Na Maryam Nassor TSJ
WANDISHI wa habari kisiwani Pemba, wametakiwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Idara ya Mazingira kutoa elimu juu ya njia zinazotumika kueneza maradhi ya kuharisha na kipindupindu.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Afya na Mazingira, Halfani Shaha Bakar alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi afisini kwake Machomane Chake Chake Pemba.
Alisema kipindupindu ni maradhi yanayosababishwa na vijidudu vidogo (bacteria) ambao husambaa kwa njia ya kula au kunywa maji yaliyochanganyika na kinyesi cha binaadamu.
Shaha alisema, iwapo wananchi wataelimishwa ipasavyo kupitia vipindi vya radio, televisheni na makala magazetini, wataweza kujiepusha na maradhi hayo.
Alisema mgonjwa huchukua muda mfupi kufariki ikiwa hakupatiwa matibabu ya haraka.
Aidha alifahamisha kuwa, ipo haja kwa waandishi wa habari kushirikiana na wizara ya afya na Idara ya mazingira, kutoa taaluma ya hali ya juu kuhusu njia zinazoeneza ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment