HOTUBA YA
RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI
WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA
DK. ALI MOHAMED SHEIN, KATIKA
MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA MIAKA 49
YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR,
TAREHE 12
JANUARI, 2013
Mheshimiwa
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Dk. Mohamed Gharib Bilal,
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Mizengo Kayanza Peter Pinda,
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Maalim Seif Sharif Hamad,
Makamu wa
Kwanza wa Rais, Zanzibar;
Mheshimiwa
Balozi Seif Ali Iddi,
Makamu wa
Pili wa Rais, Zanzibar;
Mheshimiwa
Mzee Ali Hassan Mwinyi,
Rais
Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Dk. Salmin Amour Juma,
Rais
Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa
Dk. Amani Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi;
Viongozi
Wakuu Wastaafu Mliohudhuria;
Waheshimiwa
Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar;
Mheshimiwa
Mama Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar;
Mheshimiwa
Othman Chande Mohamed, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Waheshimiwa
Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Mheshimiwa
Abdalla Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi;
Waheshimiwa
Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa;
Ndugu
Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Assalaam
Alaykum,
Naanza kwa kumshukuru Mola wetu Mwenye kustahiki
kushukuriwa na viumbe vyote; Aliyetuumba na akatupa uhai. Namshukuru kwa kutupa
fadhila ya uwezo wa kukusanyika hapa leo kuadhimisha kilele cha sherehe za
Miaka 49 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Namuomba Mola wetu awarehemu na kuwapa
malazi mema Viongozi wetu wa Mapinduzi waliotutangulia mbele ya haki; awaghufirie
makosa yao wazee, ndugu na jamaa zetu wote waliokwishapita. Atujaaliye rehema sisi tulio hai na atupe
mafanikio katika mambo yetu yote mema tunayojipangia. Yeye Ndiye Muweza wa kila kitu.
Ndugu
Wananchi,
Kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar natoa
shukurani za dhati kwako Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuja kuungana nasi katika sherehe zetu hizi
adhimu na muhimu. Vile vile, natoa shukurani kwa viongozi wote, mabalozi,
wawakilishi wa mashirika ya Kimataifa na wananchi wote kwa kuhudhuria kwenu kwa
wingi katika sherehe hizi.
Ndugu
Wananchi,
Leo tunaadhimisha sherehe za miaka 49
ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964. Kuweko pamoja nasi, mabalozi na wawakilishi
wa Taasisi mbali mbali za Kimataifa
kunatupa faraja kubwa. Kuja kwenu,
kunatudhihirishia kuwa Mapinduzi yetu yanaheshimika na yanapewa taadhima kubwa
ndani na nje ya nchi yetu.
Tunapoisherehekea siku hii hivi leo, ni vyema tukajikumbusha jukumu letu la
kuendelea kuyalinda, kuyadumisha na kuyaendeleza kwa vitendo Mapinduzi yetu
Matukufu, kwa sababu ndio yaliyowakomboa wanyonge kutokana na dhulma na
kutawaliwa na kuwaletea uhuru wa kweli.
Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 yaliyoongozwa na Jemedari, Marehemu
Mzee Abeid Amani Karume yalirudisha utu na heshima na kuondoa aina zote za
ubaguzi na yaliweka misingi ya haki na usawa kwa watu wote. Tufahamu kwamba mafanikio yote tuliyoyapata
katika kipindi cha miaka 49 na ya miaka ijayo kwenye nyanja za kiuchumi,
kijamii na kisiasa, msingi wake mkubwa ni Mapinduzi ya Januari, 1964.
Leo tunaona fahari kwamba katika kipindi
hiki cha maadhimisho ya sherehe za miaka 49, tumezidi kujenga mshikamano na
maelewano miongoni mwetu. Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa, ambayo
hivi sasa imeingia kwenye mwaka wa tatu, imepata mafanikio ya kuridhisha na
kutia moyo. Mshikamano wetu umetuwezesha
kufanya mambo mengi na kupongezwa na marafiki zetu. Ni muhimu tuendelee kushikamana na kufanya
kazi kwa bidii.
Ndugu
Wananchi,
Ushirikiano wa Serikali na wananchi umetupa
mafanikio mazuri katika kuimarisha uchumi wetu ambao mwenendo wake umeliwezesha
Pato la Taifa kufikia T.Shs. 1,198
bilioni mwaka 2011 kutoka T.Shs. 946.8 bilioni mwaka 2010. Vile vile, ukuaji wa uchumi ulitegemewa
kufikia asilimia 7.0 mwaka 2012 kutoka asilimia 6.8 mwaka 2011. Kiwango hiki ni
kikubwa ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita. Mafanikio haya yametokana na
kukua kwa sekta ya uvuvi, biashara na ujenzi wa mahoteli na mikahawa.
Ndugu
Wananchi,
Kutokana na jitihada mbali mbali
ilizozichukua Serikali, katika mwaka 2012, tumeshuhudia kushuka kwa mfumko wa
bei kutoka asilimia 20.8 mwezi Disemba 2011 hadi asilimia 4.2 mwezi Novemba
2012. Hili ni jambo la faraja kwani limesaidia kuwapunguzia makali ya maisha
wananchi.
Aidha, ukusanyaji wa mapato ya ndani
umeongezeka kutoka T.Shs. 181.4
bilioni mwaka wa fedha 2010/2011 na
kufikia T.Shs. 212 billioni mwaka 2011/2012. Hili ni ongezeko la asilimia 17. Kuongezeka
huko kumetokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha usimamizi
na udhibiti wa mapato na misamaha ya kodi,
juhudi za watendaji wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), mwamko mkubwa wa
walipa kodi wetu wa sekta binafsi na kuimarika kwa michango ya taasisi za
Serikali.
Wakati huo huo, huduma za benki
zimezidi kuimarika katika mwaka 2012,
ambapo amana za benki ziliongezeka kutoka T.Shs. 336.4 bilioni, Septemba 2011 na
kufikia T.Shs. 365.5 bilioni, Septemba 2012.
Hili ni ongezeko la asilimia 8.5. Mikopo ya benki kwa sekta binafsi
iliongezeka kutoka T.Shs. 147.5 bilioni mwezi Septemba 2011 na kufikia T.Shs.
150.9 bilioni katika mwezi wa Septemba 2012.
Ongezeko hili ni sawa na asilimia 6.4. Hali hii inaashiria kuongezeka
kwa shughuli za kijamii, kibiashara na uzalishaji mali wa wananchi na hivyo inasaidia
kuinua uchumi wa nchi.
Ndugu Wananchi,
Zao la karafuu linaendelea kuwa muhimu kwa biashara na uchumi wetu. Kwa msimu tunaoendelea nao wa
mwaka 2012/2013 hadi kufikia tarehe 8
Januari,2013, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshanunua Tani 775.3 za
karafuu kwa Tsh. 9,565.3 milioni ambazo zimelipwa taslimu kwa wakulima. Ununuzi
unaendelea vizuri. Hii ni hatua nzuri ya mafanikio. Serikali inaendelea kutekeleza azma yake ya kulinda
hadhi ya karafuu zetu na imefikia hatua kubwa ya kutekeleza mkakati wa
kuzifanyia utambulisho maalum (branding).
Tunawahimiza wakulima kupanda mikarafuu kwa wingi, kuyatunza
mashamba yao na kuachana na tabia ya kuuza karafuu kwa njia ya magendo. Lengo letu
ni kuzalisha miche 500,000 kila mwaka na kuendelea kuwapa wakulima bila ya
malipo. Kwa msimu wa mwaka 2011/2012, jumla ya miche 522,000 ilioteshwa na kutolewa
kwa wakulima.
Ndugu Wananchi,
Serikali inafahamu kuwa
mchango wa viwanda katika Pato la Taifa bado ni mdogo ambapo kwa mwaka 2011/2012 ulifikia asilimia 3.9.
Hivyo, Serikali inaendelea kujenga mazingira mazuri yatayopelekea kuvifufua na
kuvikuza viwanda, hasa vidogo vidogo, ili viweze kutoa mchango katika soko la
ajira na kuchangia zaidi katika Pato la Taifa. Miongoni mwa hatua hizo ni
kukamilisha mradi wa umeme wa uhakika na kuiimarisha miundombinu ya bandari,
uwanja wa ndege na barabara ambayo ni muhimu kwa wawekezaji wa ndani na nje ya
nchi, ili kuchangia katika kuimarisha
sekta ya mifugo, uvuvi na kilimo.
Vile vile, Serikali
imekua ikichukua hatua mbali mbali za kuwashajihisha wajasiriamali, ili nao
watoe mchango wao katika kuendeleza uchumi wetu. Miongoni mwa hatua hizo ni
kuwapa mikopo, ili waweze kuanzisha biashara ndogo ndogo. Katika jitihada hizi, masoko ya Jumapili yameanzishwa
Unguja na Pemba na yanaimarishwa hatua kwa
hatua.
Ndugu Wananchi,
Jitihada zetu za kuwavutia wawekezaji
nchini zimekuwa zikizaa matunda. Hata hivyo, kutokana na hali ya uchumi ilivyo
ulimwenguni, kasi ya wawekezaji wa nje ilipungua katika mwaka uliopita. Jumla ya miradi 29 ya uwekezaji iliidhinishwa
katika mwaka wa fedha 2011/2012. Idadi
hii ni sawa na asilimia 58 ya makadirio ya miradi 50 iliyopangwa. Katika kipindi cha miezi sita iliyopita,
Julai hadi Disemba, 2012, jumla ya miradi 17 yenye thamani ya US$ 38.86 milioni
iliidhinishwa. Miradi hii inakisiwa
kutoa ajira zisizopungua 834 kwa wananchi.
Pamoja na hali hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendeleza juhudi
za kuwavutia wawekezaji wa nje zaidi.
Vile vile, tunawashajihisha wawekezaji wa ndani wazidishe kasi yao ya
uwekezaji kwa kuzitumia fursa na rasilimali zilizopo nchini.
Ndugu
Wananchi,
Serikali yetu imeendelea kuimarisha
huduma za jamii na kiuchumi kwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
Mkuu ya CCM ya mwaka 2010/2015 kwa ufanisi, kwenda sambamba na DIRA 2020 na
MKUZA II pamoja na Malengo ya Kimataifa ya Milenia. Tathmini ya mapitio ya
mipango yetu iliyosimamiwa na Tume yetu ya Mipango na Taarifa ya Utelekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM 2010/2015, zinatoa matumaini ya mafanikio, licha ya
kuwepo kwa baadhi ya changamoto ambazo tunaendelea kuzifanyia kazi hatua kwa
hatua.
Ndugu
Wananchi,
Katika uimarishaji
wa sekta za kiuchumi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukuwa juhudi ili
kuona kuwa sekta hizo zinakua na kuchangia katika ustawi wa jamii. Sote
tunaelewa kuwa sekta ya Kilimo inaongoza
na inategemewa na zaidi ya asilimia 80 ya wananchi. Kwa wastani, inachangia asilimia 23 katika
Pato la Taifa na kiasi kikubwa katika mapato ya fedha za kigeni. Kutokana na
umuhimu huo, Serikali inaendeleza jitihada mbalimbali za kuimarisha sekta hii
ili iwe na tija zaidi kwa wakulima na kuongeza
mchango wake katika Pato la Taifa.
Mafunzo mbali
mbali yanatolewa kwa wakulima na katika
jitihada za kuimarisha huduma zao, Serikali ilinunua matrekta mapya 10 mwaka
2012 na mengine 20 yameagizwa mwaka huu. Vile vile, iliyafanyia
matengenezo matrekta 27 ya zamani na
mashine 14 za kuvunia mpunga (combine harvesters), zilinunuliwa.
