Na Ali Khamis, Pemba
WAHITIMU wa mafunzo ya utibabu wa mifugo kisiwani Pemba wametakiwa kuitumia elimu waliyoipata ipasavyo ili kufikia lengo lililokusudiwa la kuwasaidia wafugaji.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Khafidhi Suleiman Said katika ukumbi wa Idara ya kilimo na mifugo Machomane Chake Chake.
Alisema lengo la serikali la kutoa mafunzo hayo ni kuhakisha huduma ya matibabu ya mifugo inapatikana nchini kote hususan vijiji ambapo mahitaji yake ni makubwa zaidi.
“Kuna uhaba mkubwa wa madaktari wa mifugo vijijini jambo ambalo hupelekea wafugaji kupoteza mifugo yao kwa maradhi hivyo muitumie elimu mliyoipata ipasavyo na kufikisha huduma kwa walengwa,“ alisema.
Aidha ameiomba wizara ya kilimo na mifugo kufanya tathmini juu ya utendaji kazi wa wahitimu hao ili kuhakikisha wanaitumia ipasavyo elimu hiyo na kufikisha lengo la serikali la kutoa elimu hiyo.
Mapema Daktari Mkuu wa Mifugo Zanzibar, Talib Saleh Suleiman alisema ikiwa wahitimu hao wataitumia ipasavyo elimu hiyo itawapunguzia mzigo serikali wa kupambana na changamoto zinazowakabili wafugaji.
Pia aliwataka wahitumu hao kufanya kazi pamoja na Idara ya mifungo katika kupambana na changamoto zozote zitakazojitokeza wakati watakapotoa huduma hizo kwa jamii.
Kwa upande wao wahitimu wa mafunzo hayo walisema wataitumia ipasavyo elimu walioipata ili kufanikisha azma ya serikali ya kutatua uhaba wa madaktari wa mifugo nchini.
No comments:
Post a Comment