. Ingawaje bado kuna haja ya kujiridhisha iwapo vifaa hivyo vimenunuliwa na Kampuni husika ya Zanteli na havikutoka katika mikono na umiliki wa Shirika. Suala hili lilihitaji ushahidi wa kina, ingawaje Kamati ilipatiwa majibu ya mdomo tu, huku ushahidi mwengine ukikosekana.
Mheshimiwa Spika :
Sasa tuchukue hizo gharama za Vifaa Tsh. 3,247,400/- tukijumlisha na gharama za nguvu kazi Tsh. 792,379.80/- ni sawa na Tsh. 4,039,779.80/- kwa mnara mmoja tu. Sasa ukizidisha minara 46 iliyofanyiwa kazi na Kampuni nyengine binafsi, ni sawa na kusema kwamba, Shirika limepoteza jumla ya Tsh. 185,829,870.80/- kwa minara 46 iliyoungiwa umeme na Kampuni binafsi.! Kama huu sio upotevu wa mapato ya Shirika, basi hakuna lugha nyengine yoyote ya kukidhi majibu sahihi ya hoja hii?
Mheshimiwa Spika :
Tukiendelea zaidi inafahamika wazi kwamba, Kibiashara kazi kama hizo zingelichukuliwa na ZECCO (SHIRIKA) basi fedha nyingi zingelipatikana. Lakini fedha nyingi zinakosekana kutokana na maamuzi hayo yasiyozingatia uwepo wa mapato zaidi ya Shirika, kwa madai eti halina uwezo wa kununua vifaa kwa ajili ya kazi hizo. Lakini dai jengine ni muda ambao mteja angetaka kukamilika kwa kazi yake ni jambo gumu kutokana na majukumu ya Shirika yalivyo.
Mheshimiwa Spika :
Kamati imepata mashaka juu ya maamuzi hayo ambapo yanaonekana kuelekea mno kutawaliwa na tamaa binafsi kuliko uhalisia wenyewe. Hasa ikizingatiwa kwamba wanaofanya kazi hizo za GECCO ni wafanyakazi wa ZECO. Muda upi wanutumia kwa ajili ya hayo majukumu ya ZECO na muda upi wanautumia kwaajili ya kazi za GECCO, jambo ambalo linaiwezesha GECCO kukamilisha kazi hizo kwa wakati na mazingira hayo hayaliwezeshi Shirika kufanya kazi hiyo na kuweza kukidhi muda unaotakiwa na wateja.
Mheshimiwa Spika :
Hebu tuchukue mfano wa Ndg. Hamidu Saidan Ali mwenye hisa 20 na Ndg. Ali Abeid Haji mwenye hisa 15 ni wafanyakazi halali wa Shirika la Umeme, pamoja na umiliki na kufanya kazi Kampuni ya GECCO, sasa ni wakati gani wanawajibika kwa bosi mmoja kati ya hawa? Jawabu ni nyepesi mmno kwa anaetaka kuelewa. Lakini hebu na tuzingatie ufafanuzi wa GECCO kuhusu Ndg. Habibu Moh’d Ali, mfanyakazi wa ZECO lakini hutumiwa na kulipwa fedha na Kampuni ya GECCO, pale wanapona wana haja ya kutumia vifaa ama huduma ya ZECO. Kubwa zaidi wanalofanya ni kumtumia mfanyakazi huyu kwa kuwasaidia kuwa kiunganishi bora katika majukumu yao. (Ufafanuzi zaidi wa suala hili, Nawaomba Waheshimiwa Wajumbe msome Ripoti yetu kuanzia Ukurasa wa 28 hadi wa 30)
Mheshimiwa Spika :
Baadhi ya wateja kutokuwemo kwenye orodha wa mafail ya wateja wa Shirika.
Kamati ilipata orodha ya watu/wananchi ambao wanatumia huduma hiyo ya umeme bila ya kusajiliwa rasmi kwenye mtandao wa wateja kwenye Shirika. Katika kutafuta ukweli juu ya jambo hili, Kamati iliarifiwa na Shirika lenyewe  Tawi la Pemba, kwa kukiri kwamba kuna Wateja ambao taratibu za uungwaji wa umeme wao zilikuwa na utata. Utata wao ulibainika wakati wa ukaguzi wa nyumba kwa nyumba uliofanywa na Shirika na kugundua Wateja Ishirini na Tatu (23) wanatumia umeme bila ya kulipia, lakini vilevile hawamo kabisa katika mfumo wa malipo ya Wateja wa Shirika.  Orodha ya Wateja ambao Kamati imekabidhiwa na Shirika kwamba wana utata, wametajwa katika ripoti yetu kuanzia ukurasa wa 31 hadi wa 32.

Mheshimiwa Spika :
Orodha hiyo bila ya shaka inaonekana dhahir kwamba ni wananchi wale tu waliokaguliwa tena kwa baadhi ya wale walioko Pemba tu, lakini kwa sababu si nyumba zote zilizokaguliwa, maana yake ni kwamba upotevu huo wa mapato ni mkubwa kwa uhalisia wake kuliko vile unavyoonekana sasa. Kwani Kamati inaamini kuna zaidi ya wateja hao walioainishwa ambao uungwaji wa umeme wao haukufata taratibu.
Mheshimiwa Spika :
Hata hivyo kama kuna wateja wa aina hii ambao uungwaji wa umeme wao haukufata taratibu maana yake ni kuwa, Shirika limekuwa likipoteza mapato yake kila siku kwani wateja wa aina hii si tu wamekuwa wakilikosesha Shirika mapato yanayohusiana na gharama za uungwaji tu, bali hata yale mapato yanayotokana na malipo ya kila mwezi.
Mheshimiwa Spika :
Sasa hebu tujikumbushe kiasi gani zinazopotea kwa Shirika kwa mfano wa wananchi tuliowataja hapo juu, huku tukijua kwamba, hiyo ni idadi ndogo sana ya wananchi wa aina hii. Na tutoe mfano wa mwananchi mmoja angelilipa Tsh. 8,000/- za Fomu ya maombi na malipo ya kuungiwa umeme kwa nguzo 1 tu na ‘Roof Poll, ambapo malipo yake ni Tsh. 442,593/-, Jumla ya malipo kwa mtu mmoja ni Tsh. 450,593/-. Sasa iwe kwa watu wote 23, ni sawa na kusema Shirika lingelipata malipo ya Tsh. 10,363,639/-. Ukiachilia mbali huduma hiyo ya malipo ya Fomu na Kuungiwa Umeme, lakini pia kuna malipo mengine yanayotokana na malipo ya kila mwezi kwa ajili ya huduma ya umeme yanakosekana.
Mheshimiwa Spika :
Kwa mfano kila mmoja kati ya wateja hao angelikuwa analipia kiwango cha chini sana cha malipo, Tsh.5000 kwa kila mwezi, basi Shirika lingelipata zaidi ya Tsh. 115,000/- kwa mwezi, ni sawa na kupoteza Tsh. 2,645,000/- kwa mwezi, ingawaje ifahamike wazi kwamba, kiwango tulichokisia hapa ni kidogo sana cha Tsh. 5000 kwa mwezi, wakati kwa kawaida wananchi hulipia zaidi ya Tsh. 20,000/- kwa mwezi.
Mheshimiwa Spika :
WATEJA WALIOTEMBELEWA UNGUJA:
Kwa upande wa Unguja Kamati ilikabidhiwa idadi ya Wateja Wakubwa wa Shirika, wenye Mahoteli na Kampuni mbali mbali wafikao 160, kama wanavyooneka katika Kiambatanisho Namba 15 cha Ripoti yetu. Na upande wa Wateja wa Minara ya Simu wanne, ambapo Zantel pekee inamiliki vituo vya Minara vifikavyo 48, TTCL vituo 27, TIGO vituo 17 na Celtel  14 ( Angalia Kiambatanisho Namba 16 cha Ripoti). Kwa kuzingatia wingi wa wateja hao, na muda mdogo uliokabidhiwa kwa Kamati, Kamati ilifanyia kazi baadhi yao (sampling) kwa kutembelea Wateja 21 wa Makampuni ya Mahoteli, huku mijadala kuhusiana na Minara ya Simu, ikijadiliwa kwenye vikao tofauti baina ya Kamati na Uongozi wa Shirika na mara nyengine Kampuni ya GECCO, ambao kama tulivyokwishaona upande wa Pemba, pia walihusika na utoaji wa huduma ya umeme kwa Kampuni hizo.
Mheshimiwa Spika :
Aidha, Kamati ilitumia siku 3 za ziara kwa kuwatembelea wateja hao 21 na hatimae, imejiridhisha zaidi kwa kupata ufafanuzi wa baadhi yao kama ifuatavyo:
Sea Rock:
Kamati kwanza ilitembelea eneo liliopo Hoteli hii, na kugundua kwamba imeungwa umeme bila ya taratibu. Kamati ilipata pia maelezo ya Uongozi wa Shirika kwamba, wao waligundua zamani kwamba ‘Sea Rock’ wameunga umeme bila ya ridhaa zao na kinyume na taratibu zilizopo, kwani kilichogundulikana umeme wa mteja huyu umeungwa na Kampuni kutoka Tanzania Bara, ambapo umeme huo ulichukuliwa kutoka ulipokuwepo ambapo ni masafa ya nguzo kumi hadi hotelini, vifaa vilivyotumika kama vile waya nguzo pamoja na Transforma vyote havikuhakikiwa na Shirika.
Mheshimiwa Spika :
Kwa heshima nawaomba Wajumbe wasome kadhia hii katika ukurasa wa 33 wa Ripoti.
Mheshimiwa Spika :
Kwa kusoma taarifa hizo, Wajumbe watafahamu kwamba, Mteja huyu pamoja na makosa aliyoyafanya, Shirika lilieleza kwamba hatua waliyoichukua ni kuipiga faini Kampuni hii. Hata hivyo, mnamo tarehe 25/03/2010, Shirika lilipokea barua kutoka kwa ‘Sea Rock’, kutaka kuunganishiwa ‘Transforma’ ya umeme Mkubwa wa KvA 315, kupita line ya KV 33. Jambo la kushangaza ni kwamba, Shirika lilifanya kazi iliyoombwa, pamoja na ukweli kwamba, Mteja huyu amekiuka Sheria katika kujipatia umeme.
Mheshimiwa Spika :
Tunachotaka kuweka wazi katika ufafanuzi wa mteja huyu ni kwamba, Shirika halifahamu inachokifanya. Kama Mteja amevunja sheria kwa kujiungia umeme kinyume na taratibu, ni wajibu wa Shirika kusimamia Sheria zake na sio kumbembeleza mteja. Sasa kama mteja huyu anaachiwa, eti kwa kisingizio cha kuwapiga faini, ambayo imeshindwa kuthibitishwa na Kamati kwa kukosekana kielelelezo kinachothibitisha, kama vile pia ilivyoshindikana kuthibitisha uwezo wa Shirika kisheria kutoza faini, kitu ambacho kwa mujibu wa kifungu cha 39(1) cha Sheria Nam.3 ya 2006, pamoja na kutajwa adhabu ya faini kwa anaeiba umeme ama kufanya makosa yanayowiyana, basi uwezo wa kutoa adhabu hiyo kwa mujibu wa Sheria ni wa Mahakama na sio Shirika hili!.
Mheshimiwa Spika :
Kwa lugha nyengine, Kamati imejiridhisha kwamba, kuna upotevu mkubwa wa mapato ya Shirika, na pia husababishwa na uzembe na usimamizi mbovu wa dhamana za watendaji wa Shirika, waliokabidhiwa dhamana husika. Hebu kwa mfano tuchukulie mteja huyu pamoja na umeme mkubwa aliotumia, pamoja na wingi wa vifaa vilivyotumika na mambo mengine, fedha yake ya kupewa huduma iliyoingia katika Shirika ni Tsh. 12,132,760/- pekee ya gharama za nguvu kazi pekee, huku hata fedha ya malipo ya fomu, Tsh. 12,000/- zikishindikana kuthibitishwa kwamba zimelipwa.
Mheshimiwa Spika :
Ras Kichanga:
Mteja mwengine ambae Kamati imepata nafasi ya kuhojiana na Uongozi wa Shirika, ni kuhusiana na hoteli ya Ras Kichanga, iliyopo Michamvi, Mkoa wa Kusini Unguja. Wakati Kamati inafanya ziara katika eneo hilo, iligundua kwamba, kuna ‘Transforma’ ambayo ni mali ya Hoteli, nguzo 2, huku umeme katika hoteli hii unaaminika kwamba umeungwa mwaka 2004. Kuhusiana na utaratibu wa maombi kwa Mteja huyu, Kamati imeshindwa kupata uthibitisho wa barua yoyote ya maombi na hivyo imeshindwa kupata uthibitisho wa kujazwa kwa fomu ya maombi ya Mteja huyu. Kwa lugha nyengine taratibu za kuungiwa umeme kwa mteja huyu zimekiukwa.



Mheshimiwa Spika :
Tatizo liliojitokeza kuhusiana na suala hili ni kukosekana kwa faili lenye vielelezo vilivyohitajika. Kosa kubwa la Shirika ni kupoteza kumbukumbu za wateja wake, kama tutakavyoeleza suala hili hapo baadae.
Mheshimiwa Spika :
Mwamba Investment:
Hoteli hii pia iko Michamvi na imepatiwa huduma ya umeme. Kiasi ya nguzo 15 zimetumika kuutoa umeme katika sehemu moja hadi katika eneo la hoteli, huku Mteja huyu akitumia ‘Transforma’ yake mwenyewe, kama vile Kamati ilivyoelezwa kwamba, wateja wote wakubwa huwa wananunua transforma zao wenyewe kupitia Shirika la Umeme. Kampuni hii imepeleka maombi yake tarehe 14/09/2009, na kujaza fomu ya maombi tarehe 15/10/2010, na hatimae imenunua vifaa pamoja na kufanya malipo kama inavyotakiwa. Kamati imejiridhisha kwamba, Kampuni hii imejitahidi sana kufuata taratibu zilizowekwa na Shirika, na hata malipo yake yamefanyika bila ya shaka yoyote.

Mheshimiwa Spika :
Atlas Hotel:
Kwa Kampuni hii, Kamati imejiridhisha kwamba vielelezo vyote vilivyotakiwa na taratibu zilizohitajika zimefuatwa, ingawaje imetia wasi wasi kwa Kampuni vilikonunuliwa vifaa vya umeme vilivyohitajika, ambayo ni Sun General Supply, kwamba haimo katika orodha ya Kampuni zilizoruhusiwa na Shirika, kutoa huduma ya kuuza vifaa vya umeme.
Mheshimiwa Spika :
Aidha, wakati Kamati inakagua risiti zilizoambatanishwa katika faili hilo, haikuweza kupata taarifa za gharama ama manunuzi ya nguzo. Wakati inaamini nguzo hizo hazikununuliwa na kutoka katika Shirika la Umeme, ingawaje pia haikuthibitishwa wapi zimepatikana. Kamati imekuwa na wasi wasi kwamba, nguzo hizi yawezekana zimetoka katika Shirika, kinyemela!
Mheshimiwa Spika :
Kae Funk Sunset Beach:
Hii inahusika na Bungalow inayomilikiwa na Ndg. Eddie T. Mattar. Kamati ilipofika eneo liliopo Bungalow hii, Uongozi wa Shirika ulishangaa na kusema kwamba, mteja huyu hayumo katika orodha ya wateja wao. Kwa lugha nyengine, mteja huyu amejiungia umeme kinyume na taratibu. Aidha, Kamati imeshuhudia zaidi ya nguzo 30 feki, zimetumika kusambazia umeme katika Bungalow hii. Hata hivyo, wakati Kamati ilipofanya mahojiano na Uongozi wa Shirika kuhusiana na Mteja huyu, walikiri kwamba ni mteja wao halali mwenye nambari ya hesabu D36888, ingawaje wameshindwa kuthibitisha maombi yake, na namna alivyoruhusiwa kupatiwa huduma ya umeme.
Mheshimiwa Spika :
Kwa ufupi tuseme kwamba, huyu ni mteja feki wa Shirika, aliejiungia umeme bila ya kufuata taratibu zilizowekwa lakini pia amepoteza mapato ya Shirika, ingawaje Shirika lenyewe baada ya kumchukulia hatua za kisheria, bado linaendelea kumbembeleza na hatimae kufuga wizi wa meme, huku wanachokilipa mara nyingi huingia katika mifuko ya watendaji wachache wa Shirika. (Waheshimiwa Wajumbe, mtapata taarifa hizi kwa undani kwa kusoma Ripoti yetu, ukurasa wa 37-38)

Mheshimiwa Spika :
The Residence (The Hotel Property):
Mteja mwengine asiefuata taratibu za Shirika ni Kampuni hii, inayomiliki hoteli kubwa ya kitalii eneo la Kizimkazi Mchangamle, na imeungiwa umeme kwa thamani ndogo sana kulinganisha na wateja wengine kwani imetozwa Tsh. 2,311,733/- tu, huku takriban nguzo 46 zimetumika. Pamoja na Shirika kueleza kwamba, wao kama Shirika wamehusika na malipo ya ‘labour charge’. Aidha, Kitendo cha Shirika kusema kwamba aliyewapatia huduma ya umeme kwa takriban 46 kutoka bara bara kuu, kinapingana na maelezo kifungu cha 4(a) cha Sheria ya Shirika la Umeme, Namba 3 ya mwaka 2006, inayoeleza kwamba, Shirika hili ndilo pamoja na kazi nyengine, litasambaza umeme huo kwa Mtumiaji ama Mteja yoyote hapa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika :
Kendwa Beach Resort:
Barua ya maombi ya mteja huyu haikupatikana wakati wa ukaguzi wa Kamati. Aidha, kilichoweza kupatikana ni fomu ya maombi ya kuungiwa umeme, FORM 01, huku fomu ya masharti ya usambazaji (conditions of supply), ikishindwa kutiwa saini wala kujazwa chochote. Aidha, FORM B imeonekana, lakini hakuna uthibitisho wowote wa malipo yaliyofanyika kwa mteja huyu, kulipia maombi hayo. Mnamo tarehe 24/10/2011 ilipokelewa barua ya mteja huyu akiomba kubadilishiwa transfoma, huku malipo halisi ya mabadiliko hayo ni Tsh. 1,488,452/- kama inavyothibitika katika Kielelezo kinachohusika na hoja hii.
Mheshimiwa Spika :
Docrim Hotel:
Na Hoteli hii nayo imeunga umeme bila ya kupeleka maombi ya kufanya hivyo. Hata hivyo, kwa kigezo cha kujaza fomu, Hoteli hii pia haijajaza fomu hizo kisheria. Kwa maana fomu ya usaili, FORM 01, haina saini yoyote ya kuthibitisha imejazwa kisheria. Aidha, fomu inayohusiana na masharti ya kuungiwa umeme, ndio haijajazwa kabisa. Hata hivyo, FORM B ndiyo iliyojazwa huku ikikosa saini za Mkuu wa Upimaji na Mkuu wa Sehemu ya Mita na badala yake imepata kibali cha Mkuu wa Mains na Msimamizi wa kazi za uvutaji wa ‘Main Service line’. Aidha, fomu hiyo  inaonesha makisio ya kuungiwa umeme huo ni Tsh. 14,171,564/- ambazo ni nyingi sana ukilinganisha na wateja wengine, kama vile The Redisence ama ‘The Hotel Property’, wakati mteja huyu ameungiwa umeme kwa takariban nguzo 15  za Shirika.
Mheshimiwa Spika :
Shumbana Amani Karume:
Baada ya mjadala mrefu, ilikubalika kwamba, Ndg. Shumbana Karume ni Mteja Mkubwa, mwenye tranfoma ya 50 kVA, ambayo Kamati haikupata uthibitisho iwapo ameinunua kwa fedha zake na hatimae kujiridhisha kwamba imetoka kwenye Shirika. jambo la kushangaza ni kwamba, mteja huyu ametumia nguzo zaidi ya 31 kwa umbali unaokisiwa kuwa zaidi ya kilomita 2.5, huku hakuna uthibitisho uliowasilishwa kwa Kamati, kwamba nguzo hizo ni mali ya mteja, kama vile pia ilivyoshindwa kuthibitishwa kuuzwa na Shirika. Kwa lugha nyengine, gharama za nguzo hazihusiki na malipo yaliyofanywa na mteja, huku gharama alizolipa mteja huyu kwa ujumla wake ni ndogo ukilinganisha na huduma aliyopewa. (Ufafanuzi wa ziada, Waheshimiwa Wajumbe, angalieni ukurasa wa 40 wa ripoti yetu).

Mheshimiwa Spika :
The Seyyida Hotel:
Fomu za maombi ya umeme kupitia FORM 01 na FORM B, hazina uthibitisho wa saini ya Mkuu wa sehemu ya Mita wala Mkuu wa Mains; hivyo ni sawa na kusema fomu hizi hazina uthibitisho wa kisheria. Hata hivyo   jumla ya Tsh. 3,373,157.44 zimelipwa kwa kazi ya kufunga mita ya umeme pamoja na gharama nyengine zinazohusika. Kama ilivyo kwa wateja wengine, transfoma ya mteja huyu ni milki yake, ingawa wapi ameinunua na vipi Shirika liliithibitisha, ni jambo linaloendelea kuhitaji uthibitisho kwa sababu, Kamati haikupatiwa uthibitisho huo.
Mheshimiwa Spika :
Mteja huyu amesamehewa kodi ya VAT ya 18% sawa na Tsh. 514,549.44/- kati ya Tsh. Tsh. 2,858,608/-. Alizolipia huduma ya umeme, huku Kamati ikishindwa kupata maelezo yoyote mengine yanayohusiana na taratibu za kuomba msamaha huo, wala Mamlaka zenye uwezo wa kusamehe, hazijahusishwa. (Ni vyema Wajumbe mrejee ukurasa wa 41 wa Ripoti yetu).

Mheshimiwa Spika :
The Leisure Hotel:
Hakuna utaratibu wowote wa maombi ya umeme kwa mteja huyu, kama vile ilivyoweza kuthibitika fomu moja tu ‘FORM B’ inayoonesha angalau taarifa kadhaa na nia ya kuungiwa kwa umeme kwa mteja huyu. Makisio aliyofanyiwa ni Tsh. 1,387,752/- ingawaje hazihusiani na manunuzi ya vifaa, huku pia Kamati ikishindwa kukabidhiwa uthibitisho wa wapi vifaa hivyo vimenunuliwa.
Mheshimiwa Spika :
Larosa Deivent:
Hakuna barua yoyote ya maombi ya mteja huyu, huku pia hata fomu za kuungiwa umeme zilizomo katika taarifa zake, hazina saini yoyote wala taarifa zilizohitajika. Kwa lugha nyepesi, kuungiwa umeme kwa mteja huyu hakujafuata taratibu zilizohitajika. Makisio yaliyohusika na kazi hii ikiwa ni pamoja na ghama za baadhi ya vifaa bila ya kuhusisha Transfoma ni Tsh. 2,601,605/-. Tatizo linaendelea kuwa lile lile la kawaida, wapi imepatikana transfoma, kwa ushahidi upi, lakini jee Shirika liliikagua na kujiridhisha kufaa kwake? Vi masuala yaliyokosa jawabu mbele ya Kamati.
Mheshimiwa Spika :
One Stop Company:
Mteja mwengine wa Shirika ni Kampuni hii ya ‘One Stop’ iliyopo Forodhani, ambapo pamoja na kukosekana kwa barua yao ya maombi ya huduma ya umeme, wamejaza fomu zilizohusika kwa kazi hii na kupatiwa makisio ya gharama za umeme. Tatizo moja sugu ambalo hatukulieleza kabla ingawaje limeonekana sana ni makisio hayo kukosa saini ya ‘Operation Manager’ na badala yake ni ‘Planning Engineer’ pekee wa Shirika huandaa makisio hayo na kuyasaini, huku yakiwa hayajapata uthibati inayostahiki ya ‘Operation Engineer’.
Mheshimiwa Spika :
Makisio hayo yaliyogharimu Tsh. 6,341,556/- yamethibitishwa kulipwa kwa Shirika. Aidha, Kamati kwa mara ya kwanza katika wateja wote tuliowataja hapo juu, imejiridhisha kwa mteja huyu kuwa na ripoti ya majaribio ya ufungwaji wa umeme huyu (Consumer Installation Test Report), ambayo kwa ujumla wake inaonesha ni kwa kiasi gani Shirika lilivyotakiwa kufanya hivyo kwa kila mteja wake mkubwa, jambo ambalo wengine wamekosa kufanyiwa.
Mheshimiwa Spika :
Mafaili ya Wateja Wakubwa yaliyokosekana kukaguliwa na Kamati:
Ukiacha mbali taarifa za wateja tuliowazungumza hapo juu, na kwa mnasaba wa orodha ya wateja wakubwa tuliyoifanya Kiambatanisho cha ripoti hii, taarifa za wateja takriban 147 zimekosekana kwa kukaguliwa na Kamati, kwa maelezo kwamba, mafaili yaliyokuwa yanahifadhi taarifa hizo, yamerowa kwa mvua katika ofisi kongwe ya Shirika Mwanakwerekwe, kwa sababu bati la ofisi hiyo ni bovu na lilikuwa linavuja, pale inaponyesha mvua. Aidha, maelezo haya yametolewa, bila ya kujali uzito wa umuhimu wa taarifa za wateja hao, na hata kujali kwamba, taarifa hizo sio mali ya mtendaji binafsi wa Shirika, bali ni sawa na mali ya Serikali.
Mheshimiwa Spika :
Na unapofanya rejea ya Sheria zinazohusiana na nyaraka za Serikali, suala hili halitakuwa geni kwako na ingelistahili kwa Uongozi wa Shirika, kufahamu madhara wa wanachokifanya, ikiwa kwa makusudi kwa lengo la kuipotosha Kamati ama kuficha ukweli uliohusika ama kwa uzembe uliopelekea mafaili ya wateja kupotea. Hebu pia tukumbuke kwamba, kifungu cha 9 cha Sheria Namba 5 ya mwaka 1983, Sheria ya Usalama wa Taifa na Siri za Seriakali (The National Security and Official Secrets Act), pamoja na mambo mengine, kinakemea tabia hii ya Uongozi wa Shirika kupoteza taarifa za Serikali, ikiwa ni pamoja na uzembe uliofanyika hupelekea taarifa hizo kupatikana na watu wengine wasiohusika.
Mheshimiwa Spika :
ZANZIBAR DATA COM LTD:
Miongoni mwa wateja wakubwa wa Shirika la Umeme ni Kampuni ya Zanzibar Data Com, yenye mahusinao na Shirika kupita mnara wa Shirika uliopo Mtoni ambao umekodiwa na Kampuni hii. Suala hili lilianza kufahamika mara tu Kamati ilipoanza ziara ya kutembelea eneo la majenereta Mtoni, ambapo ilipohoji juu ya mnara uliopo pembeni mwa eneo hilo, iliambiwa ni mali ya Shirika, lakini umekodishwa kwa Kampuni hii. Kufuatia hili, Kamati ilitaka kuhoji juu ya umeme unaotumiwa na Kampuni hii, ambapo ilifahamishwa kwamba, Kampuni ya Zanzibar Data Com imekodishwa mnara kwa kuweka vifaa vyake vya matangazo, na kwa kuwa inatumia huduma ya umeme wa Shirika, ilipaswa kulipa na kuugiwa umeme huo kama wateja wengine. Ili kufahamu vyema kuhusiana na mteja huyu, ni vyema ukafuata utaratibu ufuatao:
Mheshimiwa Spika :
Mkataba baina ya Shirika na Kampuni ya Zanzibar Data Com Ltd:
Shirika limeingia Mkataba na Kampuni hii, kama ufafanuzi wake unavyopatikana katika ukurasa wa 43 wa ripoti yetu.
Mheshimiwa Spika :
Kitu cha msingi katika Mkataba huo ni maslahi ya ukodishaji (consideration), ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 2, Zanzibar Data Com inalazimika kulipia jumla ya USD 300, sawa na Tsh. 480,000 kwa mwezi na ni sawa na kulipia Tsh. 5,760,000/- kwa mwaka. Hata hivyo, kodi hii ilipaswa kubadilishwa kwa mnasaba wa mabadiliko ya soko na wakati husika, kwa kila baada ya miaka miwili, kwa makubaliano baina ya pande zote mbili, huku kiwango cha kodi husika, pia chaweza kubadilishwa kila mwaka. Na kwa sharti la kifungu cha 6 cha Mkataba husika, iwapo Mkodishwaji hatolipa kodi husika, Shirika litatoa taarifa kwake (notice) inayoelekeza malipo kufanyika (mara moja) na baada ya taarifa hiyo, Zanzibar Data Com inaposhindwa kulipa, Mkataba huu utakoma hapo.
Mheshimiwa Spika :
Ukweli kuhusu Malipo:
Pamoja na masharti ya Mkataba kuelekeza hivyo, Kamati imethibitishiwa kwamba, Kampuni ya Zanzibar Data Com, haijawahi kulipia Mnara iliyokodishwa kwake tangu ulipoanza kukodishwa, na ni sawa na kusema kwamba, pamoja na Kamati kutakiwa zaidi kuangalia upotevu wa Upotevu wa fedha za Shirika unaotokana na uungwaji wa umeme unaofanywa na watendaji wasio waaminifu, katika suala hili, imejiridhisha kueleza wazi kwamba, Shirika hili limekuwa likipoteza mapato mbali mbali kwa kutosimamia ipasavyo majukumu yake kwa mnasaba wa Sheria na Mikataba mbali mbali inayoingia.



Mheshimiwa Spika :
Hatua zilizochukuliwa dhidi ya deni linaotokana na kodi ya Mnara:
Pamoja na kutolipa kodi na kudaiwa deni la muda mrefu, Shirika halikuweza kuchukua hatua yoyote ya kisheria dhidi ya Kampuni hii, mbali na kumuandikia barua ambazo hazikuonesha umakini wa kulishughulikia suala hili (Waheshimiwa Wajumbe, ni vyema mkasoma ripoti yetu katika ukurasa wa 45-46 wa ripoti yetu).
Mheshimiwa Spika :
Malipo ya Umeme unaotumiwa katika Mnara wa Mtoni:
Mteja huyu hajalipia umeme aliokuwa anatumia katika Mnara wake, tokea mwezi wa Septemba 2009, kama inavyofafanuliwa kwa kina katika Ripoti yetu, ukurasa wa 46 hadi 47. Hili limethibitishwa mbele na Uongozi wa Shirika, lakini pia hakuna ushahidi wowote mwengine uliopatikana kwa Kamati, ulio kinyume na ufafanuzi wetu huu.



Mheshimiwa Spika :
Utumiaji wa huduma ya umeme katika mnara wa kampuni ya Zanzibar Data
com, Masingini-Unguja:
Mbali na kukodi mnara wa Mtoni kama tulivyoeleza hapo juu, Kampuni hii pia imekodi mnara katika maeneo ya Masingini, ingawaje mnara huu hauko katika milki ya Shirika, lakini huduma ya umeme inayopatikana kwa Kampuni hii katika kuendeshea mitambo yake ya intaneti katika mnara huo, inatolewa na Shirika.
Kama ilivyotabia yake, Kampuni hii haikuwa ikilipa madeni yake na ndipo walipokatiwa na Shirika, lakini Uongozi wa Kampuni uliomba kupatiwa umeme kutoka katika minara ya jirani, ikiwa ni pamoja na Mnara uliokodishwa kwa Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo, lakini ilikataliwa kwa sababu Kampuni hii ya Tigo ilikuwa inajua wajibu wake kisheria kwamba, wao kwa kuwa wateja wa Shirika la Umeme la Zanzibar, hawana uwezo wa kumruhusu mtu ama taasisi wala Kampuni yoyote kutumia umeme kinyume na taratibu zilizowekwa.

Mheshimiwa Spika :
Jambo la kushangaza wakati Kamati inafanya ziara katika eneo la tukio, ilikuta Kampuni hii inatumia umeme kutoka Mnara wa Shirika la Utangazaji la Zanzibar(kama ilivyokuwa inafahamika kwa jina la TVZ), Shirika ambalo bajeti yake inapitishwa kupitia pesa za walipa kodi na kuidhinishwa na Baraza la Wawakilishi. Tena basi, Taasisi hii ni ya Serikali iliyokubali kutoa huduma ya umeme kwa Kampuni binafsi, kinyume na taratibu za kisheria na taratibu za Shirika la Umeme.
Mheshimiwa Spika :
Kwa kuwa umeme huo ni wa wizi, Kamati Kamati iliagiza kukatwa kwa waya uliokuwa unapelekea umeme kutoka Mnara wa ZBC-TV hadi Mnara wa Kampuni hii, lakini baada ya siku 2 tu alirejeshewa huduma ya umeme, kwa kisingizio cha amefungiwa mita ya TUKUZA na deni lake la zamani kuhamishiwa katika mita hiyo mpya ya TUKUZA. Lakini haya yamefanyika kwa amri ya aliekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika, Ndg. Moh’d Hashim Ismail, kama inavyofafanuliwa katika ripoti yetu katika ukurasa wa 49.

Mheshimiwa Spika :
Kamati ilitumia busara ya kumwita Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Zanzibar, kwa ajili ya kufanya mahojiano nae,lakini hakuweza kufika kutokana na dharura, na hatimae aliwakilishwa na Kaimu Mkurugenzi, Ndg. Rafii ambae alikiri kulifahamu tatizo hilo na alieleza kwamba, kwa mujibu wa taarifa za mafundi wao, tatizo hilo lilianza tokea January 2012, ingawaje yeye alilitambua tatizo hilo kuanzia tarehe 09/05/2012, baada ya Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Mhe. Said Ali Mbarouk, kutembelea eneo hilo ambapo nae pia kama ilivyofanya Kamati, aliagiza kukatwa kwa huduma hii ya wizi, kinyume na taratibu dhidi ya Kampuni ya Zanzibar Data com, lakini agizo lake halikutekelezwa.
Mheshimiwa Spika :
Kufuatia hatua hii, Kamati ilimwita aliyekuwa Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika na yeye alikiri kwamba ameagiza kwa njia ya barua na kueleza sababu kumbwa ni kipaumbele kinachotakiwa kupewa kwa wawekezaji, yaani Kampuni ya Zanzibar Data Com ni mwekezaji na akipatiwa umeme, mapato ya Serikali yataongezeka.

Mheshimiwa Spika :
Hoja hizi zote hazina mashiko mbele ya Kamati, kwanza Kamati inaamini Mwenyekiti huyu hana mamlaka ya kuagiza kurejeshewa umeme mteja yoyote anaekiuka taratibu za Sheria. Wala maamuzi aliyoyatoa ama agizo halina uhalali kisheria. Kwa sababu Mwenyekiti alipotoa agizo hilo, alilitoa kama yeye (in persona) wala hajalitoa kwa kupitia Bodi ya Wakurugenzi, na hata kama angelipita kwa Bodi, ingekuwa ni sawa na kutumia mamlaka isiyopewa kisheria.
Mheshimiwa Spika :
Aidha, hoja ya kuongeza mapato ya Serikali kwa kutumia mgongo wa cheo alichokuwa nacho cha Kamishna, Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), kwa makusudi na kuruhusu kupotea kwa mapato ya Shirika la Umeme, ambayo pia ni mapato ya Serikali, ni suala lisilo kubalika na linaonesha wazi kwamba, Ndg. Mohd Hashim hakuwa na mapenzi ya dhati ya Shirika na alikitumia cheo chake cha Uenyekiti kwa manufaa yake binafsi na manufaa ya Makampuni machache ya kibiashara, huku Shirika likiendelea kukosa mapato na kuwa katika hali mbaya ya kiuchumi na kupoteza imani yake kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika :
Wateja wa Minara ya Simu:
Kama tulivyokwisha eleza awali kwamba, miongoni mwa wateja wakubwa wa Shirika ni pamoja na Kampuni za minara ya simu, ikiwa ni pamoja na Zantel, Tigo, TTCL na Celtel. Pamoja na ukweli kwamba, Kampuni hizo ni chache, kwa upande wa kila Kampuni inamiliki vituo kadhaa vya minara, na kila mnara unatakiwa kuwa na umeme wake unaojitegemea. Hivyo, kwa tafsiri hii, kila mnara ni sawa na mteja halisi, mwenye kuhitaji umeme kwa kutumia mita yake, nguzo zake na hata transfoma ya kwake pekee.
Hivyo basi, katika idadi kamili iliyowasilishwa kwa Kamati, jumla ya vituo vyote vilikuwa ni 106, vilivyomilikiwa na Makampuni hayo tofauti tuliyokwishayaeleza, ingawaje Kamati imepata taarifa ya mafaili yasiyozidi 10 tu ya vituo vyote hivyo, huku jawabu ni ile ile kwamba yamerowa kwa mvua. Tunachotaka kusema kwa ujumla wake katika kipengele hiki ni kwamba, wateja hawa wanafanana sana na Makampuni ya Mahoteli tuliyoyaeleza hapo juu, huku taratibu za maombi na hatimae kupatiwa huduma ya umeme ni hizo hizo.
Mheshimiwa Spika :
Kazi ya kuunga umeme kwa Makampuni haya, hufanywa na Shirika la Umeme, lakini pia na Kampuni binafsi ikiwa ni pamoja na Kampuni ya GECCO. Yaani, pamoja na Sheria kuwataka Shirika pekee kuhusika na kazi ya ufikishaji wa huduma ya umeme kwa wananchi, kazi hizo zimekuwa zikifanywa pia na Kampuni binafsi kinyume na sheria.
Mheshimiwa Spika :
Mara nyengine hutokea Kampuni husika kuomba kibali hicho kwa Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme, (kama ilivyofanyika kwa Kampuni ya Pomy Engineering Company Ltd, na kuthibitishwa na Kiambatanisho Nam 31 cha Ripoti yetu), jambo ambalo sio tu linakiuka Sheria, lakini pia hupoteza mapato ya Shirika na kama kazi hizi zingelikuwa zinafanywa na Shirika pekee, kama maelekezo ya Sheria Nam. 3 ya mwaka 2006, basi lingeliweza sana kutotekeleza majukumu yake kwa udhati wa maslahi na ustawi wa wananchi.
Mheshimiwa Spika :
Mfano halisi unaweza kuupata kwa kufanya rejea ya Kituo cha Zantel kilichopo Matemwe chenye Akaunti Namba D 24488 pamoja na kwamba hakuna maombi yoyote yaliyofanywa na Kampuni ya Zanteli katika kupatiwa huduma ya umeme kwa matumizi ya umeme wa kituo hicho, na pamoja na ukweli kwamba, fomu ya Usajili iliyomo katika taarifa za mteja huyu haijajazwa kikamilifu wala hazina uthibitisho wa saini kuthibitisha kweli maombi yalifanywa ama malipo husika, bado mteja huyu ameweza kulipia Tsh. 23,491,995.60 kwa ajili ya kuweka Transfoma na kujenga laini ya phase 3 na kazi nyengine zinazohusika ikiwa ni pamoja na malipo ya kazi.
Mheshimiwa Spika :
Sasa chukua mfano huu tu kwa vituo vyote 106 vya Minara ya Simu Unguja pekee, ni sawa na kusema kwamba Shirika lingeliweza kuingiza jumla ya Tsh. 2,490,151,533.60 kwa wateja wanne tu wa Kampuni za Simu, mbali na wateja wengine. Lakini kwa kuwa kazi hii hufanywa pia na Makampuni binafsi, tena Kampuni msisitizo ukiwekwa kwa Kampuni ya GECCO ambayo wamiliki wake na wafanyakazi wake ni wafanyakazi wa Shirika, ni sawa na kusema, upotevu huu wa makusudi utaendelea kuwepo, kwa sababu ya mgongano wa kimaslahi uliopo.


Mheshimiwa Spika :
Akaunti za Shirika upande wa Tawi la Pemba vipi zinahusika na upotevu wa
fedha za Shirika:
Katika kupata uthibitisho zaidi wa vipi fedha za Shirika zinapotea, Kamati imeona ni vyema kuangalia kwa kina kuhusiana na ‘Accounts’ za Shirika, na imeonekana mfano mzuri wa kuzungumzia suala hili, ni ‘Accounts’ za Shirika, upande wa Tawi la Pemba. Ambapo tutaizungumzia Akaunti Namba 173 ambayo inahusika na Matumizi Mengineyo (Other Charges), na kwa ufupi, shughuli za kila siku kwa upande wa Pemba fedha zake hutokana na ‘Account’ hii, ambapo Ufafanuzi wake unapatika katika Ripoti yetu kuanzia Ukurasa wa 53 hadi 61.
Mheshimiwa Spika :
Kuanzia tarehe 25/08/2010, ‘Account’ ilikuwa inaingiziwa Tsh. 1,000,000/- kwa kila siku, utaratibu ambao umeendelea hadi tarehe 02/03/2011 ndipo ilipoanza kuingiziwa Tsh.2,000,000/- kwa kila siku ya mauzo, alimradi tu mauzo yaende vizuri.


Mheshimiwa Spika :
Jambo la kusikitisha, matumizi ya fedha hizo hayajakaguliwa na Mkaguzi wa Ndani, na Kamati ilipohoji suala hili ilielezwa kwamba, Shirika la Umeme kwa muda mrefu lina Mdhibiti mmoja tu wa Ndani, nae yupo Makao Makuu ya Shirika, Unguja na Pemba huenda mara moja angalau kwa miezi mitatu. Pamoja na melezo hayo, Kamati imejiridhisha kwamba, matumizi ya fedha hizo hayajakaguliwa hata mara moja na Mdhibiti wa Ndani, jambo ambalo linapelekea upotevu wa fedha husika.
Mheshimiwa Spika :
Napenda Waheshimiwa Wajumbe wafahamu kwamba, suala hili halikuwa bure bure, limeandaliwa kwa hujuma za makusudi kama ninavyotoa ukweli huu ufuatao:
Ndg. Mohammed Khamis Juma (Kilindi), ni Mfanyakazi wa Shirika  aliekuwa akifanya kazi za Ukaguzi wa Hesabu za Ndani (Internal Auditor) Tawi la Shirika Pemba. Mnamo tarehe 14/04/2012 alilishauri Shirika kuwa na utaratibu mzuri wa matumizi ya fedha zake, huku akionesha mapungufu kadhaa katika ripoti yake hiyo. Akimuandikia Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme na nakla ya ripoti hiyo ambayo ni Kiambatanisho Nam 33 cha Ripoti yetu, alitoa ushauri wa kina kupitia Idara zote za Shirika, ikiwa ni pamoja na Idara ya Fedha, Biashara, Utawala na Uendeshaji, kwa lengo la kuboresha utendaji wa Shirika, katika suala zima la matumizi ya rasilimali fedha za Shirika”
Mheshimiwa Spika :
Jee, Waheshimiwa Wajumbe wanajua kilichompata Mfanyakazi huyu, Kamati imethibitishiwa kwamba Meneja Mkuu wa Shirika, badala ya kuupokea na kuufanyia kazi ushauri wa kitaalamu wenye ukweli na nia safi ya kuendeleza Shirika, alichoamua yeyé na Menejimenti yake ni kumpa uhamisho wa kumleta Unguja, bila ya kumpangia kazi yoyote ya maana yenye kuendana na ujuzi wake, huku akiacha nafasi ya Mkaguzi wa Ndani Pemba, ikiwa tupu bila ya kujali umuhimu wa nafasi hiyo katika suala zima la kutunza rasilimali za Shirika. Kwa hali hii, nani atakaepinga kwamba, Meneja huyu badala ya kuwa na mawazo ya kuliendeleza Shirika, yeyé badala yake anajenga mazingira ya kulibomoa na kuendeleza matumizi holela ya fedha za Umma.


Mheshimiwa Spika :
Uchunguzi wa Hesabu kwa mwezi wa August hadi October, 2010:
Kamati imeangalia taratibu za fedha za Akaunti hii kama zinafuatwa kwa kuchukua mfano wa baadhi ya Hati za Malipo (Payment Vouchers), ili kujiridhisha iwapo huandaliwa kwa taratibu za sheria, lakini pia kwa kuangalia vielelezo vyake kama vimekamilika ama laa, ili kujiridhisha kwa kiasi gani Sheria za Fedha na Kanuni zake zinavyoelekezwa ipasavyo.
Mheshimiwa Spika :
Kamati imepitia Hati ya malipo ya tarehe 28/09/2010 inayothibitisha makubaliano ya huduma ya ulinzi na Kampuni binafsi ya ulinzi ya ‘Sunshine General Security Services’ katika kituo cha umeme cha Shirika kilichopo Tanga, na Kamati imejiridhisha kuwemo kwa barua ya maombi, ‘invoice’ pamoja na ‘Chaque’ ya malipo hayo kupitia Benki ya Watu wa Zanzibar. Hata hivyo, Kamati imeshindwa kupata risiti za mapokezi ya malipo yaliyofanywa na ni sawa pia kwamba imekosa kupata maelezo ya Benki (Bank Statement).

Mheshimiwa Spika :
Jambo kubwa zaidi ambalo halivumiliki, ni kukosekana kwa Mkataba ulioingiwa baina ya Shirika na Kampuni hii ya ulinzi. Kwa maana nyengine, mbali na Mkataba kuwa kielelezo muhimu cha kuthibitisha malipo yaliyofanyika, katika hati hii umekosekana na Uongozi wa Shirika umekiri kutokuwepo kwa Mkataba Pemba, na ukasema yawezekana upo Unguja, lakini mpaka tunaandika ripoti hii, Uongozi wa Shirika umeshindwa kuithibitishia Kamati kuwepo kwa Mkataba huo.
Mheshimiwa Spika :
Katika kuendelea na ukaguzi wa baadhi ya Hati za Malipo, Kamati imeikagua Hati namba 30 ya tarehe 20/09/2010 inayohusu nauli ya siku 2 kwa ajili ya safari ya Unguja na kugundua kwamba, Ndg. Ali Nassor Moh’d, Mfanyakazi wa Shirika la Umeme, Tawi la Pemba, alipata safari ya kikazi, kwenda Unguja kwa muda wa siku 2, na hivyo, aliombewa posho la safari na nauli ya kwenda na kurudi Pemba, lakini hamna vielelezo vinavyothibitisha matumizi ya fedha hizo, na hivyo vilivyomo baadhi yao ni vya udanganyifu.