Kadhalika,
wakulima wanaendelea kufaidika na ruzuku za pembejeo ambapo Serikali inawafidia
kwa kiwango cha asilimia 75 ya bei ya mbolea na huduma za ukulima wa
matrekta. Vile vile, inawafidia kwa
asilimia 83 ya bei ya mbegu ya mpunga na asilimia 55 kwa bei ya dawa ya kuulia
magugu.
Ndugu
Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na juhudi za kuimarisha
miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji maji kwa kufuata Mpango Mkuu wa Kilimo
cha Umwagiliaji Maji. Juhudi zinaendelea kuchukuliwa kwa kuhakikisha kuwa jumla
ya hekta 8,521 ambazo zinaweza
kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji maji zinatumika kwa matumizi hayo ipasavyo.
Kati ya hizo, hekta 750
zimeshatayarishwa. Vile vile, Serikali ya Jamhuri ya Korea tayari imekubali kushirikiana
nasi kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji maji katika eneo la hekta zipatazo
2,200 katika mabonde ya Cheju, Kibokwa, Kilombero kwa Unguja na Makwararani na
Mlemele kwa upande wa Pemba. Nachukua fursa hii kuishukuru kwa dhati kabisa
Serikali ya Jamhuri ya Korea.
Aidha, Serikali yetu inaendeleza
juhudi za kuimarisha utafiti wa kilimo kwa mazao ya chakula na mboga mboga katika
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Kizimbani. Kadhalika,
Serikali inaendelea kukiimarisha Chuo cha Kilimo kiliopo Kizimbani ili
kiendelee kusaidia katika kukiendeleza kilimo nchini.
Ndugu
Wananchi,
Kwa kutambua
umuhimu wa ardhi, Serikali inaandaa sera mpya ya ardhi pamoja na kuzipitia upya sheria za ardhi ili ziende sambamba na malengo ya
MKUZA II ya usajili wa ardhi kwa asilimia 50, ifikapo 2015. Katika mwaka 2012 migogoro ya ardhi ya muda
mrefu, pamoja na ule wa Mchangamle-Kizimkazi na Muyuni-Matemwe, imepatiwa
ufumbuzi. Vile vile, Serikali
imekamilisha utayarishaji wa ramani za kisiwa cha Unguja na Pemba, pamoja na
ramani za mipaka ya Mikoa na Wilaya.
Hivi sasa Mipango Mikuu ya Miji inatayarishwa.
Katika kipindi
hiki, mafanikio makubwa yamepatikana katika suala la uhifadhi wa mazingira kwa
kudhibiti uingizwaji wa mifuko ya plastiki nchini na kuhamasisha upandaji wa
miti katika sehemu zilizochimbwa mchanga na mawe. Aidha, katika kuhakikisha
kuwa suala la mazingira linazingatiwa katika miradi ya kiuchumi na maendeleo,
miradi 182 inayohusisha utalii, barabara, mikahawa na mahoteli imekaguliwa na
kutolewa taarifa. Kadhalika, Serikali imeendeleza jitihada za uhifadhi wa
misitu ya asili na mikoko katika maeneo mbali mbali, ambapo hivi karibuni ilizinduliwa Sensa ya
Miti ili kuelewa idadi halisi ya mikarafuu pamoja na miti mingine tuliyonayo.
Natoa wito kwa
wananchi kuzingatia sheria na taratibu za matumizi bora ya ardhi na rasilimali
nyengine pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Ndugu Wananchi,
Kuhusu sekta ya
ufugaji, Serikali inafanya juhudi
kubwa ya kuwaendeleza wafugaji kupitia
programu mbali mbali, ikiwemo Programu ya Kuimarisha Huduma za Mifugo (ASDP-L),
yenye kutoa taaluma ya ufugaji bora.
Katika mwaka mmoja uliopita, vikundi vipya vya skuli za wafugaji 155 na
vikundi vya zamani 180 kwa Unguja na Pemba vilipewa mafunzo. Aidha, wafugaji 3,200 walitembelewa na
kupewa ushauri wa kitaalamu. Vile vile, katika kuimarisha huduma za utafiti na
utibabu wa wanyama matengenezo makubwa yamefanywa
kwenye maabara ya Maruhubi Unguja na ya Chake Chake, Pemba pamoja na
kuviimarisha vituo vya mifugo viliopo katika sehemu mbali mbali.
Ndugu Wananchi,
Katika mwaka
uliopita, juhudi kadhaa zilichukuliwa katika
kuiendeleza sekta ya uvuvi, ambazo zimezaa matunda na kufanya mchango wa Sekta hiyo katika Pato la Taifa kupanda
kutoka asilimia 6.1 mwaka 2011 hadi asilimia 6.7 mwaka 2012. Kiwango cha samaki kilichovuliwa kimeongezeka
kutoka wastani wa tani 28,759 mwaka 2011 hadi wastani wa tani 30,500 mwaka 2012.
Uzalishaji wa zao la mwani pia umeongezeka,
kutoka tani 12,529 mwaka 2011 hadi tani 13,844 mwaka 2012.
Tunaendelea
kutilia mkazo katika kuwawezesha wavuvi kwa kuwapa mafunzo ya uvuvi bora
unaozingatia uhifadhi wa mazingira pamoja na matumizi bora ya vifaa vya kisasa. Mafunzo kwa wavuvi juu ya udhibiti wa
mazingira ya baharini yamefanywa kupitia mradi wa MACEMP, pamoja na kuendeleza maeneo
ya ukanda wa pwani. Kwa mwaka wa fedha
2011/2012 jumla ya T.Shs. 163.6 millioni zilitolewa kwa ajili ya kuwaendeleza
wavuvi Unguja na Pemba. Vile vile, Serikali inaendeleza jitihada za kutafuta
wawekezaji katika uvuvi wa bahari kuu pamoja na viwanda vya usarifu wa samaki
na mazao ya baharini. Kwa kushirikiana
na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, wananchi 56 walipelekwa nchini China kwa mafunzo ya
ufugaji samaki, kilimo cha mwani na
viumbe wengine wa baharini.
