Na Abdi Suleiman, Pemba
UKOSEFU wa mashine ya kuvunjia kokoto, wataalamu wa afya, gari ya kusombea mawe katika machimbo ya Kwareni Vitongoji ni miongoni mwa changamoto zinazokikabili kikundi cha akinamama cha Umangani Cooperative Society.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Mariyam Saleh Juma, alisema mashine ya kuvunjia kokoto ndio kikwazo kikubwa kwao, kwani kwa sasa wanatumia nyundo.
Akizungumzia changamoto nyengine, zinazowakabili, alisema ni gari la kusombea mawe na wataalamu wa afya kushindwa kuwatembelea kuwapatia taaluma ya afya.
Akizungumzia lengo la kuanzisha kikundi chao, alisema ni kujikwamua na umaskini na kupunguza utegemezi walionao wanawake.
Aliwaomba viongozi wa jimbo la Wawi, kuwasaidia kwa kila hali na mali, ili kuweza kuondokana na umasikini.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Wawi, Hamad Rashid aliwataka akina mama hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku wakihakikisha wanawapeleka watoto wao skuli kwani elimu ni haki ya kila mtoto.
Aliahidi kuwaunga mkono akinamama hao ili kuhakikisha wanapata mashine wanayoihitaji.
Aidha aliahidi kuwapatia ng’ombe wawili wa maziwa ambao watasaidia kutunisha mtaji wao.
No comments:
Post a Comment