Mheshimiwa Spika :
Aidha, Kamati imepitia Vocha Namba 15 ya tarehe 08/09/2010 inayohusu malipo ya fedha kwa ajili ya Wasafishaji kwa mwezi wa July na August, 2010. Malipo ya Vocha hiyo ya Tsh. 711,000/- yamelipwa kwa Wasafishaji kwa miezi ya July na August, 2010, bila ya kuwepo maombi ya kuomba kazi hiyo kutoka kwa wasafishaji hao ambao sio waajiriwa wa Shirika, na badala yake Maombi pekee yanayohusika kwao ni kuhusu malipo ambapo barua zao zimeandikwa na Ndg. Sufe M.Nassor, Mwangalizi wa Ofisi ya Shirika, Tawi la Pemba.
Mheshimiwa Spika :
Kamati pia ilifanya ukaguzi wa Vocha Namba 47A ya tarehe 27/10/20102 inayohusiana na malipo ya fedha kwa ajili ya ulinzi wa vituo vya Umeme vilivyopo Pemba, kwa mwezi wa October, 2010. Kwa ujumla katika Vocha hii, imeambatanishwa na ‘Invoice’ pamoja na risiti za malipo, walizolipwa Kikosi cha Valantia cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikifuatiwa na barua ya maombi ya fedha Tsh. 2,550,000/- kutoka kwa Ndg. Shaib H. Kaduara. Wakati Kamati inaipitia Vocha hii, kwanza imeshindwa  kuthibitisha uhalali wa maombi ya fedha hizo, ingawa zimefanyiwa maombi. Yaani, aliyomba na kuidhinisha fedha hizo ni mtu mmoja, yaani Meneja wa Tawi, Pemba. (Ufafanuzi halisi, Waheshimiwa tuangalie ukurasa wa 58 wa ripoti yetu).
Mheshimiwa Spika :
Kikosi cha Valantia, kikiwa ni kimoja kati ya Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kinapaswa kutoa risiti za Serikali ili kuthibitisha mapokezi ya fedha juu ya huduma za ulinzi wanazozitoa, lakini pia kuthibitisha uhalali wa mapato hayo kuingia katika Mfuko wa Serikali, kama zilivyo taratibu. Kwa kuwa Kikosi hiki hutoa risiti sawa na zile zinazopatikana kwa wauzaji wadogo wadogo wa mchele mitaani, Kamati imeshindwa kujiridhisha iwapo kuna uhalali wa malipo yaliyofanyika, lakini picha inayojengeka ni kuvuja kwa mapato hayo.
Mheshimiwa Spika :
Vocha nyengine iliyoangaliwa na Kamati ni hii ya tarehe 27/10/20103 inayohusu posho la wiki 2 kwa ajili ya kushiriki mafunzo, Unguja, ambalo walilipwa Ndg Ali Moh’d Ali na Ali Nassor Ali, wafanyakazi wa Shirika la Umeme, Pemba. Wafanyakazi hawa walilipwa Tsh. 3,800,000/- ikiwa ni posho la Tsh. 1,900,000/ kwa kila mtu, huku gharama za usafiri zikiwa ni Tsh. 160,000/-. Kamati imegundua kwamba, matumizi ya fedha hizo hayakuwa sahihi kwa sababu ya kupatikana kwa  vielelezo vya udanganyifu vilivyoambatanishwa na vocha hiyo. (Nawaomba Wajumbe wasome ukurasa wa 60 wa ripoti yetu kwa ufafanuzi zaidi).
Mheshimiwa Spika :
Pamoja na kuangalia Vocha za mwaka 2010, Kamati pia ilivutika kuangalia Vocha ya mwaka 2011, inayohusiana na malipo ya posho ya safari na nauli ya siku 2 kwa ajili ya kwenda Unguja kuhudhuria kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme. Malipo hayo alilipwa Meneja wa Tawi la Pemba, Ndg. Salim M. Saleh, kwa posho la Tsh. 300,000/- na Nauli Tsh. 180,000/- . Pamoja na Meneja huyu kulipwa fedha hizo, na pamoja na kwamba yeye ndie anaestahiki kusimamia matumizi bora ya fedha kwa upande wa Pemba, kwa bahati mbaya yeye mwenyewe ndie anaevunja taratibu hizo, kwa kutofanya marejesho sahihi ya matumizi ya fedha hizo.


Mheshimiwa Spika :
Kwa kuzingatia maelezo haya, inajenga khofu na wasi wasi kwamba, matumizi ya ‘Account’ hii yamegeuka sawa na chaka la kufichia maovu ya baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu. Kwani hata wewe unapata picha gani unapofahamu kwamba, akaunti hii hukusanya 2,000,000/- kwa siku, huku haina mkaguzi wa ndani wa kuikagua, wakati huo huo unafahamu pia kwamba, wakaguzi wake walifanyiwa vitendo vya makusudi kutoendelezwa kielimu ama kupata misuko suko kadhaa ya kikazi ambayo haina ulazima wowote, na kwa kuzingatia ukweli kwamba hata matumizi yake hayafuati ipasavyo taratibu za sheria zinazohusika, ni wazi na utakubaliana nasi kwamba, Akaunti hii imegeuka kuwa chaka la watendaji wasiokuwa waaminifu na hata wakubwa wa Shirika, kutumia fedha zake watakavyo wao.
Mheshimiwa Spika :
 Muhtasari wa Mambo yaliyobainika na Kamati kufuatia Uchunguzi wake wa
Hadidu hii Rejea:
  1. Baadhi ya Wafanyakazi wa Shirika, mfano ukitolewa kwa Ndg. Zakia Juma Azan, wanahusika na upotevu wa fedha na mal iza Shirika.
  2. Shirika linapoteza fedha nyingi kutokana na udhaifu wa huduma zake pamoja na kuibiwa na baadhi ya wafanyakazi wake wasio waaminifu.
  3. Wateja wengi wa Shirika wanapata usumbufu mkubwa ikiwa ni pamoja na kuibiwa ama kulanguliwa fedha zao, pale wanapohitaji huduma ya umeme kwa Shirika.
  4. Uongozi wa Shirika unakiuka maagizo ya Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika, kwa kuruhusu Kampuni binafsi ya GECCO kufanya kazi na kutoa huduma ambazo tayari Bodi imeshakataza kufanywa na Kampuni hiyo.
  5. Shirika limepoteza taarifa muhimu za wateja wake, na upotevu huo umesababishwa na uzembe pamoja na Uongozi kutojali umuhimu wa taarifa hizo.
  6. Viongozi wa Shirika badala ya kusimamia matumizi ya fedha za Serikali kama inavyotakiwa na Sheria za Fedha, wao hugeuka wa kwanza kukiuka masharti ya Sheria hizo.
  7. Kuna upendeleo na usumbufu dhidi ya wananchi wa kawaida na Makampuni ama watu uwezo katika kupata huduma za kuungiwa umeme kutoka Shirika la Umeme la Zanzibar.

HADIDU REJEA YA TATU:
TARATIBU ZA AJIRA KATIKA SHIRIKA ZINAZODAIWA KUWA ZA
UPENDELEO, UNGUJA NA PEMBA:
Mheshimiwa Spika :
Katika hadidu hii, Kamati ilitakiwa kuchunguza ukweli wa madai kwamba Shirika la Umeme, kwa upande wa Unguja na Pemba limefanya uajiri wa wafanyakazi wake kwa misingi ya upendeleo, yaani kuajiri kinyume na taratibu za kisheria lakini pia kwa misingi isiyo ya haki na upendeleo ama wa udugu au ubaguzi wa aina nyengine yoyote.
Mheshimiwa Spika :
Katika uchambuzi wa Hadidu hii rejea, Kamati imeona ni vyema ikaifafanua kwa kutumia mitindo miwili inayotofautiana. Wa kwanza ni kuchambua taarifa za Mfanyakazi mmoja mmoja kwa mujibu wa mwaka walioajiriwa, ambapo kazi hii imefanywa katika Uajiri wa mwaka 2008, kwa upande wa Pemba. Lakini kwa kuzingatia haja ya kufupisha ripoti hii (vyenginevyo, kurasa pekee za hadidu hii zisingelipungua 200 kwa sababu waajiriwa hao ni wengi), Kamati imeona ni vyema kwa kuanzia mwaka 2009 hadi 2012, kuzingatia mambo yaliyojitokeza kwa ujumla wake juu ya suala zima la Uajiri, kwani kwa kufanya hivyo, kunarahisisha wepesi wa msomaji kufahamu mambo hayo, kwa kuzingatia ukweli kwamba, takriban yanawiyana na yale yaliyofafanuliwa kwa mfanyakazi mmoja mmoja kwa mwaka 2008 katika Tawi la Shirika, Pemba.
Mheshimiwa Spika :
Katika kuifanyia kazi hoja hii, Kamati ilianza kukutana na Uongozi wote wa Shirika siku ya kwanza ya kazi, tarehe 30/04/2012 katika Afisi za Shirika, kikao ambacho kilitoa fursa kwa kila mfanyakazi mwenye maoni juu ya utendaji wa Shirika, aeleze bila ya woga namna Shirika linavyotekeleza majukumu yake kwa mnasaba wa Hadidu rejea zilizokabidhiwa kwa Kamati, hali iliyopelekea Kamati kupata mwanzo mzuri wa uchunguzi wake, kufuatia wafanyakazi hao kutoa ushirikiao mzuri na wa aina yake. Baada ya kikao hicho, Kamati ilikutana na Uongozi wa Shirika, kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa hoja hii, na ilihitaji Uajiri ulioanzia mwaka 2008 hadi 2012 na kwa hali hii, Kamati inaona ni vyema kutoa ufafanuzi wake kama ifuatavyo :
Mheshimiwa Spika :
Uhalali wa Uajiri na Taratibu zinazofaa kufuatwa na Shirika la Umeme
katika kufanya Uajiri :
Kwa kawaida, suala la Uajiri wa Wafanyakazi wa Serikali huratibiwa na Wizara inayohusiana na Utumishi wa Umma, na kwa hali hii, mtu yoyote ambae hajui mamlaka ya Shirika la Umeme na nafasi yake, angefikiria kwamba, uajiri wa wafanyakazi wa Shirika, ungestahiki ufanywe na Wizara hii kwa niaba ya Serikali, kwa maana Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Fikira hii, ingelihusika pia kwa zile Taasisi zinazojitemea, ambazo mbali na kupewa Mamlaka ya Uajiri, lakini taratibu za uajiri huo, huongozwa na Sheria Namba 2 ya mwaka 2011 na Kanuni zinazohusika na Utumishi. Ama mtu huyu huyu kama hakupatiwa ufafanuzi mzuri, angeona ni vyema Uajiri wa Wafanyakazi hawa, utokane na Tume za Utumishi za Serikali, kama zilivyoanzishwa na kifungu cha 117 cha Katiba ya Zanzibar na kifungu cha 33 cha Sheria Namba 2 ya mwaka 2011.
Mheshimiwa Spika :
Fikira zote hizi zinatofauatiana na uhalisia wa Shirika hili, kwa sababu, Sheria Namba 3 ya mwaka 2006 iliyoanzisha Shirika la Umeme la Zanzibar, imetoa mamlaka ya Uajiri na malipo ya stahili za wafanyakazi hao kupitia Bodi ya Wakurugenzi, iliyoanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria hiyo. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 10(b) cha Sheria hii, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika, ina jukumu la kuthibitisha Muundo wa Shirika na taratibu za kazi na kufanya maamuzi juu ya masharti na maelekezo ya Utumishi, Mishahara pamoja na stahiki nyengine zinazohusika za Wafanyakazi wa Shirika la Umeme.
Mheshimiwa Spika :
Vile vile, Shirika linatumia muongozo mkuu wa uajiri kupitia Kanuni za Utumishi za Shirika la Mafuta na Nguvu za Umeme, Zanzibar, muongozo ambao tumeufanya kuwa Kiambatanisho Nam 41, zilizoidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika, na kuanzia kutumika tarehe 01/07/2005. Kanuni hizi tayari zimeshafanyiwa marekebisho (First Draft) na Uongozi wa Shirika mnamo mwaka 2011, isipokuwa Kamati imefahamishwa kwamba, bado marekebisho hayo hayajapitishwa na Bodi ya Wakurugenzi, na kwa maana hii, Kamati pia haiwezi kuzitumia kwa sababu, bado hazijapata nguvu ya kisheria, ispokuwa ieleweke kwamba, kwa kuwa bado Kanuni za Utumishi za Shirika za mwaka 2005 zipo, itafahamika kwamba, hata katika ripoti yetu hii ndio tutakayoitumia kama ni muongozo sahihi unaoonesha taratibu zote za Uajiri katika Shirika.
Mheshimiwa Spika :
Baada ya kufahamu hivyo, na baada ya siku ya kwanza ya kukutana na wafanyakazi wote wa Shirika tawi la Pemba, Kamati iliamua kuifuatilia hadidu hii, kwa kufanya mahojiano na Uongozi wa Shirika, pamoja na kuwafanyia uhakiki wafanyakazi waliohusika na hatimae kufahamu mambo kadhaa, ambayo tutayaeleza mwisho wa hoja hii. Ni vyema sasa tufahamu namna wafanyakazi hawa walivyoajiriwa, kwa kupata ufafanuzi ufuatao:
Mheshimiwa Spika :
UTARATIBU WA AJIRA, SHIRIKA LA UMEME:
Kabla ya kupata maelezo ya wafanyakazi binafsi, ni vizuri tukafahamu utaratibu wa ajira katika Shirika la Umeme. Hali hii itatusaidia pia kufahamu kiini cha hoja hii na itakuwa ni rahisi kuelewa, iwapo kweli Shirika limekiuka taratibu hizo kwa uajiri ulioanzia mwaka 2008 hadi 2012, ama laa. Basi, na tuanze kwa kufahamu kwamba, maamuzi ya uajiri ni lazima yafanywe na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika, na hii ina maana kwamba, iwapo Uongozi wa Shirika chini ya Meneja Mkuu, utaona ipo haja ya kuajiri, ni lazima mapendekezo hayo yapelekwe kwenye Bodi ili iamue kukubali au kukataa ajira mpya. Na baada ya kutoa kibali, ni lazima nafasi hizo zitangazwe katika vyombo vya habari ili watu wenye sifa waweze kuomba. Aidha, baada ya matangazo kutoka, maombi yote ya nafasi za kazi katika Shirika, yanatakiwa yawasilishwe kwa Meneja Mkuu, ambapo baadae, waombaji wanaoonekana wana sifa, huitwa kwa ajili ya usaili na hatimae kupatikana wenye sifa nzuri zaidi zilizohitajika na waliofaulu usaili huo.
Mheshimiwa Spika :
Baada ya hatua hii, waombaji waliofaulu kabla ya kuitwa kwa ajili ya kuajiriwa, taarifa zao hupelekwa G.S.O kwa ajili ya Uhakiki wa Kiusalama (Vetting) na baadae wale wataoonekana hawana matatizo ya kiusalama, huitwa na kutakiwa kufanyiwa Uchunguzi wa Kidaktari (Medical Checking) na ndipo wasiokuwa na matatizo ya kiafya, huajiriwa kwa kuingia Mikataba na Shirika ikiwa ni pamoja na kujaza Fomu za Ardhihali ya Kuingia Kazini. Hatua hii inapokamilika, Uajiri huwa umefuata taratibu zilizokubalika kisheria. Baada ya kufahamu hali hii, ni vyema sasa tuendelee na Uajiri wa wafanyakazi hao kwa Upande wa Pemba kwa mwaka  2008 na hatimae tumalizie kwa kuangalia Uajiri wa Unguja na Pemba kwa mwaka 2009 hadi 2012, kama ifuatavyo :
Mheshimiwa Spika :
UAJIRI WA WAFANYAKAZI WA SHIRIKA-UNGUJA NA PEMBA
KUTOKA MWAKA 2008 HADI 2011/2012:
Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe wasome kwa kina ufafanuzi wa suala hili kuanzia ukurasa wa 62 hadi 102 wa ripoti yetu, ingawaje pia ni vyema wakafahamu mambo ya jumla jumla yaliyojitokeza kama ifuatavyo:
Shirika kuafanya Uajiri (Pemba) bila ya kutoa matangazo ya Nafas iza kazi:
Mheshimiwa Spika :
Kamati imejiridhisha kwamba, ukiachia mbali mwaka 2011/2012, Shirika na zaidi kwa upande wa Pemba lilikuwa linaajiri bila ya kutoa matangazo ya Nafasi za kazi kupitia vyomvo vya habari. Na badala yake, taarifa za Uajiri huo huwafika wananchi bila ya utaratibu rasmi unaotarajiwa. Aidha, Kamati imejiridhisha haya kwa kukosa uthibitisho wa kimaandishi ambao ungeliweza kutumika na kuthibitisha vyenginevyo.
Kuendelea kukiukwa kwa masharti ya Uwasilishaji wa Maombi ya Ajira,
Upande wa Pemba:
Mheshimiwa Spika :
Kama tulivyokwishaeleza awali, kwamba Kanuni ya 3(7)(a) ya Kanuni za Utumishi za Shirika za mwaka 2005, Maombi ya nafasi za kazi katika Shirika, yanatakiwa yawasilishwe kwa Meneja Mkuu wa Shirika, kwa kuzingatia utaratibu ulioelezwa. Kwa bahati mbaya sana kwa upande wa Pemba, Kamati imejiridhisha kwamba, maombi yote ya kazi yaliombwa kwa Meneja wa Tawi Pemba, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Mikataba ya Ajira kutofuata masharti yote ya kisheria:
Mheshimiwa Spika :
Jambo jengine ambalo pia ni maarufu kwa mikataba ya ajira iliyoingiwa baina ya Shirika na Wafanyakazi wake, ni kukosekana kwa Saini ya Meneja Mkuu wa Shirika. Hali ambayo inaifanya Mikataba hiyo kukosa ridhaa ya Shirika kama Muajiri na badala yake huwa na saini ya Muajiriwa pekee. Mfano wa Mikataba hiyo ni pamoja na Mkatabawa wa Ndg. Salma Juma Said, Mhasibu wa Shirika Tawi la Pemba, aliejiriwa tarehe 01/11/2009, ambao katika Ripoti yetu tumeufanya kuwa Kiambatanisho Namba 51.
Mheshimiwa Spika :
Jambo la kushangaza zaidi baadhi ya Mikataba hiyo imekosa hata saini ya Mfanyakazi husika. Hili linashangaza sana kwa Taasisi kubwa yenye umuhimu wa kipekee Zanzibar. Kwa mfano Ndg. Ameir Omar Rajab, Mwajiriwa wa Shirika upande wa Unguja, aliaejiriwa tarehe 03/03/2009, hajatia saini Mkataba wake wa ajira uliosainiwa kwa upande wa Mwajiri wake tarehe 09/03/2009. Kwa maana hii, Mkataba huu hauko halali kisheira. Na ikitokezea tatizo lolote la kisheria, Mfanyakazi huyu anaweza kukosa haki zake kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Spika :
Aidha, Shirika halifuati ipasavyo masharti ya sheria katika suala zima la Mikatba yake inayoingia na Wafanyakazi wake. Mfano Ndg. Ameir Omar Rajab, Msomaji Mita alieajiriwa tarehe 03/03/2009, Mkataba wake hauna saini ya Afisa wa kazi (Kiambatanisho Nam 52), huku Kamati ikisisitiza kwamba, kama Shirika lilikuwa halioni umuhimu wa kuweka uthibitisho wa Afisa wa kazi, basi kulikuwa hakuna haja ya kuweka uthibitisho wake katika Mikataba ya Kudumu ya waajiriwa, wakati hakuna saini wala uthibitisho wowote unaofanywa juu ya Mikataba hiyo.
Uthibitishwaji wa Kazini kutofuata Masharti ya Kanuni za Utumishi za
Shirika:
Mheshimiwa Spika :
Kanuni ya 12 ya Kanuni za Utumishi za Shirika za mwakwa 2005, inazungumzia Muda wa Majaribio (Probation Period), ambao unafafanuliwa kwa masharti tofauti baina ya Mkataba wa Kudumu na Mkataba wa Muda. Kwa upande wa Mkataba wa Kudumu, masharti yake ni muda wa mwaka mmoja, kama inavyonukuliwa hapa chini na kifungu cha 12(1) cha Kanuni hizo:
“Mtu anayeajiriwa kwa nafasi ya kudumu atalazimika kuwemo katika majaribio kwa muda wa miezi kumi na mbili kuanzia tarehe ya kuajiriwa”
Mheshimiwa Spika :
Kwa maana hii, Mfanyakazi huyu Ndg. Salma Juma Said, alieajiriwa tarehe 01/11/2009 kama inavyothibitika katika Mkataba wake wa ajira ya Kudumu, alitakiwa athibitishwe baada ya kumalizika mwaka mmoja wa majaribio ambao ni sawa na tarehe 01/11/2010. Jambo la kushangaza Mfanyakazi huyu amethibitishwa miaka miwili na takriban miezi minne baada ya kuajiriwa. Yaani amethibitishwa kazini mnamo tarehe 14/03/2012, kama inavyothibitika katika Kiambatanisho Nam 53 cha ripoti yetu.


Mheshimiwa Spika :
Kichekesho ni kwamba, Mfanyakazi mmoja anathibitishwa mara mbili katika nafasi hiyo hiyo aliyoajiriwa. Kadhia hii inahusiana na Ndg. Mwadini Buzi Mwadini, alieajiriwa tarehe 01/07/2009 kama Dereva na akathibitishwa kazi mnamo tarehe 17/06/2010 kupitia barua namba ZECO/PF/M.206 na haijatosha, akathibitishwa tena tarehe 14/03/2012, siku ambayo takriban wafanyakazi wengi walipewa barua zao za kuthibitishwa (Kiambatanisho Na 54).
Na Ndg. Abdul Moh’d Seif, aliajiriwa tarehe 01/07/2009 kama Dereva, alithibitishwa mara ya kwanza kama wenzake walioajiriwa mwaka huu Unguja, mnamo tarehe 30/06/2010 na akathibitishwa tena mnamo tarehe 14/03/2012 kama inavyothibitika katika Kiambatanisho Nam 55 cha ripoti yetu. Aidha, Mfanyakazi huyu hata saini ya Mkataba wake wa ajira kuonesha ridhaa yake ya kazi, ameshindwa kuitia katika Mkataba huo.