Natoa wito kwa
vijana na wavuvi wote nchini kushirikana na Serikali katika kuiendeleza sekta
ya uvuvi yenye fursa kubwa ya kukuza soko la ajira. Nawasihi wananchi waendelee
kupiga vita vitendo vya uvuvi haramu, ili kazi ya uvuvi iwe endelevu na yenye
tija.
Ndugu Wananchi,
Miundombinu ya
kiuchumi ni chachu ya maendeleo na inajumuisha barabara, bandari, viwanja vya
ndege na umeme. Kutokana na umuhimu huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inaendelea na ujenzi wa barabara mbali mbali Unguja na Pemba, zenye jumla ya kilomita 158.2, zikiwemo zile
zinazofadhiliwa na MCC, BADEA na OPEC. Tumeshazifanyia uchambuzi yakinifu,
usanifu na utayarishaji wa zabuni barabara saba kuu (7) zinazoingia katika mji
wa Zanzibar zenye urefu wa kilomita 78.5.
Katika kuimarisha
usalama wa usafiri wa barabarani, Serikali ilizindua Kamati ya Wiki ya Usalama
Barabarani pamoja na Muongo (decade) wa usalama barabarani na kuwashirikisha
wahusika mbali mbali kwa lengo la
kuimarisha usalama na kupunguza ajali.
Vile vile,
Serikali imeendelea kuimarisha kazi za usimamizi wa usalama wa usafiri wa
baharini kwa kuimarisha na kuiendeleza Mamlaka ya Usafiri wa Baharini. Aidha, tumetengeneza Kanuni mbali mbali za
kusimamia usalama wa vyombo na udhibiti wa mashirika na taasisi zinazotoa
huduma.
Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, imeendelea na
hatua za kuliimarisha Shirika la Meli kwa madhumuni ya kuwapa wananchi wa
Zanzibar huduma zilizo bora na salama za
usafiri huo na kuwaondolea tatizo la muda mrefu la usafiri wa baharini kati ya
visiwa vyetu. Serikali imeamua kununua meli mpya ya abiria na mizigo itakayosafiri
baina ya Unguja na Pemba na mwambao wa Afrika Mashariki. Meli hiyo itakuwa na
uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 200 za mizigo. Mipango ya ununuzi wa meli hio inaendelea
vizuri.
Ndugu Wananchi,
Juhudi zetu za
kuimarisha bandari ya Malindi zinaendelea kuzaa matunda. Idadi ya mizigo
imeongezeka kutoka makontena 39,293 yaliyopokelewa mwaka 2011 hadi kufikia
49,821 mwaka 2012, sawa na ongezeko la asilimia 27. Serikali imeshanunua mashine mbali mbali za
kunyanyulia makontena zikiwemo “fork lifts” na krini maalum yenye uwezo wa
kunyanyua tani 45 ambazo zinategemewa kuwasili mwezi wa Februari, 2013, kwa
lengo la kuongeza ufanisi bandarini.
Vile vile, Serikali inaendelea
kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha mazingira ya bandari ya
Malindi kwa kujenga majengo ya kupumzikia abiria na kutoa huduma mbali
mbali. Ujenzi wa eneo la mraba la mita
1,500 unaendelea na linategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Katika hatua ya kuimarisha
usafiri wa anga, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na kazi ya kukiimarisha
Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume Unguja. Majadiliano yanaendelea kuhusu ujenzi wa jengo jipya la abiria uliokuwa
umesitishwa kwa muda kutokana na matatizo ya kiufundi. Tunatarajia kwamba kazi
hio itaanza tena hivi karibuni. Kwa
upande wa Uwanja wa ndege wa Pemba, kazi za uimarishaji huduma katika kiwanja
hicho zinaendelea vizuri.
Ndugu
Wananchi,
Katika sekta za miundombinu ya huduma
za jamii na kiuchumi, umeme wa uhakika ni jambo la lazima. Jitihada za Serikali
za kuimarisha umeme zimefikia hatua nzuri. Tunatarajia kuuzindua rasmi mradi wa
Uwekaji wa Laini ya pili ya Umeme wa “Millenium
Challenge”, hivi karibuni. Mradi huu wa kuleta umeme kutoka Ras
Kiromoni, Tanzania Bara hadi Ras Fumba, Zanzibar una nguvu ya Megawati 100, ambapo
mahitaji yetu halisi ni kiasi cha Megawati 50. Hizi ni jitihada za washirika
wetu wa maendeleo wa Marekani ambao wameamua kutuunga mkono katika kuitekeleza
mipango yetu ya maendeleo. Tunatoa shukurani
kwa ushirikiano wao huo.
Ndugu
Wananchi,
Tuna furaha kuona kuwa huduma za
mawasiliano zikiwemo huduma za simu na mtandao zinaimarika. Mradi wa
“e-government” uliogharimu US$ 19.8 milioni umekamilka kwa ufanisi na
kuzinduliwa tarehe 5 Januari, 2013. Mradi huu unatuwezesha kuunganisha Ofisi na
taasisi za Serikali kwa mitandao yenye nguvu zaidi. Hatua hiyo itaifanya Serikali kuwa na uwezo
mkubwa zaidi wa kuendesha shughuli zake na kuwahudumia wananchi pamoja na
kuimarisha huduma za mawasiliano ya ndani na nje ya nchi.
Ndugu Wananchi,
Vijana ni nguvu
kazi muhimu kwa maendeleo yetu. Upungufu
wa ajira kwa vijana ni mongoni mwa changamoto inayoikabili Serikali hivi sasa. Uimarishaji
wa uchumi wetu unazingatia mbinu mbali mbali za kuitatua changamoto hii. Katika
kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali
inaendelea na hatua ya kuwajengea uwezo wajasiriamali kwa kuwapatia mafunzo na
mikopo yenye riba nafuu kupitia mifuko mbali mbali ukiwemo Mfuko wa AK/JK. Serikali imetoa mikopo ya jumla ya shilingi
bilioni 1.5 kwa wananchi mbali mbali. Wajasiriamali 500 wa Unguja na Pemba wamepatiwa
mafunzo ya usimamizi wa fedha, masoko na
uongozi. Kadhalika, Vikundi 11 vyenye wanachama 1,526 vimeanzishwa,
Unguja na Pemba.
Kwa kushirikiana na taasisi ya Umoja wa
Mataifa inayoshughulikia masuala ya wanawake “UN WOMEN”, Serikali ya Mapinduzi
inatekeleza Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake wenye
thamani ya T.Shs. 156 milioni. Kupitia mradi huu, vikundi mbali mbali vya kinamama
na wakufunzi vimepatiwa mafunzo.
Serikali imeshafanya utambuzi wa
vikundi vya vijana katika wilaya zote kwa ajili ya kuyafahamu mahitaji yao
ambapo vikundi 789 vimeorodheshwa na baadhi yao kupatiwa mafunzo ya kitaalamu kwa
kupitia programu ya ASSP. Aidha. vikundi vya vijana 58, vinavyojishughulisha na shughuli
mbali mbali vimepewa T.Shs. 192.4 milioni kupitia Mfuko wa Vijana wenye thamani
ya T.Shs. 300 milioni.
Ndugu Wananchi,
Jitihada zinaendelezwa katika kushughulikia
masuala ya watoto ikiwa ni pamoja na kuzilinda na kuziimarisha haki zao za
elimu, afya na kuwaepusha na vitendo vya udhalilishaji kijinsia. Sheria ya
hifadhi ya mtoto Nambari 6 ya mwaka 2011 imeanzishwa ili kuzipa nguvu sheria
zinazolinda haki zao zilizokuwepo kabla. Nawasihi wananchi kuzitumia huduma
zinazotolewa katika vituo vya mkono kwa mkono vilivyoendelea kufunguliwa Unguja
na Pemba.
Vile vile, Serikali inaendelea na
jitihada za kuziimarisha huduma za watu wenye ulemavu. Zoezi la usajili kwa
ajili ya kuimarisha huduma na haki zao ikiwemo suala la elimu kwa watoto wenye
ulemavu liko katika hatua za mwisho. Vile
vile, Serikali imeanzisha mfuko wa kuwasaidia watu wenye ulemavu, uliozinduliwa
tarehe 28 Septemba, 2012 na hadi mwezi wa Disemba, 2012 jumla ya T.Shs. 211
milioni zimepatikana.
Kadhalika, Serikali imetekeleza ahadi
yake ya kuziimarisha huduma za wazee ikiwa ni pamoja na kuwapatia mahitaji ya chakula
kwa ukamilifu, posho, ulinzi na matibabu katika makaazi yao huko Sebleni; ikiwa
ni njia bora ya kutathmini michango waliotoa wakati walipokuwa wakiitumikia
nchi yetu.
Ndugu
Wananchi,
Kuhusu huduma za afya, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imo katika kutekeleza mkakati wa miaka 10 wa kuifanya
Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ya rufaa.
Kitengo maalum cha utafiti pamoja na elimu kwa wafanyakazi juu ya njia
mbali mbali za kukabiliana na maradhi kimeanzishwa. Huduma za tiba zimeimarika zikiwemo Idara ya
meno, upasuaji na kitengo cha ICU. Serikali kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha
Haukeland cha Norway, imeweka vifaa vya kisasa kwenye wodi ya watoto wachanga
wenye umri wa mwezi mmoja.
Ndugu
Wananchi,
Upandishaji hadhi wa Hospitali ya Wete
na ile ya Abdalla Mzee ya Mkoani kuwa Hospitali za Mkoa, umefikia hatua nzuri. Serikali imeshajenga Maabara mpya kwenye
Hospitali ya Wete. Vile vile, jengo
jipya kwa ajili ya wagonjwa wa akili limejengwa kwa msaada wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (ADB).
Katika kuzipandisha daraja Hospitali za
vijiji (Cottage Hospitals) ili ziwe za Wilaya, Serikali kwa kushirikiana na
Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Uingereza HIPZ (Health Improvement Project
Zanzibar) imefanya kazi kubwa ya kuimarisha huduma katika Hospitali ya
Makunduchi. Nyumba za wafanyakazi katika
hospitali ya Kivunge nazo zinafanyiwa matengenezo makubwa.
Aidha, Serikali
imejenga maabara ya kisasa ya uchunguzi wa maradhi mbali mbali katika hospitali
ya cottage ya Micheweni. Maabara hii
ilifunguliwa rasmi katika shamra shamra za miaka 49 ya Mapinduzi.
Ndugu Wananchi,
Kadhalika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imekamilisha ujenzi wa Bohari Kuu la Dawa eneo la Maruhubi, uliogharamiwa kwa
pamoja na Serikali yetu, Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na Shirika la
Misaada la Denmark (DANIDA) ili kurahisisha uhifadhi na upatikanaji wa uhakika
wa dawa nchini. Uzinduzi rasmi wa ghala
hii ulifanyika katika maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi, tarehe 6 Januari, 2013.
Mapambano dhidi ya
Malaria yanaendelezwa kwa kushirikiana na Shirika la “Research Triangle
Institute” la Marekani katika baadhi ya maeneo yanayoonekana kutoa idadi kubwa
ya wagonjwa. Jumla ya nyumba 121,471 zilipangwa kupigwa dawa katika awamu ya
saba, kati ya hizo, nyumba 114,858 (asilimia 95) zilipigwa dawa. Kadhalika,
Jumla ya vyandarua 717,000 vyenye dawa viligaiwa kwa wananchi wa Unguja na
Pemba ili kukabiliana na malaria.
