Habari za Punde

Adhabu ya bakora skuli kurejeshwa

Na Kunze Mswanyama,DSM
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Philip Mulugo,amesema serikali inaangalia upya utaratibu wa kurejesha adhabu ya bakora shuleni ambayo iliondolewa kuunga mkono azimio la kimataifa la kuzuia ukatili kwa watoto jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi na nidhamu kwa wanafunzi.

Mulugo pia alisema,wananchi waache kuwafuatafuata yeye na Waziri wake, Dk.Shukuru Kawambwa kwa lengo la kujiuzulu kwa kuwa hata kama watajiuzulu sio suluhisho la kushuka au kupanda kwa kiwango cha elimu nchini.

Akizindua tovuti ya www.shuledirect.co.tz itakayosaidia wanafunzi wa shule za sekondari kujisomea kwa njia ya mitandao jana jijini Dar es Salaam,Mulugo alisema,”nasema waziwazi serikali inapitia upya taratibu zake ili kurudisha adhabu ya bakora shuleni kwa kuwa bila bakora mambo hayaendi huko.”


Huku akitolea mfano namna alivyokuwa hodari wa kuchapa bakora katika enzi zake akiongoza shule moja ya sekondari huko Mbeya,Mulugo alijinasibu kuwa katika kuwachapa watoto hao bakora,alirudisha nidhamu shuleni hapo na kuifanya kuongoza mkoa wa Mbeya katika taaluma.

“Nilikuwa naongoza shule moja huko Mbeya,nikawa natumia nafasi aliyopewa mkuu wa shule kuchapa bakora nne,hizo ziliwafanya watoto kuwa katika mstari wa nidhamu na tukaongoza mkoani,hali hiyo iliwafanya wengi kuja kujifunza kwangu,”alisema Naibu huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu.

Alisema,kama watoto hawatachapwa hakutakuwa na mafanikio katika elimu hivyo kuwataka wanaharakati wanaotetea wanafunzi kutochapwa kuacha harakati zao kuzuia kitendo hicho kwani elimu ni ufunguo wa maisha hivyo kila Mtanzania anawajibu wa kuwa mwalimu katika jamii aliyopo.

Aidha,Mulugo ambaye alitumia jukwaa hilo pia kuwapiga vijembe wale wote wanaomfuatafuata hasa katika masuala ya elimu yake,alisema yapo mambo mengi ya kufanya lakini siyo kila wakati kukaa kwenye mitandao na kuanza kumsema yeye tu ili naye achangie neno na kuwafanya wananchi kumuona kuwa hafanyi kazi bali hushinda mtandaoni.

Alisema,wananchi wengi wanataka yeye na waziri Kawambwa wajiuzulu na kusahau dhima kubwa ya usimamizi wa shule imepewa wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa hivyo kama ni kujiuzulu waanze hao ndipo waje wao.

“Kwanza wengi hamfahamu kuwa usimamizi wa shughuli za shule za kila siku upo TAMISEMI siyo kwetu,hivyo msitufuatefuate sisi kutaka tujiuzulu badala yake wafuateni kwanza hao TAMISEMI wenye dhamana na shule za msingi na sekondari hapa nchini,” alisema.

Akiwaasa wanafunzi ambao watakuwa watumiaji wa mtandao huo kujisomea,kuuliza maswali na kufanya mitihani mbalimbali ya zamani,Mulugo aliwakanya kuacha kutumia mtandao kwa masuala ya kimahaba na kutambua dhima kubwa waliyonayo katika kulikomboa taifa kwa siku za baadae.

“Hili nalisema kweupe, msitumie mitandao kwa masuala ya mapenzi,utakuta mwanafunzi anacheza na Facebook muda wote wanatumiana ujumbe wa mapenzi tu,hayo siyo matumizi ya mtandao jamani,” aliwaasa na kuongeza;

“Natumia fursa hii kuwambia walimu wote,atakayemuona mwanafunzi shuleni akiwa na simu amnyang’anye hapo hapo,kwani zinachangia kupotosha wanafunzi hawa na kuwafanya washindwe kusoma kwa makini,ni hatari kama tutaendekeza mambo haya.”

Pia alikiri nchi kukumbwa na changamoto ya wanafunzi wengi kufeli lakini alijifariji kwa kusema ni suala la ukanda wa Afrika Mashariki yote na kwamba hata kama watajiuzulu bado siyo suluhisho la ubora wa elimu bali kila mmoja atimize wajibu wake kwa manufaa ya elimu nchini.

“Nampongeza dada Faraja Kota Nalandu kwa kuacha kuilaumu serikali kwa watoto kufeli badala yake ametimiza wajibu wake wa kuanzisha mtandao huu ambao utakuwa na vitabu vyote,walimu watakaokuwa wakijibu maswali ya wanafunzi mtandaoni,mitihani ya zamani na mambo mengi yatakayowahusu wanafunzi,kaisaidia sana serikali kuinua elimu,” alisema.

Pia alishangaa kuona walimu wanawafundisha wanafunzi kuwa 1+ 1= 11 na 3=3=33 wakisingizia ni kutaka kuikosoa serikali lakini aliwataka walimu hao kukumbuka kuwa kama vijana hao wasipopata elimu bora matatizo yatakayotokea yatalikumbuka taifa na hayatachagua wa kumkumba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.