Udanganyifu wa Vyeti vya Kumalizia Masomo:
Mheshimiwa Spika :
Pamoja na kasoro ya kuajiriwa wafanyakazi bila ya kutangazwa na kuomba kwa misingi ya sifa halisi na uwezo wao, Kamati pia ilipitia vyeti mbali mbali vya wafanyakazi hao vinavyothibitisha kumaliza na kuhitimu masomo yao. Katika zoezi hili, kama ilivyothibitika katika miaka iliyotangulia, kuna baadhi ya wafanyakazi wameshindwa kuwasilisha vyeti asili vya masomo (Original Certificates), lakini pia wapo walioghushi vyeti hivyo. Kwa kuzingatia ukubwa wa ripoti hii, Kamati inapenda kutoa mfano kwa Ndg. Omar Ali Juma, alieajiriwa kama Fundi, kwamba ameshindwa kuwasilisha vyeti asili vya kumaliza masomo yake ya Sekondari katika Skuli ya Utaani, Pemba. Aidha, kadhia hii pia inahusika kwa Ndg. Moh’d Habib Iddi, aliewasilisha kopi ya Cheti cha Form III, bila ya kuwasilisha cheti halisi kilichohitajika na Kamati.
Kutotimizwa kwa sharti la Umri, kinyume na maelekezo ya Maombi:
Mheshimiwa Spika :
Tunafahamu kwamba, katika matangazo iliyoyatoa Shirika kwa waombaji wa mwaka 2011, lilihitaji kwa kila muombaji kwa mujibu wa nafasi atakayoiombea kutovuka umri uliowekwa. Jambo la msisitizo ni kwamba, umri huu umewekwa huku ukishurutishwa katika maombi, ili kumfanya Muombaji afahamu, na hatimae Shirika liweze kupata wafanyakazi wenye nguvu watakaoweza kulitumikia kwa  muda mrefu. Hata hivyo, sharti hili limekiukwa kwa kiasi kikubwa katika maombi ya waombaji na jambo la kushangaza ni Shirika, kukubali kuwaajiri huku kabla litoa sharti hilo, bila ya kuzingatia uhalisia wa waombaji. Kwa mfano, Ndg. Ali Haji Makame, alieajiriwa kama Afisa Manunuzi (Procurement Officer), alitakiwa asizidi miaka 32, ingawaje yeye ameajiriwa akiwa na umri wa miaka 34
Mheshimiwa Spika :
Aidha, suala hili pia linamhusu Ndg. Fadhil Makungu Is-Hak mwenye umri wa miaka 30, wakati nafasi yake ya kuajiriwa (Mechanical Technicians), ilitaka asizidi miaka 25 (Kiambatanisho Nam 68). Kwa mnasaba wa maelezo haya na ushahidi ulionukuliwa, ni wazi kwamba, Shirika halikuzingatia sifa ya Umri wa waombaji wake, kinyume na maelelezo yaliyotolewa katika matangazo ya maombi. Na kwa kuwa mamlka ya idhini ya Uajiri hufanywa na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika, huku Meneja Mkuu na watendaji wenzake ni watekelezaji wa maagizo ya Bodi, ni wazi kwamba, wamekiuka maelekezo hayo, na picha inayojengeka ni kwamba, Uongozi wa Shirika hutekeleza majukumu yao kinyume na maagizo ya Bodi.
Kutoridhika kwa baadhi ya Walioitwa katika Usaili, kwa hoja ya Upendeleo na Ubaguzi:
Mheshimiwa Spika :
Shirika pamoja na nafasi nyengine za ajira kwa mwaka 2011, liliajiri ‘Cashiers’ nafasi 3 ambao ni Ndg. Tauhida S. Salum; Ndg. Adnan A. Moh’d na Ndg. Moh’d H. Moh’d. Kufuatia hali hii, Ndg. Mrzuk H. Marzuk na Ndg. Rashid K. Shimel waliokuwemo katika Usaili na hawakufanikiwa kuajiriwa, walilalamika kwa kupeleka barua Tume ya Utumishi, Serikalini, kwa lengo la kufanywa uchunguzi wa kina juu ya suala hili.
Mheshimiwa Spika :
Tume ya Utumishi Serikalini nayo ilipokea malalamiko hayo na kuyashughulikia, lakini ilikuja na maamuzi kwamba, Wafanyakazi hao wameajiriwa kisheria na wana sifa zote zilizohitajika. Kamati ilikutana na Uongozi wa Tume, pamoja na Vijana wenyewe waliokata rufaa, kama vile ilivyoweza kujadiliana na Uongozi wa Shirika na kuwahoji wafanyakazi wote watatu waliolalamikiwa kwa njia ya Rufaa. Aidha Kamati imejiridhisha kwamba, maamuzi ya Tume ya Utumishi Serikalini hayakuwa sahihi na ni kweli kwamba, waajiriwa 2, ambao ni Ndg. Tauhida S. Salum na Ndg. Moh’d H. Moh’d hawakuwa na sifa za kuajiriwa, kama tulivyofafanua katika ripoti yetu kuanzia ukurasa wa 83, Na kwa ufupi mambo haya yamebainika:
Kuajiriwa kwa watu wasio na sifa na kuacha kuajiri wenye sifa zilizohitajika:
Mheshimiwa Spika :
Kwa upande wa Kamati, baada ya kupitia taarifa mbali mbali zilizowasilishwa kwake, imegundua kwamba, kuajiriwa kwa Ndg. Tauhida Suleiman Salum hakukufuata taratibu zilizowekwa. Kwa mfano, kama utarejea barua ya Shirika la Umeme iliyoeleza kwa maandishi kwa Tume ya Utumishi Serikalini, baada ya kutakiwa kufanya hivi kwa mujibu wa barua ya tarehe 28/03/2012 yenye kumbu kumbu namba TUS/OR/MW/3 VOL.VII/78 ambayo tumeifanya kuwa Kiambatanisho Nam 61 cha Ripoti yetu, inathibitisha kwamba tarehe ya mwisho kupokea maombi ya nafasi hiyo ilikuwa ni 30/10/2011, na tarehe hii ndio pia imetakiwa kwa mujibu wa tangazo la Ajira hizo katika Gazeti la Zanzibar Leo.

Mheshimiwa Spika :
Hata hivyo, kwa mujibu wa barua ya maombi ya Ndg. Tauhida Suleiman Salum, maombi yake alipeleka tarehe 04/11/2011, sawa na siku 4 za ziada baada ya tarehe ya mwisho wa kupokelewa kwake, kama tulivyoifanya kuwa Kiambatanisho Nam 63. Hii ina maana kwamba, kupokelewa kwa maombi ya mfanyakazi huyu kunakiuka taratibu na ni sawa na kusema kwamba, kumepita upendeleo. Utathibitisha kwa uwazi zaidi na usahihi wake, kwa kufahamu kwamba, Ndg. Tauhida ni shemeji wa aliekuwa Meneja Utawala wa Shirika, Unguja, Ndg, Moh’d Haji. Kwa hali hii, ni rahisi zaidi kufanyiwa upendeleo huo, hata kama muda wa tangazo unaelekeza vyenginevyo.
Mheshimiwa Spika :
Aidha, kwa mujibu wa sifa zilizohitajika kwa ajili ya kazi ya ‘Cashier’, alitakiwa pamoja na sifa nyengine awe amehitimu na kupata cheti cha ‘Accounting’ wakati Ndg. Tauhida amemaliza masomo ya ‘Islamic Banking and Finance’ fani inayotofautiana na iliyohitajika (ingawaje inawiyana), huku walalamikaji kwa mfano Ndg. Marzuku Hussein Marzuik, amemaliza Kidato cha Sita na kuhitimu na kupata cheti cha Diploma ya ‘Accounting’ katika Chuo cha Uongozi wa Fedha, Chwaka. Kwa maana hii, Kama Shirika lilizingatia sifa walizozihitaji, ni wazi kwamba, Ndg. Marzuk ambae pia alishiriki katika usaili, alikuwa na haki ya kuajiriwa zaidi kuliko Ndg. Tauhida ambae hakuwa na sifa zilizohitajika katika nafasi hiyo.
Mheshimiwa Spika :
Aidha, kwa upande wa Muajiriwa, Ndg. Moh’d H. Moh’d, Kamati imejiridhisha kwamba, hakuwa na sifa zilizohitajika kwa sababu amesomea masuala ya Takwimu katika Kituo cha Mafunzo cha ‘Eastern Africa Statistical Centre’, kilichopo Dar es Salaam na ni sawa na kusema kwamba, hakusomea ‘Accounting’ kama vile Shirika lilivyotangaza na kuhitaji. Aidha, Kamati imejiridhisha kwamba, Mfanyakazi huyu hakupeleka maombi ya kazi katika muda uliohitajika, na badala yake ameomba tokea tarehe 23/08/2010 huku tangazo la maombi ya nafasi hizi za kazi, likitoka tarehe 12/10/2011.
Mheshimiwa Spika :
Linalowauma zaidi walalamikaji hawa, wanajua fika kama ilivyofahamu Kamati kwamba, Ndg. Moh’d H. Mohd, ambae ameajiriwa akiwa hana sifa, ni Mjomba wa Meneja Utawala Pemba, Ndg. Hafidh Tahir. Kwa ujumla, hali kama hii haiwezi kuvumiliwa na yoyote, na inakiuka Katiba ya Zanzibar na kwenda kinyume zaidi na misingi ya haki.
MAMBO MENGINE YA UJUMLA YALIYOJITOKEZA JUU YA SUALA
LA AJIRA UNGUJA NA PEMBA:
  1. Mafunzo ya Kazi:
Mheshimiwa Spika :
Kamati pia imeona ipo haja ya kuangalia suala la mafunzo yanayotolewa kwa wafanyakazi wake ijapokuwa ni kweli kwamba fursa hizo hutolewa kwa misingi ya upendeleo, kama ambavyo Kamati imeeleza kwa kina suala hili kuanzia ukurasa wa 90 hadi 101 wa ripoti yetu. Ingawaje pia ni vyema kutaja kwa muhtasari upendeleo huo kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika :
Kamati ilipata mifano ya watendaji hao, ambao pamoja na ukweli kwamba walikuwa na sifa za kuweza kupewa mafunzo ya kazi na Shirika kwa nia ya kuleta ufanisi wa kweli na wao wenyewe kuomba ufadhili, lakini vilevile kuwa tayari hata kujilipia wenyewe mradi tu wapate ruhusa kwa muajiri wao.  Hata hivyo ushahidi unaonesha kwamba Shirika liliwakatalia tena bila ya sababu yoyote ya msingi.
Mheshimiwa Spika :
Kwa mfano, Ndg. Mohammed Khamis Juma, Mfanyakazi aliekuwa akifanya kazi kama Mkaguzi wa Hesabu za Ndani (Internal Auditor) Tawi la Shirika Pemba, aliomba ruhusa ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dodoma katika mafunzo ya Shahada ya Uzamili katika uhasibu  kwa mwaka wa masomo wa 2008/2009. Barua ambayo ameiandika tarehe 17 Septemba, 2008. Meneja Mkuu wa Shirika alimkatalia ombi lake hilo tena bila ya kuainisha sababu yoyote.
Mheshimiwa Spika :
Ndugu Mohammed kwa kutambua kuwa labda Shirika halikuwa na fedha, basi aliliandikia juu ya kupatiwa mkopo kwa madhumuni ya kujisomesha mwenyewe (Tarehe 31/7/2008) na Uongozi wa Shirika kupitia barua yake ya tarehe 6/8/2008 nambari ya kumbukumbu ZECO/PE/M.149 ulikamkatalia tena. Kutokana na hali hiyo, Mfanyakazi huyu alilazimika kujisomesha kupitia nguvu zake mwenyewe.
Mheshimiwa Spika :
Hali kama hiyo pia imemkuta Ndg. Fadhila Abdallah Mbarawa, ambae nae aliajiriwa Mwezi wa Januari, 2008 kama Fundi (Technician) akiwa na mafunzo ya Cheti cha Ufundi (Full Technician Certificate) katika fani ya ‘Electrical Engineering’, na kuanza kazi ya ufungaji wa mita za Tukuza na hatimae kuhamishiwa Kitengo cha Masoko.
Mheshimiwa Spika :
Ndg. Fadhila aliomba ruhusa ya kwenda masomoni baada ya kukubaliwa na Chuo, mnamo tarehe 28/09/2010. Nae aliomba ruhusa hiyo kwa muajiri wake pamoja na udhamini. Mafunzo hayo yalikuwa katika kiwango cha Shahada ya Kwanza katika fani hiyo hiyo ya umeme, kwa kuamini kwamba kufaulu kwake kutaleta tija kwa Shirika pamoja na yeye mwenyewe. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana Shirika halikuona umuhimu wa jambo hilo kwa upande wake na alinyimwa ruhusa ya kuitumia fursa hiyo, kupitia barua ya tarehe 25/11/2010 yenye kumbu kumbu namba ZECO/PF/F.33, yaani baada ya miezi miwili tokea apeleke maombi, wakati Mfanyakazi huyu akifanya kazi hapo hapo katika Afisi ya Meneja wa Tawi, Pemba (Kiambatanisho Nam 73).   
Mheshimiwa Spika :
Ndg. Fadhila kwa busara alizokuwa nazo na kuthamini elimu katika kazi zake, hakuvunjika moyo na mwaka uliofuata aliomba tena mafunzo hayo kupitia barua yake ya tarehe 4/4/2011. Hata hivyo, Meneja huyu huyu wa Tawi, Pemba aliendelea tena kutothamini haja ya kumsomesha mfanyakazi wake huyu na ndipo tarehe 14/4/2011 alimjibu kwa barua yenye kumbu kumbu namba ZECO/OPF/F.33 kwa ufupi kabisa kwamba ruhusa hiyo haijakubaliwa, kama hapa tunavyonukuu:
“Uongozi wa Shirika unapenda kukujuulisha kuwa ombi lako la ruhusa ya masomo kwa mwaka 2011/2012 halijakubaliwa” (Kiambatanisho Nam 74).
Mheshimiwa Spika :
Bila ya shaka baada ya mwaka tu Mfanyakazi huyu alijijutia kwa nini atake kusoma na ndipo mnamo tarehe 01/03/2012 alipewa uhamisho wa ndani kutoka Kitengo cha Ufungaji Mita za Tukuza na kupelekwa Kitengo cha Marketing, sehemu ambayo sio fani yake ili kumkomesha na kumtaka akatishe haraka hamu na juhudi zake za kutaka kujiendeleza katika fani yake aliyoisomea.
Mheshimiwa Spika :
Kwa upande mwengine basi, kuna mfanyakazi Ndg. Mwawanu Ali Juma ambae ameajiriwa kama Karani Masijala. Nae, mnamo siku ya Tarehe16/2/2009 aliomba ruhusa ya kuhudhuria masomo katika Chuo cha ‘London Education and Development’ katika fani ya ‘ABE- Business Information System’ ngazi ya Stashahada ya Juu (Advanced Diploma), huku akiliahidi Shirika kwamba angelipiwa gharama zote hizo za mafunzo yake hayo na familia yake. (Ufafanuzi wa kina juu ya kadhia yake hii, unapatikana katika ukurasa wa 92 hadi 101ya Ripoti yetu.
Mheshimiwa Spika:
Kilicholeta Utata.
Aidha, pamoja na kwamba aliliahidi Shirika kwamba familia yake ndio itakayomlipia na Shirika kumruhusu kwenda masomoni likiamini tu kwamba halitatoa fedha zake kwa mafunzo hayo, Kamati ilijuulishwa kwamba, Mwawanu aliandika barua kuliomba Shirika, msaada wa gharama za mafunzo pamoja na kuambatanisha na ‘Invoice’ ya tarehe 24/5/2010, pamoja na barua ya Chuo ambacho ni tofauti na kile alichoruhusiwa na Shirika. Barua na ‘invoice’ hizo, zina jina tofauti na Chuo husika pamoja na aina ya mafunzo na muda wenyewe; wakati barua ya awali inayotoka Chuo cha ‘London Education And Development Academy’ ina jina la Chuo cha ‘City Business College’. Halikadhalika jina la mafunzo yenyewe katika barua ya mwanzo (iliyoruhusiwa na Shirika), muhusika ameomba kuhudhuria mafunzo ya ‘ABE – Business Information System’ ngazi ya ‘Advanced Diploma’ wakati barua ya msaada wa gharama za masomo inaonesha muhusika amesomea ‘Business Studies na Invoice’ inaonesha mafunzo ya Management Studies ngazi ya Diploma ya Kawaida.
Mheshimiwa Spika :
Jambo  jengine ni kwamba, inaonekana kumbe  Shirika la Umeme lilikuwa limemfadhili mfanyakazi huyu katika mafunzo hayo tangu  awali kwani katika maombi yake ya Viza, Meneja Mkuu wa Shirika aliuhakikishia Ubalozi wa Uingereza Nchini Tanzania kwamba Shirika ndilo linalogharamia mafunzo hayo ikiwemo Ada, Malazi, Usafiri na gharama nyenginezo, kama inavyosomeka nukuu ya barua ya Meneja Mkuu kwa Ubalozi wa Uingereza kwamba “Our Organization is confirming for sponsoring for the whole period of  her studies in U.K including her school fees, Accommodaton, Tuition fees, Transport and any other expenses”. Yaani, (Taasisi yetu (Shirika la Umeme) inahakikisha kufadhili masomo ya Mfanyakazi wetu huyu kwa muda wote wa masomo yake nchi Uingereza, ikiwa ni pamoja na ada ya masomo, gharama za malazi, usafiri, na ghrama nyenginezo
Mheshimiwa Spika :
Hii inaonesha kwamba, kwa mfanyakazi huyu tangu awali Shirika lilikuwa na nia ya kumfadhili masomo yake na ile barua aliyoiandika ya Tarehe 16/2/2009 kwa Shirika ilikuwa ni geresha tu, kwani haiwezikani hata kidogo kwamba mtumishi huyo aandike barua ya kulihakikishia Shirika kwamba gharama za masomo hayo yatalipwa na familia yake Tarehe 16/2/2009, lakini Tarehe 18/2/2009 na Tarehe 19/2/2009, Shirika lithibitishe kwa Ubalozi wa Uingereza nchini na kwa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi kwamba lenyewe  ndio Mdhamini wa mfanyakazi huyo kwa ajili ya kumlipia gharama za mfunzo yake na mambo mengine yote yanayohusiana na kufanikisha masomo hayo. Jambo ambalo limefanyika ndani ya siku mbili tu na wala halikuja kwa malalamiko ya baadae ya kumsaidia endapo atakuwa amekwama katika malipo ya ghrama zilizokusudiwa, wakati huo pengine tayari anaendelea na masomo yake Uengereza.
Mheshimiwa Spika :
Kuna kila sababu ya kuamini juu ya upendeleo huu. Kwanza ajira yake ni Karani Masjala, aina ya mafunzo aliyokwenda kuyasomea ni ya ‘Business Management’ ambayo hayaendani na kazi yake. Lakini jengine, mafunzo hayo hayakuwa kwenye mpango (Training Programme) wakati huo huo Shirika halikuwa na mahitaji ya mtu wa aina hii. Kwani pamoja na kumgharamia huko lakini nafasi yake ya kazi ilibaki pale pale ya Ukarani Masjala na kwa maana hiyo, ile elimu aliyoipata nchini Uingereza haitumiki kwenye Shirika, kama kuitumia basi muhusika ataitumia katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika :
Wakati Ndg. Mohammed Khamis Juma kama tulivyokwisha mueleza hapo juu, alikuwa anaomba mafunzo kwa kazi anayoifanya, na kwa uwazi yalionekana kwamba ni mahitaji ya Shirika kwani hadi Kamati inatembelea Shirika Tawi la Pemba halikuwa na Mkaguzi wa Ndani. Aidha, kama pia tulivyokwisha eleza katika hoja nzima ya Upotevu wa fedha katika Shirika hili Tawi la Pemba, miongoni mwa sababu zake ni kukosekana kwa Mkaguzi wa Ndani aliyepo huko Pemba. Sasa kama Uongozi wa Shirika ulihitaji kuangalia suala hili kwa ukaribu mno na upeo wa mafanikio kwa maslahi yake, ni kwa nini ushindwe kumuendeleza Mfanyakazi aliyepo kwa gharama ndogo zaidi kuliko fedha zinazopotea?.
Mheshimiwa Spika :
Kwa kuunganisha na mfano wa Ndg. Fadhila Abdallah Mbarawa ambae si tu alikosa ufadhili lakini hata ile ruhusa ya kwenda masomoni. Hii ni tafsiri na taswira yenye kuonesha ni kwa kiasi gani hali ya upendeleo wa waziwazi ambao katika ajira (Utumishi) ya Shirika upo na ambao unarudisha nyuma maendeleo ya watumishi na kulitia hasara Shirika kutokana na kukosa rasilimali watu zenye upeo na uwezo mkubwa wa kazi wenye kuleta ufanisi na badala yake raslimali fedha kutumika bila ya kuleta tija, na matumizi yake ni kwa maslahi ya watu binafsi.
Mheshimiwa Spika :
Kesi hizi za kuomba ruhusa ya masomo kwa wafanyakazi wa Shirika, lakini Shirika hukataa kuwasomesha, ni mashuhuri sana katika utendaji wa Shirika. Kwani hata Ndg. Aisha Omar Khamis aliyeomba tarehe 10/03/2011 alijibiwa kwamba Shirika haliwezi kumsomesha eti kwa sababu masomo yake hayamo katika mpango wa mafunzo. Masaibu haya pia yamewakumba Ndg. Saleh Mussa Alawi na hata Ndg. Salum Mussa Alawi (Kiambatanisho Nam. 82).
Mheshimiwa Spika :
Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba Shirika hili hili linasomesha wafanyakazi wengine ndani ya mwaka huo huo walioomba wenzao, ila wao labda kwa sababu wana hadhi tofauti na wengine, lakini hatimae husomeshwa tena kwa gharama kubwa, tena husomeshwa bila ya kuzingatia nafasi zao za kazi.
Utambuzi na Uhalali wa Vyeti na Mabadiliko ya Mshahara:
Mheshimiwa Spika :
Hali hiyo hiyo ya upendeleo inayopatikana katika Utumishi (Ajira) ya Shirika, inaonekana katika suala zima la kuthibitisha kipi ni cheti halali na kinastahiki kurekebishwa mshahara, kwa mtumishi ambae atakuwa amekipata baada ya kuhitimu mafunzo yake.
Kigezo kikubwa katika suala zima la utambuzi wa uhalali wa vyeti, ni wapi muhusika amekipata cheti hicho na si kwamba Cheti hicho kimetolewa na Chuo gani ambacho kinatambuliwa rasmi. Hilo limethibitishwa kutokana na baadhi ya madai ya wafanyakazi ambao wamefaulu masomo yao katika vyuo vinavyosimamiwa na Bodi moja, lakini wengine vyeti vyao vikatambuliwa vyengine visitambuliwe.
Mheshimiwa Spika :
Ndg. Fatma Mzee Said kwa mfano, aliwasilisha cheti cha ‘Advanced Diploma in Business Studies’ ambapo mitihani yake inasimamiwa na Bodi ya ICM. Sambamba na cheti alichowalisilisha Ndg. Mwawanu Ali Juma, tofauti iliyopo ni kwamba Ndg. Fatma yeye mafunzo yake ameyafanyia katika kituo cha Zanzibar wakati Ndg. Mwawanu yeye alifanyia mafunzo hayo Uingereza. Kamati imeshindwa kutofautisha vyeti hivyo kwa sababu vyote vimetolewa na Chuo kimoja, tofauti yake ni maeneo tu ya wapi Chuo na Kituo ama Tawi la Chuo kilipo, lakini Shirika lilimuarifu Ndg. Fatma Mzee Ali kwamba yeye cheti chake eti hakitambuliwi na Idara ya Utumishi, Serikalini (Kiambatanisho Nam.84), wakati Ndg. Mwawanu Ali Juma, kama alivyotambuliwa na kupatiwa ufadhili wa masomo yake, vile vile cheti chake kimetambuliwa na Shirika, bila ya hata kupelekwa Idara ya Utumishi Serikalini.
Mheshimiwa Spika :
Wakati huo huo Ndg. Faida Khamis Haji ambae ni Karani sehemu ya Utawala, nae alijiendeleza kielimu kwa gharama zake katika ngazi ya Stashahada kwa mafunzo ya kwenye Chuo cha ‘Institute of Commercial Management’ na Chuo cha ‘Cambridge International College’ vyote vya Uingereza.
Aliwasilisha vyeti vyake vya kuhitimu masomo, kwa barua ya tarehe 30/10/2007 na kukumbushia tena Tarehe 15/4/2009 kwa lengo la kubadilishiwa mshahara wake, lakini hakupata majibu yoyote. Mfanyakazi huyu hakuchoka kukumbushia na ilipofika Tarehe 27/04/2012, alikumbushia tena kwa mara nyengine (Kiambatanisho Nam 86), lakini jambo la kutia wasiwasi ni kwamba kwanini asipate majibu ama anastahiki au la. Na kwa maana hiyo alikuwa hatandewi haki si tu kwa sababu ya kuwa hajibiwi barua zake, lakini kama anastahiki basi muda unapita na haki zake zinapotea. Tunachothibitisha ni kwamba, hadi Kamati inapita kufanya kazi zake, Mfanyakazi huyu bado hajajibiwa maombi yake.
Mheshimiwa Spika :
Katika hili la upendeleo, pamoja na yote hayo, Kamati inaendelea kufafanua kwamba, kwa kiasi kikubwa upendeleo huo ulikuwa unatekelezwa kwa baadhi tu ya watumishi, ambao huduma wanazopewa ni za aina ya kuonesha kwamba wao ni watumishi muhimu mno kuliko wengine (V I Ps Status). Kwa kuchukulia mfano wa mtumishi huyu huyu Ndg. Mwawanu Ali Juma, Mkuu wa Masjala namna ya maombi yake yalivyokuwa yakishughulikiwa, Kamati iliridhika kabisa kwamba alichokuwa akifanyiwa si chengine isipokuwa ni upendeleo usiokuwa na kificho. 

Mheshimiwa Spika :
Kwa mfano, alipewa dhamana ya kuwa Mkuu wa Masjala Tarehe 28/11/2006 lakini kwa muda wote huo alipopewa dhamana hiyo hakulalamika juu ya malipo ya mshahara anaolipwa kwamba haukuwa na tofauti kulingana na dhamana aliyopewa. Cha ajabu aliliandikia Shirika malalamiko hayo Tarehe 2 Februari, 2009 ya kudai mshahara wenye hadhi na dhamana aliyonayo, lakini pia na tofauti yote (Arears) kwa miaka miwili na miezi mitatu nayo pia alipwe.
Mheshimiwa Spika :
Kamati ilikuwa na maswali mengi ya kujiuliza, Je muda wote huo, yaani tokea mwaka 2006 hadi 2009, Shirika lilikuwa halijui kama Mfanyakazi huyu alikuwa na haki hiyo? Na jee, yeye mwenyewe Ndg. Mwawanu, vile vile hakujua! Kwanini asilalamike mwanzo! Au miaka hiyo na muda tolionao sasa kulikuwa na tafauti ya Uongozi ambao ama aliogopa kwamba hata angedai haki zake za kuongezewa mshahara, basi asingeliipata au si kwa kiwango cha huduma anazozitaka yeye!. Unataka kusema kwamba, katika hali yote hii hakuna upendeleo wa dhahiri? Naamini utakubaliana na Kamati, ingawaje bado utakuwa na maswali mengi, juu ya Ukaribu ama uhusiano wa Mfanyakazi huyu kwa Meneja Mkuu wa Shirika, na tafauti iliyopo ya wafanyakazi wengine waliobakia! Ni kitendawili kinotaka uteguzi.
Mheshimiwa Spika :
Kamati hii inaamini kama Taasisi zote za Serikali zingelikuwa zinashughulikia maombi ya watumishi wake na wananchi kwa ujumla kwa kipindi kifupi tu, kama Shirika lilivyojikita kuyashughulikia ya Ndg. Mwawanu, basi Zanzibar hii ingelikuwa mbali sana kimaendeleo. Hata hivyo, kila mtu atajiuliza masuala mengi ambayo yanapata majibu tafauti, juu ya utukufu wa Ndg. Mwawanu na utumishi uliotukuka wa Meneja Mkuu kwa Mfanyakazi huyu, wakati wafanyakazi wengine ambao ni sawa na Mfanyakazi huyu kwa misingi ya Utumishi ya Shirika, wakisota na kuendelea kulalama chini kwa chini, huku wakiamini kupitia Ripoti hii, Serikali italishughulikia suala hili ipasavyo, kwa maslahi ya kuboresha shughuli za Umma.




Mheshimiwa Spika :

Muhtasari wa Mambo yaliyobainika na Kamati kufuatia Uchunguzi wake wa Hadidu hii Rejea:
    1. Uajiri wa Wafanyakazi hawa haukufuata taratibu za Uajiri kama zilivyoelezwa katika Sheria na Kanuni za Utumumishi za Shirika.
    2. Maombi ya Ajira ya Wafanyakazi wengi kwa Upande wa Pemba yameombwa kwa Meneja wa Tawi, Pemba, kitendo ambacho kinakiuka taratibu za Kanuni za Utumishi, za Shirika.
    3. Kamati haikupatiwa sifa zilizohitajika na Shirika wakati wa kutangazwa nafasi hizi, na ni sawa pia kusema kwamba, haijapatiwa Ripoti inayoonesha utaratibu mzima uliotumika tokea kufanya uteuzi wa baadhi ya wananchi walioomba (Short List), Usaili, na matokeo ya Usaili huo, kwa kipindi cha mwaka 2008 hadi 2010, na badala yake taratibu hizo zilifuatwa kwa mwaka 2011 Pekee.
    4. Kuanzia mwaka wa 2008 hadi 2009, Wafanyakazi waliajiriwa bila ya kufanyiwa Uhakiki wa Kiusalama (Security Vetting) na Mamlaka inayohusika na suala hili (G.S.O).
    5. Tume ya Utumishi Serikalini haikufanya ipasavyo katika uchunguzi wa malalamiko ya wananchi watatu kuhusiana na nafasi ya Cashier kwa mwaka wa ajira 2011.
    6. Kuna upendeleo mkubwa sana katika upatikanaji wa fursa za kusoma na kudhaminiwa na Shirika, pamoja na ubadilishwaji wa mshahara kwa muamala wa elimu husika dhidi ya wafanyakazi wa Shirika hili.
Mheshimiwa Spika :
HADIDU REJEA NAM. 4
IWAPO MALI ZA SHIRIKA ZINAUZWA KWA KUFUATA TARATIBU ZA SHERIA YA UUZWAJI NA UGAVI WA MALI ZA SERIKALI NA SHERIA NYENGINE ZINAZOHUSIKA.
Mheshimiwa Spika :
Ni jambo lisilo na shaka yoyote juu ya Muongozo wa kuuza mali za Taasisi yoyote ya Serikali, ikiwa ni pamoja na Shirika la Umeme la Zanzibar, kwa kufuata masharti yaliyoelekezwa na Sheria ya Ununuzi na Uuzaji (Ugavi) wa Mali za Serikali, Namba 9 ya mwaka 2005. Katika kufahamu hili, Kamati ikiongozwa na Sheria husika, ilikutana na Uongozi wa Shirika pamoja na kufanya ziara kadhaa katika mali za Shirika, kwa malengo ya kuona, namna gani Shirika hili linauza mali zake.
Mheshimiwa Spika :
Katika hadidu hii rejea, Kamati imetakiwa kuchunguza namna gani Shirika linauza mali zake kwa kufuata masharti yaliyowekwa na Sheria hii Namba, 9 ya mwaka 2005, pamoja na Sheria nyengine zinazohusika. Suala hili linahitaji kufahamika kwa makini kwa sababu, pamoja na muda uliokabidhiwa Kamati, na mali nyingi za Shirika, kama Kamati ingelifanyia kazi kwa kuchunguza mali zote zinazomilikiwa na Shirika, (huku ikifahamika hata nguzo na mita zote za wateja wake ni mali za Shirika, pamoja na kwamba zinanunuliwa na wateja wenyewe wakati wanapohitaji huduma ya kuungiwa umeme), ingelitosha kupewa angalau miaka miwili au zaidi, na Kamati ingelazimika pia kufanya kazi bila ya kupumzika. Hata hivyo, kama tutakavyoona hapo baadae, Kamati imejiridhisha kuifanyia kazi hoja hii, kwa kupata mfano tu wa mali hizo.
Utaratibu wa Uuzwaji wa Mali za Shirika kwa mujibu wa Sheria
inayohusika :

Mheshimiwa Spika :
Katika kuutekeleza utaratibu wa kuuza mali za Shirika, kwa mujibu wa kifungu cha 40(1)(a) cha Sheria hii, Namba 9 ya mwaka 2005, Shirika lingeliweza kuuza mali zake kupitia njia ya Mnada wa hadhara, ambapo mali husika ya Shirika, ambapo gharama halisi ya mali hiyo ama hizo, haitazidi kiwango kilichofanyiwa tathmini ya kitaalamu na kuelezwa katika muongozo wa tathmini hiyo.
Mheshimiwa Spika :
Shirika pia linaweza kuuza mali zake kupitia mapatano ya moja kwa moja, pale ambapo mauzo hayo katika soko lililo wazi, litahusisha masuala ya haki za binaadamu na thamani halisi ya bidhaa hiyo haipungui ile iliyowekwa katika thatmini ya kitaalamu kama ilivyofanywa.
Mheshimiwa Spika :
Kuiharibu mali hiyo, nayo ni njia moja wapo ya Ugavi wa Mali za Shirika, ingawa hii kwa mujibu wa Sheria hiyo,  hukubalika kuwa ni sawa na kuuza ama kwa lugha nyengine, kuhaulisha mali husika. Njia hii itatumika pale ambapo mali hiyo imeshapoteza thamani yake na wala haina maslahi ya umma wala haina athari ya kiusalama.
Mheshimiwa Spika :
Aidha, Kifungu hiki cha 40(1)(d) pia kimeeleza njia ya kuiuza mali husika kama mali kachara au kuibadili na kuwa na hadhi hiyo. Huku pia njia ya kuiuza mali husika, ikiwa ni njia moja ya hizo zinazokubaliwa kufuatwa wakati wa uuzaji wa mali za Shirika. Kama pia ilivyokubalika kukihaulisha ama kuipeleka mali hiyo kwa chombo chengine cha Shirika chenye mamlaka yanayohusiana na mali za Shirika, kama njia hii inavyokubaliana na maelekezo ya kifungu cha 40(1)(f) cha Sheria hiyo.
Hali Halisi ya Uuzwaji wa Vifaa Vichakavu vya Shirika, katika Tawi la
Pemba:
Mheshimiwa Spika:
Kuhusiana na viifaa chakavu vilichopo kwenye Tawi la Pemba, ilistahiki kwa Kitengo cha Watumiaji husika, kufuata taratibu tulizokwishazieleza hapo juu, ili ziweze kuuzwa kwa misingi ya sheria. Na kutokana na ukweli kwamba, Shirika la Umeme Tawi la Pemba, lilikuwa linahitaji kuvihaulisha baadhi ya vifaa vyake ambavyo kwa wakati huo vilikuwa havihitajiki tena kwa matumizi ya Shirika. Katika kutimiza azma hiyo liliandaa mazingira ya uuzwaji wa vifaa hivyo. 



Kilichobainika na Kamati
Mheshimiwa Spika:
Barua ya tarehe 12/12/2010 yenye kumbu kumbu namba ZECO/8/8/VOL 1/133 ambayo katika ripoti yetu ni Kiambatanisho Nam 89, inahusiana na ruhusa iliyoombwa na Meneja Mkuu kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, kuruhusiwa Shirika lake kuuza vifaa chakavu, baada ya kukiri katika barua hiyo kwamba tayari walikwishapata idhini ya Bodi ya Zabuni ya Wakurugenzi. Pamoja na hatua hii, suala hili kwa Kamati linahitaji kwanza kuthibitishwa iwapo kweli Bodi ya Zabuni ilikaa na kuridhia, lakini je hapo kabla, kuna kikao chochote cha Kitengo cha Manunuzi kilichokaa kupitia orodha ya mahitaji ya kuuzwa kwa vifaa hivyo kutoka Kitengo cha Watumiaji? Masuala haya hayajithibitishwa uhalali wake mbele ya Kamati.
Mheshimiwa Spika:
Hata hivyo, kufuatia barua hiyo tuliyoinukuu hapo juu, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo aliruhusu uuzwaji wa vifaa chakavu, kupitia barua yake ya tarehe 17/1/2011 yenye kumbu kumbu namba MFEA/M.30/4/02/VOL.VII/, ingawaje Gari Land Rover yenye namba SLS 1023 na Toyota Pick Up yenye Namba SLS 1045, hazikuwemo katika mali zilizoruhusiwa kuuzwa ama kutiwa thamani yake.
Mheshimiwa Spika:
Aidha, Barua yenye kumbu kumbu namba ZECO/MUMW/VOL.1/206, inaagiza Meneja wa Tawi auze vifaa hivyo kwa njia ya mnada, kwa kile kilichofahamishwa kwamba, tayari uuzaji wake umeshapata idhini ya Bodi ya Wakurugenzi. Hapa tunapata shaka, kwamba ni nani alieuza vifaa hivyo, ni Meneja wa Tawi ama Kitengo cha Manunuzi cha Shirika? Iwapo tunahitaji majibu ya kisheria, basi kifungu cha 175(3) cha Kanuni za Sheria Namba 9 ya mwaka 2005, kinatosheleza kwa sababu kimeeleza uuzwaji wa mnada ufanywe na Kitengo cha Manunuzi kwa mujibu wa Kanuni hizo, lakini kwa kuwa Kamati imeelezwa kwamba uuzaji wake umefanywa na Uongozi wa Shirika, Tawi la Pemba, inatosheleza pia kuthibitisha kwamba, taratibu za uuzaji huo hazikuridhiwa na Sheria zinazohusika.
Mheshimiwa Spika:
Lakini pia ni vyema kufahamu kwamba, Barua hiyo ilipokelewa Afisi ya Tawi,  Pemba kutoka Unguja ni ya Tarehe 17/12/2011, siku hiyo ya Jumamosi, ambapo kwa Kawaida Shirika halifanyi kazi na zaidi za Kiutawala. Sasa tuseme kwamba ni kweli barua hiyo inakubaliwa katika taratibu za kiutawala? La kushangaza zaidi ni kwamba, imepokelewa siku hiyo hiyo Jumamosi  na wala haikutumwa kwa njia ya Fax au Email, sasa ni kweli kwamba iliandikwa ama imefuata baada ya kukamilika kwa njia na taratibu zote za uuzaji. Basi mambo ndio yaliendelea hivyo, na baada ya kupokelewa barua hiyo Pemba, Meneja wa Tawi alimuandikia Dokezo Afisa Utawala kwa hatua ya usimamizi, wakati Afisa huyo wa Utawala alimwandikia Dokezo Afisa Uagiziaji kwa hatua za mnada siku ya Jumapili ya Tarehe 18/12/2011. Mnada wenyewe nao ulikuwa siku hiyo hiyo ya Jumapili, ni vitu vya kutia shaka sana.
Mheshimiwa Spika:
Aidha Barua hiyo ya kuruhusu iliyotoka kwa Meneja Mkuu wa Shirika zaidi ya kueleza juu ya idhini ya Bodi na kusisitiza kufuatwa kwa taratibu za mnada ili kuondosha malalamiko, hakukuwa na maelezo mengine ambayo ni ya msingi ya kuonesha Orodha halisi ya vifaa ambavyo vinahitajika kufanyiwa mnada huo na wala hakukuwa na marejeo ya Barua nyengine yoyote yenye kuonesha kupatikana kwa orodha hiyo.

Mheshimiwa Spika:
Kwa maana hiyo kulikuwa na utata juu ya ruhusa hiyo ya Bodi ama ilikuwa haina orodha kamili ya vifaa vinavyohitajika kuuzwa, au kulikuwa na ongezeko la vifaa vyengine ambavyo havikuwemo katika orodha ya mwanzo na kwa hivyo kukosa   baraka ya ruhusa ya Bodi. Hilo lilidhihirika wazi kwani hata ile orodha aliyokuwa nayo Afisa Uagiziaji, ambae ndie aliyepewa jukumu la kusimamia mnada huo ilitafautiana na vifaa halisi vilivyopigwa mnada siku hiyo.
Ripoti ya Mnada wa Kuuza Vifaa Chakavu Uliofanyika Tarehe 18/12/2011

Mheshimiwa Spika:
Afisa Uagiziaji ambae ndie alieachiwa kusimamia uuzwaji wa vifaa hivyo kwa upande wa Shirika, akishirikiana na madalali mmoja kutoka Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo (Afisi ya Unguja) na mwengine kutoka Wizara hiyo hiyo Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo  (Afisi ya Pemba), aliviainisha vifaa vilivyouzwa siku hiyo ya Tarehe 18/12/2011 kwa Taarifa aliyoiandika Tarehe 27/12/2011 ni kama ifuatavyo :-
  1. Gari Defender SLS 1025, ameuziwa Ndg. Shaibu Hassan Kaduara, (Mfanyakazi wa Shirika la Umeme, Tawi la Pemba) kwa thamani ya Tsh. 3,550,000/- na kwa tarehe hiyo, alikuwa tayari ameshalipa jumla ya Tsh. 2,550,000/-.
  2. Gari Toyota Hilux, aliuziwa tena Mfanyakazi huyu huyu wa Shirika Tawi la Pemba, Ndg. Shaibu Hassan Kaduara kwa thamani ya Tsh.2,250,00/- na kwa tarehe hiyo alikuwa tayari ameshalipa jumla ya Tsh.1,850,000/-.
  3. Makachara ya Transformer  ameuziwa Ndg. Ali Makame Issa  kwa thamani ya Tsh. 2,020,000/- na kwa Tarehe hiyo alikuwa tayari  ameshalipa Tsh. 505,000/-.
JUMLA YA MAUZO YOTE YALIKUWA NI TSH. 7,820,000/-
Toa 10% ya Kamisheni ya Dalali zinabaki Tsh. 7,038,000/-. Kilicholipwa ni Tsh. 1,905,000/- ukitoa cha Dalali ambacho ni Tsh. 782,000/- zitabaki Tsh. 1,123,000/-.
Mheshimiwa Spika:
Pamoja na orodha hiyo kuelezwa hapo juu, vifaa vilivyouzwa havihusiani na vile vilivyoombewa ruhusa na idhini kama tulivyokwisha eleza hapo kabla, na ndio maana Kamati ikawa na wasi wasi sana juu ya Meneja Mkuu wa Shirika kuagiza kwa Meneja wa Tawi juu ya kuuzwa kwa vifaa kachara bila ya kuviainisha vifaa gani. Lakini kama haitoshi, kwa nini Kamati isipatiwe utaratibu uliokamilika wa kuuzwa kwa vifaa hivi, na badala yake kupewa taarifa vipande vipande.
Mchanganuo zaidi
Mheshimiwa Spika:
Taarifa ya Afisa Utawala imeonesha kwamba, miongoni mwa vifaa vilivyouzwa ilikuwa ni mauzo ya jumla ya  Transformer  sita (6), wakati taarifa ya aliyesimamia mnada huo (Afisa Uagiziaji) mchanganuo wake unaonesha kwamba Transformer zilizopigwa mnada siku hiyo, tena zilikuwa ni makachara ambayo ni ya Transformer ya KVA 500 (mbili), KVA 100 (moja) na ya KVA 50 (moja) jumla yake ni Transformer  nne (4). Aidha Transformer House na Transformer Single Phase nazo zilikuwemo kwenye mnada huo. Lakini Transformer ya 1500KVA moja haimo kwenye orodha wa vifaa vilivyopigwa mnada aliyonayo Afisa Uagiziaji na wala hana taarifa nayo. Lakini alikiri kwamba Transformer hiyo iliondolewa katika eneo ilipokuwepo.
Mheshimiwa Spika:
Vifaa vyenginevyo ambavyo havikuwemo kwenye orodha hiyo ni ‘Propeller shafts’ nne, ‘Starter House’ moja na Mapande ya machuma mchanganyiko. Ingawa mauzo ya mapande ya vyuma tu ndiyo Afisa huyo aliyashuhudia baada ya kupata maelekezo baadae wakati mnada wa awali umeshamalizika. Hata hivyo Transformer hiyo haipo kwenye nafasi yake.
Mheshimiwa Spika:
Pamoja na yote hayo Kamati haikuweza kuiona Barua inayoonesha kwamba Tawi la Shirika Pemba lilikuwa linahitaji kuuzwa kwa vifaa hivyo. Na badala yake, imekuwa kama Shirika Makao Makuu, ndilo lenye nia hiyo na Tawi la Pemba kazi yake ni kutekeleza tu. Jengine ni kwamba Bodi ya Zabuni ya Shirika haikushirikishwa kwenye mchakato huo jambo ambalo ni kinyume na Sheria. Kamati haikuarifiwa juu ya hata kuwepo kwa Bodi hiyo, licha ya kuhusishwa kwake.
Mheshimiwa Spika:
Kutokana na utata huo Kamati imeamini kabisa kulikuwa na kutokufatwa kwa taratibu za kisheria katika mauzo hayo, jambo ambalo limesababisha ubabaishaji wa kutokufahamika hata vifaa halisi vilivyouzwa na hatimae ‘Transformer’  moja kupotezwa katika mazingira hayo tatanishi.   
Mheshimiwa Spika:
Niwaombe waheshimiwa Wajumbe wasome ufafanuzi wa kina kuhusiana na namna magari ya Shirika yanavyotumiwa na hatimae kuuza magari yake katika ripoti yetu kuanzia ukurasa wa 110 hadi 113.
Mheshimiwa Spika:
Muhtasari wa Mambo yaliyobainika na Kamati kufuatia Uchunguzi wake wa
Hadidu hii Rejea:
  1. Shirika linauza mali zake bila ya kufuata utaratibu ulioelezwa na Sheria Namba 9 ya mwaka 2005 na Sheria nyengine zinazohusika.
  2. Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika ambao wamepewa dhima ya Udereva, hawajali thamani halisi ya Gari za Shirika na matokeo yake hupelekea ajali za mara kwa mara dhidi ya gari za Shirika.
  3. Shirika linaingia hasara zisizo za lazima kwa kukodi magari kwa lengo la kutekeleza majukumu ya Shirika huku magari ya Shirika yakitumia bila ya uangalifu na hatimae hupata ajali zisizo za lazima.


