Na Miza Kona- Maelezo Zanzibar 20/02/2013
Waandishi wa habari wametakiwa kubadilika katika fani yao kwa kuandika habari zenye maslahi kwa jamii badala ya kuandika habari za viongozi wa kisiasa na watu maarufu pekee.
Wito huo umetolewa na Mwandishi mwandamizi na Mkufunzi wa Fani ya Uandishi wa habari Salim Said Salim wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar katika ukumbi wa Wizara ya habari Kikwajuni mjini Zanzibar.
Amesema fani ya Uandishi wa habari inaendana na wakati hivyo waandishi wanapaswa kujifunza zaidi kila wanapopata nafasi ili kukabiliana na mabadiliko yanayotokea katika tasnia ya habari.
Salim amesema miongoni mwa mabadiliko muhimu yanayopaswa kupewa kipao mbele katika uandishi ni kuandika habari zinazohusu matatizo ya vijijini ili jamii iweze kuyafahamu badala ya kuandika habari za mijini pekee.
Aidha amewasisitiza Waandishi kufanya uchunguzi wa kina bila kuegemea upande wowote katika kuandika habari zao ili kuondoa sintofahamau zinazoweza kujitokeza.
“Andikeni habari za uhakika na mnapoandika habari zenye pande mbili hakikisheni kila upande mnaupa haki sawa dhidi ya upande mwingine, kama mtu mmoja mkimpa paragrafu nne na mwingine apewe hizo hizo” alisisitiza Salim.
Awali akifungua Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na UNESCO Mkurugenzi Sera Mipango na Utafiti wa Wizara ya habari, Mwita Mashengo Hassan amesema kwa kufahamu umuhimu wa kujiendeleza Wizara imeamua kuwajengea uwezo waandishi wa Idara hiyo ili waweze kukabiliana na mabadiliko ya kiuandishi.
Mkurugenzi Mwita amesema uandishi wa habari ni kipaji hivyo Wanahabari wanapaswa waendelee kujifunza fani hiyo ili kukuza vipaji vyao na kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
Aidha amewataka waandishi hao kuwa makini katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na kusikiliza maagizo yote yatakayotolewa na Mwalimu wao.
Mafuzo hayo ya siku tano ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Idara ya habari Maelezo Zanzíbar yamefadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR 20/02/2013
No comments:
Post a Comment