Na Kija Elias, Moshi
MBUNGE wa jimbo la Moshi vijijini, Dk. Cyrill Chami, ametoa rai kwa wananchi wake kumuunga mkono Mkuu wa Mkoa huo, Leonidas Gama, kutekeleza mpango wa hifadhi ya mazingira kwa kupanda miti itakayosaidia kurejesha uoto wa asili.
Dk. Chami alitoa rai hiyo jana wakati akizungumza na wanachama wa vikundi 12 vya wanawake wajasiriamali wa kijiji cha
Mnini, kata ya Uru Mashariki, juu ya mikakati ya serikali inayopaswa kuungwa mkono na wananchi ambao ni wadau wakuu.
Alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa, ni vyema wajasirimali na wananchi wote kwa
ujumla kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo, ambalo litasaidia kuongeza kiwango cha maji kitakachotosheleza mahitaji kulingana na ongezeko la watu.
Alisema uhaba wa maji unachangiwa na uharibifu wa mazingira, ambao umeleta changamoto nyingi katika maeneo mengi nchini, yakiwemo maeneo y jimbo kadhaa ya jimbo hilo.
“Tatizo la maji ni matokeo ya uharibifu wa mazingira, na limeyakumba maeneo mengi sana hapa nchini, katika jimbo langu maeneo ya tambarare imekuwa ni changamoto kubwa hali ni mbaya na hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa,” alisema.
Kutokana na changamoto hizo, alisisitiza haja kwa wadu wote kuanza kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti, na utekelezaji wa mpango wa uchimbaji visima kwa ajili ya kuvuna maji ya ardhini kwa matumizi ya kawaida na umwagiliaji.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo aliwataka wananchi kujipanga kuchagua viongozi watakaowawakilisha na kuzipatia ufumbuzi kero kijamii zinazowakabili.
Kuhusu maeneo ya ukuaji wa uchumi wa wananchi katika jimbo hilo, alisema ni wakati mzuri kwa wajasiriamali kuanza kujipanga na kuunda vikundi vitakavyopatiwa mikopo kutoka taasisi za fedha.
Dk. Chami, amekuwa akifanya ziara ya mara kwa mara kutembelea miradi inayotekelezwa katika jimbo lake, ikiwemo ya barabara,Elimu na afya.
No comments:
Post a Comment