Mheshimiwa Spika:
HADIDU REJEA YA TANO:
IWAPO UPATIKANAJI WA MAJENERETA 32 YALIOPO MTONI  ULIFUATA SHERIA ZINAZOHUSIKA NA KWA NINI HAYATUMIWI KWA MANUFAA YA WANANCHI WA ZANZIBAR.
Mheshimiwa Spika:
Kamati ilitakiwa kufuatilia na kujiridhisha kuhusu upatikanaji wa majenereta 32 yaliyokuwepo Mtoni kama ulifuata Sheria zinazohusika na kama hayatumiwi kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar. Kwa ufupi, Kamati ilifuatilia hoja hii kwa siku tatu zinazohusisha mjadala wa pamoja na Shirika, kufanya ukaguzi wa majenereta hayo katika eneo la Mtoni na kupata ufafanuzi unaohusiana na hoja hii, pamoja na kukutana na Kampuni iliyopewa kazi ya kuleta na kuyafunga iitwayo, Mantrac Tanzania Ltd iliyopo Dar es Salaam, Tanzania.
Mheshimiwa Spika:
Unapofanya marejeo ya hoja hii, kuna vitu viwili vinahitaji kuangaliwa kwa karibu mmno, suala la kwanza ni taratibu zilizotumika hadi kupatikana kwa majenereta hayo, hii ina maanisha pamoja na taratibu za manunuzi zilizoelezwa kwa ufasaha katika Sheria ya Manunuzi na Ugavi wa Mali za Serikali, Namba 9 ya mwaka 2005 pamoja na Kanuni zake, na sehemu iliyobakia ni Kamati kujiridhisha iwapo majenereta hayo yanatumiwa ama hayatumiwi kwa matumizi yaliyokusudiwa. Na kwa hali hiyo, ufafanuzi wa hoja hii utahusiana zaidi kuangalia maeneo hayo mawili makuu. Ili kupata usahihi wa ufafanuzi wake, ni vyema tukafuata maelekezo yafuatayo:
Utata wa Ufafanuzi wa Fedha za Kunulia Majenereta 32:
Mheshimiwa Spika:
Katika kuhoji juu ya haja na sababu ya upatikanaji wa majenereta 32 yaliyopo Mtoni, ambapo Kamati imepewa kazi ya kuyafuatilia, ni kuwepo kwa utata mkubwa juu ya usahihi wake, huku kukiwa na kauli tofauti kutoka kwa Uongozi wa Shirika na kauli za Serikali, ikiwa ni pamoja na Wizara inayolisimamia Shirika hili kwa ujumla. Kuna kauli kwamba, Majenereta hayo yamenunuliwa kwa fedha za Mradi wa MDRI, kwamba ni fedha zinazotokana na msamaha wa Madeni, ambapo Tanzania hunufaika, lakini na Zanzibar nayo hunufaika kwa upande wake. Kwa lugha hii, unapohitaji kufahamu juu ya taratibu zilizotumika kununuliwa kwa majenereta hayo, unalazimika pia kufahamu taratibu za matumizi ya fedha hizo za Msamaha wa Madeni. Ikiwa ni pamoja na utaratibu wa matumizi ya fedha za MDRI kutokabidhiwa kwa taasisi inayopatiwa fedha, kwa maana hii Shirika la Umeme, lakini hupatiwa bidhaa/huduma ilizohitaji, yaani Majenereta 32 na malipo hufanywa moja kwa moja na IMF Kupitia Benki Kuu ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika:
Kauli hii pia imetofautiana na ufafanuzi uliopewa Kamati hapo awali, kwamba, fedha za kununulia majenereta hayo, zinatokana na Ufadhili uliofadhiliwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, juu ya haja ya kujinasua na hali tete ya kukosa umeme kwa kipindi chote cha miezi mitatu. Kwa ufahamu huu, unapotaka kuhoji juu ya taratibu za manunuzi ya Majenereta hayo na matumizi ya fedha hizo, jawabu inakuwa ni nyepesi tu, kwamba maelekezo ya Wafadhili ndio yaliyofuatwa zaidi kuliko hata taratibu nyengine, kwa maana, Wafadhili wana taratibu zao na Sheria zao za Fedha na matumizi ya fedha hizo, kwa Kawaida hufahamu wao wenyewe, kwani Shirika lilipewa tu majenereta hayo bila ya wao kuhusika na ununuzi wake.
Mheshimiwa Spika:
Aidha, pia kuna kauli kwamba, Serikali kweli ilipewa msaada na Wafadhili, lakini msaada huo ulikuwa wa fedha, na tokea awali fedha hizo zilikabidhiwa kwa Serikali, na ikabakia dhima ya kuyanunua Majenereta hayo. Katika hali hii, kwanza fedha hizi huwa ni za Serikali kama fedha nyengine za Msaada, na hakuna sababu yoyote ya kuzitumia, bila ya kufuata taratibu za Sheria za Fedha za Umma. Na hivyo basi, kama taratibu za Sheria ya Manunuzi na Ugavi wa Mali za Serikali, Namba 9 ya mwaka 2005 na Sheria za Fedha zingelifuatwa ipasavyo, basi Shirika lingelinunua Majenereta linaloona yanafaa kwa matumizi yao, huku Wafadhili wakitaka tu waone umeme  umepatikana na wajisikie wametoa mchango wao wa kuisaidia Serikali na nchi ya Zanzibar kwa ujumla.
Haja ya kupatikana kwa Majenereta 32:
Mheshimiwa Spika:
Kamati ilielezwa kwamba, majenereta hayo yamenunuliwa kutokana na kuzimika kwa umeme nchi nzima (Unguja) kwa muda wa miezi mitatu, kuanzia Disemba 2009 hadi Machi.
Lakini kabla ya kujadili hili, kuna suala jengine muhimu sana kujiuliza; nalo ni sababu zipi zilizopelekea kukosekana kwa umeme Unguja kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu mfululizo? Je, Serikali imetoa ripoti gani kuhusiana na tatizo hilo kubwa lililowakabili wananchi wa nchi hii na kukwaza shughuli mbali mbali za kiuchumi na kimaendeleo! Kwa ufupi, Kamati haikupata majibu ya kuridhisha kuhusiana na sababu zilizopelekea kukosekana kwa umeme kwa kipindi chote hicho, na imebakia kuwa na shaka kubwa ambayo haitaodoka mpaka pale itakapoundwa Tume huru ya Uchunguzi juu ya kadhia hii.
Mheshimiwa Spika:
Kwa mfano, eti Kamati ilipokutana na Uongozi wa Shirika la Umeme na kuhoji suala hili, ilielezwa kwamba, kulikuwa na fundi aliekuwa anaezeka kibanda kilichopo katika eneo linalohusika na waya, na katika ujenzi wake aliwahi kudondosha nyundo ambayo ilikwenda kugonga sehemu yenye Tenki ambalo ni la kioo na kufanya ufa ambao uliruhusu kidogo kidogo kuingia hewa, na hatimae mripuko mkubwa ukatokea. Jambo la kushangaza ni majibu haya ambayo hayana hata hadhi ya kitaalamu, lakini pia Kamati imefichwa kwa kutopatiwa jina la fundi huyo aliyehusika na uekezaji wa kibanda, na hivyo haifahamiki kama alikuwa mtu binafsi, Mfanyakazi wa Shirika ama Kampuni nyengine inayohusika na kazi hizi.
Mheshimiwa Spika:
Jambo la ajabu zaidi ni kukosekana kwa Ripoti yakinifu inayozungumzia suala hili kwa undani, ikiwa ni pamoja na sababu zake, gharama zilizotumika kurejesha umeme huo, hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika na mambo mengine. Kwa ufupi, Serikali imekaa kimya mpaka leo, haina hata haja ya kulizungumzia suala hilo, basi hata historia yake isiekwe na kuwasaidia wazanzibari wajao baadae!
Mheshimiwa Spika:
Na miongoni mwa masuala ya msingi (ambapo pia tutafahamu baadae) ni ile shaka ya haja ya kununuliwa kwa majenereta hayo na mazingira ya kuharibika kwa umeme Zanzibar. Yaani, Kamati ilipokuwa inafanya mahojiano na Kampuni iliyouza Majenereta hayo (Mantrac) ilieleza kwamba, kwa kawaida wao hawatengenezi ama hawaagizi majenereta ya aina hii mpaka wapate oda maalum kwa ajili ya kununuliwa. Na hii ina maana, Shirika kuamua nunua majenereta hayo, kama tutakavyoona baadae, na kwakuwa sababu ya kukosekana kwa umeme ina utata, ni wazi kwamba shaka ya kuwepo kwa uharibifu wa makusudi wa umeme uliokosekana miezi mitatu Unguja, itaendelea kuwepo, kwamba ni hujuma zaidi kuliko sababu nyengine inayoweza kuelezeka.


Mheshimiwa Spika:
Na katika maeneo ambayo ni muhimu kushughulikiwa ni kufanyika kwa  ukaguzi wa fedha zilizotumika kurejeshea huduma ya umeme baada ya kukatika kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu, mbali na majenereta 32 ambayo mpaka leo hayatumiki ipasavyo!. Lakini je, vipi fedha za wananchi walipakodi zinathaminiwa matumizi yake? Kamati kwa upande wake ilielezwa na Uongozi wa Shirika la Umeme kwamba, wao tu kama Shirika, mbali na fedha za Serikali, wametumia fedha zisizopungua Bilioni moja! Lakini ni nani anaethubutu kukagua fedha hizo? Na ni nani anaepinga kwamba, kuna shaka nyingi za matumizi halali kisheria ya fedha hizo, ukizingatia kwamba mambo yalilazimika yafanywe tu, kwa namna yoyote iwayo, alimuradi umeme urudi!
Mheshimiwa Spika:
Tukirejea katika hadidu hii, Kamati ilielezwa kwamba, yametokana na Ufadhili wa nchi ya Norway, Sweden na Uingereza, ambazo ndizo nchi tatu zilizohusika na ufadhili, huku Kamati ikielezwa kwamba, nchi ya Norway ndio ilichukua jukumu lote la usimamizi wa kupatikana kwa majenereta hayo na hivyo ni sawa na kusema kwamba, nchi ya Norway ndio iliyomtafuta Mshauri Mwelekezi wa kuishauri Serikali juu ya hatua zilizohitajika kufuatwa na kupatikana kwa majenereta hayo. Katika hali kama hii, ni sawa na kusema kwamba, Shirika la Umeme baada ya kushiriki katika kutoa ushauri wa kupatikana kwa majenereta ya dharura, haikupata fursa ya kushirikishwa juu ya aina gani ya majenereta yanayotakiwa kwa ajili ya kuondosha tatizo hili na kwa matumizi mengine ya dharura, wala wapi yangelipatikana, kwa ufupi wa maneno ‘Haikushirikishwa’!.
Taratibu za Sheria zilizotumika kununuliwa kwa Majenereta hayo:
Mheshimiwa Spika:
Wakati Kamati inahojiana na Uongozi wa Shirika na hata katika kikao cha pamoja na Kampuni ya Mantrac, ilipata jawabu moja kwamba, hakukuwa na mpango wowote wa kununuliwa kwa majenereta hayo hapo kabla na haja yake imetokana na nchi kuwepo katika giza la miezi 3. Aidha, suala hili pia linahusisha kukaa ama ununuzi wa majenereta hayo kupitishwa na Bodi ya Zabuni ya Shirika ama ya Serikali, baada ya kupokea haja ya ununuzi wake kutoka Kitengo cha Watumiaji au kwa kupitia utaratibu mwengine wowote unaohusika. Kwa ujumla, hakukuwa na Bodi ya Zabuni yoyote iliyokaa na kujadili haja ya kununuliwa Majenereta hayo.
Mheshimiwa Spika:
Yote haya yamefanywa kwa kukidhi hali ya dharura iliyokuwepo wakati huo na ni sawa na kusema kwamba, kazi ya kumtafuta Mshauri Mwelekezi wa Ununuzi wa Majenereta, kazi ya kuiteua Kampuni ya Mantrac iliyouza na kuyafunga majenereta hayo, kazi ya kuweka msingi (Base line) wa eneo la kuwekea majenereta hayo hapo Mtoni, badala ya kufanywa na Mamlaka husika za Manunuzi, ikiwa ni pamoja na Bodi ya Zabuni, Kitengo cha Manunuzi, Kitengo cha Watumiaji (User Department) ama Kamati ya Tathmini, zimefanywa na Mshauri Mwelekezi wa Norway. Na kwa hali hii, Kamati imejiridhisha bila ya shaka yoyote kwamba, taratibu za Sheria ya Ununuzi wa Majenereta hayo hazikufuatwa, bila ya kujali sababu zilizoelezwa na kuonekana ni za msingi.
Utaratibu uliotumika kununuliwa kwa Majenereta hayo 32:
Mheshimiwa Spika:
Kwa kuwa katika Ununuzi wa Majenereta 32 yenye gharama kubwa na umuhimu wa kipekee kwa Taifa, ulistahili kufanywa kwa njia ya Zabuni, lakini haikufanyika, aidha na kwa bahati mbaya hata njia ya ‘qoutation’ iliyoelezwa kwamba imetumika imeshindwa kuthibitishwa kwa Kamati. Na kwa kuwa mazingira yaliyojiri wakati huo yalihitaji majenereta hayo kununuliwa kwa haraka mno na kwa dharura, ingawaje pia Bodi ya Zabuni ilitakiwa iidhinishe njia mbadala badala ya Zabuni, kama inavyoelezwa na kifungu cha 32(2) cha Sheria Namba 9 ya mwaka 2005, jambo ambalo halikufanywa. Ni vyema sasa tukafahamu utaratibu uliotumika katika ununuzi wa majenereta hayo kwa kuyapitia kwa kina maelezo haya.
Mheshimiwa Spika:
Hatua ya kwanza, ni kufanyika kwa kikao cha Maafa cha Makatibu Wakuu na kujadiliana juu ya suala zima la kutafuta suluhisho la tatizo hili, huku Shirika la Umeme nalo likiwakilishwa na Ndg. Abdalla Haji Steni, ambae kwa wakati huo alikuwa ni Mkuu wa Mains. Kufuatia kikao hicho, Njia ya msingi ya dharura iliyoonekana inafaa ni kutafutwa kwa Umeme wa Majenereta yenye uwezo mkubwa wa kutosheleza haja, huku suluhisho la kudumu la kupatikana kwa umeme huo likiendelea kufuatiliwa kidogo kidogo. Kamati ilielezwa kwamba, baada ya kikao hiki kukaa, maamuzi yaliyowafikiwa  ni kutafutwa kwa Wahisani watakaoisaidia Serikali kwa kuipatia fedha za ununuzi wa majenereta yaliyohitajika. Hata hivyo, Kamati haikuweza kupatiwa taarifa zozote juu ya aina ya majenereta yaliyotakiwa ama kupendekezwa na kikao hicho kama vile ilivyokoseshwa gharama za majenereta hayo.
Mheshimiwa Spika:
Hatua iliyofuata ni kuwatafuta Wafadhili hao, ambapo Kamati imeshindwa kupata uhakika wake, ni nani na kupitia Mradi gani, Wafadhili hao wamejuilishwa juu ya haja ya ununuzi wa majenereta. Hii ni kwa sababu, wakati wa mahojiano, Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme amekiri mbele ya Kamati kwamba, yeye hafahamu chochote iwapo ni Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo ama ni kikao hicho maalum cha Maafa, kilichosimamiwa na Makatibu Wakuu ndicho kilichohusika na kupeleka ombi (Proposal) la Mradi huo kwa Wafadhili. Hata hivyo, Kamati imejiridhisha kwamba, wafadhili hao ambao ni Norway, Uingereza na Sweden, walipatikana na kukubali kuisaidia Zanzibar kutokana na hali ya giza ambapo Msimamizi Mkuu wa matumizi ya fedha zilizotolewa na Wahisani hao, ilikuwa ni nchi ya Norway na kwa hatua hii ndie alieteua Mshauri Mwelekezi ambapo Kamati ilijuilishwa ni Kampuni ya ‘Norplan’ iliyopo Norway.

Mheshimiwa Spika:
Baada ya Kampuni ya ‘Norplan’ kuteuliwa na Ubalozi wa Norway kuwa Mshauri Mwelekezi wa Mradi ama Ununuzi wa Majenereta yote 32, Kamati imejuilishwa kwamba, Kampuni hii ndio iliitafuta Kampuni ya Mantrac na kuipa kazi ya kuleta majenereta hayo na kuyafunga (Supply and Installation) katika eneo la Mtoni- Zanzibar, huku ikiingia Mkataba na Kampuni ya Salcom Contractor, iliyopewa kazi ya kueka msingi (Base Line) ya eneo lilitumika kukaa majenereta hayo. Tunapenda ifahamike kwamba, ufafanuzi huu ndio uliotolewa na Uongozi wa Shirika kwa Kamati, ingawaje kwa uchambuzi wa Kamati, suala la nani aliehusika na ununuzi wa Majenereta hayo, litaelezwa hapo baadae.
Kampuni ya Mantrac na Mahusiano yake na Shirika:
Mheshimiwa Spika:
Kamati imeelezwa kwamba Kampuni ya ‘Unatrac International’ yenye makao yake makuu nchini Marekani, ni Kampuni iloyopewa ruhusa kamili na Kampuni ya ‘Caterpillar’ yenye makao makuu yake nchini Marekani, ya kuuza vifaa vyote vinavozalishwa na Kampuni hii ya ‘Caterpillar’. ‘Unatrac International’ iliyopo Marekani ndio yenye dhamana hiyo huku ikiwa na matawi yake katika nchi 5 za Afrika, ikiwa ni pamoja na nchini Tanzania. Kwa lugha hii, Kampuni hii ya Mantrac Tanzania Ltd, nayo imepewa ruhusa kamili ya kuuza bidhaa za Kampuni ya ‘Caterpillar’ nchini na kupata msaada kamili wa Kampuni ya ‘Caterpillar’ juu ya bidhaa zozote itakazoziuza ama kuvifanyia biashara yoyote kwa Kampuni hii ya ‘Mantrac Tanzania Ltd’.
Mheshimiwa Spika:
Meneja wa Kampuni hii akitoa ufafanuzi wake kuhusiana na namna gani walilifahamu Shirika la Umeme, kiasi ya kuweza kupewa kazi husika, alithibitisha kwamba, waliwahi kufika katika Shirika na kuzieleza kazi zao tokea hata halijatokea tatizo la kuzimwa kwa umeme katika kipindi cha miezi mitatu mfululizo. Alisema kwamba, baada ya kutokezea tatizo la umeme, wao waliitwa (akikusudia kupitia tangazo la ‘Qoutation’) na kufanikiwa kupeleka maombi yao na hatimae walifanikiwa kushinda na kupewa kazi hiyo ya ‘supply and installation’ ya majenereta.
Mheshimiwa Spika:
Hata hivyo, suala la msingi lilikuwa, je fedha zilizolipwa kununulia majenereta hayo zimetoka katika Mfuko wa Shirika, Akaunti maalum ya Mradi iliyosimamiwa na Shirika ama zimetoka moja kwa moja kutoka mikononi mwa Wahisani (Uingereza, Sweden na Norway)? Katika kutoa ufafanuzi wa suala hili, Meneja wa Shirika alieleza Kamati kwamba, fedha hizo hazitokani na Akaunti yoyote inayoihusisha Shirika lake, yaani sio kupitia Akaunti ya Shirika wala Akaunti iliyolipwa kutoka katika Mradi huu. Hata hivyo, baada ya kuwasili Ndg. James Serre, Meneja Mauzo wa Kampuni ya Mantrac, aliithibitishia Kamati kwamba wao wamelipwa USD 1,208,800 kupitia Cheki iliyotolewa na Benki ya Watu wa Zanzibar, ambayo tumifanya kuwa Kiambatanisho Nam 94.
Uhalisia wa Mkataba baina ya Kampuni ya Mantrac Tanzania Ltd na Shirika
la Umeme:
Mheshimiwa Spika:
Pamoja na maelezo ya hapo juu, Kamati ilipofika mbele ya Kampuni ya Mantrac ili kupata ufafanuzi wa mambo mbali mbali, walijisafisha kwa kueleza kwamba, wamefuata taratibu zilizopo katika kuuza majenereta hayo, na zaidi maelezo yao wakiyasimamia kwa Mkataba ulioingiwa baina yao na Shirika la Umeme. Kamati nayo imeupitia Mkataba huo na nawaomba Waheshiwa Wajumbe waupitie kama unavyotolewa ufafanuzi katika ripoti yetu kuanzia ukurasa wa  119 hadi 126 ya ripoti yetu, ila tunachotaka kieleweke kwa urahisi ni kwamba, majenereta hayo yamenunuliwa kwa tuhbitisho wa Mkataba ambao unadhihirisha wazi kwamba, Shirika la Umeme limehusika moja kwa moja katika kupatikana kwa majenereta hayo.
Mahusiano ya Shirika la Umeme na Kampuni ya China Railway Jianchang
Engineering Co. (T) Ltd:

Uhalisia wa Mkataba baina ya Kampuni ya Mantrac Tanzania Ltd na Shirika
la Umeme:
Mheshimiwa Spika:
Kama tulivyokwisha eleza hapo kabla, kwamba mara tu baada ya Kampuni ya Mantrac kupewa kazi ya kuwauzia Majenereta Shirika la Umeme na kuyafunga, kama Kampuni, walilazimika kumtafuta Mjenzi wa Msingi (Civil Works) na kuweka hali ya usafi kwa eneo lote litakalotumika kuwekea majenereta hayo. Kazi hiyo kwa bahati njema, iliombwa na Kampuni kuu mbili; moja ni hii ya Kichina, ya China Railway Jianchang Engeneering Co. (T) Ltd, ama umaarufu wake ni (CRJE), na Kampuni ya pili ni Salem Construction ama umaarufu wake ni (SALCON). Kampuni hizi ziliingia katika ushindani wa bei na namna ya kufanya kazi hiyo, ambapo kwa Upande wa Kampuni ya CRJE walitaka kupewa kazi hiyo kwa gharama za USD 600,413.58 wakati Kampuni ya Salcon, wangeliifanya kwa USD 431,622.80.
Mheshimiwa Spika:
Ili Kampuni iridhiwe, ni lazima ikubaliwe na Shirika  pamoja na kupata idhini ya Kampuni ya Mantrac. Kwa bahati njema, Shirika halikuwa na pingamizi ya kupewa kwa Kampuni yoyote hapo kabla, ingawaje walikiri kwamba, Kampuni ya Salcon ina nafasi nzuri ya kushinda kwa sababu hata bei yake ni ndogo kwa ghrama ya USD 168,790.78.
Mheshimiwa Spika:
Kwa upande wa Kampuni ya Mantrac waliieleza Kamati kwamba, wao tokea mwanzo kama ndio waliopewa kazi kuu ya kuyafunga Majenereta hayo, walitaka kazi ya kuweka Msingi wake (Civil and Electro-mechanical works at the power plant) ifanywe na Kampuni ya Salcon. Hata hivyo, kwa mujibu wa barua ya Tarehe 1/03/2010 yenye kumbu kumbu namba ZECO/CONF.2/10/2/GEN/VOL.11/367 iliyoandikwa na Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika, ambae sasa ndie Meneja Mkuu, Ndg. Hassan A. Mbarouk, inaelekeza kama kwamba, Kampuni ya Mantrac ilihitaji zaidi kuipa Kampuni ya Kichina ya CRJE zaidi kuliko ya Salcon na hivyo, Shirika kwa barua hiyo imeitambua Kampuni hiyo ya CRJE kuwa ndio iliyopewa kazi.
Mheshimiwa Spika:
Aidha,  mnamo wiki tu baadae, Meneja Mkuu huyu huyu wa Shirika la Umeme, ameweka bayana kwamba, kumbe ni Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika, ndiyo iliyoamua kazi hiyo apewe Kampuni ya Kichina ya CRJE badala ya Kampuni ya Salcon na matokeo yake, kazi hiyo ikaanza kufanywa na Kampuni ya CRJE. Kwa hali yoyote ile iwayo, jambo la msingi ni kufahamu kwamba, Kampuni ya Salcon haikupewa kazi hiyo kabla, mbali na kuonesha uwezo wao wa kuifanya kazi hiyo kwa ubora na gharama ndogo zaidi.
Mheshimiwa Spika:
Jambo la kusikitisha ni kwamba, Kamati ilielezwa na Uongozi wa Mantrac kwamba, Msimamizi wa Mradi huu Kampuni ya Norplan, haijakubali kazi hiyo kupewa Kampuni ya CRJE na wakatishia kujitoa katika Mradi na hili liliwashtua Uongozi wa Shirika na kuamua kukubaliana kwa shingo upande na matakwa ya Mfadhili ambae anasimamiwa na Mshauri Mwelekezi ‘Norplan’. Matokeo yake, Kazi hiyo ikanyang’anywa kwa Kampuni ya CRJE na kupewa Kampuni ya Salcon.
Mheshimiwa Spika:
Jambo hili ilikuwa ni sawa na kuvunjwa kwa Mkataba kwa Kampuni ya CRJE na ni sawa na kusema ‘wamenyang’anywa tonge mdomoni’ na kwa namna yoyote ile walidai fidia ambao ingeligharimu USD 86,613.07 ingawaje baadae ilikubalika kulipwa USD 20,786.00 ambazo kwa wakati huo ni sawa na Tsh. 31,179,000/- zilizotoka katika Account ya Shirika la Umeme, kwa kile kinachoitwa uzembe na uroho wa kulazimisha mambo kwa utashi wa viongozi wachache wa Bodi ya Wakurugenzi, iliyofanya maamuzi bila ya kuzingatia uhalisia wa kazi na ufanisi wake.
Mheshimiwa Spika:
Katika waraka Namba 438 Uongozi wa Shirika uliomba idhini kwa Bodi hii hii ya Wakurugenzi, iliyosababisha hasara hizo, kutoa idhini ya kulipwa kwa CRJE fedha hizo USD 20,786.00 na Kamati imehakikishiwa kwamba idhini hiyo ilitoka kama ilivyoombwa na hatimae CRJE walilipwa.

