Na Fatuma Kitima, Dar es Salaam
KIJANA aliyetambuliwa kwa jina la Barnaba Venant (18) amejinyonga kwa kutumia kamba ndani ya nyumba yao baada ya kupata matokeo mabaya katika mitihani ya kidato cha nne.
Taarifa kutoka jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam zinaeleza kuwa kijana huyo alijinyonga juzi Februari 19 maeneo ya Nzasa wilaya ya Temeke jinini Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa sababu ya kujinyonga kijana huyo ni kutoridhishwa na matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa wiki hii, ambapo asilimia 60 ya watahiniwa wamepata alama sifuri.
Marehemu wakati wa uhai wake alikuwa akisoma katika shule ya sekondari Debrabant iliyopo Mbagala.
Maiti imehifadhiwa katika hospitali ya Temeke na upelelezi bado unaendelea.
Katika tukio la pili mtu mmoja alietambuliwa kwa jina la Mzee Seleman amekufa mara baada ya kudondoka katika sehemu ya mapokezi ya hoteli ya Mikocheni Resort huku akiwa na mwanamke aliyetambulika kwa jina moja la Fadhila.
Tukio hilo lilitokea saa 2 :00 usiku katika hoteli hiyo.
Mtoa taarifa Abdul Hamis dereva taxi mkazi wa Mikoroshini alidai kuwa saa hizo alikuwa katika maegesho yake eneo al Shoppers Plaza ambapo alipigiwa simu na mteja wake afike hotelini hapo amchukue yeye pamoja na mwanamke aliyekuwa nae aitwae Fadhila.
Lakini baada ya kufika katika eneo hilo alimkuta marehemu akiwa hajitambui akiwa eneo la mapokezi na mwanamke huyo.
Chanzo cha kifo chake bado hakijafahamika na maiti imehifadhiwa hospiatali ya Mwananyamala kwa uchunguzi.
No comments:
Post a Comment