Habari za Punde

Makamu wa Kwanza akibidhiwa Mipira ya Kukuza Vipaji kwa Vijana Zanzibar.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akipokea mipira kutoka kwa mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar Bi. Sharif Khamis, katika hafla fupi ya kukabidhi mipira hiyo iliyofanyika ofisini kwake Migombani.(Picha na Salimin Said OMKR)

Hassan Hamad, OMKR. 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea haja ya kupitiwa upya kwa sheria na sera ya michezo Zanzibar ili ziendane na mahitaji ya sasa ya kimichezo.

Amesema katika mapitio hayo ni vyema kulipa nguvu Baraza la Michezo Zanzibar  ili liwe na uwezo wa kuingilia migogoro inayojitokeza mara kwa mara katika vyama vya michezo nchini.

Maalim Seif ameeleza hayo ofisini kwake Migombani katika hafla fupi ya kukabidhiwa mipira na kamati ya ugawaji wa mipira chini ya mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar Bi. Sharifa Khamis.

“Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, ina kazi kubwa ya kuipitia sera nzima ya michezo ili iendane na wakati, na kulipa meno Baraza la Michezo kuweza kuingilia kati migogoro hii ya mara kwa mara  ndani ya vyama vyetu vya michezo”, alisisitiza Maalim Seif.

Katika hatua nyengine Maalim Seif ameelezea umuhimu wa  kuanzishwa kwa chuo maalum cha kuendeleza vipaji kwa vijana ili kukuza vipaji hivyo na kuwa na wachezaji bora hapo baadae.

“Michezo ni uchumi, lakini pia michezo ni afya, kwa hivyo tuwahamasishe watu wetu washiriki michezo, na vile vile tuibue na kuviendeleza vipaji vya vijana wetu”, alifahamisha Maalim Seif.

Akizungumzia kuhusu ugawaji wa mipira, Maalim Seif amelipongeza Baraza la Michezo Zanzibar kwa kujenga uaminifu kwa wahisani na kupelekea kupata misaada mikubwa ya kuendeleza michezo.

Amesema hatua ya upatikanaji wa mipira hiyo kupitia mradi wa ugawaji wa mipira chini ya ufadhili wa Shirika la Kimataifa la kuwalinda watoto “Save the Children” ni kubwa na inaweza kuisaidia Zanzibar kurejesha hadhi yake ya kimichezo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar Bi. Sharifa Khamis amewaomba viongozi wakuu wa Serikali kusaidia ugawaji wa mipira katika maeneo  mbali mbali ili kuhakikisha kuwa inawafikia walengwa.

Amemuhakikishia  Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa kazi ya ugawaji wa mipira inafanywa kwa umakini mkubwa, na kwamba itawafikia walengwa kupitia mkakati maalum wa kufanya uhakiki kwa kila Wilaya za Unguja na Pemba.

Amesema miongoni mwa watakaonufaika na mradi huo ni timu za vijana wadogo wa mitaani zilizosajiliwa na zisizosajiliwa, ili kuwapa motisha wa kuendeleza michezo na kuibua vipaji.

Nae Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar Bw. Khamis Abdallah Said amesema mradi huo wa ugawaji wa mipira unakwenda sambamba na ujumbe wa “kampeni dhidi ya unyanyasaji wa watoto”.

Amefahamisha kuwa Mradi huo mkubwa wa ugawaji wa mipira, tayari umezaa mradi mwengine ujulikanao kwa jina la “Coaches Across Continent” ambao utahusika na ufundishaji wa makocha, ili kuwajengea uwezo wa kufundisha vyema katika timu zao.

Hassan Hamad, OMKR.

1 comment:

  1. acheni upumbavu , nchi haina mambo muhimu ya kijamii , nyie mmeshikilia mipira tu hamna lingine , maji hakuna visiwani , watu wabebe madoo na madumu kutafuta kitu ambacho ni cha msingi kwa maisha , haya nendeni mkakate viuno huko mipirani, kuna wasenge wa vitendo , na kuna wasenge wa tabia ....

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.