Hoja kuhusiana na Taratibu za Manunuzi:
Mheshimiwa Spika:
Bila ya shaka bado ipo haja ya kuweka wazi mtazamo wa Kamati juu ya taratibu za upatikanaji wa Majenereta 32 kama ulifuata Sheria, na zaidi kwa kuzingatia kwamba, suala hili limeonekana kupokea miono tofauti inayokinzana, baina ya Uongozi wa Shirika, Uongozi wa Kampuni ya Mantrac na Kamati hii. Kwa hivyo, hebu sasa tuzingatie ile hoja iliyotolewa na Kampuni ya Mantrac juu kununuliwa kwa Majenereta haya kwa Njia ya Dharura (Emergency Procurement).
Mheshimiwa Spika:
Kama tulivyokwisha eleza kwamba, kama utafanya rejea ya maneno ‘Emergency Procurement’ katika Sheria Na.9 ya mwaka 2005 na Kanuni zake, utakutana na kanuni ya 27(1) inayozungumzia suala hili kwa uwazi wake. Hebu na Tujikumbushe kwa kunukuu haya yafuatayo:
“Katika mazingira yasiyo ya kawaida na ya dharura, pale ambapo Afisa Mhasibu atazingatia kwa maslahi ya Umma, kwamba manunuzi yafanywe, ambayo gharama zake zinazidi kiwango kilichopewa katika Kanuni hizi na muda hauruhusu mamlaka kutumia njia ya kawaida, (Afisa huyo Mhasibu) kwa kuwajibika yeye mwenyewe juu ya manunuzi hayo (atafanya manunuzi hayo), lakini mara tu baada ya kufanya manunuzi hayo, atamuarifu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, akimueleza sababu zilizompelekea yeye kuacha kufanya manunuzi kwa njia ya kawaida na kopi ya barua hiyo itapelekwa kwa Bodi yenye mamlaka ya kuthibitisha (kwa Shirika, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika) na Idara ya Uhakiki Mali na Mitaji ya Umma4
Mheshimiwa Spika:
Ukifanya rejea ya nukuu hiyo hapo juu na zaidi katika maneno yaliyokozeshwa,  yatakufahamisha kwamba, pamoja kukubaliana kwamba, kweli ununuzi wa majenereta hayo ulifanywa katika kipindi cha dharura kubwa, lakini jee taratibu za ununuzi wa dharura kwa mujibu wa Sheria zilifuatwa? Jawabu yake kwa Kamati ilikuwa nyepesi mno, kwamba haikufuatwa kwa sababu Uongozi wa Shirika umeshindwa kuthibitisha kufuata kwa taratibu hizo kwa kumuarifu Katibu Mkuu anaehusika na Fedha ama kopi ya barua hiyo kupelekwa kwa Bodi na Idara ya Uhakiki Mali na Mitaji ya Umma.
Mheshimiwa Spika:
Kama hili halitoshi, unaweza pia kufanya rejea ya kifungu cha 32(2) cha Sheria Namba 9 ya mwaka 2005, ambapo utakutana na maelezo yafuatayo”
“The choice of a procurement method shall first be approved by the Tender Boards”
Mheshimiwa Spika:
Kwamba, Ni Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme iliyokuwa na wajibu wa kuthibitisha haja ya kutumika kwa njia ya ‘Emergency Procurement’ na sio Kikao chochote ikiwa cha Makatibu Wakuu ama chenginecho. Kwa kuwa Kamati imeshindwa kupata uthibitisho wa kuidhinishwa na Bodi, aidha kwa kuridhishwa kwamba, hakuna Bodi yoyote ya Zabuni ya Shirika iliyokaa na kuridhia njia hii, hakuna haja ya kurefusha sana maneno ya ufafanuzi wa hoja hii, Kamati imejiridhisha kwamba, manunuzi ya majenereta hayo hayakuwa halali kisheria.

Matumizi ya Majenereta 32:
Mheshimiwa Spika:
Kama tulivyokwisha eleza awali, kwamba, kwa namna yoyote hoja hii ili ijibike vizuri, ni lazima tuangalie iwapo majenereta yote 32 yaliyonunuliwa kwa utaratibu wa hapo juu yanatumika ipasavyo kama ilivyokusudiwa kwa maslahi ya wananchi wa nchi hii. Kamati ilitembelea eneo la majenereta hayo yaliyopo eneo la Mtoni na kuzungumza na mhusika aliyekuwepo katika eneo hilo na kupata maelezo kwamba, majenereta yote isipokuwa moja, yanatumika na kufanya kazi kama kawaida, Kamati pia ilitaka kujaribiwa kwa kuwashwa ili ijiridhishe, jambo ambalo limefanyika kwa uzuri kabisa.
Mheshimiwa Spika:
Wakati Kamati inahoji juu ya jenereta moja ambalo halikuwepo wakati wa ukaguzi, ilielezwa kwamba liliharibika wakati wa kuletwa kwake na hivyo ikalazimika kurejeshwa kwa Kampuni ya Mantrac. Hata hivyo, katika kikao cha pamoja na Kampuni hiyo, Dar es Salaam, ilielezwa kwamba tayari jenereta hilo limeshawasilishwa na kufungwa katika eneo la Mtoni na linafanya kazi. Kwa maana hii, Kamati imejiridhisha kwamba, majenereta yote 32 yanafanya kazi.
Mheshimiwa Spika:
Pamoja na maelezo haya, ni vyema sasa tukaingia ndani kidogo katika ufahamu wa hoja husika inayohoji “Iwapo upatikanaji wa majenereta 32 yaliyopo Mtoni ulifuata sheria zinazohusika na kwa nini hayatumiwi kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar?”. Hoja hii kwa upande wa maneno tuliyoyakozesha inahoji juu ya sababu zinazopelekea majenereta hayo kutotumiwa kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar. Yaani, ili kuijibu vizuri, ni lazima kwanza ufahamu iwapo bado yanafanya kazi ama laa, lakini hoja yenyewe inakubali kwamba majenereta yapo na yanafanya kazi, lakini kwa nini hayafanyi kazi iliyokusudiwa kwa ufanisi wake ili wananachi wa Zanzibar wakaondokewa na tatizo la mgao ama kukosa umeme wakati wowote wa maisha yao ya sasa!
Mheshimiwa Spika:
Sasa ni vyema tukajikumbusha kwamba, majenereta haya yamenunuliwa wakati wa kukosekana kwa umeme Unguja na kwa ajili ya kuondosha tatizo kama hili wakati wowote wa dharura, yaani yalipaswa yatumike ipasavyo wakati huo wa uhaba wa umeme lakini pia kusiwe na haja yoyote ya kuwepo kwa mgao wa umeme wakati huu tunaondelea nao. Yaani kwa kuwa hivi sasa wananchi wote wa Unguja wanakosa umeme kwa muda wa saa 1:30 katika kipindi cha usiku, kulikuwa hakuna haja ya kuwepo kwa hali hii, kwa sababu majenereta 32 kama yatatumika ipasavyo na kwa lengo lililokusudiwa, tatizo hili halitakuwepo. Aidha, pia hakukuwa na haja ya wananchi kukosa huduma ya umeme kutokana na kuzimwa masaa 12, 6 ama hata saa 1, kama inavyofanyika takriban katika siku nyingi za mapumziko na siku za kawaida wakati wa asubuhi, mchana na usiku.
Mheshimiwa Spika:
Kama hali ndio hii, jawabu ya wazi ni kwamba, majenereta hayo 32 hayatumiwi ipasavyo kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar ambao bado wanaendelea kupata machungu ya kukosa umeme wa uhakika na matokeo yake ni kuharibikiwa katika shughuli zao za maisha ya kila siku. Tunapenda ifahamike wazi kwamba, wakati wote wa kazi za Kamati, mjadala juu ya kutotumika ipasavyo kwa majenereta hayo haukubishaniwa. Yaani hata Shirika linakiri kwamba kuyaendesha majenereta hayo ni gharama kubwa na ni sehemu ya kulitia hasara Shirika, lakini jambo muhimu ni kufahamu sababu zipi zinazopelekea majenerea hayo kutotumika kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika:
Kabla ya kuanza kueleza sababu hizo, Uongozi wa Shirika umeieleza Kamati kwamba, majenereta hayo baada ya kumalizika kipindi cha miezi mitatu ya giza Unguja nzima, sasa yanatumika kupunguza mzigo wa usumbufu wa umeme kwa wananchi kwa kuwashwa wakati umeme unapozimwa. Yaani kama umeme ungelistahiki kuzimwa kwa masaa matatu (kwa mfano), saa 1 ama 12 wakati wa asubuhi, mchana na usiku; basi kwa kutumia majenereta hayo, umeme ungelipatikana kwa kutumiwa majenereta hayo kama mbadala wa umeme husika. Pia husaidia kupunguza mzigo wa matumizi ya umeme wakati wa matumizi makubwa kutokana na shughuli ama tukio Fulani. Kwa mfano wakati wa sikukuu yoyote ile, umeme hutumika kwa kiwango kikubwa, na majenereta hayo husaidia kuongeza uzalishaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika:
Kwa maelezo haya, ni wazi kwamba majenereta hayo yanatumika, labda tukitaka yatumike ipasavyo, ndio jambo linaloshindikana. Na hili linatokana na sababu kadhaa, lakini kubwa ni ile inayoelezwa na Shirika wakati wote kabla ya Kamati hii kulifanyia kazi suala hili, nayo ni kukosekana kwa mafuta ya kuendeshea majenereta hayo. Hoja hii pia ilisimamiwa wakati wote wa kazi za Kamati, na ilifahamika kwa uwazi wake pale Kamati ilipokutana na Kampuni ya Mantrac. Yaani muda wote huo Kamati ilielezwa kwamba, mafuta yaliyohitajika kuendeshea majenereta hayo ni ghali sana na ni tofauti na mafuta ya kawaida ambayo hutumika kwa majenereta ama mashine nyengine.
Mheshimiwa Spika:
Wakati Kamati inapata ufafanuzi wake, ilielezwa na wauzaji wa majenereta hayo kwamba yanatumia mafuta ya Diesel kama diesel nyengine, ingawaje wao kama Kampuni na zaidi wakati wa ‘warranty’ ya majenereta hayo, waliwashauri Shirika kwa maslahi ya uhai wa muda mrefu wa majenereta wasitumie diesel hii, ambayo mara nyingi huwa na ‘calcium’ ambayo huathiri kidogo kidogo uimara wa majenereta. Kwa maana hii, Kamati imeridhika kwamba, majenereta hayo hayatumiwi ipasavyo kwa sababu Shirika halina uwezo mkubwa wa kununua mafuta yanayohitajika.
Mheshimiwa Spika:
Wakati Kamati inataka kujua sababu zipi zinazopelekea Shirika hili kushindwa kumudu gharama za mafuta, wakati lilishiriki ipasavyo kununuliwa kwake, na lilipaswa kuyaona haya kabla ya majenereta hayo kununuliwa, ilielezwa na Meneja wa Shirika kwamba, hawapati msaada wowote wa uendeshaji wake kutoka Serikalini (Administrative Costs), kinyume na ushauri ambao wataalamu wa Shirika waliutoa wa kuitaka Serikali ama ingeongeza kodi wakati wa kuingizwa kwake, ama kuchangia huduma za uendeshaji kama vile ambayo hata TANESCO wanapata kutoka kwa Serikali ya Muungano. Kama ni hivi, si vibaya kusema kwamba, Serikali Kuu imelibebesha Shirika mzigo usiouweza wa kuyasimamia na kuyashughulikia Majenereta yanayotumia mafuta ya gharama kubwa.
Mheshimiwa Spika:
Muhtasari wa Mambo yaliyobainika na Kamati kufuatia Uchunguzi wake wa
Hadidu hii Rejea:
  1. Unununi wa Majenereta 32 umefanywa na Shirika la Umeme kupitia Ufadhili wa USD 1,208,800.00 na kwa namna hii, Shirika lililazimika kununua Majenereta hayo kwa kufuata Sheria zinazohusika na Manunuzi ya Mali za Serikali, Zanzibar.
  2. Shirika limekiuka taratibu za manunuzi kwa kutoshirikisha vyombo vyake vinavyohusika na kazi ya manunuzi, ikiwa ni pamoja na Bodi ya Zabuni ya Shirika na Kitengo cha Manunuzi (PMU).
  3. Shirika limeingia hasara ya Tsh 31,179,000/- ya malipo ya faini kwa Kampuni ya Kichina (China Railway Jianchang Engeneering Co. (T) Ltd (CRJE), ambapo hasara hii imesababishwa na uzembe na ubinafsi wa aliekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Wajumbe wote wa Bodi hii kwa ujumla.
  4. Majenereta 32 hayatumiwi ipasavyo kinyume na makusudio ya kununuliwa kwake, kwa sababu Shirika lilikurupuka kuyanunua bila ya kuangalia ukubwa na uzito wa gharama za uendeshaji wake.
  5. Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme ametoa maelekezo yasiyo ya kweli kwa kukana Shirika lake kuhusika moja kwa moja na ununuzi wa majenereta 32.
  6. Serikali haijalichukulia kwa makini tatizo la kukosekana kwa umeme kwa muda wa miezi mitatu mfululizo mwaka 2010 kisiwani Unguja, ikiwa ni pamoja na kutofanya ukaguzi wowote wa matumizi ya fedha zilizotumika kurejeshea huduma hiyo; kufanya utafiti na kufahamu chanzo cha tatizo na utatuzi wake; pamoja na kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria wale wote waliohusika na kadhia hii.
  7. Shirika halikuzingatia uwezo wa kuyaendesha majenereta waliyoyanunua na hivyo kununuliwa kwake kumebakia kuwa mzigo mzito wa Shirika na Serikali kwa ujumla, huku Serikali pia haioni haja ya kusaidia uendeshaji wa majenereta hayo.
  8.   Kwa vile  gharama za kununua mafuta ya disel maalum ni kubwa, na kwa sababu majenereta hayo yakitumi mafuta ya disel hii ya kawaida hayatakuwa na madhara, basi ni vyema Shirika litumie mafuta hayo kwa dharura.  
Mheshimiwa Spika:
HADIDU REJEA YA SITA:
KIWANGO CHA DENI LINALODAIWA ZANZIBAR NA TANESCO, NA IWAPO KUNA SABABU ZA MSINGI ZA KUENDELEA KUWEPO KWA DENI HILO NA ATHARI ZAKE KWA MASLAHI YA ZANZIBAR.
Mheshimiwa Spika:
Hadidu hii rejea ilimalizia kufuatiliwa Tarehe 01/10/2012 baada ya Kamati kukutana moja kwa moja na Uongozi wa Shirika la Umeme la Tanzania, TANESCO na Shirika la Umeme la Zanzibar liliwakilishwa na Meneja Mkuu aliefuatana na Meneja wake wa Fedha, Ndg. Riziki Faki Hamad. Kabla ya kikao hicho kilichofanyika Dar es Salaam, Kamati iliwahi kupata maelezo ya hoja hii kutoka kwa Uongozi wa Shirika na ndipo ilipoamua kwenda Dar es Salaam na kukutana na TANESCO. Kwa namna Kamati ilivyolifuatilia suala hili, inaona busara ufafanuzi ufuatao ukapatikana:
Historia ya Deni:
Mheshimiwa Spika:
Historia ya deni la Shirika la Umeme la Zanzibar inaanza katika mwaka 2008, kuanzia Tarehe 1 Januari. Inawezekana sana kukawa na deni kabla ya muda huo, jambo kubwa la kuzingatia ni taarifa iliyowasilishwa kwa Kamati, inayoonesha mchanganuo wa deno hilo kuanzia muda tuliokwisha kuueleza (Kiambatanisho Nam 99), huku maelezo yote kuhusiana na deni hili kutoka kwa Meneja wa ZECO na hata Uongozi wa TANESCO, yanakubaliana kwamba deni hilo lilianza wakati huo. Kwa muda huo deni lililokuwa linadaiwa kwa ZECO ni Tsh. 1,871,545,517.70 na kulipwa kidogo kidogo, mara mbili kwa mwezi, ila kutokana na sababu kadhaa, deni hilo hadi kufikia Tarehe 1/06/2012 linakisiwa kufikia Tsh. 22,767,047,816.06
Mheshimiwa Spika:
Inaelezwa pia kwamba, Shirika la Umeme la Zanzibar linalifahamu deni hilo katika ngazi mbili. Sehemu ya kwanza ni deni halali wanalodaiwa na TANESCO ambalo hili halibishaniwi na sehemu ya pili ya deni hilo ni deni ambalo Shirika hili linaona halina usahihi wowote ule wa kudaiwa na TANESCO. Katika hali hii, inafaa upatikane ufafanuzi juu ya madai hayo ya Shirika, na hoja zinazofuata zinatoa ufafanuzi huo:
Msingi wa Deni na kuendelea kwake:
Mheshimiwa Spika:
Miongoni mwa vipengele muhimu katika kutoa ufafanuzi wa hoja hii, ni pamoja na kujiridhisha juu ya sababu za msingi zinazopelekea kuwepo kwa deni hilo. Na inafahamika pia kwamba, Umeme ambao Zanzibar tunatumia unatoka Tanzania bara, ambapo Shirika la Umeme la Tanzania, TANESCO ni wakala wa Serikali ya Tanzania lenye jukumu la kununua na kusambaza ama kutoa huduma ya umeme Tanzania bara. Wakati huo huo ifahamike kwamba, TANESCO hununua umeme kutoka nchi jirani ambazo ni Uganda, Zambia na Kenya, na katika hali hii kwa namna yoyote ile, haliwezi kumuuzia mtu ama taasisi nyengine kwa hasara.


Mheshimiwa Spika:
Lakini pia imeelezwa kwamba, TANESCO hununua umeme huo kwa nchi hizo bila hata ya kupunguziwa bei, na kwa kawaida kila nchi kati ya hizo, kuna chombo kinachodhibiti bei, ambacho kwa kawaida huwa na asilimia moja ya mauzo ya kila mwezi, ambayo kupatikana kwake kunatokana na kukatwa asilimia moja ya fedha hizo kupitia mapato ya Mashirika ya Umeme na hatimae huchangia kuendesha shughuli za Mamlaka hizo za kudhibiti bei. Kwa Tanzania bara, kuna chombo kiitwacho EWURA (Mamlaka ya Udhibiti wa Masuala ya Nishati na Maji, Tanzania), ambayo pamoja na majukumu mengine, ina dhima ya kudhibiti bei ya umeme unaosambazwa kwa wananchi na watumiaji mbali mbali nchini Tanzania. Na kwa maana hii, kuongozeka kwa bei ya Umeme dhidi ya ZECO, pia kunanasibishwa sana na udhibiti wa bei ya umeme kuanzia mwaka 2008, chini ya EWURA.
Mheshimiwa Spika:
Kwa maana nyengine, kabla ya mwaka 2008, TANESCO ndio iliyokuwa inadhibiti bei ya umeme kwa wateja wake wote, ikiwa ni pamoja na Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO), lakini kuanzia mwaka 2008, suala la bei ya umeme kwa wateja wake, TANESCO ilitakiwa kutoa kiwango ambacho EWURA wamekiidhinisha, hali ambayo sio tu kulifanya Shirika hili la TANESCO kutoza bei iliyoidhinishwa na EWURA, lakini pia hulazimika kutoa asilimia moja ya mapato yake na kuipa EWURA, Mamlaka ambayo inategemea kujiendesha kupitia fedha hizo za asilimia moja, zinazotozwa kwa TANESCO na wateja wengine ama vyombo vilivyo chini ama katika mamlaka yake.
Mheshimiwa Spika:
Katika kulisisitiza suala hili, Uongozi wa ZECO ukiwa pamoja na Uongozi wa TANESCO, waliieleza Kamati kwamba, kuanzia Januari 2008, bei ya umeme iliyokuwa inauzwa kwa ZECO ni Shilingi 34/- kwa Uniti (kWh); Shilingi 4,755/- kwa kVA na Shilingi 8,534/- kama ‘Customer Service Charge. Kwa maana hii, maelezo ya Uongozi wa ZECO yalithibitisha kwamba, Shirika lao lilikuwa angalau linamudu kulipa gharama hizo za umeme kwa TANESCO, kwa kiwango kinachoridhisha. Na kwa wakati huo, ilielezwa kwamba, katika mwaka wa 2008 Shirika la Umeme la Zanzibar, lilikuwa linadaiwa Tsh. 1.871,545,517.70, wakati ambao EWURA bado haijakabidhiwa dhamana ya kusimamia bei husika kwa TANESCO.

Mheshimiwa Spika:
Aidha, kuanzia mwezi wa Januari, 2011, bei ya umeme iliongozeka kwa wastani wa asilimia 18%.  lakini kutokana na hali kuwa mbaya kila siku na mzigo wa madeni kuongozeka, na zaidi baada ya usimamizi wa EWURA, sasa deni hilo limeongezeka zaidi na kufikia Tsh. 22,767,047,816.06 na Kamati imethibitishiwa kwamba, deni hilo litaendelea kukua siku hadi siku kutokana na utaratibu wa malipo uliopo hivi sasa. Kwa mantiki hii, Kamati imeelezwa kwamba, baada ya kuwepo kwa shughuli za EWURA, ZECO hulazimika kulipia asilimia 3 (Tariff 3) na hii ni baada ya kutoa gharama za usambazaji (Cost of  Distribution) ambazo ni asilimia 21.6. Ni sawa na kusema kwa utaratibu huu kwamba, bei ya umeme ilikuwa shilingi 65.86 kwa kWh; Shilingi 8,114.40 kwa kVA na Customer Service Charge ni Shilingi 10,146.00.
Mheshimiwa Spika:
Vile vile kuna jambo la msingi kuhusiana na kuwepo na kuendelea kwa deni hilo. Kamati imeelezwa kwamba, kwa mujibu wa huduma ya umeme unaouzwa kwa ZECO, Shirika hili hulazimika kulipia takriban Bilion 3 kwa kila mwezi, wakati uwezo wa Shirika hili la Umeme la Zanzibar, ni kulipia Bilioni 1.6 tu, tena hulipia kwa awamu (Installments) mbili kwa mwezi. Aidha, Kamati imefahamishwa kwamba, makusanyo ya ZECO kwa malipo ya humua yote wanayoitoa Zanzibar, ni sawa na Bilioni 3 kwa kila mwezi, na ni hizo hizo wanazotakiwa kulipa kwa  TANESCO kwa mwezi, kwa maana hii, iwapo ZECO wataamua kulipia deni wanalodaiwa na TANESCO, hawataweza kujiendesha.
Mheshimiwa Spika:
Kutokana na hali hii, ndio maana ZECO hulipia Bilioni 1.6 (tena kwa kujitutumua), wakati ilitakiwa ilipie Bilioni zote 3. Hoja kubwa iliyoelezwa kwa Kamati kuhusiana na suala hili, ni malipo makubwa (Tariff) inayotozwa kuanzia mwaka 2008, kiasi kikubwa cha hali hii kimesababishwa na EWURA. Madai haya yaliifanya Kamati kuona ipo haja ya kukutana na EWURA, ili kujiridhisha juu ya maelezo yaliyotolewa na Shirika la Umeme la Zanzibar na kuthibitishwa na Uongozi wa TANESCO, lakini kutokana na uchache wa muda, Kamati haikupata nafasi ya kukutana na Uongozi wa EWURA.


