Habari za Punde

Madiwani Musoma wamuonya Mkurugenzi


Na Pascal Buyaga,Musoma
BARAZA  la Madiwani manispaa ya Musoma limemuonya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,  Ahmad Sawa kwa kitendo cha kuwasilisha rasimu ya  bajeti, Wizara ya Fedha bila kufuata utaratibu wa kupitia vikao  vya halmashauri.

Kauli hiyo ilitolewa na Madiwani hao Jumamosi  katika kikao maalum kilichokuwa kikijadili hoja hiyo ambayo ilileta mvutano mkubwa baina ya Madiwani huku baadhi wakitaka baraza lijigeuze kama kamati ili kumjadili Mkurugenzi kulinda heshima ya Meya wa manispaa ya Musoma, Alex Kisurura.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na sakata hilo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Ahmad Sawa alisema Januari 21 aliitwa ofisi ya Mkuu wa  Mkoani wa Mara na kuagizwa kuwasilisha rasimu ya  bajeti ya mwaka wa fedha 2013 /2014 haraka iwezekanavyo kabla ya  Januari 30.

Sawa alisema baada ya agizo hilo, manispaa walianza   kuandaa rasmu ya  bajeti kwa kushirikiana na wakuu wote wa idara  na hatimaye kufanikiwa  kuwasilisha kama maagizo ya serikali yalivyotolewa ambapo  walifanya hivyo  kwa ajili ya maslahi ya halmashauri  na wananchi.


Hata hivyo kutokana na kanuni juu ya uwasilishwaji wa bajeti inapaswa ipitie Baraza  la Madiwani ili kutoa fursa kwa  madiwani kuwasilisha vipaumbele vyao vya  maendeleo katika  Kata  na kumuomba  Katibu tawala wa Mkoa wa Mara  kuwaandikia barua ikieleza mabadiliko hayo ili Madiwani wajiridhishe.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Kisurura alisema  agizo hilo lilikuwa la nchi nzima hivyo Mkurugenzi asingekaidi na kuwaomba  Madiwani kujali uwakilishi wao kwa wananchi  kwa kutumia busara  kulijadili suala  hilo kwani ni makosa yaliyofanyika na badala yake mapungufu yaliyojitokeza yafanyiwe marekebisho na watalaamu.

Kisurura ameliambia baraza la Madiwani kuwa mabadiliko hayo yametokana na mfumo wa nchi za Afrika Mashariki ambazo bajeti huwasilishwa Aprili na kutoa nafasi kwa serikali kutoa fedha za miradi mbali mapema iwezekanavyo.

Diwani wa kata ya Nyakato (CCM) ambaye ni Meya mstaafu, Swahib Mohamed  alisema suala hilo lilitekelezwa na menejimenti ambapo meya hakujua mchakato mzima sambamba na kamati ya fedha na kuhoji udharura  huo ulikuwa  ni wa maslahi ya nani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.