Kwa upande wa VVU/UKIMWI, hadi mwezi wa
Septemba 2012, idadi ya vituo vya upimaji vimeongezeka kutoka vituo 56 mwaka
2011 hadi kufikia vituo 76 mwaka 2012. Idadi
ya wagonjwa 6,793 wamesajiliwa na kupatiwa huduma katika mwaka 2012 ikilinganishwa
na wagonjwa 5,935, mwaka 2011. Aidha, wagonjwa 3,868 wameanzishiwa dawa za ARVS
hadi Septemba 2012, kutoka wagonjwa 3,185 mwaka 2011. Kati ya wagonjwa hao 376 ni watoto.
Ndugu Wananchi,
Hali za afya za baadhi ya wananchi wetu na hasa vijana
zinaendelea kuathiriwa kwa matumizi ya dawa za kulevya. Serikali kwa kushirikiana na jumuiya mbali
mbali zisizokuwa za Kiserikali inaendelea kuchukuwa hatua za kukabiliana
na biashara na matumizi ya dawa hizo kwa
kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Uratibu
wa Dawa za Kulevya inaendelea kutoa
taaluma kwa umma juu ya athari ya dawa
hizo. Napenda kuzipongeza taasisi zote
zinazotoa huduma katika nyumba zote wanazoishi vijana walioamua kuacha matumizi
ya dawa za kulevya. Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hizo, ili kwa
pamoja tuweze kulipunguza tatizo hilo.
Ndugu Wananchi,
Katika hotuba
yangu ya maadhimisho ya sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi, nilielezea jitihada
za Serikali za kuwapatia wananchi huduma za maji safi na salama kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Mkopo huo ni kwa ajili ya mradi wa maji ya vijijini Unguja na Pemba pamoja na
Miji ya Pemba. Ni jambo la faraja kwamba wakandarasi watatu tayari wamepatikana
kwa miradi hiyo na baadhi ya kazi zilianza
tangu mwezi wa Julai, 2012. Kadhalika,
katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa maji kwenye Mkoa wa Mjini Magharibi. Serikali inaendelea kushirikiana
na Serikali ya Japan katika kuendeleza Awamu ya Pili ya Mradi wa Maji wa Mkoa huu.
Katika
maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi, miradi kadhaa ya maji safi na salama ilifunguliwa
katika maeneo ya Fumba, Dunga Bweni na Chaani kwa Unguja; Kojani na mradi wa maji
safi na salama wa Chokocho na Michenzani huko Pemba. Ufunguzi wa miradi hio utasaidia sana katika kupunguza
tatizo la upatikanaji wa huduma hii kwa wananchi wa Chokocho, Kisiwapanza,
Michenzani na Makoongwe.
Ndugu Wananchi,
Kuhusu elimu,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba, inaendelea kuimarisha ubora
wa elimu katika ngazi zote na kuhakikisha kuwa watoto wote waliofikia umri wa
kuanza skuli, wanapata fursa hiyo.
Katika kipindi
cha mwaka mmoja uliopita, idadi ya skuli za maandalizi zimeongezeka kutoka 244
mwaka 2011 hadi 253 mwaka 2012. Uandikishaji wa watoto wanaoanza darasa la
kwanza umeongezeka kutoka watoto 31,146 mwaka 2011 hadi kufikia 34,155 kwa
mwaka 2012. Ongezeko hili ni asilimia 9.7. Skuli 13 za msingi za Unguja na
Pemba zilifanyiwa matengenezo makubwa na kujengwa madarasa mapya 116.
Ndugu Wananchi,
Katika
kuimarisha elimu ya sekondari, skuli
nane mpya za sekondari kati ya 21 zilizoanishwa kwenye Ilani ya CCM ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2010/2015, zimefunguliwa katika kusherekea miaka 49 ya Mapinduzi.
Aidha, ujenzi wa skuli mpya za ghorofa 5 unaendelea vyema katika maeneo ya
Kiembesamaki, Mpendae, Kwamtipura na Kibuteni kwa Unguja na Mkanyageni kwa
Pemba, ili kutoa nafasi zaidi kwa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya
sekondari.
Serikali
inaendelea na juhudi zake za kuimarisha elimu ya amali ili iweze kusaidia katika kutoa ajira kwa
vijana. Jumla ya wanafunzi 336 wanaendelea na mafunzo ya Diploma ya Ufundi
katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume na vijana 720 wanaendelea kupata mafunzo ya amali katika
Vituo vya Mafunzo ya Amali vya Mkokotoni na Mwanakwerekwe viliopo Unguja na Vitongoji,
kiliopo Pemba.
Ndugu Wananchi,
Idadi ya
wanafunzi wanaojiunga na vyuo vyetu vikuu viliopo hapa Zanzibar imeongezeka
kutoka 3,914 mwaka 2011 hadi 4,812 mwaka 2012 kwa vyuo vyote vitatu. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 23. Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar (SUZA) idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 916 mwaka 2011 hadi 1,440
mwaka 2012. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 57. Aidha, Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar imeongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo kutoka T.Shs. bilioni 4 mwaka 2011
hadi T.Shs. bilioni 8 mwaka 2012, ili kuweza kuwahudumia wanafunzi wengi zaidi.
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa
Sekta ya habari, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua mbali mbali za kuimarisha
vyombo vyake vya habari vikiwemo redio, televisheni na magazeti. Ujenzi wa studio za masafa ya kati katika eneo
la Bungi umekamilika na tayari
umezinduliwa. Aidha, Serikali inakamilisha hatua za kiufundi ili kuweza kuhama
kutoka kwenye mfumo wa utangazaji wa analojia na kuingia katika mfumo mpya wa dijitali,
mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu. Vile vile, kupitia mfumo mpya matangazo
ya televisheni ya ZBC yatatolewa kupitia chanali 38.
Matangazo ya
redio na televisheni kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) yameimarika
kwa ubora wa vipindi na muda wa matangazo umeongezwa hadi kufikia saa 24 kwa
siku. Aidha, gazeti la Zanzibar Leo limeimarishwa
zaidi na hivi sasa linawafikia wasomaji wengi zaidi wa vijijini na hata
Tanzania Bara.
Ndugu Wananchi,
Katika
kutekeleza ahadi ya Serikali ya kuwajengea wasanii wetu studio ya kisasa ya
kurikodia muziki na michezo ya kuigiza, Serikali imelifanyia matengenezo
makubwa jengo la zamani la Sauti ya Unguja liliopo Rahaleo kwa ajili ya
kutumiwa na wasanii wetu ili waweze kurikodia kazi zao. Jengo hilo lilizinduliwa tarehe 8 Januari,
2013. Matumaini yangu ni kwamba, kuwepo
kwa studio hio kutachangia sana kukuza utamaduni na ajira kwa vijana wetu wenye
vipaji mbali mbali.
Vile vile, Serikali
imeimarisha shughuli za michezo na utamaduni kupitia matamasha mbali mbali ya
sanaa za maonesho na maigizo ambayo yanaendelea kufana kila mwaka. Michezo mbali mbali ikiwemo mpira wa miguu,
mpira wa vikapu, riadha pamoja na vikundi vya mazoezi nayo imeimarishwa.
Jitihada zinafanywa ili kuirudishia
Zanzibar hadhi yake ya michezo na kulirudisha vugu vugu la michezo hasa
maskulini. Napenda kuchukua fursa hii
kuipongeza timu yetu ya Taifa ya mpira wa miguu “Zanzibar Heroes” kwa kupata
ushindi wa tatu katika mashindano ya CECAFA yaliyofanyika Uganda mwezi wa
Disemba mwaka jana na katika mashindano ya nchi zisizokuwa wanachama wa FIFA
yaliyofanyika nchini Kurdistan.
Kadhalika, nazipongeza timu zetu nyengine zilizotuletea ushindi na
medali ikiwemo timu ya judo, karati, wanyanyua vitu vizito na timu ya mpira wa mikono ya vijana.
Ndugu
Wananchi,
Katika
jitihada za kukuza utalii nchini, Serikali imeifanyia mapitio Sheria ya Utalii Namba 6 ya mwaka 2009 na
sasa Sheria mpya Namba 7 ya mwaka 2012 inatumika ambayo inakwenda sambamba na
dhana ya “Utalii kwa Wote”. Juhudi za
kuitangaza Zanzibar zinachukuliwa kwa kuiwezesha Kamisheni ya Utalii kwa kuipa
nyenzo na vifaa ili iweze kutekeleza jukumu lake, ili lengo la “Utalii kwa
Wote” liweze kufikiwa. Vile vile,
Serikali kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wawekezaji katika Sekta ya Utalii
(ZATI), Jumuiya ya Makampuni ya Watembezaji Watalii (ZATO) pamoja na jumuiya
nyengine itaendelea kujenga mazingira bora ya kuuendeleza utalii.
Wananchi wanahamasishwa kutumia vivutio
vyetu vya utalii ili kukuza utalii wa ndani. Kwa pamoja tutaendeleza juhudi za kukuza sekta
ya utalii kwa kauli mbiu ya “Utalii kwa
wote” ili iendelee kuwa na mchango
mkubwa zaidi katika soko la ajira, kuingiza fedha za kigeni na katika kukuza Pato
la Taifa kwa jumla.
Ndugu Wananchi,
Katika
kuimarisha utawala bora, Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Namba
1 ya mwaka 2012, ambayo itasimamia mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya
ya mitaji ya umma. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, Serikali imeanzisha Mamlaka ya Kupambana na Rushwa Zanzibar na tayari
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo ameshateuliwa. Ni imani ya Serikali kwamba
wananchi sote tutashirikiana na Mamlaka hii ili kuhakikisha kuwa suala la
rushwa na uhujumu uchumi linapigwa vita na kila mmoja wetu.
Aidha, Serikali
inatambua umuhimu wa kuimarisha maslahi bora kwa watumishi wote. Kwa lengo la
kutekeleza azma hiyo, Serikali tayari
imeandaa Miundo ya Utumishi ya Wizara na Taasisi zake mbali mbali na
utekelezaji wake utaanza hivi karibuni. Hatua hii itasaidia kuleta uwiano wa kimaslahi
kwa kuzingatia viwango vya elimu na uzoefu wa utumishi kwa wafanyakazi.
Serikali itaendelea kuimarisha mishahara
na stahili nyengine za wafanyakazi kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu, ili iwasaidie
katika kuendesha maisha yao. Kadhalika, suala la mafunzo ya watumishi
limeendelea kuzingatiwa kwa kukiimarisha
Chuo cha Utawala wa Umma kwa kukipatia jengo jipya huko Tunguu, ambalo
lilizinduliwa tarehe 5 Januari, 2013.
Ndugu Wananchi,
Katika kuleta
mageuzi kwenye mfumo wetu wa kiutawala na kuzipa uwezo zaidi Serikali za Mitaa
kufanya shughuli za maendeleo na kufanya uamuzi kulingana na mahitaji yao,
Serikali tayari imeandaa Sera ya Serikali za Mitaa. Pamoja na Sera hiyo, mpango
wa utekelezaji nao tayari umeshaandaliwa.
Katika kuipa nguvu
za kisheria Sera hiyo na utekelezaji wake, Sheria Namba 3 na 4 ya mwaka 1995 na
sheria Namba 1 ya mwaka 1998 zimeanza kufanyiwa marekebisho. Kukamilika kwa
marekebisho hayo ya sheria kutaongeza kasi ya mageuzi ya Serikali za Mitaa.
Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba
inaendelea na juhudi zake za kuimarisha umoja, mshikamano na maelewano miongoni
mwa wananchi; ambayo ndio siri kubwa ya kuendelea kuwepo amani na utulivu yenye
kuimarisha maendeleo yetu. Hata hivyo,
katika kipindi cha mwaka 2012 kwa nyakati tafauti tulishuhudia vitendo vya
vurugu na fujo ambavyo vilidhibitiwa na vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama. Serikali haitovumilia kufanyika kwa vitendo
hivyo na itaendelea kuchukua hatua madhubuti kwa mujibu wa sheria kwa
watakaofanya vitendo hivyo. Zanzibar iko salama na Inshaallah itaendelea kuwa
salama.
Wito wangu kwenu ni kuzidi kuuimarisha
umoja na mshikamano wetu ambao umeleta amani na utulivu na mafanikio tuliyoyapata.
Ndugu
Wananchi,
Muungano wetu upo imara na katika
kipindi chote tangu ulipoasisiwa, nchi yetu imepata heshima kubwa katika
Jumuiya ya Kimataifa. Kadhalika,
tumepata mafanikio makubwa ya kisiasa, kiuchumi na ustawi wa jamii, ingawa zimekuwepo
baadhi ya changamoto ambazo zinaendelea kushughulikiwa hatua kwa hatua. Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ inayoongozwa
na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itazipatia ufumbuzi
changamoto zilizosalia.
Napenda kukuhakikishieni wananchi wote kwamba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza muungano wetu na kuwatumikia
wananchi wote.
Ndugu
Wananchi,
Kwa niaba yenu nataka nitoe shukurani
kwa nchi zote marafiki, washirika wetu wa maendeleo, taasisi na mashirika ya
Kimataifa zinazoshirikiana nasi kwenye mipango yetu ya maendeleo. Kadhalika, natoa shukurani zangu tena kwa
viongozi wote waliohudhuria hapa wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Natoa shukurani maalum kwa Makamu wa
Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais,
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, kwa ushauri wao na kunisaidia katika kuiongoza
Zanzibar. Kadhalika, nawashukuru Mawaziri,
Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wafanyakazi wote kwa jitihada zao za kuwatumikia
wananchi.
Navishukuru tena vikosi vyote
vilivyozipamba sherehe zetu na jinsi gwaride lilivyochangamsha uwanja
mzima. Aidha, nawashukuru wale wote
walioshiriki kwenye maandamano na wale waliotupa burudani ya aina yake ambayo
sote tumezifurahia. Kadhalika, natoa
shukrani zangu kwa waandishi wa vyombo vya habari kwa kuzitangaza shughuli zetu
hizi kwa ufanisi.
Ndugu
Wananchi,
Nakamilisha shukurani zangu kwa
kukushukuruni sana wananchi nyote wa Zanzibar kwa mambo yafuatayo:-
Kwanza, kwa kushiriki kwa wingi katika
kutoa maoni yenu ya kupatikana Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Ninakusihini muendelee
kushiriki kikamilifu katika hatua zilizobakia, kwa mujibu wa utaratibu
utakaopangwa na Tume inayoratibu maoni hayo.
Zingatieni amani na utulivu viwepo wakati wote.
Pili, ninakushukuruni kwa kushiriki
vizuri na kwa idadi kubwa katika Sensa ya Watu na Makaazi ya tarehe 26 Agosti,
2012. Matokeo ya sensa hii yalitangazwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete hapo
tarehe 31 Disemba, 2012. Kutokana na
sensa hiyo, idadi ya Watanzania sasa imefikia 44,929,012 na idadi ya watu wa
Zanzibar ni 1,303,560. Changamoto iliyo mbele yetu ni kuhakikisha kuwa
tunafanya kazi kwa bidii ili uchumi wetu uendelee kukua kwa kasi zaidi ili pasiwe na athari katika upatikanaji wa
huduma muhimu.
Tatu, ninakushukuruni kwa kuendelea
kushiriki katika kujiandikisha kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa. Ninakuhimizeni muendelee kujiandikisha kwa
haraka bila ya kuchelewa. Hii ni haki
yenu msidanganyike wala msibabaishwe.
Nne, nakushukuruni kwa kuwa pamoja na
Serikali zetu mbili pale nchi yetu ilipokumbwa na maafa ya kuzama kwa meli ya
M.V. Skagit. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kutupa subira na awape malazi
mema ndugu zetu waliofariki katika ajali hiyo.
Tano, ninakushukuruni nyote
mliohudhuria hapa na wale ambao kwa sababu mbali mbali hawakuweza kuhudhuria,
lakini walikuwa wakifuatilia sherehe hizi kwenye vyombo vya habari.
Napenda niishukuru na niipongeze sana
Kamati ya Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho kwa mwaka huu wa 49 wa
Mapinduzi inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais. Mmefanya kazi nzuri na ndio iliyofanikisha
sherehe zetu. Hongereni sana. Ninakutakieni wananchi nyote kheri ya Mwaka
Mpya wa 2013.
MAPINDUZI DAIMA
MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Mhe. Rais hotuba yako nzuri lakini inabidi na utekelezaji wake uwe wa kweli isiwe mnatudanganya kama ilivyo siku zote zilizopita.
ReplyDeleteIngekuwa jambo jema na lafaraja kuomba m/mungu akusaidie kama unavyo sema katika uongozi wako? kuwatowa wale binadamu wanaoteseka Gerezani bila kosa Mashekhe wetu wa jumuia ya Uamsho.
ReplyDeleteJee kosa lao nini wale? ikiwa Mandamano Basi hata mtwara walifanya na hatukuona kuona kutiwa ndani mtu.
Tokea Eddi na hizi sherehe Bado wanasota tu na mumewatia kufuli za mdomo hata kuwapa fursa ya kuzungumza na kueleza walichonacho mumewazuwia kweli wewe unataka Amani kwa Allah au unawafurahicha wakubwa Zako(Wakoloni wa kitanganyika tu?)