Mheshimiwa Spika:
Hata hivyo, Kamati inakubaliana kwamba, Shirika la Umeme halina uwezo wa kulipa deni la TANESCO kwa ukamilifu wake, lakini pia hali hii, pamoja na mzigo wa lawama kutupiwa EWURA, Kamati inaamini kama ZECO wangelisimamia ipasavyo vyanzo vyake vya mapato, na kurekebisha kasoro nyingi za utendaji, kama tulivyozieleza hapo awali katika hadidu rejea zilizotangulia, basi isingelikuwa na mzigo wa deni kubwa kama ililonalo na kama ingelilazimika kuwa na deni hilo, basi ukubwa wake na athari zake kwa wananchi wa Zanzibar, zingelipungua sana.
Hatua zilizochukuliwa na Serikali kulipatia ufumbuzi deni la ZECO kwa TANESCO:
Mheshimiwa Spika:
Wakati Kamati inafanya mahojiano na Mkurugenzi kuhusiana na hoja hii, ilifahamishwa kwamba, pamoja na deni linaloikabili Shirika la Umeme la Zanzibar, deni hilo lilikuwa kubwa zaidi hapo awali na hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ilifuatilia suala hili kwa kukaa pamoja na Wizara ya Nishati na Madini ya Tanzania, pamoja na Uongozi wa mashirika yote mawili, ZECO na TANESCO, Tarehe 27/01/2012, kwa ajili ya kuzungumzia namna gani deni hilo litashughulikiwa, lakini pia ilikuwa ni sehemu ya ZECO kuwasilisha malalamiko yao na kero zao, juu ya upatikanaji wa huduma ya Umeme kutoka kwa Kampuni ya TANESCO.
Mheshimiwa Spika:
Kikao hicho kilichokuwa na ajenda kuu mbili, ambazo ni deni la Shirika la Umeme la Zanzibar kwa TANESCO na ajenda ya pili ilihusiana na Ongezeko la bei za umeme kwa Shirika hili la Umeme la Zanzibar (ZECO). Kikao hicho pia kilikusudia kuondosha kasoro zilizopo na mzozano wa siku nyingi, kilihimiza sana ushirikiano wa pamoja kwa Taasisi mbili hizi, huku kikijikita kufanya maamuzi kama yanavyofahamika katika Kiambatanisho Namba 100 cha ripoti yetu.
 Deni halisi linalodaiwa kwa ZECO:
Mheshimiwa Spika:
Deni halisi lililokuwa linadaiwa kwa Shirika la Umeme la Zanzibar, ambapo kabla ya kufanyika kwa kikao cha pamoja baina ya Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wizara ya Nishati na Madini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shirika la Umeme la Zanzibar lilikuwa na deni la Tsh. Bilioni 62.37, lakini kutokana na mazungumzo hayo, iliwafikiwa kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano italipa tofauti ya Tsh. 39 bilioni Nukta 7 (39,719,620,794.42) huku deni linalobakia, yaani Bilioni 22 (22,654,923,389.22) litaendelea kuwa chini ya ZECO.
Mheshimiwa Spika:
Aidha, imeelezwa kwamba, ili deni hilo la Bilioni 22 kuweza kulipwa, mchanganuo uliokubalika ni pamoja na ZECO kutakiwa kulipa Tsh. 5,067,297,860.18 kwa deni linaloanzia mwezi wa Januari 2008, hadi Disemba 31, ya mwaka 2010. Sambamba na hili, pia walitakiwa kulipa kwa kipindi kilichoanzia Januari 1, 2011 hadi Januari 14, 2012 jumla ya Tsh. 17,587,625,529.04.
Mheshimiwa Spika:
Pamoja na ufafanuzi huo hapo juu, kuhusu kima halisi cha malipo ya TANESCO ambayo ni dhima ya ZECO kuhakikisha kinalipwa, Kamati imefahamishwa kwamba, mwelekeo wa malipo hayo utapatikana mara tu baada ya EWURA watakapokamilisha tathmini ya gharama. Hii ni kwa sababu, mpaka Kamati inafika kuifanyia kazi hadidu hii rejea, EWURA bado hawajakamilisha kufanya tathmini halisi ya TANESCO, ili kujua namna gani wateja wake, ikiwa ni pamoja na ZECO watalazimika kulipia gharama ya umeme kwa mnasaba wa mabadiliko yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika:
Hata hivyo, Kamati ilifahamishwa kwamba, kwa matarajio ya ZECO, tathmini hiyo ilitarajiwa iihusishe kwa ukamilifu wake kwa mnasaba wa hoja kwamba, Shirika la Umeme la Zanzibar linatofautiana sana na wateja wengine wa TANESCO, lakini pia, haja ya kufanyika kwa tathmini hiyo imetokana na mgogoro wa muda mrefu, unaohusiana na uhalali wa bei ya umeme baina ya ZECO na TANESCO. Hivyo basi, kwa namna yoyote ile iwayo, EWURA wanalazimika kukutana na Uongozi wa ZECO, ili utoe maelezo yao ya kina kuhusiana na suala zima la huduma ya umeme wanayoipata kutoka TANESCO.
Mheshimiwa Spika:
Kwa maana nyengine, EWURA wametafuta Mshauri Mwelekezi, mwenye dhamana ya kufanya utafiti kamili juu ya mapato yanayotokana na TANESCO na hatimae aishauri EWURA juu ya njia bora za kutumika kuhakikisha mapato hayo yanapatikana kwa wakati na kwa manufaa ya Taifa. Katika kufanya utafiti huo, Mshauri Mwelekezi amekutana na TANESCO mara kadhaa na kupata idadi halisi ya wateja wake wanaopata huduma za umeme, lakini kwa bahati mbaya, pamoja na umuhimu wake, Mshauri huyu Mwelekezi, bado hajakutana na Uongozi wa ZECO, ili nao ukatoa maelezo yao kuhusiana na kazi waliyopewa.
Athari za Deni hilo kwa Maslahi ya Zanzibar:
Mheshimiwa Spika:
Kwa ujumla wake inaaminika na kukubalika kwamba, deni hilo lina athari kubwa kwa Zanzibar, za kiuchumi, kisiasa pamoja na kijamii. Kamati ilielezwa hoja hii kwa mnasaba wa Mtumiaji wa mwisho (End User), maelezo haya pia yalisisitizwa kwa kutolewa mfano wa Kampuni za biashara zinazomilikiwa na Mfanya biashara maarufu nchini, Ndg. Salum Bakhressa, ambazo kwa kawaida baadhi yao hupatikana sehemu zote za Jamhuri ya Muungano, kwamba, zinapokuwa Tanzania bara, zinatozwa na kulipia gharama za umeme kwa thamani ya ‘Unit’ moja kwa Tsh. 118 wakati huo huo zinazofanyakazi Zanzibar, hutozwa kwa gharama ya kila ‘Unit’ kwa Tsh. 210. Hii ina maana kwamba, ukichukua gharama za umeme pekee, ni wazi kwamba, wafanya biashara watakimbilia kufanya biashara na kuanzisha viwanda vikubwa nchini Tanzania bara, huku wakiikimbia Zanzibar kwa sababu ya gharama kubwa za umeme.
Mheshimiwa Spika:
Sambamba na hilo, miongoni mwa athari za wazi wazi ni pamoja na mzigo mzito wa gharama za umeme unaowakabili wananchi wa Zanzibar, kutokana na kulazimika kulipia umeme kwa gharama ya juu, huku uwezo wa wananchi walio wengi ni mdogo na kipato chao hakilingani na gharama za umeme wanazolipa kwa ZECO. Suala hili liko wazi, kwamba, mara nyingi husababishwa na ongezeko la gharama za umeme kwa upande wa ZECO, ambapo pia hulazimika kwa namna yoyote ile kuwauzia wananchi kwa gharama ya juu zaidi, ili waweze kujiendesha kwa faida na kuendeleza uhai wa Shirika.
Muhtasari wa Mambo yaliyobainika na Kamati kufuatia Uchunguzi wake wa
Hadidu hii Rejea:
Mheshimiwa Spika:
i.    Shirika la Umeme la Zanzibar hadi mwezi Juni 2012 lilikuwa linadaiwa    Tsh.22,767,047,816.06/- na TANESCO.
ii.      Shirika linashindwa kulipa deni linalodaiwa na hii pia inatokana na kuwepo kwa Uongozi unaoshindwa kusimamia ipasavyo mapato halisi ya Shirika.
iii.   Deni linalodaiwa Shirika la Umeme lina athari kubwa za kiuchumi kwa wananchi na nchi ya Zanzibar.
SEHEMU YA TATU:
HITIMISHO:
Mheshimiwa Spika:
Kwa kawaida katika muongozo wa namna gani Kamati za Baraza zingelimalizia uandishi na uwasilishaji wa ripoti yake, kama ilivyoelekezwa na kanuni ya 121(5) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi, ni kuzungumzia katika sehemu ya tatu ya ripoti husika, Hitimisho ama muhtasari wa mambo ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya Kamati juu ya kazi waliyokwishaifanya. Kabla ya kutoa mapendekezo ya Kamati hii, ni vyema kukupongeza wewe Mhe. Spika na Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa maamuzi yao ya kuipa kazi maamulu (yenye hadhi sawa na Kamati Teule), Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika (P.A.C), jambo hili ni la kihistoria kwa Kamati ya P.AC ya Baraza, mbali na zile kazi zake za kila siku, kama zinavyoelezwa katika Kanuni ya 118(2) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la 2012, leo tunahitimisha kazi maalum ya kuchunguza utendaji wa Shirika la Umeme, tunashukuru na kupongeza hatua hii.
Mheshimiwa Spika:
Ni wazi kwamba, kazi hiyo iliyohitaji utaalaumu wa kina katika kuchunguza na hatimae kutoa ripoti ya Shirika la Umeme la Zanzibar, inaashiria wazi kwamba, Wajumbe wa Kamati hii wamefainikiwa kwa kiasi kikubwa kueleza walichokigundua katika uchunguzi wao, aidha, ni vyema pia tukafahamu kwamba, haikuwa rahisi hata kidogo kuifanya kazi hii, ukizingatia ukweli kwamba, Shirika hili linafanya kazi ya kitaalamu na pasipo kutoa ushirikiano wao wa dhati kwa Kamati, hali ya ugumu wa kupatikana taarifa sahihi pamoja na namna ya kuzitolea ripoti, ingeliikwaza Kamati. Tunapenda tutoe shukurani zetu kwa Watendaji na Viongozi wote wa Shirika, waliotoa mashirikiano yao kwa Kamati, na zaidi kwa zile Taasisi zilizohusika na kazi za Shirika, ikiwa ni pamoja na Uongozi wa Kampuni ya Mantrac ya Dar es Salaam na Shirika la TANESCO, na taasisi nyengine zilizohusika.

Mheshimiwa Spika:
Pamoja na pongezi hizo, Kamati haitaacha kusema kuhusiana na baadhi ya Watendaji ikiwa ni pamoja na Meneja Mkuu wa Shirika, kwa baadhi ya wakati kutotoa mashirikiano yao ya dhati kwa Kamati na hata kujaribu kuficha ukweli, kwa lengo la kuifanya Kamati ishindwe kutimiza wajibu wake. Tunapenda kuwakumbusha kwamba, maamuzi ya Baraza la Wawakilishi, kuipa Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika, kazi maalum ya kuchunguza utendaji wa Shirika la Umeme, badala ya kuunda Kamati Teule, hayakuwa na maana ya kutaka kuukomoa Uongozi wa Shirika ama kutoa hujuma na hutuma dhidi ya Shirika lenyewe.
Mheshimiwa Spika:
Kwa ujumla wake, kazi hii kukabidhiwa kwa Kamati hii, imefanywa kwa nia njema na kuisaidia Serikali pamoja na Shirika lenyewe katika utekelezaji wa majukumu yake,  ili lile lengo la kuanzishwa na kuwepo kwake liweze kuinufaisha nchi hii, lakini zaidi kuwa fanisi katika kutoa huduma zake kwa wananchi. Haitakuwa pia uungwana kwa Kamati kuacha kuwaomba radhi watendaji wa Shirika na Uongozi wake, iwapo kulitokezea kukwaruzana na Wajumbe ama Sekretarieti ya Kamati yetu. Tunafahamu kwamba, Zanzibar ni ndogo na takriban watu wake ni ndugu, na inapotokezea kazi kama hizi za kiuchunguzi kwa lengo la kuwasaidia wananchi wetu, kujuana huku ama muhali kwa namna yoyote hulazimika kuwekwa pembeni, ili ukweli uweze kuchukua nafasi yake.
Mheshimiwa Spika:
Kamati inaendelea kuchukua fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru zaidi wananchi mbali mbali wasiokuwa wafanyakazi wa Shirika ambao waliotembelewa na Kamati na kutoa mashirikiano yao mazuri kwa kueleza taarifa za kweli ambazo zimeisaidia sana Kamati kukamilisha kazi yake. Sambamba na hili, Kamati pia inawashukuru Viongozi wa Bodi ya Wakurugenzi, Tume ya Utumishi Serikalini, Shirika la Utangazaji la Zanzibar na wengine, kwa mashirikiano yao mazuri waliyoyatoa pale walipoitwa na Kamati na kwa utaratibu mwengine uliotumiwa na Kamati kupata taarifa ilizozihitaji, kwa ujumla Kamati inawapongeza na kuwashukuru.
Mheshimiwa Spika:
Kamati inashukuru kumaliza kwa salama kazi hii nzito iliyotumwa kuifanya huku ikifahamu kwamba, Serikali, Shirika la Umeme la Zanzibar na zaidi kwa Bodi mpya ya Wakurugenzi iliyoteuliwa mwaka uliopita, wataifanya ripoti hii sawa na kioo cha kujitizamia na kuona kasoro ziko wapi, lakini msisitizo wa Kamati unaelekezwa kwa Serikali kuwa jasiri katika kufanya maamuzi magumu ya kuondosha na kutokomeza kabisa, mapungufu yote yaliyoelezwa wazi katika ripoti hii, bila ya kuwa na muhali kwa maslahi ya nchi na wananchi wake. Si vyema kuendelea kuficha uovi wa wachache, huku madhara yake yakaendelea kuisakama na kuihujumu nchi na wananchi.
Mheshimiwa Spika:
Kamati inaamini kwamba, Ripoti hii ni kisima cha elimu na hekima kisichokauka, iwapo itafanyiwa kazi, na ni sawa na kidonda kisichopoa, iwapo Serikali bado itaendeleza kile wananchi wanachokiita ‘Kulindana’ kwa maslahi ya wachache. Kwa Ripoti hii, Baraza linaendelea kutekeleza vyema majukumu yake ya kusimamia maslahi ya wananchi, na ni Ripoti itakayosaidia sana elimu na maarifa ya wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, lakini wasomaji  wanaoutumia muda wao mwingi kujisomea taarifa mbali mbali za Baraza na Mabunge mengine, wamepata rejea itakayotosheleza kiu zao. Kwa kupitia ripoti hii, mambo mbali mbali ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ni kilio kwa wananchi dhidi ya utendaji wa Shirika, yamewekwa wazi na kufahamika na hivyo, upeo wa wananchi hao na uelewa wa yepi yanayofanyika katika Shirika, kwa kuisoma ripoti hii yatafikia matilaba.
Mheshimiwa Spika:
Kubwa zaidi, baada ya maelezo yote hayo ni kwamba, Kamati itatoa mapendekezo yake kwa mtindo wa kujumuisha hadidu rejea zote zilizohusika na kufanyiwa kazi, na utaratibu huu unaelekezwa na kanuni ya 121(5) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi Toleo la 2012, ingawaje haujazoeleka katika Ripoti za Kamati hii ya P.A.C, na ripoti nyengine za Baraza, ambazo hueleza mapendekezo yao katika sehemu ya Maudhui ya ripoti, lakini kwa kukidhi masharti ya kanuni hii, mapendekezo hayo hufanyiwa muhtasari wake katika sehemu ya Hitimisho. Kwa Ripoti hii, Mapendekezo ya kazi ya Uchunguzi kuhusu Utendaji wa Shirika la Umeme kwa mnasaba wa hadidu rejea zilizokabidhiwa kwa Kamati, yataelezwa katika sehemu hii ya Hitimisho kama kanuni inavyoelekeza moja kwa moja katika fasiri yake.
Mheshimiwa Spika:
Tumefanya hivyo kwa lengo la kuipa wepesi Serikali kutekeleza mapendekezo machache watakayoweza kuyatekeleza kwa ufanisi, ili ile sababu ya uzito wa utekelezaji wake, isiendelee kuelezwa, kwani sio tu huidhalilisha kwa kuonekana haiko makini katika dhamira yake ya kupiga vita dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya watendaji wa Taasisi na Mashirika yake, ambapo katika lugha nyepesi ya kileo huitwa ‘UFISADI’, lakini wananchi wa nchi hii na zaidi wale wanaofuatilia kwa makini shughuli za Baraza, hupoteza imani na mapenzi kwa Serikali yao, jambo ambalo haliridhishi na linahitaji kuondoshwa kwa umakini wa kutekeleza mapendekezo ya Kamati za Baraza lakini pale yanaporidhiwa hugeuka na kuwa maagizo ya Baraza la Wawakilishi.
MAPENDEKEZO YA KAMATI KUHUSIANA NA HADIDU REJEA
ZILIZOHUSIKA:
Mheshimiwa Spika:
Kwa mnasaba wa maelezo ya hapo juu, Kamati inatoa mapendekezo yafuatayo kwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ili iiagize Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na kuitaka itekeleze mambo yafuatayo:

  1. Viongozi wa Bodi ya Wakurugenzi waliomaliza muda wao 2012, misisitizo ukiwekwa kwa aliekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Ndg. Mohd Hashim Ismail, wachukuliwe hatua za kisheria kwa kuliingizia Shirika hasara zisizo za lazima, (Tsh.31,179,000/-) kwa malipo ya faini kwa Kampuni ya Kichina (China Railway Jianchang Engeneering Co. (T) Ltd (CRJE), ambapo hasara hii imesababishwa na uzembe na ubinafsi wa aliekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Wajumbe wote wa Bodi hii kwa ujumla.
  2. Menejimenti ya Shirika la Umeme ichukuliwe hatua za kinidhamu, kwa uzembe wa kutosimamia ipasavyo majukumu ya Shirika, kuleta migogoro miongoni mwa wafanyakazi wake, kushindwa kulisimamia Shirika, Shirika kupoteza mapato yake, kujenga mazingira ya upendeleo yenye kuleta ubaguzi katika kazi na kupunguza ufanisi katika utendaji wa Shirika la Umeme kwa ujumla.
  3. Wafanyakazi wote wa Shirika waliotajwa kuhusika moja kwa moja ama kwa namna yoyote ile katika ripoti hii, pamoja na Watendaji wa Serikali waliokuwa sio waajiriwa wa Shirika ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC-TV) alieruhusu Kampuni ya Zanzibar Data Com kutumia umeme kinyume na taratibu na Sheria, wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria kutokana na kuhusika kwao katika kulihujumu Shirika kwa njia yoyote ile.
  4. Serikali ipige marufuku na isimamie kwa udhati Kampuni zote binafsi, ikiwa ni pamoja na Kampuni ya GECCO kufutiwa vibali (ambavyo Kamati inaamini vimetoka kinyume na Sheria ama kwa namna yoyote iliyo), na badala yake kazi zinazohusiana na utoaji wa huduma ya umeme ziendelee kufanywa na Shirika la Umeme pekee, kama Sheria Nam 3 ya mwaka 2006, inavyoelekeza.
  5. Watendaji wa Shirika ambao pia ni wafanyakazi ama wamiliki wa Kampuni ya GECCO (pamoja na wafanyakazi wa Shirika wanaosaidia kazi za GECCO) kama walivyotajwa moja kwa moja ama kwa utaratibu wowote katika ripoti hii, wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa kudhoofisha utendaji kazi na ufanisi wa Shirika.
  6. Kwa kuwa uendeshaji wa majenereta 32 umekuwa ni mzigo mkubwa kwa Shirika, Serikali ama ichangie ruzuku katika Uendeshaji wake, au kutafutwe utaalamu utakaowezesha majenereta hayo kutumia diseli ya kawaida iyenye gharama nafuu au yauzwe na badala yake yatafutwe mengine kwa mujibu wa Sheria, yatakayoweza kutumika kama inavyokusudiwa.
  7. Kwa kuwa Kamati imepata wasi wasi kwamba kuna hujuma imefanyika iliyopelekea kukosekana kwa umeme Unguja ndani ya miezi mitatu 2009/2010, Serikali, ndani ya kipindi cha miezi mitatu baada ya kuwasilishwa ripoti hii, iunde Tume iliyohuru ya Kuchunguza chanzo na sababu zilizopekea kukosekana kwa umeme huo na ripoti yake iwasilishwe na kujadiliwa katika Baraza la Wawakilishi.
  8. Kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Serikali, kupitia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, ifanye ukaguzi wa fedha zilizotumika kurejesha huduma ya Umeme, Unguja baada ya kuzimika na kukosekana kwa kipindi cha miezi mitatu (Disemba hadi Machi, 2010).
  9. Bila ya kuathiri masharti ya Katiba, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ifanye ukaguzi maalum wa Hesabu za Shirika kwa kipindi cha miaka mitatu (2009-2012).

  1. Kwa kuwa Zanzibar hakuna chombo kinachoratibu bei ya umeme, kama vile EWURA kule Tanzania bara, na kwa kuwa ZECO hujipangia bei kwa matakwa ya EWURA, Serikali ilete Sheria ya kuanzisha chombo kitakachohusika na kudhibiti bei ya umeme Zanzibar, ambapo pamoja na majukumu yake mengine, kitashauriana kwa karibu na EWURA ili ZECO iweze kutoa huduma bora na fanisi na kupatikana kwa muafaka wa bei ya umeme Zanzibar.
  2. Kwa kuwa moja kati ya dosari kubwa ya deni la umeme inalodaiwa ZECO na TANESCO inatokana na Zanzibar kukosa umeme wake, na kwa kuwa katika hili wananchi wa kawaida ndio wanaoumia na kuathirika zaidi, Serikali ihakikishe Zanzibar inazalisha umeme wake wenyewe na sio kuendelea kutegemea umeme kutoka Tanzania bara.
Mheshimiwa Spika:
Kama nilivyotangulia kueleza awali mwanzoni mwa ripoti hii kuwa Baraza letu kama chombo cha wananchi, limo katika mageuzi makubwa ya kufikia matakwa kamili ya utekelezaji wa DHANA YA UTAWALA BORA . Hapa nakusudia kusisitiza umuhimu wa Baraza kwamba ni chombo kilichopo kwa niaba ya wananchi, kuweza kufahamu na kutekeleza wajibu wake kwa maslahi ya wananchi. Aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Marekani Bw. Alexander Hamilton, aliwahi kusema kuwa “Those who stand for nothing fall for anything”.
Kwa upande mwengine Serikali nayo kwa upande wake haina budi kutekeleza wajibu wake wa kutekeleza maagizo ya chombo hichi, maagizo ambayo ndio kauli ya wananchi.
Mheshimiwa Spika:
Kamati yetu imefanya kazi kubwa na ngumu. Lengo la ripoti hii na mapendekezo yake kwa Baraza ni nyenzo ambayo itaisaidia Serikali kulifanyia mageuzi makubwa shirika la umeme ili liweze kutekeleza vyema majukumu yake kwa ufanisi. Serikali ina wajibu wa kuona na kukubali ukweli kwamba Shirika la umeme linakabiliwa na changamoto kubwa na nyingi, changamoto zinazohitaji kupatiwa majibu ya haraka sana kwa nia ya kulinusuru na hivyo kurejesha imani na matumaini ya wananchi. Katika kulisisitiza hili nakumbuka maneno yaliyotamkwa na mwandishi na mwanasayansi mmoja maarufu Benjamin Franklin aliyesema, “the way to see by faith is to shut the eye of reason”.
Ni matumaini yangu kama yalivyo matumaini ya Kamati kwamba, Wajumbe wa Baraza hili wanamatumaini makubwa sana ya kufanyika mageuzi makubwa kwa Shirika letu la Umeme, ili malengo na mafanikio yake, yawanufaishe wananchi waliotutuma.
Mheshimiwa Spika:
Naomba nimalizie kwa kukushukuru kwa mara nyengine tena kwa kunipa nafasi hii na kutumia muda mwingi wa Baraza lako katika kuwasilisha ripoti hii. Aidha naomba niwashukuru sana wajumbe wenzangu kwa utulivu, usikivu na umakini mkubwa waliouonyesha wakati wakifuatilia uwasilishaji wa ripoti hii ambapo mimi nimeiwasilisha kwa muhutasari lakini mikononi mwenu muna ripoti kamili pamoja na orodha kubwa ya viambatanisho, kama sehemu ya ushahidi kwa kile
tulichokielezea katika ripoti hii. Ni imani yangu kuwa waheshimiwa wajumbe mutapata muda mzuri wa kutafakari, kuvichambua na kuichangia kwa nia ile ile ya kuisaidia Serikali yetu katika kuliimarisha Shirika hili.


Mheshimiwa Spika:
Tunazidi kupendekeza kwamba, ripoti hii na ibakie katika Maktaba ya Afisi ya Baraza la Wawakilishi, ili iwe rahisi kwa kila mtumiaji wa maktaba hiyo kuipata ripoti hii kwa wepesi, igawaje pia kwa kuzingatia masharti na taratibu za maktaba zilizowekwa. Mwisho kabisa na kwa msisitizo wa kipekee, Kamati inaliomba Baraza hili tukufu iiagize Serikali iyatekeleze mapendekezo ya ripoti hii ndani ya miezi 3 kutoka tarehe ya kuwasilishwa kwa ripoti hii na hatimae Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wake katika Baraza hili tukufu.
Mheshimiwa Spika:
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza na sasa NAOMBA KUTOA HOJA.
Imesainiwa na kuthibitishwa na
Mhe. Omar Ali Shehe,
Mwenyekiti,
Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.
1 Hansard, Baraza la Wawakilishi, tarehe 12/04/2012.
2 Tarehe ya Vocha hii imekosewa, yaani imeandikwa 27/06/2010, wakati inahusika na mwezi wa October, 2010.
3 Vocha hii nayo imekosewa kitarehe kwa kuandikwa 27/06/2010, wakati tarehe sahihi ni 27/10/2010.
4 Tafsiri ni yetu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.