Habari za Punde

KIU walalamikia kutozwa 3m/- maafisa wa mizani



Na Kunze Mswanyama,DSM
UTARATIBU wa upimaji wa mabasi na malori ya mizigo katika mizani mbalimbali nchini,umetajwa kuwa chanzo kitakachoichelewesha Tanzania kufikia maendeleo ya haraka mara baada ya soko la pamoja la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki litakapoanza.

Kauli hiyo imetolewa juzi jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Msafara wa Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kampala (KIU), Shakur Wahad, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  juu ya matatizo waliyokutana nayo katika mizani wakati  wakiingia nchini kushiriki michezo ya vyuo vikuu vya Afrika Mashariki na Kati, inayoendelea katika chuo kikuu cha Dar es Salaam

Akizungumzia kuhusu matatizo hayo,Wahad alisema anashangazwa na utaratibu huo wa upimaji wa magari katika mizani tofauti na nchi nyingine za Afrika Mashariki, huku wakilalamikia kutozwa kiasi cha  zaidi ya shilingi milioni 3 kama faini baada ya  basi lao mali ya chuo hicho walililokuwa wakisafiria  kuonekana kuzidi uzito zaidi ya viwango vilivyowekwa na Wakala wa Barabra nchini (Tanroads).


“Kama Tanzania itataka kufika mahali ikajivunia kimaendeleo inapaswa kulitazama eneo hilo, tumetoka Uganda, tumepita Kenya hatujakutana na kikwazo chochote hadi tulipoingia Namanga kwa upande wa Tanzania ndipo balaa lilipoanza, hii ni kikwazo kwa maendeleo ya Tanzania ikizingatiwa kuna mipango ya kuingia katika soko la pamoja,” alisema.

Alisema walipofika katika  mizani ya Namanga, basi lao lilitozwa faini kwa kuzidisha uzito, na baadae tatizo kama hilo liliwakuta tena  walipofika  mizani iliyopo njia  panda ya Himo mkoani Kilimanjaro na kisha katika mizani ya Mkata iliyopo mkoani Pwani.

Aidha alisema matatizo hayo waliyokutana nayo, yanatokana na wao kutofahamu juu ya uwepo wa utaratibu wa upimaji katika mizani jambo lililowafanya waamini kuwa safari yao ilikuwa salama pasipo tatizo lolote hususani linalohusiana na masuala ya matumizi sahihi na sheria za barabara.

Wahad alisema  anaamini Tanzania ina fursa nyingi za kimaendeleo na kwamba ili iweze kujihakikishia inatimiza ndoto zake kuendelea kukua kiuchumi, ni vyema ikatazama maeneo muhimu yanayochangia kukua  kwa uchumi huo ikiwemo njia ya usafirishaji hasa  barabara.

Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema wizara inalifuatilia suala hilo ili kufahamu undani wa tatizo walilokutana nalo wanafunzi hao katika mizani na kisha atalitolea ufafanuzi baadae.

 “Kiasi fulani nimesikia taarifa kuhusiana na suala hilo, lakini naomba nipe muda ili niweze kulifuatilia kwa ajili ya kupata taarifa kamili halafu nitakujulisha kila kitu juu ya kilichokuwa kimetokea,” alisema.

Akizungumzia kuhusu utaribu wa upimaji mabasi katika mizani, Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania(TABOA) Enea Mrutu, alisema Tanzania inapaswa kujifunza kutoka katika nchi zingine kama kweli ina nia ya kuboresha sekta ya usafiri.

Alisema inashangaza kuona utaratibu huo kuwepo Tanzania pekee suala alilosema ni vyema kama litatazamwa upya  kwa lengo la kuondoa dosari zilizopo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.